TUCTA: Rais kadanganywa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

TUCTA: Rais kadanganywa

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Zak Malang, May 5, 2010.

 1. Zak Malang

  Zak Malang JF-Expert Member

  #1
  May 5, 2010
  Joined: Dec 30, 2008
  Messages: 5,410
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 0
  Rais kadanganywa

  * Watoa barua kuonyesha hawakuchelewa kikao


  MIEZI michache kabla ya Uchaguzi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete ameingia katika mgogoro mkubwa na wafanyakazi wanaodai amedanganywa na wasaidizi wake kwa kutumia baadhi ya taarifa zisizo sahihi katika hotuba yake kali ya kuwatuhumu aliyoitoa Jumatatu.

  Jana Jumanne, wafanyakazi walitangaza kuahirisha mgomo wao uliokuwa uanze leo, lakini wakasema wanashangazwa na kauli za vitisho na shutuma za Rais Kikwete walizodai zilitokana na yeye kutumia taarifa zisizo sahihi.

  Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUTCA), Omary Juma, alisema Rais Kikwete hakuwatendea haki wafanyakazi kwa kuwahukumu bila kuwasikiliza.

  Alisema Juma katika taarifa ya maandishi ya TUCTA : “Tunaomba wananchi watambue kuwa viongozi wa TUCTA hatukuwa waongo wala wanafiki. Rais pia hakututendea haki kwa kutuhukumu bila kutusikiliza, bali alitumia maelezo ya upande mmoja katika hotuba yake. Mfano barua ya Katibu Mkuu wa Hazina iliyotualika saa nane na nusu na wala si saa nne kama ilivyoeleza.

  “Katika nchi ya demokrasia na Utawala Bora kama Tanzania si vema Rais kuzungumza lugha ya vitisho na kutumia silaha za moto kwa wafanyakazi kwa jambo la kudai haki zao kisheria.”

  Katika hotuba yake hiyo iliyodumu kwa takriban saa moja na nusu juzi, Rais Kikwete, pamoja na mambo mengine, aliweka bayana kuwa viongozi wa TUCTA waliitwa kwenye kikao kwa ajili ya kuwasilisha mada kuhusu utozaji kodi kwa wafanyakazi na badala ya kufika saa nne kama walivyopaswa wao walifika saa nane.

  Lakini jana TUCTA katika mkitano uliofanyika katika Ofisi za Shirika la Kazi Duniani (ILO) Dar es Salaam walionyesha barua ya mwaliko inayotaja muda waliopaswa kufika kuwa ni saa nane na si saa nne kama alivyokuwa amesema Rais Kikwete juzi katika hotuba yake.

  Barua hiyo yenye kumbukumbu namba TYC/B/280/69 ya Aprili 22, 2010, ikiwa imeandikwa kutoka Wizara ya Fedha na Uchumi, ikiwa saini Shogholo Msangi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, inawaalika TUCTA kuhudhuria kikao hicho Aprili 23, 2010.

  Inasema barua hiyo: “Nimeagizwa nikualike tarehe 23/04/2010 saa 8:30 mchana ili uwasilishe mada yenye hoja ya Shirikisho la Wafanyakazi inayohusu kodi wanayotozwa wafanyakazi. Tunategemea ushirikiano wako katika suala hili.”

  Nakala ya barua hiyo ilitolewa kwa waandishi wa habari mara baada ya kukamilika kwa kikao cha uongozi wa TUCTA katika ofisi za ILO, Dar es Salaam.

  Aidha, katika hatua nyingine, TUCTA wanadai kuwa uamuzi wa Rais Kikwete kutangaza katika hotuba yake kuwa mgomo ni batili si jukumu lake kwa mujibu wa sheria namba sita ya mwaka 2004 na kwamba hiyo ni sawa na kuingilia uhuru wa Mahakama.

  “Tunasisitiza pia kuwa mamlaka sahihi ya kubatilisha mgomo kwa mujibu wa sheria namba sita ya mwaka 2004 ni Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi,” inaeleza taarifa ya TUCTA.

  Wakuzungumzia majadiliano ya kiwango cha mshahara, TUCTA walieleza kuwa Serikali iliwaita kwenye mazungumzo Machi mwaka huu, mazungumzo ambayo walifafanua kuwa yalikuwa yamepitwa na wakati kwa mujibu wa sheria ya majadiliano ya watumishi wa umma namba 19 ya mwaka 2003.

  Katika hotuba yake, Rais Kikwete aliwaita wafanyakazi wa TUCTA kuwa ni wanafiki na kuonyesha kuwa Serikali haina uwezo wa kulipa mishahara ya kima cha chini cha Sh 315,000 kama walivyopendekeza wao na kwamba bajeti ya kulipa mishahara hiyo inazidi mapato yanayokusanywa na serikali.

  Rais aliweka bayana pia kuwa TUCTA ilikubali kuendelea na mazungumzo Mei 8, mwaka huu na kwamba anashangazwa na uamuzi wao wa kuitisha mgomo ilihali wamekubali kuendelea na mazungumzo.

  Kutokana na hali hiyo, Rais Kikwete alionya wafanyakazi nchini kutogoma na kama wakigoma watawajibishwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za ajira na kuweka bayana kuwa yeye ndiye mwajiri mkuu kwa upande wa Serikali.

  Taarifa zilizotufikia tukienda mitamboni zilieleza kwamba kulikuwa na hofu miongoni mwa watendaji wa TUCTA na kwamba kulikuwa na uwezekano kwamba walikuwa wanatishwa.

  Lakini pamoja na hatua ya uongozi wa TUCTA kutangaza kuahirisha mgomo hali ya mambo ilikuwa tete jana kutokana na wafanyakazi mbalimbali kukasirishwa na kauli walizoziita za vitisho za Rais Kikwete.

  Baadhi ya wafanyakazi wakiwamo wa taasisi nyeti za Serikali walieleza kushangazwa na kusikitishwa na kauli ya Rais Kikwete, wakielezea kwamba ilijaa jazba na haikufaa kutolewa wakati huu.

  Katika kuonyesha hali si shwari, mkutano wa TUCTA na waandishi wa habari uliokuwa ufanyike jana katika ofisi za shirikisho hilo eneo la Mnazi Mmoja, ulihamishiwa katika jengo la ILO lililopo katikati ya jiji katika mazingira ya kutatanisha.

  Mbali ya viongozi wa TUCTA, kuna taarifa za kuwa baadhi ya watu mashuhuri wakiwamo wanasiasa na wanaharakati wameanza kufuatiliwa wakihofiwa kuchochea mgomo wa wafanyakazi kwa maslahi yao kisiasa.

  Mvutano baina ya Serikali na TUCTA ni wa muda mrefu ukilenga zaidi maslahi ya wafanyakazi ambayo TUCTA wanadai ni duni na mwaka huu mwanzoni uliongezwa makali kutokana na hatua ya TUCTA kutangaza kwamba safari hii Rais asingealikwa kama mgeni rasmi siku ya Mei Mosi.

  Mvutano huo ulionekana dhahiri Jumamosi ya Mei Mosi baada ya wafanyakazi kufanya sherehe mbili moja ikihudhuriwa na viongozi wa serikali nyingine ikihudhuriwa na viongozi wa Upinzani.

  Chanzo: Raia Mwema

   
 2. Zak Malang

  Zak Malang JF-Expert Member

  #2
  May 5, 2010
  Joined: Dec 30, 2008
  Messages: 5,410
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 0
  Liko la ziada la kulisema hapa? Yaani mbali na 'INATIA KINYAA?'
   
 3. jmushi1

  jmushi1 JF-Expert Member

  #3
  May 5, 2010
  Joined: Nov 2, 2007
  Messages: 17,569
  Likes Received: 1,935
  Trophy Points: 280
  Nadhani Mh Rais amekurupuka wapi shuka wakati tayari kwesha kucha.....Wapinzani wana nafasi ya "Kukaa vizuri" na wafanyakazi ili wachanganye kura za "kupewa" na zakwao,maana mh rais si alidai hataki kura?
   
 4. m

  macinkus JF-Expert Member

  #4
  May 6, 2010
  Joined: Sep 15, 2007
  Messages: 260
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 33
  “Nimeagizwa nikualike tarehe 23/04/2010 saa 8:30 mchana ili uwasilishe mada yenye hoja ya Shirikisho la Wafanyakazi inayohusu kodi wanayotozwa wafanyakazi. Tunategemea ushirikiano wako katika suala hili.”

  Mwenye nakala ya barua hii iliyotolewa na TUCTA kwa waandishi wa habari naomba aiweke picha yake hapa janvini

  macinkus
   
Loading...