TUCTA `yageuka` chama cha upinzani | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

TUCTA `yageuka` chama cha upinzani

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mutu, May 3, 2010.

 1. M

  Mutu JF-Expert Member

  #1
  May 3, 2010
  Joined: Mar 30, 2008
  Messages: 1,333
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 0
  CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
  Na Waandishi wetu
  2nd May 2010

  Yataka wafanyakazi kutochagua wasiowatetea
  Yawahimiza kujitokeza kwa wingi uchaguzi mkuu


  Rais wa Tucta, Ayub Omar
  Pamoja na kusisitiza kuwa mgomo wa wafanyakazi utaanza tarehe 5 mwezi huu, Shirikisho la Wafanyakazi nchini (Tucta), limekunjua makucha na kuwaelekeza wanachama wake kutowachagua viongozi wasioweza kutatua matatizo yao, wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao .

  Shirikisho hilo limetoa maelekezo hayo kwa wanachama wake wakati wa Sherehe ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani, iliyofanyika kitaifa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam jana.

  Akizungumza kwenye sherehe hiyo iliyohudhuriwa na mamia ya wafanyakazi kutoka vyama mbalimbali vya wafanyakazi nchini, Rais wa Tucta, Ayub Omar, ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi, aliwataka wafanyakazi kote nchini kutumia muda wa kutosha kuwapima wale wote wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi kabla ya kufanya uamuzi.

  Alitoa wito kwa wafanyakazi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura mwezi Oktoba mwaka huu na kuwachagua viongozi wanaoumizwa na matatizo ya wafanyakazi na wenye dhamira ya dhati kuyaondoa mataizo hayo.

  "Nawasihi wafanyakazi kote nchini kuhakikisha mnajitokeza kwa wingi kupiga kura ya kuchagua viongozi bora. Tuachane na ushabiki wa vyama vyetu vya siasa, tuangalie zaidi sera na uwezo wa viongozi wa vyama vinavyotaka kuunda serikali...tunataka viongozi watakaotuvusha kutoka katika kundi la umasikini, fursa za maendeleo zipo nyingi, watu wapo, kinachokosokana ni uongozi bora" alisema.

  Rais huyo wa Tucta ambaye alikuwa akishangiliwa mara kwa mara na wafanyazi waliohudhuria sherehe hiyo, alisema kauli mbiu ya wafanyakazi kwa mwaka huu ni 'Uchaguzi Mkuu 2010 uwe ufumbuzi wa kero za wafanyakazi' na kuifafanua kuwa ina lenga kuwataka wafanyakazi wote nchini kuwa makini katika kuchagua viongozi wa kuongoza.

  "Ni wajibu wetu kuionyesha serikali kuwa haturidhiki na mweleko wa nchi kisiasa na kiuchumi." alisema.

  Alisema kauli ya mara kwa mara ya serikali kutokuwa na uwezo wa kulipa mishahara inayokidhi mahitaji kutokana na ufinyu wa bajeti inasababishwa na mbinu chafu za matajiri za kuikosesha serikali mapato, huku ikiwa haichukuwi hatua zozote dhidi yao.

  Aliikosoa serikali kuwa imekosa umakini katika kusimamia sera za uchumi, huku baadhi ya maafisa wake waandamizi wakikosa uzalendo, hali ambayo inawaumiza wananchi masikini.

  "Wameingiwa na roho ya ubinafsi ya kutaka kujitajirisha kwa haraka tena bila ya ukomo, hawatosheki, wamesahau dhamana waliyopewa ya kuitumikia nchi kwa uaminifu na uadilifu ili nchi iweze kupata maendeleo kwa manufaa ya wote, kila leo utasikia taarifa za wizi au upotevu wa fedha za umma mabilioni kwa mabilioni ambazo zingeweza kusaidia kuboresha maisha ya wananchi masikini vijijini na mijini"

  "Hatujaona hatua madhubuti zikichukuliwa dhidi ya hawa wanaohujumu taifa, maelezo kuwa serikali inashindwa kuwachukulia hatua kwa kukosekana ushahidi yanadhihirisha udhaifu wa vyombo vya serikali", aliongeza kusema.

  Akizungungumzi mgomo, Juma, alisema hadi ifikapo tarehe 4 mwezi huu kama hakutakuwa na makubaliano yoyote na serikali juu ya madai yao, ifikapo tarehe 5 Mei wafanyakazi wote nchi nzima wa sekta ya umma na binafsi watashiriki katika mgomo huo.

  Alieleza kuwa mgomo huo utafanyika kisheria kwa kuzingatia taratibu zote kama zinavyoelezwa kwenye kifungu cha 85 cha Sheria ya Ajira na Mhusiano Kazini namba 6 ya mwaka 2004 iliyopitishwa na Bunge.

  "Katika vikao vyote vya Tucta vya kitaifa vya kikatiba vimeamua na kupitisha uamuzi wa kutumia njia zingine mbadala za kisheria zitakazotuwezesha kufanikisha madai yetu na njia pekee iliyokubalika na Baraza Kuu la Tucta katika utekelezaji wa agizo la Mkutano Mkuu wa Kazi wa Oktoba 2009 ni kuitisha mgomo wa wafanyakazi wote nchini walioko katika sekta za umma na binafsi kwa sababu kwa namna moja ama nyingine wafanyakazi wote tunaguswa na matatizo haya", alisema.

  "Nafahamu katika hatua hii ya mgomo watakuwepo waoga, wanafiki na wasaliti, hawa tunapaswa kuwafahamu na kuwatenga ili lengo letu liweze kufanikiwa, wafanyakazi mtambue kuwa silaha yetu kuu ni umoja na mshikamano wetu tukikubali kugawanjwa tumekwisha, tusikubali mtu kuchezea umoja na mshikamano wetu huyo atakuwa adui yetu namba moja", alisisitiza.

  Awali, akisoma risala kwa niaba ya wafanyakazi, Kaimu Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholas Mgaya, alisema wafanyakazi wamefikia hatua ya kugoma baada ya kuona serikali imekuwa ikipuuza malalamiko yao kwa muda mrefu, huku wakiendelea kukabiliwa na hali ngumu ya maisha.

  Alisema katika kipindi cha zaidi ya miaka 14 iliyopita cha uongozi wa awamu ya tatu na nne vyama vya wafanyakazi kupitia Tucta vimekuwa vikiwasilisha kwa serikali hoja za kutaka kuboreshwa kwa mishahara ya wafanyakazi, kupunguza kodi ya mishahara na kurekebisha matatizo yaliyoko katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, lakini wamekuwa wakipuuzwa.

  "Matatizo haya tumekuwa tukiyawasilisha serikalini katika vikao mbalimbali kati ya Mheshimiwa Rais na viongozi wa vyama vya wafanyakazi na katika hotuba za wafanyakazi siku za sherehe za Mei Mosi kila mwaka, lakini hadi leo hayajapatikana mafanikio ya kuridhisha," alisema..

  Akielezea tofauti ya hali ya maisha ya miaka ya nyuma na sasa, Mgaya, alieleza kuwa miaka ya nyuma wafanyakazi walikuwa wakilipwa mishahara midogo lakini waliweza kuishi maisha mazuri tofauti na sasa.

  "Kipindi cha nyuma wakati nchi yetu ikifuata siasa ya ujamaa na kujitegemea huduma nyingi za jamii kama elimu na afya zilikuwa bure, lakini tangu tuanze kutekeleza sera ya kurekebisha uchumi na ubinafsishaji, ruzuku katika huduma za jamii ziliondolewa lakini bila ya kufanya marekebisho yoyote ya mishahara ili kumwezesha mfanyakazi kulipia mwenyewe huduma hizo muhimu" alifafanua.

  Alisema kuwa kutokana na hali hiyo Tucta inaitaka serikali ipandishe mshahara wa kima cha chini hadi kufikia Sh 315,000 kwa mwezi bila ya fedha hizo kukatwa kodi, ili wafanyakazi angau waweze kumudu hali ya maisha.

  Aliongeza kuwa Tucta pia inaitaka serikali ishushe kiwango cha asilimia cha kuanza kukata kodi ambacho kisizidi asillimia 9 kwa viwango vya mishahara yote.

  "Kitendo cha serikali kukata kodi bila ya kuzingatia ni msharaha upi unamwezesha mfanyakazi kumudu mahitaji muhimu ya maisha ni kitendo cha unyanyasaji na cha kumwongezea mfanyakazi mateso, serikali iache upendeleo kwani wafanyabiashara na wawekezaji wanatozwa kodi baada ya kuondoa gharama za uzalishaji na uendeshaji, sasa kwa nini mfanyakazi asikatwe kodi katika mshahara wake baada ya kuondoa gharama za mahitaji muhimu katika maisha kama chakula, nyumba, mavazi, elimu, matibabu, usafiri wa kwenda na kurudi kazini na akiba ya dharura?" alisema.

  Mgaya, alieleza kuwa wafanyakazi wanaamini kuwa kiwango hicho cha msharaha wa Sh 315,000 kwa mwezi kinaweza kulipwa endapo serikali itapunguza posho na huduma wanazolipiwa watumishi wa ngazi za juu, kupunguza misamaha ya kodi, kuzuia udanganyifu unaofanywa na wafanyaabiashara katika bei kwa bidhaa na huduma zinazouzwa nchi za nje kwa nia ya kukwepa kodi na kudhibiti mianya na matumizi mabaya ya fedha za serikali.

  Awali, kabla ya sherehe hizo kuanza, zilitanguliwa na maandamano ya wafanyakazi kutoka sekta ya umma na binafsi, huku wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali unaoelekezwa kwa serikali.

  Baadhi ya mambo hayo yalisomeka, Uchaguzi 2010 uwe ufumbuzi wa kero za wafanyakazi, Mshahara laki moja nauli, ada, chakula, kodi ya pango, matibabu na umeme- inawezekana?, Kodi ya mapato kwa wafanyakazi ipunguzwe na keki ya taifa igawanywe sawa.

  Mengine yalisomeka, Ongezeko la mishahara sekta binafsi ni danganya toto, maisha bora ni ongezeko la kodi ya mishahara ipunguzwe na ajira kwa wananchi ni haki siyo hisani kwanini kodi kubwa kwa wafanyakazi?.

  Pamoja na viongozi wa vyama mbalimbali vya wafanyakazi, sherehe hizo pia zilihudhuriwa na wanasiasa kadhaa wa vyama vya upinzania, akiwemo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, Katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi, Sam Ruhuza na Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Joran Bashange.

  Wakitoa maoni hayo mara baada ya sherehe hizo, viongozi hao waliunga mkono msimamo huo wa wafanyakazi, wakisema kuwa ni matokeo ya ukaidi wa serikali kutosikiliza matatizo ya wananchi wake na kuyapatia ufumbuzi.

  Dk. Slaa, alisema: "Naunga mkono wafanyakazi kwani majadiliano yanaposhindikana mgomo ni haki yao, serikali isipokuwa sikivu haya ndiyo matokeo yake na kinachouma zaidi wafanyakazi wanateseka serikali inaogelea kwenye dimbwi la anasa".

  Kwa upande wake, Bashange, alisema kuwa ni haki ya wafanyakazi kugoma kwani kwa muda mrefu wameachwa yatima, hawasikilizwi huku wakilipwa ujira mdogo usiolingana na hali ya maisha.

  Katika sherehe hizo hakualikwaa kiongozi yoyote wa ngazi ya juu wa serikali kuwa mgeni rasmi kama ilivyozoeleka na badala yake, Rais wa Tucta ndiye alikuwa mgeni rasmi.

  Akielezea hali hiyo, Ruhuza, alisema hatua hiyo ya Tucta ya kutoalika kiongozi yeyote wa serikali kuwa mgeni rasmi ni kama shirikisho hilo limezaliwa upya.

  "Serikali ni lazima itambue kuwa Tucta ni shirikisho linalojiendesha lenyewe si taasisi yake hivyo linahaki ya kupigania haki za wanachama wake bila ya kuingiliwa", alisema.

  Wakati hayo yakiendelea, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, amewataka wafanyakazi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kazi kudai haki na maslahi yao kabla hawajaingia kwenye mgomo.

  Lukuvi aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana alipokuwa akihutubia sherehe za sikukuu ya wafanyakazi kwa wanachama wa vyama 10 vya wafanyakazi mbavyo haviungi mkono mgomo uliotishwa na Tucta.

  Alisema njia pekee ya kupata suluhu pindi matatizo yanapoibuka sehemu za kazi ni mazungumzo kati ya waajiri na wafanyakazi na kwamba mgomo unapaswa kutumika kama silaha ya mwisho pindi mazungumzo yanaposhindikana.

  Lukuvi alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe hizo baada ya Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya, ambaye alialikwa kama mgeni wa heshima kutohudhuria.

  "Njia kuu ya kumaliza matatizo sehemu za kazi ni mazungumzo baina ya pande zote, nitamshangaa sana mfanyakazi au mwajiri atakayekataa kukaa kwenye meza ya mazungumzo...lakini mgomo ulioandaliwa kwa kufuata sheria na taratibu ni ruksa kabisa," alisema Lukuvi.

  Alisema hakuna mtu au kiongozi yeyote atakayeshangaa wafanyakazi wakidai maslahi kwa kuwa mishahara haitoshelezi mahitaji yao.

  "Hakuna anayesema mishahara ama posho mnazopata zinatosha...hakuna anayeshangaa wafanyakazi wanapogoma kudai maslahi bora," alisema.

  Alivipongeza vyama hivyo 10 kwa kuungana na kuwa chini ya mwavuli wa Fibuca ambao hata hivyo alieleza kwamba hakuwa anafahamu muungano huo.

  Awali, Kaimu Rais wa shirikisho hilo, Doscavu Vuhaula, alisema muungano wa vyama hivyo ulianzishwa Julai mwaka jana kwa kuunganisha wafanyakazi wa taasisi za kifedha yakiwemo mabenki, watafiti, biashara, viwanda vya usindikaji na maji.

  Nako huku Zanzibar, Rais Amani Abeid Karume, amesema serikali imeamua kufanya utafiti wa viwango vya mshahara ili kuwapunguzia ukali wa maisha wafanyakazi katika sekta ya umma na binafsi kushirikiana na Shirika la kazi Duniani (ILO).

  Akihutubia katika maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi jana katika ukumbi wa Bwawani hotel, Rais Karume amesema viwango vya mshahara vinavyotumika hivi sasa havilingani na mahitaji yake.

  Rais Karume, alisema Shirika la kazi Duniani tayari limeshateua mtaalamu atakayefanya kazi hiyo na ripoti ya utafiti wake iwe imekamilika kuanzia Juni mwaka huu.

  “Tayari serikali kwa kushirikiana na Shirika la kazi Duniani inaangalia utaratibu bora wa upandishaji mishahara,” alisema Rais Karume na kuibua shangwe kwa Wafanyakazi.

  Kuhusu watumishi wa umma alisema serikali inatayarisha mfumo mpya wa utumishi serikalini ambao utazingatia suala la kupandisha viwango vya mshahara na kuweka utaratibu mzuri wa uwajibikaji katika maeneo yao ya kazi.

  Alisema kwamba serikali kwa kushirikana na Benki ya Dunia (WB) inatayarisha mpango huo wa kupitia mfumo wa utumishi wa umma utakao saidia kuweka maslahi mazuri kwa watumishi wa serikali.

  Wafanyakazi Zanzibar wamekuwa wakilipwa mshahara wa kima cha chini shilingi 100,000 kutoka 80,000 baada ya serikali kupandisha kiwango hicho mwaka wa Fedha 2009/2010.

  Hata hivyo aliwataka Wafanyakazi kutumia Taasisi za Fedha na mifuko ya mikopo iliyoanzishwa ukiwemo mfuko wa mkopo ulioanzishwa na Rais Jakaya Kikwete, na yeye kuchangia kuitumia kuanzisha miradi ili kujiongezea kipato na kufanikisha Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini kwa Wananchi wa Zanzibar (MKUZA).

  Aidha, alisema serikali itaifanyia kazi ombi la kuongeza pesheni kwa wastaafu ili kuwapunguzia ukali wa maisha kwa vile tayari sekali imeshafanikiwa kujingea uwezo na kuweza kulipa mafao ya wastaafu na mishahara kwa muda muafaka.

  Alisema kwamba kutokana na udhibiti mzuri wa mapato ya serikali kuanzia mwaka 2005 hadi 2009 serikali imeweza kutumia sh. bilioni 26.2 kulipa mafao wastaafu 8,609.

  Mkoani Dodoma, Shirikisho la Wafanyakazi nchini (Tucta), mkoani humo, limeshutumu kitendo cha baadhi ya waajiri mkoani hapa kuwazuia wafanyakazi wao kushiriki katika sherehe za sikukuu ya wafanyakazi ya Mei Mosi.

  Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu wa Tucta mkoani hapa, Joseph Sayo, wakati akizungumza katika viwanja vya Jamuhuri mjini Dodoma jana.

  Aliwataja waajiri ambao wamewazuia wafanyakazi wao kuhudhuria katika sikukuu hiyo ni Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ofisi ya makao makuu Dodoma.

  “Katika mchakato wa kuandaa sherehe hizi tumekumbana na vikwazo vingi ambavyo vimesababisha baadhi ya waajiri kuwazuia wafanyakazi wao kufika katika sherehe hizi,” alisema.

  Hata hivyo, Sayo hakufafanua sababu iliyofanya kuzuiwa kwa wafanyakazi hao kushiriki katika sikukuu hiyo.

  Awali maandamano hayo yaliyopokelewa na Mjumbe wa Baraza Kuu la Tucta, Zuhura Luhonga, wafanyakazi walibeba mabango mbalimbali ya kudai haki zao.

  Katika sehemu kubwa ya ujumbe uliobebwa katika mabango hayo ni “uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi ni suluhisho la migogoro makazini, jasho tuvuje sisi, keki yote ta taifa wale wao, kwanini?

  Kutoka Arusha, Tucta imewataka wafanyakazi kuacha kuvumilia hali ngumu ya maisha badala yake watumie silaha yao ya mwisho ya kugoma ili kuishinikiza serikali na waajiri kuwapatia haki wanazostahili.

  “Tukikubali umoja wetu kuchezewa, tumekwisha,” alisema Mjumbe wa Tucta, kutoka makao makuu Dar es Salaam, Herizon Kaaya, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, yaliyofanyika jana kimkoa katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Karume.

  Katika kutekeleza azma hiyo, Tucta, imesema inatambua kwamba wapo baadhi ya wafanyakazi watakaoumia, watakaopoteza viungo na uwezekeno wa wengine kufa, lakini watashiriki mgomo huo kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

  “Haki haiwezi kuja kwa kuchekacheka tu…katika kutafuta haki kuna watu wataumia, watapoteza viungo na wengine wanaweza kufa, lakini tupo tayari kwa ajili ya vizazi vijavyo,” alisema.

  Kaaya alisema, Tucta, haina ugomvi na serikali, lakini imetangaza kuwepo kwa mgomo huo kwa kuwa serikali imeshindwa kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

  Alisema serikali inatakiwa kuongeza mishahara ya wafanyakazi, kupunguza kodi kubwa inayokatwa kwenye mishahara na kurekebisha mafao madogo wanayopata kutoka mifuko ya pensheni baada ya kustaafu.

  “Serikali haijachukua hatua madhubuti kuboresha maisha ya wafanyakazi kwa kuwalipa mishahara inayostahili na ndio maana waajiri wamekuwa na kiburi na hivyo kushindwa kuheshimu sheria za kazi,” alisema na kuongeza, “maisha ya wafanyakazi ni duni, na tunaadhimisha Mei Mosi katika hali ambayo si ya furaha, kwani tupo katika mgogoro na serikali wa kutaka haki zetu.”

  Alisema ni wajibu wa Tucta kuwaieleza serikali kwamba inakowapeleka siko na hawaridhiki.

  “Haturidhiki na hatua ambazo serikali inachukua za kuwaondelea kero wafanyakazi, hivyo ni wajibu wao kutumia silaha yao ya mwisho kisheria ya kufanya mgomo,” alisema.

  Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na maelfu ya wafanyakazi kutoka serikalini, sekta za umma na binafsi baada ya kushiriki maandamano ya watembea kwa miguu na maandamano ya magari.

  Mabango mengi yaliyobebwa na wafanyakazi hayo yalikuwa na ujumbe Uchaguzi mkuu wa 2010 utafute ufumbuzi wa kero za wafanyakazi.

  Maandamano hayo yaliwashirikisha wafanyakazi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Walimu, Hospitali ya Mkoa na Manispaa ya Arusha.

  Wengine ni Shirika la Hifadhi ya Wafanyakazi (NSSF), Benki Kuu ya Tanzania, Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Shirika la Simu Tanzania (TTCL), Shirika la Posta Tanzania, Tanapa, Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro, Veta, Sido na mashirika mengi ya watu binafsi.

  Mjini Morogoro, wafanyakazi nchini wametakiwa kuwa makini katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu kwa kuchagua viongozi bora wenye nia na moyo wa kutetea maslahi ya wafanyakazi ili kuleta tija kwa wafanyakazi nchi nzima.

  Wito huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi Raawu wanawake Taifa Asia Kapoyi wakati wa madhimisho ya siku ya wafanyakazi yaliyofanyika mkoani Morogoro ambapo alisema kuwa kwa kuchangua viongozi bora na sio bora viongozi wataweza kufikia malengo thabiti ya kupata haki zao kama wafanyakazi.

  Kapoyi ambaye pia ni mjumbe wa baraza kuu la shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tucta aliwataka wafanyakazi wote kuacha ushabiki wa vyama vya kisiasa na kuhakikisha wanachagua viongozi bora watakaowafaa katika kupigania maslahi yao sambamba na vyama vyao vya wafanyakazi.

  Akisisitizia kuhusu suala la mgomo wa wafanyakazi Mei 5, mwaka huu alisema kuwa wafanyakazi wote hawana budi kuitikia mgomo huo ikiwa muafaka baina ya Tucta na serikali haujafikiwa.

  Alisema kuwa wanachongoja ni kujua kama muafaka umekubaliwa kwa maana ya kupata haki zao za msingi wanazodai ikiwemo wafanyakazi wengi kuwa na kima cha chini cha mishahara, kukatwa kodi mbalimbali na pensheni ambazo zimekuwa zikiwasumbua wafanyakazi wengi.

  Kutoka Mbeya, Tucta imemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwawajibisha viongozi wa Serikali wa mikoa ambao wamewazuia wafanyakazi kuadhimisha sherehe za wafanyakazi katika mikoa yao.

  Akihutubia katika sherehe ya wafanyakazi maarufu kwa jina la Mei Mosi, zilizofanyika kimkoa katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokonne mjini Mbeya, Mjumbe wa Baraza la Tucta Taifa Joachim Masami ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema Shirikisho hilo linamtaka Rais Kikwete kuwachukulia hatua kali za kinidhamu viongozi hao, kama hakuwatuma kufanya hivyo.

  Alisema viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza wilaya na mikoa, kupiga marufuku sherehe za wafanyakazi katika mikoa yao si kitendo cha uungwana kwa sababu sherehe ya Mei Mosi ni sherehe ya dunia nzima na Serikali ya Tanzania imeridhia, hivyo akadai kuwa hana uhakika kama waliofanya hivyo wametumwa au ni kwa matakwa yao binafsi.

  Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Tucta wa Mkoa wa Mbeya, Alinanuswe Mwakapala alisema wafanyakazi wa Mkoa wa Mbeya wanalaani kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kufuta sherehe hizo mkoani humo.

  Alisema Tucta sio mara ya kwanza kutowaalika viongozi wa Serikali kuhudhuria sherehe za Mei Mosi kwani wakati wa Serikali ya awamu ya pili waliacha kumwalika aliyekuwa Rais Ali Hassan Mwinyi lakini sherehe zilifanyika kama kawaida.

  "Mwaka 1994 na 1995 hatukumualika Rais Ali Hasan Mwinyi, badala yake tukamwalika Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akahutubia, kwa hiyo hili tendo walilolionyesha Serikali limeonyesha kuwa awamu hii ya nne ni Serikali ya Visasi na sisi hatuwezi kukubaliana kabisa na visasi, maana hii wanatuchochea na kutujengea chuki wafanyakazi nchi nzima," alisema Mwakapala.

  Alisema vyama hivyo ni sawa na vya upinzani, ambavyo alidai kuwa huwenda vimeundwa na waajiri ili kudhoofisha nguvu za wafanyakazi.
   
 2. Rev. Kishoka

  Rev. Kishoka JF-Expert Member

  #2
  May 3, 2010
  Joined: Mar 7, 2006
  Messages: 4,470
  Likes Received: 277
  Trophy Points: 180
  Nashangaa sana kwa Vyama vya Upinzani kujivutavuta kuwa upande mmoja na Wafanyakazi wanaoandaa mgomo!
   
 3. Abdulhalim

  Abdulhalim JF-Expert Member

  #3
  May 3, 2010
  Joined: Jul 20, 2007
  Messages: 16,472
  Likes Received: 126
  Trophy Points: 160
  Tanzania hakuna pressure groups..lets face it mazee..kuna wachumia tumboni tu kila mahali.
   
 4. Nemesis

  Nemesis JF-Expert Member

  #4
  May 3, 2010
  Joined: Feb 13, 2008
  Messages: 3,833
  Likes Received: 1,089
  Trophy Points: 280
  Huyu mwandishi wa habari yupo biased au amekuwa influenced na bossi wake ili ku-discourage mgomo. Katika makala yake hajaandika chochote kinachofanya TUCTA kuwa chama cha siasa. Suala la kuhamasisha uchaguzi na kuwataka wafanyakazi kuchagua viongozi wanaoyajali maslahi ya wafanyakazi si kigezo cha TUCTA kuwa chama cha siasa. Poor media....
   
 5. andrewk

  andrewk JF-Expert Member

  #5
  May 3, 2010
  Joined: Apr 13, 2010
  Messages: 3,103
  Likes Received: 55
  Trophy Points: 145
  Huo ndio mkakati wa chama tawala kuwanunua wahalili, angalia coverage haikuwa ya kutosha kwenye magazeti yote ya jana,
   
 6. Mkaa Mweupe

  Mkaa Mweupe JF-Expert Member

  #6
  May 3, 2010
  Joined: Jun 29, 2007
  Messages: 654
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 35
  Uzandiki mtupu!

  Uhamasishaji ni sehemu ya uraia na wala si upinzani. Huyo jamaa alikuwa akitoa elimu ya uraia ila huyo mwandishi ni kilaza sana!
   
 7. K

  Kikambala Senior Member

  #7
  May 3, 2010
  Joined: Jun 28, 2008
  Messages: 163
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 35
  Nadhani ni mhariri wake ndie kilaza lakini tunalijua kampuni hii hata 1995 ilikuwepo na habari ya Rwanda kabla ya uchaguzi hatushangai
   
 8. Ochu

  Ochu JF-Expert Member

  #8
  May 3, 2010
  Joined: May 13, 2008
  Messages: 972
  Likes Received: 7
  Trophy Points: 35
  hata hivyo mtu kudai haki yakle ni upinzani?
   
 9. Power to the People

  Power to the People JF-Expert Member

  #9
  May 3, 2010
  Joined: Jul 11, 2007
  Messages: 1,193
  Likes Received: 238
  Trophy Points: 160
  ndio maana huyu mwandishi hakutaka kuandika jina lake, huu ni ujinga mtupu . so embarassing
   
 10. Kiby

  Kiby JF-Expert Member

  #10
  May 3, 2010
  Joined: Nov 16, 2009
  Messages: 5,202
  Likes Received: 1,007
  Trophy Points: 280
  .
  Kwa nini kichwa cha habari hakishahibiani na habari yenywe? Hapa ktk hii nipashe nahisi pana mkono wa Mengi. Makampuni yake ni mengi na anahisi wafanyakazi wakidai haki zao ipasavyo itakula kwake.
   
Loading...