Tubadili Katiba tuulinde Muungano-2 | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tubadili Katiba tuulinde Muungano-2

Discussion in 'KATIBA Mpya' started by MziziMkavu, May 13, 2009.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  May 13, 2009
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,613
  Trophy Points: 280
  Kwa upande mwingine, katiba na sheria zetu zinakataza wananchi kuvunja Muungano, hii ikitafakariwa kwa kina inamaanisha hata kubadili mfumo wa muungano ulioko nk. Mathalani katiba inawataka viongozi wa kitaifa kula kiapo cha kuulinda Muungano kabla ya kuanza kazi yao aidha, sheria ya vyama vya siasa inakiondolea sifa ya kusajiliwa chama chochote cha siasa ambacho katiba yake au sera zake ni za kutaka kuvunja Muungano.

  Katika hali hii, ili kulinda muungano ni lazima hatua za haraka zikuchuliwe na umma kuhakikisha siri za muungano zinafichuliwa na katiba inabadilishwa ili kulinda Muungano.

  Ukichambua kwa kina utaona mapungufu mengi ya muungano yanatokana na matatizo ya kimaumbile ya toka wakati wa kuundwa kwa muungano.

  Hivyo suluhisho la kudumu ni kuusuka upya muungano kupitia katiba mpya. Hii iende sanjari na kuweka misingi madhubuti, wa wazi na wenye kutoa majibu. Katika hili ni ukweli ulio wazi kuwa hoja inayopigiwa upatu zaidi ni ya serikali kuwa na serikali ya shirikisho (ufiderali).

  Suala hili ni moja ya hoja muhimu za Sera ya Chadema ya Mfumo Mpya wa Utawala maarufu zaidi kama sera ya majimbo.

  Ripoti ya Tume ya Nyalali, imechambua vizuri hoja hii. Hata hivyo, upinzani wa hoja hii umejikita katika hofu juu ya kuvunjika kwa Muungano wakati wa mchakato wa katiba mpya ama kura ya maoni (referundum) hivyo wanajenga hoja kwamba Muungano unaweza kudumishwa katika muundo huu huu kwa kuchota uzoefu wa nchi za Skandinavia kama Finland na Denmark ambapo visiwa vyake kama Faroe, Aaaland na Greenland vinayo mamlaka yake katika maeneo mbalimbali ndani ys serikali ambazo si za shirikisho (kifiderali). Ama mfano wa Uingereza na Ireland ya Kaskazini.

  Lakini uzoefu wa kimataifa unaonyesha kwamba kuunda serikali ya shirikisho si kuvunja Muungano, ni kutengeneza muungano wenye kuweza kuridhiwa na kudumu zaidi.

  Kwa upande mwingine, liko ombwe kiuongozi na kitaasisi/kimifumo Zanzibar ambalo kwa ujumla wake linaelezwa kuzaa kile kinachoitwa mpasuko wa kisiasa.

  Sababu ya haraka inayotolewa ni kutokuwa na chaguzi huru na za haki ambazo huzaa migogoro na mivutano mara baada ya chaguzi.

  Suluhisho la muda mrefu linaloelezwa ni kuweka mazingira ya haki katika chaguzi na ushindani wa kisiasa, na daraja kuelekea hali hiyo inaelezwa kwamba ni kuunda serikali ya mseto chini ya kile kinachoelezwa kuwa ni ‘muafaka’.

  Hii inaelezwa kuwa ni muhimu katika kutibu majeraha ya kihistoria. Hata hivyo, ukifanya uchambuzi wa ndani hali inaonyesha kwamba marekebisho hayo pekee hayawezi kuweka misingi ya kuziba ombwe la kiuongozi/kimfumo katika sehemu ya Muungano yenye katiba na sheria ya Zanzibar.

  Ni katika hali hiyo, ndipo unaposikia vilio vya ubaguzi katika Zanzibar yenyewe; ambazo kwa kiasi zimeibua hata hoja ya Pemba kutaka iachiwe ijitawale ndani ya Muungano. Wakati huo huo, mfumo wa sasa wa Muungano hauruhusu kwa uwazi pande mbili za Muungano kutawaliwa na vyama tofauti. Kwa kuwa nchi ipo katika mfumo wa vyama vingi upo uwezekano wa vyama tofauti kushinda katika pande mbili. Hili likitokea patakuwa na matatizo ya kiutawala.

  Changamoto hizi haziwezi kukabiliwa na uchaguzi huru pekee, wala kuundwa kwa serikali ya mseto au ya umoja wa kitaifa. Haya ni mambo yanayohitaji mabadiliko katika mfumo wa utawala kama nilivyodokeza hapo juu. Ambayo pia yatahusisha mageuzi katika utamaduni wa kisiasa na mahusiano ya kijamii. Lakini yanapaswa kuhusisha pia marekebisho katika mfumo wetu wa uchaguzi na uwakilishi.

  Kwa sasa, Tanzania kwa ujumla inatumia mfumo wa uchaguzi wa ‘wengi wape’ ama ‘mshindi anachukua vyote’. Matokeo ya mfumo huu ni kuwa pamoja na vyama vya CUF na CCM kuwa na ushindani katika pande mbili za visiwa hivyo, kila kimoja kina uwakilishi wa upande wake pekee kutokana na ushindi.

  CUF inaongoza kisiwa cha Pemba, na ina jimbo moja tu la Mji Mkongwe kwa upande wa Unguja. Na CCM inaongoza unguja na haina jimbo hata moja huko Pemba.

  Hii ni kwa sababu, chini ya mfumo wa sasa, hata kama wagombea wote wa chama X Unguja wakipata wastani wa kura wa asilimia 45, wa chama Y wakapata asilimia 7 na chama Z asilimia 48; basi wabunge wote na wawakilishi wa upande wa Unguja watatoka chama Z pekee.

  Chama X na Y havitaambulia chochote pamoja na kuwa na wananchi takribani asilimia 52 wanaounga mkono vyama hivyo. Mfumo huu wa uchaguzi unaendeleza ufa na matabaka katika visiwa hivyo. Ndio maana Mwalimu Nyerere alifikia hatua ya kubashiri kwamba nje ya Muungano, hakuna Zanzibar alipofananisha dhambi ya ubaguzi na kula nyama ya mtu.

  Hata hivyo, kama kukiwa na mfumo wa uchaguzi wa mchanganyiko au mchanyato wenye uwakilishi wa uwiano; maana yake ni kwamba kura ambazo CUF itapata Unguja hata zinaweza kutafsiriwa kuwa viti vya ubunge na uwakilishi na kufanya chama hicho kiwe na wawakilishi na wabunge wengi toka Unguja.

  Kadhalika, kura ambazo CCM kwa kawaida huwa inaokoteza kwa upande wa Zanzibar, zinaweza kabisa kujumlishwa na kupata wabunge na wawakilishi wa upande Pemba na hivyo kupunguza mpasuko wa kisiasa.

  Kwa hiyo suala si kuwa na uchaguzi huru na haki pekee bali kuwa pia na mfumo wa uchaguzi ambapo kila kura itakuwa na thamani na kuwakilisha kikamilifu nguvu ya umma katika utawala na uongozi baada ya uchaguzi.

  Kadhalika kama sehemu ya kushughulikia mtanziko wa kisiasa kwa upande wa Zanzibar nakubaliana na tafakuri ya Hayati Profesa Abrahaman Babu kuhusu haja ya vyama mbadala vya kisiasa Zanzibar na pengine kuwa chama mbadala cha tatu (third party alternative) katika siasa za Zanzibar.

  Hii ni kwa sababu siasa za Zanzibar zinachochewa na mgawanyiko unaotokana na vyama viwili vya CUF na CCM. Hii inaelezwa pia na ripoti za waangalizi mbalimbali wa uchaguzi mathalani NORDEM.

  Inatajwa bayana kuwa ingawa Mwafaka umechangia kuleta mapatano ya muda mfupi, mwafaka huo huo kwa kujikita kwa vyama viwili pekee umeendelea kujenga ufa baina ya pande mbili. Kwa vyovyote vile nguvu ya tatu inahitajika katika siasa za visiwani. Hii ni kwa sababu siasa za Zanzibar na Muungano ni kama kuku na yai.

  Pamoja na udhaifu wa katiba za sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile Zanzibar, bado kuna mambo yangeweza kabisa kushughulikiwa. Mathalani, Utaratibu wa kuingiza mambo katika orodha ya Muungano uwe wazi na msingi wake uwe ni pande zote mbili kuridhia wakati wote. Pamoja na kuwa suala hili limewekewa misingi katika hati ya muungano na katiba, bado utekelezaji wake unaacha maswali. Hii itaondoa mgogoro mathalani unaofukuta hivi sasa ambapo

  Zanzibar inahoji ni vipi mafuta yaliingizwa katika orodha ya Muungano na dhahabu almasi kuachwa kuwa si masuala ya Muungano.

  Binafsi, nimeiona hati inayosemwa kuwa ni hati ya Muungano. Serikali haijawahi kuyakana maudhui ya hati hiyo, ingawa inasema si hati halisi ya Muungano.

  Wakati umefika wa kuunganisha nguvu ya umma ili kuitaka Serikali iweke wazi nakala halisi ya mkataba wa Muungano. Siri ya Muungano inapaswa kuwa ya Watanzania wote sio kikundi cha watawala wachache. Serikali itekeleze kikamilifu hati ya Muungano ikiwemo kuanzisha Mahakama ya Muungano ya Katiba.

  Pazia kubwa zaidi la usiri katika masuala ya Muungano lifunuliwe. Maamuzi ya kuhusu Muungano yalifanywa na wazee wetu, kwa kuzingatia mazingira ya wakati wao.

  Mataifa ya nje wanao utaratibu kati nchi zao wa kuweka wazi kwa umma, baada ya miaka fulani nyaraka ambazo zilikuwa zinahesabika kama ni siri kuu ya serikali (Top classified secret). Mathalani, tayari Marekani imeshaweka hadharani nyaraka za siri za taifa lao ikiwemo kuhusiana na ushiriki wao katika suala la Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar.

  Nyaraka hizo za wazi zinajumuisha ripoti, faksi na mazungumzo mengine ambayo yalifanyika wakati huo ikiwemo mambo ambayo yamefanywa na Shirika la Ujasusi la Marekani(CIA).

  Nimepitia na kutafakari kwa kina baadhi ya nyaraka hizo ambazo wamezitoa. Si lengo la makala haya kueleza kwa undani ambayo yametolewa hadharani, ila inatosha tu kusema kwamba Serikali ya Marekani imekiri wazi wazi kumshinikiza Mwalimu Nyerere na serikali yake ya wakati huo kutaka Tanganyika ijiunge na Zanzibar.

  Kati ya mawasiliano yalitolewa hadharani kuonyesha hali hiyo ni pamoja na ya Frank Carlucci, balozi wa Marekani nchini Zanzibar katika kipindi cha Muungano.

  Huyu baadaye alikuja kufukuzwa Zanzibar kutokana na shughuli za CIA katika visiwa hivyo, na baadaye alipanda cheo na kuwa mkurugenzi wa shirika hilo la kijasusi na hatimaye baadaye kuwa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo.

  Kwa kiasi kikubwa, Marekani ilihofia wakati huo wa vita vya baridi kukua kwa ukomonisti katika eneo la Afrika ya Mashariki kutokana na msimamo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya wakati huo. Kwa ujumla, Zanzibar ilionekana kama Cuba ya Afrika Mashariki, wakati Cuba ikilisumbua taifa hilo upande wa Amerika ya Kusini.

  Wakati umefika sasa na Tanzania kuweka wazi nyaraka zote za siri kwa upande wake, miaka 45 ya Muungano. Hususani nyaraka za takribani miaka 25 iliyopita za kati ya mwaka 1960 mpaka mwaka 1980 wakati wengine tulipozaliwa.

  Kuwekwa wazi (declassification) kwa baadhi ya siri hizi, ikiwemo zile zilizomo katika himaya ya Idara ya Usalama wa Taifa ni muhimu kwa mabadiliko katika nchi yetu. Ni lazima kizazi cha sasa cha watanzania kiwezeshwe kuyaelewa mazingira ya wakati huo na ya sasa; na kufanya maamuzi sahihi kuhusu mwelekeo wa Taifa.

  Nihitimishe salamu zangu za mshikamano kwa kutoa masuala na maswali ya kuchokoza mjadala. Mjadala kuhusu Muungano si suala la kufanywa katika Siku ya Maadhimisho pekee, ni hitaji endelevu mpaka pale tutakapokuwa na mfumo wa kiutawala unaokidhi kwa kiwango cha kutosha matakwa ya umma.

  Tujiulieze: Washiriki wa Muungano ni kina nani? Wako wapi? Wanawakilishwa vipi? Wanamamlaka gani? Tuhoji: Mambo ya Muungano ni yapi? Kwa nini? mipaka ya upatikanaji wake ni ipi?yanaheshimiwa?

  Tudadisi: Mzanzibar ni nani? Mtanzania bara ni nani? Nini athari za sifa zao kwa mahusiano na madaraka? Tutafakari: Tanzania ni nchi ya chumi ngapi?

  Hili linaathari gani kwa Muungano? Mwalimu Nyerere, katika Kitabu chake cha Uongozi wetu na Hatma ya Tanzania, pamoja na kutetea muundo wa sasa wa Muungano anakiri kwamba umma wa watanzania unayo kabisa ridhaa ya kuufanyia mabadiliko Muungano.

  Tofauti yake na wabunge wa CCM wa wakati huo ilikuwa ni katika mchakato tu wa kutimiza azma hiyo. Wakati huo, alieleza wazi kwamba kile walichokuwa wakikisimamia hakikuwemo katika ilani ya wakati huo waliochaguliwa nayo.

  Akawataka kama wanataka mabadiliko katika Muungano basi wajiuzulu, na nchi iende katika uchaguzi. Wananchi wakichagua mabadiliko hayo, basi hiyo ndio itakuwa msingi wa kuusuka upya Muundo wa Muungano.

  Hivyo, mabadiliko katika Muungano wetu yanawezekana, na sehemu muhimu ya kuanzia ni kupitia uchaguzi. Kwa mantiki hiyo basi, siri zifichuliwe, tuchague viongozi bora, tubadili katiba ili tulinde Muungano wetu. Umoja ni Nguvu, utengano ni udhaifu.
   
 2. P

  Pakacha JF-Expert Member

  #2
  May 13, 2009
  Joined: Apr 15, 2008
  Messages: 816
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  Fedaralism gani hiyo unayoitaka ndugu yangu katika mfano wa Tanzania. Hebu angalia ukubwa wa Tanganyika na udogo wa Zanzibar-Hivyo kweli kutakuwa na federalism hapo? Kama muungano huu wa hivi sasa umechukua miaka 45 (na tunaona mfumo wa serikali mbili haufai) na hakika federalism haitochukua hata muhula mmoja wa miaka mitano. Bara (Tanganyika) watakuwa wameuchoka na Zanzibar hali kadhalika. Usiumize kichwa chako bure ndugu yangu tatizo la Muungano wetu sio mfumo , bali ni utekelezaji wa mfumo wenyewe. sasa ugumu wa kutekeleza sijui uko wapi. kwani wote walio Tanganyika na walio Zanzibar hawautekelezi mfumo huu ( Serikali Mbili) sawa sawa. Na hii imekuwa ikifanyika tokea wakati wa mwenyewe muasisi (Mwalimu Nyerere). Sasa kwa nini ilikuwa hivyo na kwa nini iko hivyo hadi hivi sasa nafikiri ni vitu vya kutafakari. Kuukoa Muungano ni kuukubali kwa dhati mfumo wa serikali mbili na kuutekeleza ipasavyo bila ya ubabaishaji.
   
 3. SaidSabke

  SaidSabke JF-Expert Member

  #3
  May 13, 2009
  Joined: Sep 28, 2006
  Messages: 1,968
  Likes Received: 222
  Trophy Points: 160
  Ni kweli Pakacha unavyosema ni kweli muungano wa nchi nyingi hutokana na historia zao kuiga hautadumu.tatizo hapa kwetu ni kushindwa kutekeleza yale yanayotakiwa.wala si mfumo.kaka nakwambia nje ya mfumo wa sasa basi tujitayarishe kusema byebye muungano
   
Loading...