Tujiandae kuchukua hatua

Josh Michael

JF-Expert Member
Jun 12, 2009
2,523
77
Edward Kinabo


NDUGU wananchi, nimetoa mchango wangu wa fikra kwa muda sasa, nikijaribu kuchochea wajibu na haki za raia katika kufanikisha ukombozi mpya wa taifa hili dhidi ya ujinga, umaskini, maradhi na ufisadi.
Huu unapaswa kuwa mwaka wa kutekeleza fikra za ukombozi. Tuna fursa ya kufanya hivyo na fursa hiyo ni Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani.
Hata hivyo, ni fursa inayohitaji maandalizi sahihi na ya kutosha ili kuweza kuitumia kikamilifu, vinginevyo haitakuwa fursa yetu. Itakuwa fursa ya wale waliolitafuna na kulikwamisha taifa letu kuweza kupata kipindi kingine cha kuendelea kufanya hivyo. Tujiandae kuchukua hatua.
Siku zote mtazamo, imani, msimamo na harakati zangu zimekuwa zikihamasisha mabadiliko ya uongozi na mfumo wa utawala wa nchi hii kama ufumbuzi wa msingi dhidi ya matatizo mengi yanayotukabili kama taifa.
Nimefanya hivyo si tu kupitia safu hii bali kupitia kila fursa niliyoipata, iwe kwenye uongozi wa asasi za kiraia, chama cha siasa, kwenye warsha, makongamano au kwenye mikusanyiko mbalimbali ya kijamii iliyo rasmi na isiyo rasmi.
Nimetoa mchango wangu wa kifikra nikiamini pasipo shaka yoyote kuwa ukombozi wa kifikra ndiyo msingi wa kufikia mabadiliko yote yanayohitajika katika taifa hili. Kupitia fikra binadamu huweza kupambanua vyanzo, vikwazo, udhaifu na fursa zilizopo katika kumaliza kero na matatizo yanayomkabili.
Katika moja ya maandiko yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Mama Ananilea Nkya, alipata kuandika hivi, ninamnukuu:
“Tulikotoka ni mbali na tunakokwenda ni mbali, hakuna mapambano magumu duniani kama mapambano ya kubadilisha fikra, desturi na mazoea (mila na desturi) ya binadamu. Watanzania tunaishi maisha ya mazoea katika dunia hii inayobadilika kwa kasi na inayohitaji mabadiliko makubwa ya kifikra ili kuweza kukabiliana na utandawazi wizi uliojaa rushwa na uchafu wa kila aina (ufisadi).
Hebu niambieni wenzangu ni wananchi wangapi siyo tu vijijini hata mijini (wasomi na wasiosoma) wanaojua thamani ya kura yao? Ni wananchi wangapi wanaojua kuwa kura yake ikichanganywa na kura za wenzake inaweza kuwa mwisho wa kuwa na mikataba inayosainiwa kwa siri kuuza rasilimali zetu kwa wawekezaji (wezi au matapeli wasiojali utu wa binadamu maana wanaweza kuwanywesha hata sumu ya kufua madini bila huruma?)
Ni wananchi wangapi wanaojua kuwa kura yake ina thamani ya mamilioni ya dola au shilingi na inaweza kujenga barabara ambayo ni kero kijijini au jimboni kwake?
Ni wananchi wangapi wanafahamu kuwa kura yake inaweza kujenga hospitali au zahanati nzuri na kuweka madaktari, dawa na vifaa vya kutosha ili watu wasife kwa malaria au kukosa pitosin (dawa yenye thamani ndogo kuzuia kuvuja damu mjamzito anapojifungua?
Ni wananchi wangapi wanaofahamu kuwa kura yake inaweza kuleta mabadiliko si tu yeye binafsi kuwa tajiri wa kudumu bali pia yeye na Watanzania wote?
Ni wangapi (mijini na vijijini) wanaopiga kura baada ya kufanya uchunguzi binafsi (bila ushabiki wa vyama) na kufahamu uwezo na nia ya mtu aliyempigia kura ya ndiyo maana ndiye atakayekuwa kinara wa kuwezesha mabadiliko hayo.
Kila mmoja wetu pale alipo awe ni mwanasiasa mwadilifu, mwanahabari mwadilifu, mwalimu mwadilifu, polisi mwadilifu, hakimu mwadilifu, mfanyakazi wa tume mwadilifu, mwanaharakati, akichochea mapinduzi ya fikra miongoni mwa watu na uwajibikaji wa viongozi, maendeleo yatapatikana. Tunahitaji wanasiasa wanaojitoa mhanga na zaidi tunahitaji wapiga kura wanaojitoa mhanga kupambana na vishawishi vya rushwa.” Mwisho wa kunukuu.
Bila shaka ujumbe wa mama huyo ni mzito, umepangiliwa vizuri na umesadifu vema dhana na umuhimu wa falsafa ya ukombozi wa kifikra au kama alivyoiita yeye ‘mapinduzi ya kifikra’.
Hata hivyo, lazima jamii yetu ifikie hatua ya kutekeleza fikra zake maana fikra zisizotekelezwa ni sawa na njozi za mchana. Tumelalamika na kufikiria sana, tumehoji na kujiuliza sana ni lini umaskini, ujinga, maradhi na ufisadi ndani ya nchi hii vitakwisha au angalau kupungua. Huu ni mwaka wa kila mmoja wetu kuwa wakala wa kupigania utekelezwaji wa fikra ili kufikia mabadiliko anayotaka kuyaona.
Binafsi nimeamua kuzipigania fikra zangu na za wanyonge wenzangu. Nimeamua kuchukua hatua katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari likiwemo gazeti hili, nimetangaza azima yangu ya kuwania ubunge mwaka huu. Naomba niitumie fursa hii kusisitiza japo kwa muhtasari juu ya azima yangu hiyo, kabla sijaainisha hatua kadhaa zinazopaswa kuchukuliwa na kila mmoja wetu tunapojiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Ni kweli, nimeamua kugombea ubunge katika Jimbo la Rombo mkoani Kilimanjaro kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Nawania ubunge Rombo ili nipate mamlaka ya kutosha ya kuweza kuwawakilisha na kuwaongoza wakazi wa jimbo ninalolifahamu vema kwa kuwa mwenyeji wake lakini zaidi kwa kusukumwa na matokeo ya utafiti wangu uliozingatia vigezo vya kitaalamu nilioufanya mwaka jana.
Kupitia utafiti huo, nina majibu na ufumbuzi wa uhakika juu ya matatizo na kero za msingi zinazowakabili wakazi wa Rombo, hususan tatizo kuu la umaskini wa kipato na uwajibikaji usioridhisha wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rombo inahitaji mbunge na diwani mkweli, msikivu, mnyenyekevu na anayewajibika kwa wakati. Nitafafanua kila kitu kwa kina kupitia ilani ya uchaguzi wakati muafaka ukifika.
Nawania ubunge Rombo ili nipate fursa ya kuiongezea wingi na nguvu kambi ya wabunge makini wa upinzani waliojitahidi kuwatetea na kuwapigania Watanzania kwa bidii na uadilifu mkubwa.
Hawa mara zote wamekuwa wakiangushwa na uchache wao, hivyo kutoa mwanya kwa wabunge wengi wa CCM kupitisha sheria na maamuzi mazito yanayokwamisha na kuchelewesha harakati za raia mmojamoja kujiendeleza.
Nawania ubunge Rombo nikiwa kijana mwenye umri wa miaka 29, nataka nipate fursa ya kuongeza idadi ya uwakilishi wa vijana bungeni.
Wakati vijana na watoto ni takriban asilimia 60 ya watu wote wa nchi hii, idadi ya wabunge vijana (miaka 21- 35) ni chini ya asilimia mbili.
Taifa makini huwekeza kwa vijana wake, tunahitaji mabalozi wengi zaidi wa vijana bungeni. Sauti ya vijana ikiendelea kuzimwa, taifa litazidi kuyumba. Sishawishi, bali ni ukweli unaozingatia historia na matokeo ya tafiti.
Huu ni wakati wa Rombo na majimbo mengine kuandika historia ya kuingiza vijana bungeni. Hata hivyo nitahadharishe kuwa kigezo kisiwe ujana tu, bali pia utashi na utayari wa kijana huyo.
Nawania ubunge Rombo nikiwa nimeitathmini nafsi yangu na kuupima uwezo na uzoefu wangu katika siasa na uongozi.
Niko tayari kujitoa mhanga kuwapigania wakazi wa Rombo na Watanzania kwa ujumla kwa bidii, umakini na uadilifu mkubwa.
Utashi na uzoefu nilionao vinanitosha sana kufanya maajabu niliyoyadhamiria, vinanitosha kuwaunganisha wananchi wa Rombo kuleta mabadiliko wanayoyatamani.
Nina mikakati na uwezo wa kuongoza vuguvugu la kisiasa la kuikomboa Rombo, ni mikakati ya kisayansi inayoweza kuhimili vishindo vya siasa za ushindani. Pamoja tunaweza, pamoja tutashinda.
Nawania ubunge Rombo nikiwa nimesukumwa pia na wito wa wakazi wa kata mbalimbali za jimbo hilo waliohudhuria mikutano yangu mbalimbali ya kuwanadi wagombea wa vijiji na vitongoji walioshiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika nchi nzima Oktoba 25 mwaka jana. Hawa walionekana kuguswa na hotuba zangu.
Niliporuhusu maswali kwangu na kwa wagombea niliowanadi, baadhi yao walipopanda jukwaani walivuka mpaka, badala ya kuuliza swali juu ya uchaguzi ule wakahoji kwanini nisigombee ubunge mwaka huu? Kabla ya kujibu, umati wa mkutano nao ukasisitiza “gombea, gombea, gombea.”
Hali hiyo ilinikuta zaidi katika vijiji vya Tarafa ya Mengwe na ikajitokeza tena katika vijiji vingine.
Wale waliobahatika kuhudhuria mikutano hiyo watakumbuka kuwa ilipojitokeza hali hiyo nilijibu hivi: “Nawashukuru kwa kuona kuwa nitawafaa nikiwa mbunge wenu, msihofu muda bado haujafika. Tupo kwenye uchaguzi wa vijiji na vitongoji, mkinipa wenyeviti wengi wa vijiji na vitongoji mtakuwa mmenirahisishia kazi yangu ya kuwatumikia pindi mtakaponipa ubunge. Uchaguzi huu ndio muhimu kwanza.”
Katika kata moja nilipomaliza mikutano yangu, kikundi kidogo cha wazee, baadhi wana-CHADEMA na wasio wana-CHADEMA, kilisisitiza haja hiyo ya kugombea ubunge mwaka huu. Licha ya kujiamini kwangu, naomba nikiri kuwa wito huo ulichochea sana kunifikisha kwenye uamuzi kamili wa kugombea ubunge katika jimbo hilo.
Nawania ubunge Rombo kupitia CHADEMA, nimechagua kuwapigania wana Rombo na Watanzania wote kupitia chama hiki, kwani ndicho ninachokiamini kuwa hakiwezi kukwamisha wala kusaliti harakati za vijana makini walioamua kujitoa mhanga kuutafuta ukombozi mpya wa taifa lao.
Nimekuwa katika chama hiki kwa miaka sita sasa, nimelelewa na kujengwa kisiasa na chama hiki. Nimeiva kuitumikia jamii kupitia mamlaka ya kisiasa. Pamoja tunaweza, pamoja tutashinda.
Nimetoa mchango wangu wa mawazo na kiutendaji katika ujenzi wa chama hiki na mara zote umethaminiwa.
Naamini katika sera, itikadi, dira, uongozi na mikakati ya CHADEMA. Ni chama kinachotoa fursa nzuri kwa kila mwenye mawazo ya kukiimarisha na kukitumia katika kupigania masilahi ya taifa.
Huu ni wakati wangu wa kutimiza wajibu mzito zaidi kupitia CHADEMA iliyokomaa, si kwa masilahi ya wana-Rombo tu bali kwa masilahi ya Watanzania wote wanaohitaji upinzani imara bungeni ili matakwa yao yasimamiwe na serikali iwaheshimu.
Pamoja tunaweza, pamoja tutashinda, nawaomba wana-Rombo waendelee kuniunga mkono. Nawaomba Watanzania wote bila kujali itikadi zenu mniunge mkono. Wiki ijayo nitachambua wajibu wa raia wote kuelekea Uchaguzi Mkuu. Tujiandae kuchukua hatua.


h.sep3.gif


juu
blank.gif
blank.gif
 
Joseph selasini amekaa kimya sana,kinabo pia CV yake inahitajika hapa
Kinabo ni mtu makini sana na amekuwa ana mchango mkubwa sana katika sekta ya habari Tanzania na pia walikuwa karibu sana na John Mnyka kama Meneja wake wa kampeni Ubungo mwaka 2005 na Kazi buti Kinabo
 
Saa nyingine watu wenye taaluma ndio wanaharibu sana mambo mengi katika taifa letu


Mkuu,

Heshima mble..so unataka kusema nini hapa?

Sidhani kama tunaweza ku-ignore role ya taaluma katika kutunga sheria,kutunga sera na kuichambua bajeti yetu kupitia mwakilishi wetu bungeni.

Kwa hiyo hatuwezi hata kidogo kupuuza taaluma kwa kuwa wenye taaluma waliharibu mambo.It's like ukipeleke mtoto hospitali halafu akafa kwa sababu ya daktari ku-overdose basi tukatae tabibu zote za kisayansi turudi kwa watabiri na mitishamba?

I'm not saying kwamba umesema hivyo but this is what your post likely to suggest!

Still taaluma ina umuhimu,tutakua bunge la aina yake duniani tukijazana tu vihiyo.Lazima mtu awe na taaluma na uwezo wa kufanya kazi.

so nasizitiza Curriculum vitae(CV) yake ya kitaaluma ikoje?
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom