Tujikumbushe: "Amri Kumi za Mafisadi!" | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tujikumbushe: "Amri Kumi za Mafisadi!"

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Buchanan, Nov 17, 2009.

 1. Buchanan

  Buchanan JF Diamond Member

  #1
  Nov 17, 2009
  Joined: May 19, 2009
  Messages: 13,096
  Likes Received: 247
  Trophy Points: 160
  HIZI ndizo amri kumi kubwa kwa mafisadi popote pale wanapopatikana chini ya Jua la Mwenyezi Mungu. Wote huziheshimu amri hizo kama wanavyoheshimu nafsi zao na punde mmoja akivunja yoyote kati ya hizo shuruti atoswe na kundi. Naam, hizi ndizo zinazoleta madhila kwa mamilioni ya watu wanaokufa kwa kukosa chakula, dawa, maji na kupukutika kwa magonjwa yanayozuilika.

  Amri ya kwanza; usiwe na dhamiri ya woga juu ya kile ukifanyacho kwa ajili ya faida yako binafsi na mafisadi wengine popote walipo. Mafisadi ni ndugu mmoja bila kujali nasaba ya damu. Ukiwa na dhamiri inayokuuma kwamba unapotwaa bila halali unasababisha madhara kwa umma utashindwa kukomba. Watoto wa mjini wanakuambia ‘zubaa uchekwe'. Hakikisha umeua dhamiri yako ili uwe na roho mbaya kuliko hayawani wa mwituni wasiojua uchungu wa vifo vya watoto chini ya miaka mitano, vifo vya akina mama wanaojifungua na madhila ya kunywa maji yenye kinyesi. Ua dhamiri yako.

  Ufisadi ni vita na fisadi ni kamanda. Kamanda hapaswi kuwa mwoga maana atashindwa. Ukithubutu kuiogopa dhamiri yako kuhusu hicho wanachokiita ‘ubinadamu' ujue ufisadi sio anga zako na itakuwa afadhali ukaenda kutafute maisha ya watu kama Kwame Nkrumah au Julius Nyerere ujaribu kuyaishi maisha yao. Dhamiri safi ni adui mkubwa wa ufisadi. Usiruhusu hilo asilani.

  Amri ya pili;
  Chao-chako, chako-chako. Huu ni msingi muhimu sana kwa ufisadi. Chochote unachokitazama mbele yako fanya bidii kukinyakua na kukitia kibindoni. Hakikisha macho yako yanatazama huku na huko. Pua yako inuse kule na kulee. Popote penye harufu ya ulaji jiongezee ili utwae bila kujali kama hicho ni chao. Chao kifanye chako na chako kibakie kuwa chako. Angalia hazina ya nchi, kama kuna kautobo donoa sarafu uiweke kwenye pochi yako. Chungulia misaada inayoletwa, usijali kama imelenga waathirika au waadhirika, kama kuna nafasi ya kudonoa, chomoa maana chao ni chako! Usijidai ‘mlokole'.

  Paramia bila kujali mali husika iko majini, ardhini au hata chini ya miamba. Usijali kama ni madini, kimiminika au gesi. Unapoweza kuvuna vuna maana chao ni chako. Zuia chako kisichukuliwe maana chako ni chako. Kilicho chako kizuie kwa nguvu zote; iwe kwa mikataba wanayoita mibovu, sheria za kodi, mianya ya rushwa usijali. Sifa kuu ya fisadi ni kuzuia chake na kuchukua vya wengine. Kusanya usipotawanya, lakini kamwe usiruhusu mtu achukue vilivyo kwenye ghala zako.

  Amri ya tatu;
  Usimwogope Bwana Mungu wako. Hii inafanana sana na amri ya kwanza. Lakini hapa unapaswa kuwa mcha Mungu machoni pa watu lakini ibilisi ndani ya nafsi yako. Wakienda kuabudu nenda nao. Wakifanya toba, shiriki nao lakini watakapokosea hesabu komba kila iwezekanavyo. Kuwa mstaarabu jukwaani, lakini fisadi ofisini. Usiogope kuwa chui katika ngozi ya mwanakondoo. Vuna kwa kutumia jina la misaada, ufadhili na huduma kwa umma. Lakini daima iambie nafsi yako usimwogope Mungu ili usije ukaona ufanyacho ni dhambi. Usije ukawaza habari za maisha baada ya kifo. Kazi ni moja tu; ponda raha kufa kwaja.

  Amri ya nne; tafuta mamlaka ya ulimwengu huu. Ikiwa kwa sababu zisizozuilika umeshindwa kuwa miongoni mwa wenye mamlaka, enzi, ukuu, utukufu na sifa basi shuruti uwe mpambe wao. Hakikisha unakula nao, unacheka nao, unatembea nao na ikiwezakana unaishi nao. Kuwa mpambe maana wanasema mtoto akinawa mikono anaweza kula na mfalme. Kama wewe sio Kiongozi basi takasa mikono yako ule na viongozi. Ukiwa fisadi bila kuwa karibu na wenye enzi utaishia nyuma ya nondo za gereza. Huko siko kwa watu wa ina yako ewe fisadi. Huko ni kwa ajili ya walioiba kuku wa jirani au walioomba rushwa ya dinari mbili! Fisadi unatakiwa ufaidi ufisadi wako ukiwa huru wewe na wapambe wa wako na wapambe wa wapambe wako.

  Usiogope kutumia fedha yako ili kuwa karibu na wazito walishika hatamu. Tumia jina lolote; iwe ni ufadhili au mshikamano, haina tabu. Changia bila kuogopa pale ambapo ni dhahiri kwamba unayemchangia si sawa na punda ambaye shukrani kwake ni mateke. Wewe ishi kwa falsafa isemayo tenda wema na subiri wema hapo hapo. Usiogope kudai ulichowekeza. Wanasema tumia hela upate hela. Huo ndio uwe msaafu wako. Kukaa na wakubwa si rahisi maana ingekuwa hivyo hata hohehahe nao tungewaona wakiingia kwenye sebule za waliotukuka. Fedha sabuni ya roho. Takasa mikono yako ewe fisadi ule na wafalme.

  Amri ya tano; usijiwekee mipaka. Usikubali kuwa na mipaka katika shughuli zako za kifisadi. Kama kuna uwezekano wa kufanya ufisadi fuatilia popote pale pawapo. Usijali kama ‘dili' inafanyikia Uingereza au Uitaliano au hata Beirut. Tuma maajenti wako au nenda mwenyewe. Ni kosa kujiwekea mipaka katika ufisadi. Vyote vilivyomo ulimwenguni. Utandawazi ni jambo jema mno kwa fisadi. Hubiri na kuutetea huo utandawazi ili uwapige ‘changa la macho' wanaoweza kudanganyika.

  Tumia huo ili mirija yako ya unyonyaji ipate baraka na ithibati za wenye mamlaka. Tumia jina hilo ili asije mtu akathubutu kukuita mwizi. Wezi ni wale wanaochomwa moto kwa kukwapua hereni ya mwanamama au kuchomoa simu ya mkononi. Hao ndio wezi. Ninyi mafisadi ni wadau wa soku huria na utandawazi. Baadhi yenu ni makuwadi wa soko huria. Uhuria wa soko hauna mipaka. Pora, vuna na chukua chochote unachoweza kukifikia popote pale kilipo bila kujali gharama utakazosababishwa kwa wengine. Faida yako ndio mpaka wako.

  Pia usijiwekee mipaka ya unachopora. Hata ikibidi kupora maiti sawa. Dawa za hospitali zikikaa kwenye kona mbaya usiogope. Poara tangu fedha hadi nyumba. Tangu madini hadi mafuta. Pora bila ukomo wa aina ya bidhaa inayostahili kuporwa ikiwa wataka kuwa fisadi. Pia usijiwekee mipaka ya unayempora. Awe kikongwe anayestahili haki, fumba macho. Sema kimoyomoyo kwamba huyo haki ataikuta kwa Mungu. Fisadi hana ukomo wa uporaji. Hata taifa likizubaa litajikuta limeporwa utaifa wake.

  Amri ya sita; Uwe na ushawishi kwenye vyombo vya habari. Hili ni jambo muhimu sana ewe ndugu fisadi. Kumbuka ncha ya kalamu ni kali kuliko ile ya upanga. Kalamu inatosha kukupa umaarufu mkubwa. Inaweza kukupamba. Inaweza kukunyanyua juu sana. Kalamu hiyo hiyo inaweza kukuporomosha. Hivyo hakikisha una ushawishi mkubwa kwenye vyombo vya habari.

  Ukipata ushawishi huu machafu yako yataachwa chini ya zulia. Yale mema yatatangazwa kwa sauti kubwa kuliko baragamu. Ni muhimu kuwa karibu na vyombo hivi maana utavitumia sana katika shughuli zako.

  Ukiwa na ushawishi stahili katika vyombo hivi utakuwa unajijengea himaya kubwa na pia daima utavitumia kujitakasa. Kwani hamjui watu wanaviamini sana vyombo vya habari? Mipango yako ya kifisadi ipachike majina mazuri na tumia vyombo vya habari kuitangaza. Utashangaa namna wanaodanganyika watakavyoamini kila kisemwacho.

  Unaweza kujidai kwamba wewe unakuja kutoa huduma ya dharura au kutoa suluhu ya tatizo fulani. Jitangaze kwamba wewe ndiye kimbilio pekee. Hakuna atakayegundua kwamba nyuma ya huduma yako kuna ufisadi usiomithilika.

  Watu watakuona wewe ni mdau katika maendeleo na bila shaka watashiriki nawe, tofauti ni kwamba wewe utakuwa unavuna na wenyewe watakuwa wanaendelea na maumivu bila kinyongo!

  Amri ya saba; Usiogope kusema uongo. Hii ni amri muhimu sana. Kama utakuwa umetekeleza vema amri ya sita hutapata tatizo kubwa kwenye kutekeleza amri hii. Kwa maneno mengine uongo unaotakiwa kuusema hapa sio uwaeleze mkeo au mumeo. Ni uongo unaopaswa kupasua anga. Uufikie umma.

  Hata ikibidi mchana wa jua kali kuuita usiku fanya hivyo. Kanusha vyote vinavyokuharibia sifa yako bila kujali ushahidi unaotolewa. Halalisha yale yote uliyoyafanya bila kujali hoja ulizo nazo. Kazi ni moja tu; tumia maneno kujilinda na kuendeleza ufisadi wako. Usiogope kusema usichomaanisha na kumaanisha usichosema.

  Uongo wako unatakiwa uwe katika nyanja zote ikiwa wataka kuwa fisadi aliyekubuhu. Danganya tangu bei za manunuzi hadi za matanuzi. Inapowezekana nunua hata matumizi hewa. Unapoweza kulipa mishahara bila kuwapo wafanyakazi fanya hivyo. Unapoweza kushinda mamlaka kwa kutumia uongo usijivunge ewe fisadi. Maandiko yanasema shetani ndiye baba wa uongo, basi ujue pia kwamba uongo ni mhimili muhimu mno kwa fisadi. Sema uongo bila kuona haya. Mtaani wanasema mdomo haulipiwi kodi.

  Amri ya nane; Maslahi binafsi yatangulie yale ya umma. Huu ndiyo mzizi hasa wa ufisadi. Ukifanya kosa ukatanguliza maslahi ya umma mbele utakuwa fisadi goi goi. Fisadi mkakamavu hana simile linapokuja suala maslahi ya binafsi.

  Ubinafsi kwanza hayo mengine yafuate. Kwamba kwa ufisadi wako hakutakuwa na vifaa mahospitalini hiyo si kipau mbele chako. Kwamba ufisadi wako utadidimiza elimu na kuongeza ujinga pia hilo sio jambo la kukusumbua kichwa. Kumbuka amri ya pili inasema chako ni chako na chao ni chako! Yote hii ni kulinda maslahi yako binafsi ewe fisadi.

  Katika kulinda maslahi hayo usitegemee utafanikiwa kufuata taratibu, kanuni na sheria husika. Utalazimika kusigina taratibu na kanuni. Utatofautiana na wengi lakini kumbuka fisadi ana wajibu wa kulinda maslahi binafsi hivyo wapuuze wote watakaodai eti hukufuata taratibu stahili.

  Tumia vyema amri ya sita na saba ili kuhalalisha mapungufu utakayolazimika kuyafanya katika utendaji wako. Tumia vyombo vya habari kutoa ufafanuzi. Tumia uongo kuzima hoja. Ukifanya hivyo utakuwa katika nafasi nzuri sana ya kuendeleza ufisadi pasi kuona soni.

  Katika kuangalia maslahi binafsi usitishwe na maneno kama vizazi vijavyo havitatuelewa, maliasili ya taifa inapotea, wanatuachia mashimo, wanatunyonya, na mengine kama hayo. Ukosefu wa uzalendo ni mhimili muhimu kwa fisadi. Angalia unachotaka na kitekeleze kwa gharama yoyote.

  Hasara ya umma si hasara yako. Kwanza unajali kuhusu huduma bora hapa kusudi iweje? Matarajio ni kwamba fisadi na familia yake wanapata huduma nzuri popote ulimwenguni zinakopatikana kwa ubora stahili. Shule na hospitali zitafuatwa na fisadi popote pale zilipo kwa faida yake na familia yake ndogo. Ubinafsi ni wimbo usiopaswa kukukauka katika kinywa chako ewe bwana fisadi!

  Amri ya tisa; Inapobidi cheza rafu, usitegemee kile kinachoitwa ‘fair play'. Hiyo waachie FIFA na wenzake. Katika hili unatakiwa ujifunze falsafa moja muhimu, falsafa hii ni kwamba mwisho unahalalisha njia. Kwa maneno mengine fisadi usiogope kutumia njia haramu kufikia mwisho unaoutaka.

  Ndivyo wafanyavyo fisadi wenzako popote pale ulimwenguni. Kama mafisadi wasingecheza rafu basi ujue wangekwama sehemu nyingi, rafu hii ichezwe kwa yeyote anayejaribu kukuzuia kufunga goli lako la kifisadi. Gharama ya rafu inaweza kuwa kubwa kwa anayechezewa lakini kumbuka amri ya kwanza ya fisadi ni kutokuwa na dhamiri ya woga.

  Usiogope nani anapoteza nini katika ufisadi wako. Kama ulivyoamriwa katika amri ya nane, maslahi binafsi ndiyo hasa yanapaswa kuwa lengo lako. Kama utatekeleza amri inayokutaka utafute mamlaka katika ulimwengu huu hupaswi kuhofu kuhusu matokeo ya rafu utakayocheza maana kwa mamlaka hayo usishangae mtuhumiwa akaingilia mlango wa hakimu!

  Amri ya kumi;
  Uwe mtengeneza mfalme. Ni muhimu katika chochote unachofanya ewe fisadi uhakikishe unakuwa katika nafasi ya kuamua nani awe nini katika mfumo wa utawala. Ukifanya hivyo utakuwa na hakika ya kutokuingiliwa kirahisi na watawala wasio mafisadi.

  Ukijiweka katika nafasi ya ‘kingmaker' - huwezi kuwa na hofu ya kuhukumiwa katika siku za usoni na watwala mtakaotofautiana, utakuwa umejitengezea duara la kurithishana mamlaka. Wewe utawaachia mamlaka wanao na wao watawaachia mamlaka wajukuu wako.

  Duara la mamlaka na ufisadi vitadumu kwa namna hii, ukikatili mduara huu ipo siku utaporomoka na kujikuta mkimbizi, ukikimbia si tu taifa lako bali na mali uliyoichuma. Bahati mbaya kuna wakati muda unakatili duara hili na hapo wenye nchi huwaondoa mafisadi katika nafasi na kuwapa adhabu stahili. Uwe mwangalifu wa alama za nyakati utambue lini hili linakaribia kutokea.

  SOURCE: http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/12/2/makala1.php
  pia SOURCE: http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/12/9/makala13.php

  Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu; 0784 265072 au barua pepe: kevinmakyao@hotmail.com
   
 2. Buchanan

  Buchanan JF Diamond Member

  #2
  Nov 17, 2009
  Joined: May 19, 2009
  Messages: 13,096
  Likes Received: 247
  Trophy Points: 160
  Wadau leteni maoni kama yapo!
   
 3. Tumain

  Tumain JF-Expert Member

  #3
  Nov 17, 2009
  Joined: Jun 28, 2009
  Messages: 3,158
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 0
  Amri kumi kwa mujibu wa kitabu kipi?
   
 4. K

  Karandinga Member

  #4
  Nov 17, 2009
  Joined: Jun 25, 2008
  Messages: 66
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Ufisadi 101 by Rostam Aziz........
   
 5. Serendipity

  Serendipity JF-Expert Member

  #5
  Nov 18, 2009
  Joined: Jan 24, 2009
  Messages: 475
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 35
  I think this is very clear, the ten Mafisadi's commandments are according to Buchanan himself! i.e Kitabu cha Buchanan
   
 6. Junius

  Junius JF-Expert Member

  #6
  Nov 18, 2009
  Joined: Mar 11, 2009
  Messages: 3,183
  Likes Received: 14
  Trophy Points: 133
  Nilikuwa naangalia amri ya sita nilifikiri inafanana fanana kidogo.
   
 7. Masanilo

  Masanilo JF-Expert Member

  #7
  Nov 18, 2009
  Joined: Oct 2, 2007
  Messages: 22,319
  Likes Received: 144
  Trophy Points: 160
  Kuna watu humu hawatazipenda hizi amri! this is great jamaa anawajua mafisadi
   
 8. Buchanan

  Buchanan JF Diamond Member

  #8
  Nov 18, 2009
  Joined: May 19, 2009
  Messages: 13,096
  Likes Received: 247
  Trophy Points: 160
  Sure, kuna watu zinawauma kweli!
   
 9. Buchanan

  Buchanan JF Diamond Member

  #9
  Nov 18, 2009
  Joined: May 19, 2009
  Messages: 13,096
  Likes Received: 247
  Trophy Points: 160
  Inafanana na ipi?
   
 10. FirstLady1

  FirstLady1 JF-Expert Member

  #10
  Nov 18, 2009
  Joined: Jul 29, 2009
  Messages: 16,382
  Likes Received: 307
  Trophy Points: 180


  asante sana mleta mada tuwe tunakumbushana
   
 11. Msanii

  Msanii JF-Expert Member

  #11
  Nov 18, 2009
  Joined: Jul 4, 2007
  Messages: 6,418
  Likes Received: 347
  Trophy Points: 180
  No comment zaidi ya kudos
   
 12. Buchanan

  Buchanan JF Diamond Member

  #12
  Nov 18, 2009
  Joined: May 19, 2009
  Messages: 13,096
  Likes Received: 247
  Trophy Points: 160
  Mafisi-adi wa inji hii wanafit kwenye amri hizi au "wanaonewa sana" kama alivyolalamika mmoja wakati "anaachia ngazi?"
   
 13. Buchanan

  Buchanan JF Diamond Member

  #13
  Nov 18, 2009
  Joined: May 19, 2009
  Messages: 13,096
  Likes Received: 247
  Trophy Points: 160
  Hawa mafisi-adi dawa yao ni kuwasema mara kwa mara mpaka waone ubaya wa fedha haramu!
   
Loading...