Tujadili upatikanaji wa Mwanasheria Mkuu (Attorney General) wa Serikali ya Tanzania

Apr 24, 2011
29
542
Tujadili upatikanaji wa Mwanasheria Mkuu (Attorney General) wa serikali ya Tanzania

Ofisi ya Mwanashera Mkuu wa Serikali Tanzania inatajwa kuwa ni taasisi inayojitegemea ndani ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mujibu wa Kanuni Na. B.2 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma Toleo la mwaka 2009.

Ofisi ya mwanasheria Mkuu wa serikali ya Tanzania imeanzishwa chini ya Ibara ya 59 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yamwaka 1977 pamoja na Sheria yaUtekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sheria Na.4 ya Mwaka 2005.

Majukumu yote ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania yanasimamiwa na Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura ya 268 na Muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, zikiwepo na sheria nyingine kadhaa.

Baadhi ya sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Mwenendo wa Mashauri dhidi ya Serikali (The Government Prosecuting Act) (Cap 5); Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Sura 20); Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai (Sura 33); Sheria ya Kanuni za Adhabu (Sura 16);

Sheria ya Utekelezaji Haki za Msingi na Wajibu (The Basic Rights & Duties Enforcement Act)(Cap 3); Sheria ya Tafsiri ya Sheria (The Interpretation of Laws Act)(Cap 1); Sheria ya Mahusiano ya Kusaidiana katika Masuala ya Jinai (The Mutual Assistance in Criminal Matters) (Cap 254);

Sheria ya Urejeshwaji wa Watuhumiwa katika Nchi waliyofanya Kosa (The Extradition Act) (Cap 368); Sheria ya Ubia Baina ya Umma na Watu Binafsi (The Public Private Parthership Act) (Cap 103). Hizo ni sheria zinasimamia na kuongoza majukumu ya Ofisi ya Mwanashera Mkuu wa Serikali

Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali ni ofisi muhimu kwa sababu imebeba majukumu makubwa kwa Jamhuri (Republic). Mwanasheria Mkuu wa Tanzania anateuliwa na Rais kwa matakwa na mtazamo wa Rais aliyepo madarakani. Huu ustaarabu ni tofauti na nchi nyingi Duniani. Tuangazie Colombia

Mwanasheria Mkuu wa serikali ya Colombia (Colombia Attorney General), anachaguliwa na pia kuthibitishwa na majaji wa mahakama ya juu ya Colombia, kutoka katika majina ya wanasheria wazoefu watatu ambao wanapendekezwa na Rais.

Mwanasheria mkuu wa serikali ya Colombia baada ya kuthibitishwa na chombo maalum ataitumikia nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka 4. Kuthibitisha kura za mwisho, mahakama ya juu (supreme court), inapaswa kutimiza kura 16 katika ‘quorum’ yenye uhitaji wa kura 23 (2/3 ya kura zote)

Nifafanue kidogo kuhusu hii Supreme Court of Justice of Colombia (mahakama ya juu ya haki ya Colombia) inayotakiwa kumpigia kura mwanasheria mkuu wa serikali ya Colombia inaundwa majaji 23, ambao wanateuliwa na ‘Superior Council of Judicature’ kwa kipindi cha miaka 8.

‘Superior Council of Judicature’ ni baraza la mhimili wa mahakama (Judiciary of Colombia) yenye jukumu la kuanda taarifa ya mwaka ya masuala ya utendaji kazi kushughulika na haki wa mhimili wa mahakama na kuwasilisha bunge la Colombia (Congress of the Republic of Colombia)

Baraza (Superior Council of Judicature) pia linaanda mpango wa maendeleo kwa ajili ya mhimili wa mahakama (Development plan for the judicial branch) na kuwasilisha kwa Rais wa Colombia ili kujumuishwa katika mpango wa maendeleo wa taifa (Colombian National Plan of Development)

Baraza hilo la mahakama ya juu, linatengeneza taratibu na kanuni kwa ajili ya idara zote za utoaji haki. Wajumbe wa baraza wanachagua Rais wa baraza hilo. Majukumu ya baraza hilo yametajwa katika ibara ya 79, sheria Na. 270 ya mwaka 1996 katika katiba ya Colombia ya mwaka 1991.

Rais wa baraza la mahakama ya juu ya Colombia anaongoza baraza, na ana wajibu wa kisheria wa taasisi kutoa uwakilishi katika taasisi nyingine katika mhimili wa mahakama na pia kwa watu wa kawaida, raia. Analo jukumu la kuchagua makamu wa Rais wa baraza hilo pia.

Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali ya Colombia ni sehemu ya mhimili wa mahakama na ofisi hiyo ina haki ya kiutawala na bajeti yake. Mwanasheria mkuu na ofisi yake wanayo mamlaka katika mipaka yote inayounda jamhuri ya Colombia.

Ofisi ya mwanasheria mkuu wa Colombia inahusisha; Deputy Assistant Attorney General, the National Director of Prosecutor’s Office, the Sectional Directors of Prosecutor’s Office, the Prosecutors attached to Special Prosecutors’ Units and Special Delegate Prosecutors.

Mwanasheria Mkuu wa serikali msaidizi (Deputy Assistant Attorney General), anateuliwa na Mwanasheria mkuu wa serikali ya Colombia, kumwakilisha katika shughuli zote ambazo atapangiwa za kijamii na kisheria.

Mwanasheria Mkuu wa serikali, mwanasheria mkuu msaidizi, na ofisi yote ya mwendesha mashtaka, wanatekeleza majukumu yao mbalimbali ya mamlaka ya kijinai, maamuzi na madaraka yote ndani ya nchi ya Colombia kwa kufuata taratibu zote zilizowekwa na kutajwa na sheria.

Mwanasheria mkuu wa Tanzania, anatajwa ibara ya 59 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano Sheria ya 1984 Na.15 ibara 9 Sheria ya 1992 Na.4 ibara 16 ambaye anateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mtu hatastahili kuteuliwa kushika madaraka ya Mwanasheria Mkuu isipokuwa tu kama kwa mujibu wa Katiba hii ana sifa maalum, kama ilivyofafanuliwa katika ibara ya 109(8) zinazomwezesha kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano au Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar,

Ibara ya 109(8) inazungumza kuhusu madhumuni ya ufafanuzi wa ibara ndogo ya (7), ya (9) na ya (11) ya ibara hii, “sifa maalum” maana yake ni sifa zilizotajwa katika Sheria ya Mawakili (au Sheria nyingine yoyote inayobadilisha hiyo sheria ya Mawakili au inayotumika badala yake)

Ambazo ni lazima mtu awe nazo mojawapo ya sifa hizo ili aweze kukubaliwa kuandikishwa kama Wakili Tanzania Bara. Hivyo na mwanasheria Mkuu wa serikali, anatakiwa kukidhi matakwa ya ibara hiyo na amekuwa na mojawapo ya hizo sifa maalum kwa muda usiopungua miaka mitano.

Mwanasheria Mkuu atakuwa ndiye mshauri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo ya sheria na, kwa ajili hiyo, atawajibika kutoa ushauri kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuhusu mambo yote ya kisheria, na kutekeleza shughuli nyinginezo zozote zenye asili ya au kuhusiana

Na sheria zitakazopelekwa kwake au atakazoagizwa na Rais kuzitekeleza, na pia kutekeleza kazi au shughuli nyinginezo zilizokabidhiwa kwake na Katiba hiyo au na sheria yoyote. Na Katika kutekeleza kazi na shughuli zake kwa mujibu wa ibara hiyo mwanasheria mkuu wa serikali

Atakuwa na haki ya kuhudhuria na kusikilizwa katika Mahakama zote katika Jamhuri ya Muungano. Pia, Mwanasheria Mkuu wa Tanzania atakuwa Mbunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na wadhifa wake, na atashika madaraka yake mpaka pale ambapo;

(a) uteuzi wake utakapofutwa na Rais au (b) mara tu kabla ya Rais mteule kushika madaraka ya Rais, na atalipwa mshahara, posho na malipo mengine kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge. Hivyo uteuzi wake unatoka moja kwa moja kwa Rais bila utaratibu mwingine wa uhakiki kufuatwa

Mwanasheria mkuu wa Tanzania katika katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania anatajwa ibara ya 59 ambayo ina ibara ndogo (5) ambazo hazijawekewa misingi ya kutekeleza majukumu yake kwa haki na uhuru bila kuingiliwa na mhimili wa serikali. Hii ni ofisi nyeti. Lazima izingatiwe.

Majukumu ya msingi ya mwanasheria Mkuu wa serikali ya Tanzania yametajwa na kuainishwa kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 48 la mwaka 2018. Hapa, nitajaribu kutaja baadhi ya hayo majukumu muhimu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania.

Kuishauri Serikali katika masuala ya Mikataba na uandishi wa sheria; Kuratibu na kutoa ushauri wa kisheria; Kuendesha majadiliano kwa niaba ya Serikali katika Mikataba yote; Kupitia mikataba ya kibiashara na ya kimataifa kwa niaba ya Serikali na kuishauri Serikali ipasavyo

Kusimamia wajibu wa kimikataba wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Kuandaa miswada ya sheria ya kupitishwa Bungeni; Kuandaa hati zote za kisheria na maazimio kwa ajili ya kuidhinishwa na Bunge; Kushauri Wizara, Idara za Serikali na taasisi nyingine za Serikali;

Kushiriki katika kudhibiti nidhamu ya Mawakili wa Kujigetemea kupitia Kamati ya Maadili ya Mawakili ( Advocates Committee); Kuendesha na kusimamia mafunzo kwa njia ya vitendo kwa wanafunzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa vitendo;

Kuwasimamia Maafisa Sheria na Mawakili wa Serikali wote walioko katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali katika kutekeleza majukumu yao ya kisheria; Kushauri kuhusu Sera za Nchi kuhusiana na usimamizi wa utawala wa Sheria Tanzania pamoja na kusimamia taaluma ya Sheria;

Kutoa ushauri kuhusiana na Nyaraka za Baraza la Mawaziri (cabinet papers), memoranda na ufuatiliaji wa ahadi za utekelezaji wa maamuzi yanayohitaji kutungwa kwa sheria ama kuundwa chombo chochote cha kisheria; hapa inamaanisha ndiye mshauri mkuu wa Baraza la mawaziri.

Pia mwanasheria Mkuu wa serikali ya Tanzania ana jukumu la kutekeleza jukumu lolote linaloweza kuwa muhimu kwa utekelezaji ulio na ufanisi wa majukumu na utekelezaji wa mamlaka ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Unaweza kuona ofisi hii ilivyo muhimu sana kwa nchi yetu.

Tunalazimika kulitazama, mwanasheria Mkuu wa serikali, anateuliwa na Rais na anawajibika kwake na anaweza kutenguliwa naye. Haitoi nafasi ya ofisi hii kutenda majukumu yake kwa haki na uhuru. Muhimu kuipata KATIBA MPYA, kuweka misingi ya ofisi ya mwanasheria Mkuu wa serikali.

MMM, Martin Maranja Masese
 
Mkuu kwa sie tunafwata common law
Much less mambo ya ithibati ya kusibitishwa haina mashiko
Ni swala la unamjua nani na si wajua nini mkuu
Colombia walisha tengeneza mfumo na si blabla
 
3 Reactions
Reply
Back
Top Bottom