Tuhakikishe tatizo la sukari linaisha

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
UHABA wa sukari umekuwepo nchini kwa muda sasa. Hali hiyo imesababisha bidhaa hiyo kuuzwa kwa bei ya juu ya hadi 4,000 katika baadhi ya maeneo, badala ya bei elekezi ya serikali ya Sh 1,800.

Tatizo hilo limesababishwa na sababu kadhaa, ambapo ya kwanza ni viwanda kusimamisha uzalishaji kwa miezi mitatu ili kuruhusu ukarabati na pili ni mahitaji makubwa ya bidhaa hiyo, ambayo ni zaidi ya tani 420,000, lakini kiwango kinachozalishwa ni kidogo.

Tunampongeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kauli yake aliyotoa mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa tatizo hilo la sukari litamalizika hivi karibuni. Alisema hayo alipozungumza na mashehe na viongozi wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam, alipowaalika katika futari aliyoiandaa nyumbani kwake.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, viwanda vya sukari tayari vimefunguliwa na vimeanza uzalishaji. Kwa mfano, tani 300 zitatoka katika Kiwanda cha Sukari cha Kagera na zitasambazwa mkoani Kigoma katika wilaya za Kakonko, Kibondo, Kasulu, Uvinza na Kigoma ili kutosheleza maeneo hayo.

Nao uongozi wa kiwanda cha TPC mkoani Kilimanjaro, umetangaza kuanza uzalishaji wa sukari tani 450. Wananchi wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Tanga na Singida wataanza kupata sukari ya uhakika kutoka TPC kwa bei elekezi ya serikali kuanzia kesho.

Uzalishaji katika viwanda vya Kilombero na Mtibwa mkoani Morogoro, ulianza mwishoni mwa mwezi uliopita. Tuna imani uzalishaji katika viwanda vyote hivyo vikubwa vinne, utakuwa wa kasi kwa lengo la kukabiliana na upungufu wa sukari sokoni. Tunahimiza wafanyabiashara wakubwa na wa reja reja nchini, watakaopokea sukari hiyo, kuiuza kwa wananchi kwa bei ambayo haitazidi Sh 1,800.

Tunaomba serikali iwachukulie hatua kali mawakala wa sukari na wafanyabiashara wa rejareja, watakaoficha bidhaa hiyo baada ya viwanda hivyo kuanza uzalishaji.

Maofisa biashara katika halmashauri zote nchini, wafuatilie katika maduka ili kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana na hakuna mfanyabiashara atakayeificha. Mawakala na wafanyabiashara, watakaojiingiza kwenye mchezo mchafu wa kuhodhi bidhaa hiyo, waburutwe mahakamani.

Wananchi wanatakiwa kuwa na subira kwa kuwa katika siku chache zijazo, tatizo hilo litakuwa historia. Kila mmoja ajitahidi kuhakikisha tatizo hilo linakwisha. Hali kadhalika, katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, tunaomba wafanyabiashara wakubwa na wa reja reja, waache kupandisha bei za vyakula.

Wafanyabiashara wanatakiwa kumuogopa Mwenyezi Mungu kwa sababu wakipandisha bei, watawapa wakati mgumu wafungaji. Kufunga Ramadhani si jambo la anasa, na si matashi binafsi, bali ni jambo la kiimani, hivyo wasipandishe bei ya bidhaa kwa lengo la kuwaadhibu Waislamu kwa sababu tu wamefunga.
 
ndg yangu muogope mungu kwa kupindisha ukweli wa sababu hasa ya kilicho sababisha hali hii.mbona unaungulia ndani kiasi hicho?kuwa huru bana!!
 
Back
Top Bottom