SoC01 Tufungue Milango ya ajira za nje kwa wahitimu wetu

Stories of Change - 2021 Competition

From Chugga

New Member
Aug 22, 2021
4
9
Wakati tunahamasisha wahitimu wetu kuingia zaidi kwenye ujasiriamali kama njia ya kukabiliana na ukosefu wa ajira, ninaamini bado kuna nafasi katika soko la ajira la nje hatujaitumia vema. Kwa sababu kama soko la ajira la ndani limekuwa gumu kuna uwezekano wa kutafuta ajira nchi zingine. Hapa mtu anawezakuguna, kuwa tunashindwa ndani nje tutawezaje.

Lakini jirani zetu wanatumia njia hii, wanajitahidi kutafuta nafasi za ajira nje na wanapozipata huitana na wenzao. Huku kwetu pia kulikuwa na idadi kubwa ya waalimu shule za English Medium kutoka Kenya na Uganda.

Kwa bahati mbaya sisi hatuitumii sana njia hii nna tunakiri kuwa watanzania professionals wanye ajira Kenya ni wachache kuliko idadi yao huku kwetu. Hii ingesaidia kupunguza makali ya ukosefu wa ajira kwa wahitimu wetu ambao wengi wapo mitaani na ndio tunwashauri waingie kwenye ujasiriamali.

Kwa asilimia zote ninakubaliana na ujasiriamali, ni jambo jema sana, tena linamuweka mtu huru na kumpa wigo mpana zaidi wa kujiendeleza.....lakini bado ajira ni nafasi nzuri zaidi ya mtu kujikuza professionally kwa sekta aliyosomea.

Kwa sababu kwenye ajira kunakuwa na nafasi za kupata ujuzi zaidi kupitia nafasi za mafunzo zinazotolewa na makampuni kwa watumishi wao. Huko mtu anaweza kujifunza mapya yaliyo katika sekta husika kwa wakati huo. Mfano ni mifumo mbalimbali ya usimamizi wa hesabu na TEHAMA, ambazo huboreshwa mara kwa mara.

Ajira pia hutoa firsa ya kukutana na professionals wengine ambao ni muhimu sana kwenye kubadilishana ujuzi na taarifa. Binafsi nikiri kuwa tangu nimeajiriwa nimekutana na watu wengi wa ndani na nje ya nchi na nimeshatembelea nchi kadhaa ambazo huenda nisingeweza kufika kama si ajira yangu.

Changamoto za ndani ya ajira zinahamasisha kusoma zaidi, mtu akiwa na Bachelor Degree anajitahidi afanye Masters na kuendelea ili kuongeza thamani ya nafasi yake. Hii ni njia ya kuongeza wataalamu nchini, siku hizi kuna usemi wa Bachelor haitoshi kwa sababu kumekuwa na idadi kubwa sana ya vijana wanaomaliza kwenye ngazi hiyo.

Sasa, kwa nini vijana wetu hawajitoi kutafuta ajira nje ya nchi? Ni swali wengi tunajiuliza lakini hatuna jibu la koja kwa moja.

Kwanza kuangalia faida za ajira za nje ya nchi ni kuwa mtu anapata fursa ya kuendelea zaidi kitaaluma na kifikra. Hata akirudi nchini anakuwa na ujuzi na fikra tofauti, ambazo zinaweza kufaidisha wengine. Kadhalika hii ni njia ya kuitangaza nchi, na kama wanaopata ajira hizo wakiwa vizuri kwenye vitengo vyao wanaweza kufungua milango zaidi kwa wengine.

Tunakubaliana hii ni njia nzuri ya ustawi wa kiuchumi kwa sababu kule wanalipwa kuzingatia viwango vya kimataifa ambavyo ni vikubwa kuliko vya ndani. Inawezekana baada ya muda mtu akawa na mtaji wa kuwekeza na zaidi atakuwa na ujuzi wa kiwango kizuri na fikra pana.

Tukirudi kwenye swali kwa nini idadi ya vijana wetu wanaopata ajira nje si kubwa, naomba niseme kwa nini naona jambo hili ni muhimu; ikiwa huko nje hatujulikani vizuri uwezo wetu katika kazi inakuwa vigumu kwa wawekezaji wanaokuja nchini kutuamini kirahisi kutupatia nafasi kubwa na muhimu. Utaona wawekezaji wengi kutoka nje wanaleta wataalamu kutoka nje pia kushika nafasi za juu hata tukalazimika kuweka sheria zakuwabana juu ya idadi ya wataalamu wanaoweza kuwaleta ili waangalie pia wataalamu wa ndani. Kutkujulikana katika ajira kimataifa kunachangia hili.

Hii ni ishara kuwa nafasi yetu katika soko la nje la ajira ndogo na sababu zinaweza kuwa nyingi ila kati ya hizo inawezekana hatuna kiwango bora au hatujui kujiuza.

Ikiwa sabau ni hatujui kujiuza; kuna haja ya kutengeneza mpango wa kuwauza vijana wetu nje kama tunavyofanya kwenye soko la utalii. Wizara za ajira na uwekezaji wanapofanya mikutano ya kuwakaribisha wawekezaji watumie fursa hiyo pia kuwatangaza vijana wetu wasomi ambao nao wanaweza kuwa mabalozi wazuri kuitangaza nchi na kukaribisha wawekezaji zaidi.

Ikiwa sababu ni hatuna kiwango bora kwa vigezo vya kimataifa, tunaangalia wapi penye tatizo tuparekebishe. Hili likizungumzwa fikra zetu zinaenda moja kwa moja kutafakari aina na kiwango cha elimu kinachotolewa na vyuo vyetu. Kwa sababu kumekuwa na maswali na wengine wakipendekeza vyuo na shule zetu zibadili mtindo wa ufundishaji.

Sioni tofauti sana kwenye mtindo wa kufundisha wa vyuo vetu kulinganisha na wa nchi jirani zetu, wenye ujuzi juu ya hili watatueleza zaidi, ila kuna sehemu ambazo tunahitaji kuboresha. Nikisema hivi ninamaanisha kuwa kwa mtindo huu tulionao sasa tunaweza kutoa vijana wazuri "competitive" kama tutarekebisha vitu kadhaa.

Kikubwa tunachohitaji ni waalimu na wanafunzi kufungua fikra zaidi na kuangalia uhitaji wa soko la ajira kimataifa badala ya kuegemea tu kwenye soko la ndani. Wanapaswa kuangalia ni vigezo gani vinahitajika huko nje ili wajitahidi kuwa navyo. Vyuo vinaweza kuwa na program maalumu za kufanya tafiti na kutengeneza mitalaa ya kuwanoa vijana wetu.

Tofauti kubwa ninayoiona kati ya wahitimu wetu na wa nchi jirani zetu ni suala la kujiamini na kuthubutu, hivyo tunahitaji kuangalia kipengele hicho kwa sababu ni kigezo muhimu katika kujitangaza soko la nje ingawa kinaweza kudharaulika.

Nahisi mitindo yetu ya maisha na malezi yana mchango katika hili, kwa sababu tunaona wanafunzi wanaotoka shule za English Medium wanakuwa na kujiamini zaidi kuliko wanaotoka shule za kawaida ambao ni wengi zaidi. Kwa hili inabidi jamii, wazazi na waalimu wa ngazi za chini wakumbushwe juu ya umuhimu wa kumkuza vema mtoto kisaikolojia. Ni vitu tunapuuza ila madhara yanakuja kuonekana ukubwani.

Tukirudi vyuoni, ni muhimu sana fikra za walimu ziendane na wakati kwa sababu wao wana nafasi ya kwanza ya kuwa role models na kufungua fikra za vijana. Lakini walimu wengi wamekuwa tofauti na hili, wanataka kuwafundisha wanafunzi wa sasa kwa mbinu na kauli zilezile walizosomeshewa na walimu wao miaka ya nyuma.

Hapa sizungumzii mitalaa ya masomo, ila namna ya ufikishaji wa taaluma na mazungumzo mengineyo yanayotokea nyakati za vipindi. Wanafunzi huwa makini sana kusikiliza walimu wakiongelea kitu cha nje ya somo zaidi ya wanavyosikiliza somo. Mwalimu akionesha ni mpana wa fikra wanafunzi wanajenga ukaribu zaidi kwake na huenda wakamfuata kwa ushauri na kujifunza zaidi.

Mwalimu akiwa ni mtu wa kusema "focus" kwenye masomo tu bila kuzingatia dunia ya utandawazi inayomzunguka kijana kuna uwezekano kijana akatafuta inspiration sehemu tofauti. Mwanafunzi anahitaji mwalimu anayeelewa alama za nyakati na kusaidia kijana kwenda vema na wakati badala ya kuishia kusema akili za vijana zimeharibika. Fikra hii hujenga ukuta kati ya mwalimu na mwanafunzi na kupunguza nafasi ya mwanafunzi kujifunza kwa mwalimu.

Mmoja wa washindi wa taji la urembo nchini aliwahi kunisimulia kuwa alipata tabu chuoni baada ya kutoka kwenye mashindano ya kutafuta mrembo wa dunia. Baadhi ya walimu walimpa wakati mgumu wakimwambia kwa kebehi asingeweza kuchanganya urembo na masomo. Akaweka jitihada kuwathibitishia tofauti na sasa ni mtu ana kazi yake nzuri sana.

Zaidi tuna mifano ya watu kama Nancy Sumari, Faraja Kota, Angela Damas, Basila Mwanukuzi, Jokate Mwegelo, Irene Kiwia na Hoyce Temu ambao wapo kwenye nafasi nzuri na walipita mkondo huohuo. Nadhani njia sahihi ni kumshauri kijana njia ya ku-balance masomo na mengine ya nje na huo ndio upana wa fikra.

Tuna tatizo la wahitimu wetu wengi kushindwa kujielezea na kuandika, na hizi ni skills zilipaswa kukuzwa mapema. Fikiria mtu anaitwa katika usaili na anaambiwa ajielezee "weakness and strength" au "hobbies" mtu anaanza kubabaika. Au mtu anaulizwa kiasi cha mshahara anachohitaji anaanza kujiuma na kujibu kuwa anaachia kampuni imuambie imeandaa kiasi gani kwa nafasi hiyo. Hii ni kusema kuwa huyu kijana haijui thamani yake kwa uwezo wake wa kuzalisha.

Unakuta muhitimu wa chuo ameandika kwenye barua pepe ya kuomba kazi "am Tanzanian gal, 28 years old..."! Sitashangaa kusikia mtu huyu ameshatuma maombi ya kazi zaidi ya mia lakini hajaitwa kwenye usaili hata mara moja.

Somo la Development Studies hasa kipengele cha Communication Skills kinaweza kutumika kuwafundisha vijana kujiamini, jinsi ya kujielezea na namna ya mawasiliano ya viungo vya mwili kuliko kufundisha "tenses" ambazo zinafundishwa tangu shule ya msingi. Sisemi kuwa hizi si muhimu bali nasema muda wa somo hili ni mdogo na ungetumika kufundisha ambavyo havifundishwi kwingine.

Somo hili pia lizingatie umuhimu wa kujifunza kutoka kwa watu ambao tayari wapo katika ajira, wangekuwa wanaalikwa kuongea na wanafunzi nyakati za somo ili kuwapa ushauri wa kufanyia kazi kujijenga.

Jitihada za makusudi zifanyike kwa vyuo kuwapatia wanafunzi nafasi za kujifunza kwa vitendo kwenye makampuni/taasisi katika kipindi cha masomo au wakati wa likizo. Katika course work kunakuwa na kipengele cha field study time na mtu anapewa idadi ya saa za kukamilisha kwa kila semester.

Mpango huo utawezekana kama vyuo vitachukua jukumu la kuweka makubaliano na makampuni kuliko ilivyo sasa wanafunzi wanaachiwa kutafuta sehemu za kufanyia field. Faida ya mpango huu ni kuziba kipengele cha “uzoefu kazini” na kuongeza nafasi ya kupata ajira wanapohitimu. Nchi za wenzetu wana kipindi cha internship baada ya kumaliza chuo lakini kwetu ni ngumu kufanya kwa sababu hatuna ruzuku kwa wahitimu kujikimu na tena wanaharakishwa kuanza kurejesha mkopo wa chuo.

Haitakuwa vibaya tukiwaiga wenzetu kwenye kusaidiana na kupeana taarifa panapokuwa na nafasi za ajira nje, tuache tabia ya “kuzibiana”. Wenzetu wametushinda kwenye kusaidiana katika elimu na ajira; hufanya harambee kusaidia watoto waliofaulu na wakiwa kwenye ajira wanaitana na kusaidiana, tofauti sana na sisi. Sehemu pakiwa na mtanzania, ukiulizia nafasi utasikia "siku hizi hatuchukui...... tukianza kuchukua nitakujulisha....", ilimradi kukatishana tamaa.

Nina imani kuwa wahitimu wetu wakigawanyika, wengine wakapate ajira nje na wengine waingie kwenye ujasiriamali, baada ya muda wataweza kushirikiana kwa mbinu za kiushindani kwenye soko la uzalishaji na kukua pamoja.
 
Kaka haya madini ni Tanzanite. Though nimechelewa kuisoma lakini nashukuru kuna jambo nimejifunza.
 
Tumekosa tu viongozi wanaofikiri kuweza kuzitumia fursa tele nchini kuzalisha ajira
 
Kaka unamaanisha hivo viwilii vinatosha kabisa kumaliza tatizo la ajira kwa vijana?
Naomba ufafanuzi kidogo hapo.
 
Back
Top Bottom