Tuendako: Lowassa anaisubiri hukumu ya Kikwete

Keil

JF-Expert Member
Jul 2, 2007
2,214
803
Lowassa anaisubiri hukumu ya Kikwete

Absalom Kibanda

MANENO rahisi yalitushinda wanahabari. Haya si mengine, bali yale yaliyotokana na utafiti wa siku mbili uliofanywa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) katikati ya mwezi Oktoba mwaka huu.
Vyombo takriban vyote vya habari viliukwepa mtego rahisi wa REDET ilioutega na ambao kwa bahati mbaya ukanasuliwa na wao wenyewe - watafiti hao.

Ni bahati mbaya kwamba, REDET taasisi ya kisomi, ikitumia ujuzi wa ‘shule’, iliamua kwa makusudi kumung’unya maneno na ikakiuka misingi ya awali ya utafiti wake.

Kwa bahati njema, baadhi yetu tuliweza kuubaini mtego wa kumung’unya maneno wa REDET kwa sababu, gazeti hili wiki kadhaa kabla ya matokeo ya utafiti huo kutangazwa, liliandika taarifa kuhusu jambo hilo.

Ni ajabu kwamba, kile ambacho gazeti hili ilikiandika kuwa sehemu ya maswali yaliyokuwa katika hojaji hiyo ya REDET, hakikuonekana katika majibu yaliyotangazwa wiki iliyopita.

Moja ya maswali katika hojaji hiyo ya REDET ilisomeka; “Kama Rais Kikwete angeamua leo kubadilisha baraza lake la mawaziri, ni waziri yupi usingependa ateuliwe tena katika serikali?”

Katika kipengele hiki, watu waliohojiwa na REDET walitakiwa kutaja jina la waziri au baadhi ya mawaziri wasiostahili kuwemo kwenye baraza jipya litakaloundwa na Kikwete, ambalo kila mtu anayefikiri sawa sawa amekuwa akilisubiri kwa hamu.

Baadhi yetu tulipopata taarifa kuwa utafiti ule ulikuwa umekamilika na matokeo kutangazwa, kikubwa tulichokiangalia kilikuwa ni waziri gani (mawaziri gani) alikuwa amechangia kuiangusha serikali (kwa mtazamo wa wananchi).

Kwa sababu ambazo binafsi sizijui, REDET hawakuweka bayana majibu ya kipengele hiki muhimu na badala yake wakaishia tu kutamka kwamba, Rais Kikwete alikuwa amelipiku baraza lake la mawaziri kwa kukubalika.

Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, hata sisi wanahabari kwa sababu ambazo bado zisielewi, tuliingia katika mtego wa matokeo hayo ya REDET na tukasalimu amri kwa kuyatii na kuyaona yakiwa yamekamilika. Katika hili tumefichwa kitu muhimu.

Pamoja na kutambua na kukubali kuwa kazi iliyofanywa na REDET pamoja na kufinyangwafinyangwa imetoa matokeo yenye mwelekeo stahili, binafsi nayaona matokeo hayo kuwa yaliyotolewa yakificha taarifa nyeti iliyopaswa kuwekwa hadharani kwa maslahi ya taifa hili.

Baadhi yetu tunaamini kuwa, matarajio ya matokeo ya hojaji hiyo ya REDET, yalipaswa kukamilika kwa kututhibitishia iwapo yale yanayoandikwa na tunayosikia kuhusu akina Edward Lowassa, Zakia Meghji, Nazir Karamagi, Andrew Chenge na mawaziri wengine wengi, yamepenya vichwa vya wananchi na kuathiri muonekano wao katika jamii.

Kwangu mimi taarifa hizo zingesaidia kujua athari za sifa na tuhuma wanazomwagiwa mawaziri wetu kupitia katika vyombo vya habari, ambavyo mara kadhaa viongozi hao hao wamekuwa wakivinyoshea vidole kwa kuripoti masuala ya kubuni.

Pamoja na udhaifu huo wa REDET ambao unaweza ukawa ni wa makusudi (si wa bahati mbaya), bado tunaamini kuwa matokeo yake yatakuwa changamoto muhimu katika mabadiliko makubwa yajayo.

Haihitaji kuwa na akili za ziada kutambua kuwa, matokeo ya REDET yanayomuweka Kabwe Zitto, mbunge wa upinzani katika nafasi ya pili kwa kukubalika katika utendaji wake wa kazi akivuna asilimia 10 dhidi ya asilimia 30 ya Rais Kikwete akimchukua Waziri Mkuu aliyepata 5.8% ni ya kuifedhehesha serikali na chama tawala.

Ni jambo lisilohitaji elimu ya chuo kikuu kuyaona matokeo yanayoonyesha kuporomoka kwa umaarufu wa Rais Amani Karume Zanzibar kutoka asilimia 47.8 za mwaka jana hadi kufikia 35.5% za sasa kuwa huenda yanahusiana na hali tete ya kisiasa ya huko visiwani na kuporomoka kwa utendaji wa serikali yake.

Kama hiyo haitoshi, habari kwamba, Rais Kikwete aliyevuna asilimia 80 ya kura zote katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na mwaka mmoja baadaye kura ya maoni ikamuona akikubalika kwa asilimia 67 kabla ya sasa kufikia asilimia 44 ni mbaya na isiyopaswa kuachwa ikaendelea kubakia ilivyo.

Lakini pengine jambo baya na la lazima kufanyiwa kazi na Kikwete mwenyewe, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali kwa ujumla, ni lile linaloonyesha kuwa rais wetu anapendwa na watu wenye elimu ndogo zaidi kuliko wale waliosoma vyema.

Ni jambo la hatari na fedheha kwamba, rais wetu anaungwa mkono zaidi na watu wasiosoma shule kabisa na wale wenye elimu ya msingi kuliko ilivyo kwa watu wenye elimu ya sekondari na walioelimika zaidi ya hapo.

Watanzania tunapaswa kuikataa fedheha hii ya wajinga kutuchagulia viongozi na aibu ya kiongozi wetu mkuu kutoungwa mkono na wasomi wetu.

Ni kwa sababu ya kujua hatari hiyo ambayo sasa imethibitishwa na REDET, ndiyo maana miezi takriban miwili iliyopita, kupitia safu hii hii, nilipata kumtahadharisha rais wangu kuhusu tukio la kuanguka kwake machoni mwa wapigakura.

Katika makala hiyo, nilimtahadharisha rais kuwa macho na wanaounda baraza lake la mawaziri ambao sifa kubwa inayowatia nguvu ya kuendelea kujiona wakistahili kushiriki katika ‘ufalme’ wa Kikwete si rekodi zao za utendaji, ukada wenye utii na wa mfano kwa chama chao, mchango wao kwa maendeleo ya taifa, uadilifu na umakini walionao katika kazi, bali ushirika wao na Jakaya zama zile kabla hajawa mkuu wa nchi.

Katika moja ya aya za makala hiyo, niliandika maneno yafuatayo; “Katika mazingira ya kusikitisha, miongoni mwao hawa, ndiyo wale wale ambao, uamuzi wa Kikwete kuwapa nafasi za uteuzi katika baraza lake la kwanza la mawaziri wakiwa mawaziri kamili au manaibu, leo hii unawaweka katika kundi la watu ambao hawana hata jambo moja la wazi unaloweza kusema wanajivunia katika utendaji wao wa kazi.

“Pasipo kutafuna maneno, hawa ndio waliomuangusha Kikwete. Hawa ndio waliowasaliti Watanzania. Hawa ndio wale ambao baada ya kupewa dhamana ya kuwatumikia wananchi, wameshindwa kuitambua dhamana hiyo na kuiona kuwa ni wajibu mzito mabegani mwao, uliokuwa ukihitaji uchapakazi usiomithilika, uadilifu usio na shaka na visheni yenye kujenga misingi imara ya kuliondoa taifa hili kutoka katika msongamano wa matatizo yanayojenga usugu kila kukicha. Hawa ndio ambao Kikwete anapaswa kuwang’oa.”

Sikuishia hapo, niliandika bayana kwamba, miezi takriban 22 (wakati huo) tangu Rais Jakaya aingie madarakani mawaziri na manaibu wa namna hii, ndio waliosababisha yeye rais na Waziri Mkuu wake, Edward Lowassa wageuke wao ndio wasemaji na watendaji wa kila kitu kikubwa serikalini hata katika masuala ambayo yalipaswa kuamuliwa katika ngazi za wizara.

Leo hii hayo si maneno ya magazeti kama walivyozoea kutuambia wasaidizi wakuu wa Kikwete na Lowassa, bali ni kilio cha wananchi wengi waliohojiwa na REDET.

Binafsi naamini kwamba, iwapo REDET wangepata ujasiri wa kuyataja majina ya mawaziri ambao wamekataliwa na wananchi katika kura ya maoni iliyoendeshwa nchi nzima, leo hii mambo yangekuwa magumu kweli kweli serikalini.

Hata hivyo, pamoja na udhaifu katika ripoti hiyo ya REDET, ukweli unabakia pale pale kwamba Baraza la Mawaziri la Kikwete limepwaya, umaarufu wa rais mwenyewe umeporomoka na imani ambayo wananchi waliijenga miaka miwili iliyopita imeendelea kupotea.

Kwa kutambua uhalisia huo usiopingika, Kikwete anapaswa kufanya jambo moja tu, kugeuka nyuma na kusikiliza wasia wa Nyerere na kuchukua maamuzi magumu ilimradi tu yawe ni kwa maslahi ya taifa.

Katika kufanya hivyo, anapaswa kuanza na Waziri Mkuu Lowassa. Ampime kwa vigezo vya kiutekelezaji, kimaamuzi na kimaadili na ampe hukumu anayostahili. Kama atajiridhisha kwa moyo wake wote kwamba amekuwa msaada mkubwa kwake katika maeneo hayo matatu aendelee kumpa fursa ya kuwaongoza mawaziri na kusimamia utendaji serikalini.

Katika kulitekeleza hili, anapaswa kutogeuka nyuma na kuangalia upacha wao kisiasa tangu walipokutana miaka ya mwanzo ya 1970, wakajaribu kwa pamoja mwaka 1995, wakapanda ngazi pamoja serikalini na wakashirikiana tena kwa ajili ya mwaka 2005. Huko kutakuwa ni kuwasaliti Watanzania milioni tisa na ushee waliompa kura za ndiyo.

Katika hili anatakiwa kumpa Lowassa hukumu anayostahili. Anawajibika ama kumlinda kwa mema au kumwadhibu kwa makosa. Katika hili haitaji kuwa vuguvugu. Analazimika kuwa ama moto au baridi. Analazimika kusuka au kunyoa.

Atakapokuwa amemalizana na Lowassa, ageukie kwa mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wa wilaya. Kazi itakuwa rahisi kabisa, hakuna atakayekuwa na ubavu wa kusema lolote kwani watajua kwa uhakika kabisa kuwa umeamua kwa haki. Huko ndiko tuendako.
 
Hakuna hukumu yoyote JK na EL hawawezi kupeana talaka, waliopewa talaka ni Watanzania.
 
Naamini huyu ndg Kibanda huwa anasoma hapa, kwa hiyo bila shaka ataziona pongezi zangu. Hongera ndugu, umeandika na kuchambua vizuri mno. Binafsi nimekuwa nikijiuliza sana kama utaratibu wetu wa uchaguzi unafaa, na nisichokifurahia hata kidogo ni hili suala la "mtu mmoja kura moja". Hii ndiyo inayotufanya tuwe na viongozi ambao kwa kiasi kikubwa wamechaguliwa na "wajinga", na kwa hiyo si ajabu asipokusikilizeni ninyi mnaojiita "wasomi". Angalia hesabu hizi: Kama wenye elimu ya chuo kikuu kwa mfano ni chini ya 1%, kuna haja gani ya kukubembelezeni (achilia mbali kukusikilizeni), iwapo kura zenu hazifiki 1%? Imagine watu wanaofahamu undani wa siasa na uchumi wa nchi yetu kwa mapana kama akina Prof Haroub Othman, Prof Issa Shivji, Mzee Warioba, na wengine wanaofanana na hao, na huku JF wako wengi tu, ati nao wana kura ileile moja kama mtoto wa miaka 18 anayeanza kupiga kura leo, au mwanakijiji fulani illiterate huko Madongo-kuinama! Hii ni sawa kweli? Wajinga wataendelea kutuchagulia viongozi sijui hadi lini!
 
Kithuki,

Challenge iwe ni kuweka mikakati ya kuwafanya watu wengi waelimike na siyo kuleta mambo ya apartheid.Watanzania wote wana haki siyo tu ya kuwa na kura sawa (wenye sifa za age and sanity) bali pia kupata huduma jamii sawa ikiwamo elimu.

Mwandishi anaandika kama vile ana imani na huyo rais Kikwete, kama vile ame swallow magirini ya REDET bait and hook kwamba "rais anapendwa ila anaangushwa na baraza la mawaziri".Mwandishi anamlaumu Kikwete kwa kuchagua mawaziri na manaibu wao wasio na track record, anategemea vipi mtu asiye na track record akafanya track record kuwa priority?

Kikwete mwenyewe ana track record gani kama siyo IPTL na Richmond?
 
Mawaziri walio `mizigo` watupiwe virago sasa

na julian msacky

TAASISI huru iitwayo Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET), ilipotangaza ripoti yake juu ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Nne, viongozi wengi hawakuamini masikio na macho yao.

Ilifanya hivyo baada ya kupata maoni ya wananchi mbambali nchini, na kuonyesha kwamba idadi kubwa ya wananchi wamepoteza imani na viongozi wao, hasa Baraza la Mawaziri, lakini huo ndio ukweli wenyewe.

Baadhi ya viongozi walichukulia utafiti wa REDET kama sehemu ya kujikweza kwa taasisi hiyo kwa umma ili ijipatie umaarufu. Maoni ya REDET yanaonyesha kwamba, bado wananchi wana imani na Rais Jakaya Kikwete, lakini si kama ilivyokuwa mwaka jana. Rais wetu mwaka jana wananchi walimwamini kwa asillimia 67.4, lakini sasa ni asilimia 44.4. Kwa maana nyingine ni kwamba, imani ya wananchi kwa Rais wao imeanza kufifia.

Moja ya sababu zilizomfikisha Rais Kikwete kwenye kiwango hicho ni kwamba, wananchi wanadai kuwa hatekelezi ahadi alizotoa, au haangalii kwamba zinatekelezwa. Wanamlalamikia kuendelea kuchagua viongozi wasio na sifa. Hiki ni kibarua ambacho Rais anatakiwa kukifanyia kazi, ili dhana yake ya maisha bora kwa kila Mtanzania ionekane. Maisha bora hayawezi kuja kama kile alichoahidi mhusika hakina utekelezaji. Na hicho ndicho wananchi walicholalamikia REDET.

Mbali na Rais, utafiti wa REDET ulionyesha kuwa, asilimia 19.2 hawaridhishwi na utendaji kazi wa Baraza la Mawaziri la Rais Kikwete. Lakini, kama tutakumbuka vizuri, Rais Kikwete kuna wakati aliwaweka mawaziri wake kiti moto ili waende pamoja kiutendaji chini ya dhana yake ya ukombozi kwa Watanzania - ya ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya.

Hapa mawaziri walipelekwa Arusha katika Hoteli ya Ngurdoto na kupewa semina elekezi, nini ambacho walitakiwa kufanya kama mawaziri. Haikuishia hapo. Makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya nayo walikimbilia Arusha, pengine kwa maelekezo ya nini cha kufanya ili wamsaidie Rais aweze kuwapatia wananchi wake maisha bora kwa kila Mtanzania.

Tumeingiwa na hofu kubwa tuliposikia kupitia ripoti ya REDET kwamba, wananchi wamepoteza imani na Mawaziri wa Rais Kikwete licha ya semina hizo za Ngurdoto ambazo bila shaka zilisaga kodi za Watanzania.

Udhaifu unapowaandama mawaziri kiutendaji, maana yake ni kwamba atakayelaumiwa na wananchi ni rais mwenyewe. Ni rais kwa sababu ndiye huwateua mawaziri na wanapoboronga wa kuwawajibisha ni rais huyo huyo.

Hata hivyo, hatutashangazwa na utafiti huo wa REDET, hasa tunapokumbuka kuwa, kwa siku za nyuma kumeibuka staili mpya ya wananchi kuzomea viongozi wao wanapokuwa mikoani kuelezea hili na lile. Kwa wale wanaojua kusoma alama za nyakati, zomea zomea hiyo ndicho kilichoibuliwa na REDET hivi sasa. Ndio maana nasema kwamba, hatutakiwi kushangazwa na ripoti ya REDET. Je, haikusemwa kwamba dalili ya mvua ni mawingu?

Kwa utafiti huo wa REDET, Serikali ya Rais Kikwete inatakiwa kujipeleleza ili kujua kwa nini wananchi wamechoshwa na mawaziri wake mapema kiasi hiki, ikiwa ni miaka miwili tu ya uongozi wake madarakani?

Tutarajie nini miaka inayokuja kama dalili zenyewe ndizo hizi zinalipuka hata kabla ya jua kukaribia kuzama? Hatukutarajia kwamba Serikali ya Rais Kikwete ingelegea mapema hivi kiutendaji, ila akiendeleza ukimya kwa mawaziri wake bila kuwanyooshea kidole wanapovurunda, wananchi hawataacha kuikaba koo Serikali yake.

Kuna mambo ambayo Rais Kikwete aliyakataza yasifanyike, lakini hakuna aliyesikia la mtu, zaidi ya kupiga makasia. Mgogoro uliolipuka bungeni huku baadhi ya wabunge wakihoji juu ya kusainiwa kwa mkataba wa Buzwagi, wakati Serikali ilishasema kilichobakia ni kupitia mikataba iliyopo kwanza ili iweze kuinufaisha nchi, nalo lilizua maswali mengi kuliko majibu.

Au kwa Serikali kusaini Mkataba wa Biashara na Umoja wa Ulaya unaokwenda kwa jina la EPA huku ikiashiria kutunyonya damu wazi wazi, nalo halitaachwa kuulizwa pengine kila mara, hasa ikizingatiwa kuwa mikataba mingi ambayo tumeingia imekuwa na kelele za kutuumiza badala ya kutuletea neema.

Swali linalohojiwa hivi sasa na Watanzania wengi ni hili: Rais Kikwete anaweza kutuliza mzuka wa wananchi hivi sasa ambao wamekosa imani na baadhi ya viongozi wake kiutendaji? Au Rais wetu atasema kwamba, kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kulala? Wananchi wanakosa imani na viongozi wao kwa sababu, wanapoahidiwa maisha bora hayaonekani na badala yake tunachosikia kila mara ni wananchi kulalamika hali ni mbaya. Kwa nini?

Wakati wao wakilialia hali mbaya, viongozi wao hujitokeza na kusema kwamba uchumi wa nchi unapaa. Hatuwezi kusema uchumi unapaa, wakati wananchi wameendelea kuishi chini ya dola moja ya kwa siku. Pia hatuwezi kupiga makofi ya kinafiki kwamba uchumi unapaa, wakati huduma muhimu kwa binadamu kama umeme, maji, afya, usafiri zinazidi kushika makali badala ya kupungua. Hiki ndicho kinachochefua wananchi wengi hivi sasa. Mwananchi aliyezungukwa na hali tete namna hiyo huwezi kumwambia uchumi unapaa, halafu akusikilize.

Viongozi wa Serikali wanatakiwa kujipanga upya kuhudumia jamii na si kuzunguka nchini kuelezea uzuri wa bajeti. Nani ambaye alikuwa hajui kwamba bajeti imesomwa na wananchi wakiwa na wawakilishi wao bungeni?

Kama bajeti ilisomwa na wananchi wakaisikilza kupitia redio, kusoma magazeti na kuwaona mawaziri kupitia kwenye televisheni jinsi walivyopambana kujibu maswali, kipi walichofuata tena mikoani kama si kukaanga fedha za walipa kodi? Tunavyojua ni kwamba, kiongozi anatakiwa kuwa makini kwa kila jambo analofanya. Lakini hiki cha mawaziri kuzunguka mikoani kuelezea bajeti, linazua maswali kuliko majibu.

Leo hii wanaotuongoza wanatakiwa kutambua kwamba, wanaongoza jamii nyingine si ile ya miaka ya 1960. Kuna uelewa mpana sana wa wananchi na umakini wa kufuatilia kile viongozi wao wanachoahidi. Jamii inapoelimika, watawala nao hupata kazi ya kuwaongoza. Tazama Nigeria au Kenya.

Lakini si hivyo tu, Mwalimu Julius Nyerere naye aliwahi kusema; "uongozi unaweza ukawa mzuri au mbaya au usiojali, lakini kama wananchi wameamka na wanajitambua wenyewe kutoshirikishwa kwa mawazo na jamii hakutaendelea kwa muda mrefu."

Hiki ndicho Serikali ya Rais Kikwete inachokabiliwa nacho. Anachosema Mwalimu Nyerere ndicho walichosema wananchi kwa REDET, kwamba uongozi wetu hautujali. Je, mkuu wa nchi anaweza kufumbia macho kelele za umma? Jibu ni hapana. Kama Mwalimu anavyosema, kwamba wananchi wakiwa wanajitambua na kile wanacholalamikia kutofanyiwa kazi, kutokusikilizwa kwao hakutachukua muda mrefu.

Ni matumaini yetu kwamba, Rais Kikwete atafanyia kazi kile wananchi wanacholalamikia kuhusu udhaifu wa viongozi wetu kiutendaji. Kiongozi ni mtumwa wa wale anaowatumikia, hivyo viongozi wanatakiwa kutumikia na si kutumikiwa.

Ni kwa sababu hiyo, wananchi wengi huchagua mmoja kuwawakilisha kwa niaba yao, hasa bungeni. Hivyo kauli za viongozi kuubeza utafiti wa REDET kwa vile umewauma, kwamba, ni wa kujitafutia umaarufu si sahihi. Walichofanya REDET ni kuwakilisha maoni ya wananchi na si vinginevyo.

Nani asiyejua kwamba, nchi ina tatizo la rushwa na kwamba inazidi kukunjua makucha? Hatua waliyofikia wananchi kutopenda kusikia hata wabunge wao, hapo ujue kuna kazi.

Kwa nini mara hii wananchi wamelikunjia ngumi Baraza la Mawaziri tofauti na lilivyoanza mwanzoni kiutendaji? Kipi kinakwenda mrama na Rais Kikwete kukaa kimya? Inapotokea wananchi kukosa imani na serikali yao ni hatari na inapoachwa ikomae, wananchi huamua wenyewe nini cha kufanya. Tunamwomba Rais Kikwete asisubiri wananchi wafikie huko.

Rais Kikwete anapoona kiongozi fulani anageuka mzigo katika uongozi wake, ampumzishe ili asimwaribie sifa aliyo nayo kwa wananchi wake.

Hapana, kila mtu afe na msalaba wake mwenyewe. Katika kuongoza, woga wa kuwajibishana ni sumu ya maendeleo. Au tuseme kwamba hapa Serikali ilipofikia ni utabiri wa Mwalimu Nyerere unatimia?

Chini ya Kitabu chake; ‘Uongozi wetu na hatma ya Tanzania', Mwalimu anasema: "Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wake, mazoea ya watu, na ubovu wa vyama vya upinzani, kinaweza kuendelea kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa n hi yetu unataka yasemwe." Kwa kauli ya Mwalimu Nyerere ambaye ni mwasisi wa chama hicho, ukiyatazama maneno hayo na ukali wake, utabaini kuwa hata malalamiko ya wananchi juu ya utendaji duni kwa viongozi wao yanastahili kufanyiwa kazi.

Ndio maana mkongwe wa siasa nchini, ambaye pia ni Waziri wa Nchi ya Ofisi ya Rais (Siasa na Uhusiano ya Jamii), Kingunge Ngombale – Mwiru, anasema kwa kifupi kwamba REDET hakuna walichokosea. "Utafiti wa REDET hauwezi kupuuzwa, kwani ni wa kitaalamu na umefanyika kisayansi," alisema Kingunge.

Tunampongeza mzee Kingunge kwa kukubali utafiti huo kuliko wale wenye shingo ngumu ambao hawataki kukiri ukweli. Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alinukuliwa akisem: "Inashangaza sana haya matokeo. Kanuni zetu ni mpya na nzuri. Inawezekana hii taasisi (REDET) iliyofanya utafiti ni chombo tu kinajitafutia umarufu."

Wakati utafiti wa REDET ukiwashangaza baadhi ya viongozi, tulishtushwa tuliposikia kwamba, kati ya wanasiasa mashuhuri ambao wananchi waliwapa ‘ujiko' ni Rais Kikwete, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto na Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Tunaelezwa kwamba mawaziri wengine hawakusikika na baadhi walipata takwimu ndogo kupita kiasi. Sasa hapa ukiangalia Baraza la Mawaziri la Rais Kikwete ambalo ni kubwa na pengine, halijashuhudiwa tangu uhuru, unajiuliza, kweli hali ni shwari?

Inavyoelekea na huenda ndivyo ilivyo, Rais Kikwete ana kazi ya kuwa na viongozi ambao wanaaminika kwa wananchi. Hatusemi kwamba Rais Kikwete aanze timua timua, hapana. Awajulishe viongozi wake kwamba wanatakiwa kubadilika na kuwa karibu na mbavu za wananchi. Endapo Rais Kikwete hatawapa ukweli wa hali halisi jinsi wananchi wanavyowatazama, kuna hatari umma ukaendelea kupoteza imani na Serikali. Tusifikie huko.

Ni kweli siasa ni ngumu kuliko fizikia kama alivyopata kusema mwanasayansi Albert Eisten. Lakini pamoja na yote hayo, hatuwezi kukumbatia wanasiasa wasiokubalika na umma kwa sababu hiyo. Ni lazima kuwa na wanasiasa ambao wanakubalika na jamii husika na wanaojua wajibu wao kwa umma.

Ni matarajio yetu kuwa hali iliyojitokeza kupitia REDET, Rais Kikwete ataifanyia kazi ili wananchi wazidi kuwa na imani na Serikali yao. Wahenga walinena kwamba linalowezekana leo lisingoje kesho. Na Rais wetu afanye hivyo.

Source: Rai
 
Naamini huyu ndg Kibanda huwa anasoma hapa, kwa hiyo bila shaka ataziona pongezi zangu. Hongera ndugu, umeandika na kuchambua vizuri mno. Binafsi nimekuwa nikijiuliza sana kama utaratibu wetu wa uchaguzi unafaa, na nisichokifurahia hata kidogo ni hili suala la "mtu mmoja kura moja". Hii ndiyo inayotufanya tuwe na viongozi ambao kwa kiasi kikubwa wamechaguliwa na "wajinga", na kwa hiyo si ajabu asipokusikilizeni ninyi mnaojiita "wasomi". Angalia hesabu hizi: Kama wenye elimu ya chuo kikuu kwa mfano ni chini ya 1%, kuna haja gani ya kukubembelezeni (achilia mbali kukusikilizeni), iwapo kura zenu hazifiki 1%? Imagine watu wanaofahamu undani wa siasa na uchumi wa nchi yetu kwa mapana kama akina Prof Haroub Othman, Prof Issa Shivji, Mzee Warioba, na wengine wanaofanana na hao, na huku JF wako wengi tu, ati nao wana kura ileile moja kama mtoto wa miaka 18 anayeanza kupiga kura leo, au mwanakijiji fulani illiterate huko Madongo-kuinama! Hii ni sawa kweli? Wajinga wataendelea kutuchagulia viongozi sijui hadi lini!

Kwahiyo miaka 18 mtu m1 kura1
Miaka 32 mtu m1 kura2
Miaka 50 mtu m1 kura3



RubiiKimimi
 
Yupo na magazeti yake mengi yanaishia kufungiwa.......anatumika sana na wenye pesa.......na wachumia tumbo
 
Back
Top Bottom