Tuijadili dhana ya 'Maslahi ya Taifa' tukitumia mifano ya Tanzania kama rejeo

Keynez

JF-Expert Member
Feb 12, 2007
2,397
3,884
Kwa miaka mingi taifa kubwa la Marekani, linaposimama kutoa misimamo yake juu ya mijadala mbalimbali hasa ya nje ya nchi yao, wamekuwa wanaongelea jinsi mijadala hiyo inavyohusu 'maslahi ya taifa' au, 'national interest' ya taifa lao. Hii ni dhana pana ambayo wengi huwa wanashindwa kuielewa.

Wengi huwa wanawatuhumu Wamarekani kwa kuingilia siasa, uchumi na mambo ya ndani ya nchi zingine lakini tunakuwa tunasahau kuwa katika tafsiri yao, Wamarekani wamejenga dhana yao ya 'maslahi ya taifa' kwa upana zaidi kutokana na sera zao za mambo ya nje zilivyo lakini pia kwa kuwa wana uwekezaji mkubwa huko nje ukiachilia mbali ushindani wa kiushawishi kutoka mataifa mengine makubwa. Hii dhana ya maslahi ya taifa ndiyo huwa kipimo cha kuamua ni kiasi gani Marekani itumie nguvu za ziada dhidi ya nchi fulani au mgogoro fulani. Huu uingiliaji au intervention una ngazi nyingi na zote zinategemea ni kwa kiasi gani suala husika limegusa au kutishia maslahi ya taifa lao.

Bila kuwachosha zaidi, ingawa maelezo haya hapo juu yana umuhimu mkubwa katika mjadala huu, kama mpaka hapo tunakwenda pamoja, embu tuiangalie dhana hii kwa minajili ya nchi yetu ya Tanzania.

Tanzania hatuna uwekezaji wowote kibiashara wa maana nje ya nchi. Hata lile wazo la 'Sovereign Wealth Fund' la kipindi cha Kikwete lilikufa kabla hata halijaanza. Kwa maana hiyo, maslahi yetu ya taifa mpaka sasa yamejikita zaidi katika masuala ya usalama ya mipaka inayoizunguka nchi yetu. Nadhani tunaweza sana kujua nini kinaendelea kwenye masuala ya kiusalama kwenye nchi zinazotuzunguka. Ila inapokuja kwenye masuala ya ndani ya nchi, tuna mapungufu makubwa au upofu unaosababishwa na maslahi ya wachache inayotufanya tushindwe kuona vizuri.

Embu tuangalie jinsi tunavyofanya chaguzi zetu za kisiasa ambazo kimsingi bado hatujayahusisha na maslahi ya taifa, isipokuwa pale tunapotaka kuwapaka wapinzani wetu matope kwa tuhuma zisizo na uthibitisho za kutumiwa na watu au mataifa ya nje. Tukienda mbali zaidi, labda tutabinya uhuru wa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii hasa pale mijadala inapokuwa mikali inayogusa hisia za jamii yetu kwa upana. Kwa lugha rahisi, dhana yetu ya 'maslahi ya taifa' iko kulinda maslahi ya kikundi fulani cha kisiasa na siyo maslahi mapana ya taifa.

Maslahi ya taifa hayatakiwi kuangalia sura ya mtu, chama chake cha siasa wala kundi analoliwakilisha. Kuna mifano mingi duniani kuthibitisha hilo. Bado hatujaona au kukubali kuwa kufanya chaguzi safi na za haki kuwa ni kwa maslahi ya taifa na hii haina uhusiano wowote na vigezo au vitisho vya kutoka taasisi au mabalozi wa nje bali ni kwa kuangalia tu faida za kupata viongozi kwa njia iliyo halali na ya wazi.

Kuna mambo mengi ambayo yamekuwa yanatokea na kufanyika Tanzania, yakifanywa na watendaji wa Serikali au Taasisi za Umma au wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo kimsingi ni kinyume cha Maslahi ya Taifa hili kama kweli tunaielewa dhana hii na umuhimu wake. Kwa nini nasema hivi?

Ukiangalia kwa makini, haya matendo na maamuzi yanaweza kuwa yanatuletea manufaa ya muda mfupi, na hapa neno 'manufaa' linaweza lisiwe sahihi sana. Manufaa hayo yanaweza kuwa kupunguza au kuzima pressure za kisiasa ambazo kweli zingeweza kuleta mtafaruku, au pale tunapotaka kumlinda kiongozi wa nchi pale ambapo ananyooshewa kidole kwa tuhuma zinazoweza kuitikisa nchi.

Inaweza pia kuwa yanafanywa ili tu kuwathibitishia mataifa ya nje kuwa Tanzania ni nchi huru, na kwamba hata tukimwaga damu au kufanya maamuzi yoyote hata yakiwa ya hivyo, watuache tu kwa kuwa sisi ni taifa huru. Lakini swali la kujiuliza, in the long run, maamuzi haya yana hasara kiasi gani kwa maslahi ya nchi? Je uwiano wa faida za muda mfupi na hasara za muda mrefu uko vipi?

Tuna miaka karibia 30 toka mfumo wa vyama vingi uanzishwe nchini Tanzania. Tujiulize, tumewezaje kuujumlisha mfumo huu katika dhana nzima ya maslahi ya taifa letu? Je, kwa kuurasimisha rasmi katika sheria zetu, tumekubali kama taifa kuwa mfumo huu ni nguzo muhimu katika maslahi yetu kama taifa? Kama ni ndiyo, wale wanaoonekana kuukandamiza kwa njia yoyote, hatuhitaji kuwahesabu kama maadui wa taifa hili?

Ukimuuliza kiongozi yoyote wa Serikali, dira ya taifa letu leo ni nini, sijui kama ataweza kukupa jibu linaloendana na hali halisi iliyopo nchini. Si katika uchumi, si katika siasa, kote inaonekana tumepoteza muelekeo na hatuna dira inayoeleweka. Kwa maana hiyo, hatuwezi kuwa na msimamo thabiti wa maslahi ya taifa bila kuwa na dira ya taifa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inayoeleweka na kukubaliwa na jamii nzima ambayo hakuna kiongozi, kikundi, taasisi au chombo chochote kitakachokuwa na ushawishi, ujasiri au uwezo wa kisheria wa kuipindisha.

Kuna wakati taifa hili lilikuwa na dira ya taifa. Ukienda huko Nachingwea, au Lushoto au Ujiji, unaikuta hiyo dira inatekelezwa. Ukikutana na mwanadiplomasia ya Kitanzania huko Brussels au New York unakuta kweli anachokwambia ndicho ambacho kama nchi tunakisimamia bila aibu wala kigugumizi. Leo hii tumekuwa taifa la ndimi mbili. Si katika vitabu vyetu vya sheria, si kwa kauli za viongozi wetu. Tunasema hiki lakini tunafanya kile. Hili si jambo la kujivunia hata kidogo kama taifa.

Turudi tujenge taifa ambalo watu wetu wataweza kusimama popote pale duniani na kuheshimika na kuaminiwa. Tusikubali kujenga taifa la watu wa hovyo hovyo. Mambo tunayofanya gizani na wakati mwingine waziwazi yanatuathiri mmoja mmoja na kama taifa zaidi ya tunavyodhani na itachukua muda mrefu sana kuirudisha heshima tunayoipoteza. Haya ndiyo maslahi ya taifa tunayotakiwa kuyalinda na kuyapigania.
 
Taifa ni watu, hivyo maslahi ya taifa maana yake ni maslahi ya watu "wananchi"

Lakini nchi yetu kama zilivyo nchi nyingne za kishenzi huwa zinaogopa gharama za kuwekeza kwa watu, hivyo hujitahid kuwahonga watu vitu "maendeleo ya vitu" ili wasahau maslahi yao ambayo ni "maslahi ya taifa"

Thanks
 
Waasisi wa Taifa walianza vizuri na kauli ya kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa. Walijenga vyuo vya kilimo, ukizingatia na ardhi tuliyonayo tulipaswa kuwa wazalishaji wakubwa wa vyakula na matunda Afrika.

Ufugaji wa kuku wa biashara ungewezekana, tungeweza kuwa na uzalishaji mkubwa kiasi ambacho kuku kuwa kitweo cha kila siku hata wa hali za chini wangeweza. Hii ingetupunguzia pia matatizo ya utapia mlo kwa watoto wa chini ya miaka motano.

Tulichokosa ni uongozi bora tulicho nacho ni bora uingozi.
 
Maslahi ya taifa ni dhana inayotumiwa vibaya na watu walifanikiwa kuwa na mamlaka ya kidola.

Pamoja na kuwa mfumo wa vyama vingi uko rasmi kikatiba na kisheria, leo baada ya kile kilichoitwa uchaguzi mkuu, viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani waliojaribu kusimamia maslahi ya vyama vyao wako magerezani kwa tuhuma za uhujumu uchumi, kuendesha magenge ya uhalifu na wengine kuumizwa vibaya na hata kuuwawa.

Maslahi ya taifa yamekuwa ni maslahi ya CCM na viongozi wanaonufaika moja kwa moja na mfumo uliopo.

Maslahi ya taifa kwa utawala tulionao ni kichaka tu cha kuhalalisha uovu, uonevu, utesaji wa wakosoaji wao.

Kama yangelikuwa ni maslahi ya taifa ya ukweli kusingekuwa na hofu CCM na viongozi wake kufanya uchaguzi huru na haki kukidhi matakwa ya kidemokrasia.
 
Back
Top Bottom