Tuchape kazi - Diwani mwanamama wa CCM aonyesha mfano...

kbm

JF-Expert Member
Oct 5, 2012
5,222
1,670
“Kila mmoja akitimiza wajibu inawezekana. Maendeleo yatafika kwa kila mwanamke na Watanzania wote. Wanawake tuache fikra za utegemezi hasa kwa wananume, sasa tuwe wabia wao na siyo kusubiri watuletee. Vijana na wananchi wote tuwe na moyo wa kizalendo kwa taifa letu, tuchape kazi, kulala ni bahati, hakuna kulala.”
Hiyo ndiyo imani ya Sharifa Abebbe iliyobeba rai kwa Watanzania hasa wanawake.
Sharifa ni kiongozi wa kisiasa akiwa pia mkulima na mjasiriamali, anaanza maelezo yake kwa kutoa historia fupi ya maisha yake hadi kufikia alipo sasa.
Mwanamke huyu ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kwamgwe wilayani Handeni Mkoa wa Tanga alizaliwa mkoani Arusha takriban miaka 45 iliyopita na kusoma Shule ya Msingi Kaloleni na baadaye Arusha sekondari, kisha kozi ya kompyuta.
Anaeleza kuwa baada ya kuhitimu masomo yake alianzisha mradi wa saluni ya wanawake mkoani Arusha iliyojulikana kwa jina la Samia Saluni, huku akiwa tayari ameanza kujishughulisha na biashara ya madini ya Tanzanite tangu akiwa mdogo.
Mwaka 2002 alihamia jijini Dar es Salaam baada ya kuolewa, wakati huo pia akiendelea na biashara ya madini katika mkoa huo, Dodoma na Tanga na kuyasafirisha kwenda nchini Hong Kong.
Anasema kuwa mwaka 2008 aliamua kuacha biashara hiyo baada ya kuwaza atawezaje kuendelea kufanya kazi hiyo atakapokuwa mzee, au kupatwa na maradhi kwa kuwa kazi hiyo ni ya pilikapilika wakati wote.
“Nilifikiria tunapoelekea, umri unasonga. Niliona biashara ya madini ni ngumu na inahitaji kila wakati mtu uwepo , tofauti na shamba ukiwa na mazao ya kudumu kama embe au machungwa, ukifuga samaki au nyuki utaishi, siyo lazima uende kutafuta miguu yako, nikaamua kuwa mkulima,”anaeleza Sharifa.
Anafafanua: “Nimehamia shambani Handeni, Kijiji cha Kwadoya tangu mwaka 2009, huku nimepata ndugu zangu, kilimo kinaleta tija kuliko biashara ya madini. Sasa nalima mahindi, mbogamboga na matunda. Pia nimeanzisha mradi wa kuzalisha mbegu bora, nasambaza kwa wakulima wenzangu nikitoa pia elimu ya matumizi bora ya mbegu hizo.”
Maisha kijijini na siasa
Akizungumzia maisha yake kijijini na katika siasa, Sharifa anasema kuwa amekuwa akishirikiana na wanakiji wenzake katika mambo mbalimbali ya kijamii, hali iliyowafanya wazee katika Kata ya Kwamgwe kumwomba kuwania kiti cha udiwani katika uchaguzi mkuu mwaka 2010.
“Walipitia kwa mume wangu, wakaomba namba kisha kunipigia kuniomba nigombee udiwani, awalli nilikataa, nikashawishiwa kukubali, nikaafiki. Nilipita bila kupingwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwenye uchaguzi nilionja upinzani, lakini nilishinda kwa kura 1300, huku mgombea wa chama cha CUF aliyekuwa mwanamume alipata kura 300. Kwa uchaguzi ujao kama watapenda, nitaendelea kuwatumikia.”

Kuhusu mafanikio katika uongozi wake Sharifa anaeleza kuwa alipochaguliwa kuwa diwani kata hiyo haikuwa na shule ya sekondari, lakini kwa ushirikiano na wananchi wa kata hiyo wamefanikiwa kujenga sekondari na ofisi inayotarajiwa kufunguliwa mwakani, pamoja na vijiji vya kata hiyo kuwamo katika mpango wa kupata umeme katika mwaka ujao ili kuongeza kasi ya maendeleo.
“Pia tunajenga Zahanati Kwamgwe, Kwadoya tunajenga nyumba za madaktari, pia Shule ya Msingi Muungano sasa ina hadi darasa la tatu, Shule ya Msingi Mto Mchafu inajengwa. Tupo mbioni kununua trekta letu moja kubwa na moja ndogo. Kata yetu pia imefanikiwa kuchimba visima 15 kwa msaada wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), namshukuru Mungu pia nimewezesha kuwasaidia wanawake wenzangu kupata huduma za afya hasa za mama na mtoto, wauguzi wanakuja kila wiki Kwamgwe badala ya wananchi kufuata huduma umbali wa kilometa 25,” anaeleza Sharifa.
Anaongeza kuwa ndoto yake ni kuhakikisha anaondoa umaskini kwa wananchi wa Kata ya Kwamgwe kwa kutoa elimu kuhusu kilimo akiwashauri kilimo cha biashara hasa mazao ya alizeti, ufuta na mahindi.
“Nawapelekea mafanikio, binafsi nina kampuni ya mbegu bora, naitumia waione, waiamini nawashauri watumie mbegu bora, nawakopesha, nawalimia kwa trekta, wakivuna wanalipa, nimeleta wataalamu wa Vicoba kutoka Dar es Salaam, tumeanza kuwafundisha utengenezaji batiki, sabuni, chaki na usindikaji. Nia yangu kujikwamua kiuchumi, tuache kununua kwa wengine,” anasema Sharifa na kuongeza:
“Mtazamo wangu ni kwamba, wananchi wabadilike kila mmoja ajiweze kiuchumi, tusiwe tegemezi wala ombaomba. Tukijiweza, chuki fitina zitaondoka maendeleo yatakuja na hiyo ndiyo ndoto yangu.”
Sharifa ambaye ni mama wa familia anamshukuru mumewe John Sallu, familia yake, viongozi wote katika Kata ya Kwamgwe na madiwani wenzake huku akiwasihi vijana kufuata ushauri wa waliowatangulia kimaendeleo.

Chanzo: MCL
 
Kweli huyu mama ni wa mfano kabisa. Vijana ebu tufuate nyayo za huyu mama yetu wallahi tutatoka...
 
Back
Top Bottom