Tuanze maandalizi ya kuinusuru Tanzania isije ikawa kama Zimbambwe

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,792
287,994
Posted Date::5/5/2008
Tuanze maandalizi ya kuinusuru Tanzania isije ikawa kama Zimbambwe
Na Elias Msuya
Mwananchi

KWA hakika sasa hakuna ubishi kwamba hali ya maisha ya Zimbabwe imekuwa mbaya sana. Tangu Rais Robert Mugabe alipowafukuza wazungu na kuwanyang'anya mashamba, hali iligeuka ghafla.

Ni kweli Rais Mugabe alikuwa na sababu za msingi za kufanya hivyo, hasa kwa kuwa lengo la kuikomboa nchi yake lilikuwa ni kuwapa ardhi wananchi wake na siyo kuwaachia wazungu wachache.

Lakini Rais Mugabe amekuwa akitumia sera hiyo kuwa kama fimbo ya kuwachapia wapinzani wake kisiasa. Kwamba kwa kuwa yeye alipigana vita vya msituni basi anastahili kutawala milele na kamwe mtu yeyote ambaye hakupigana vita vya msituni hana sifa ya kuiongoza Zimbabwe.

Kwa maneno mengine ni kwamba Mugabe hana jipya la kuwaeleza Wazimbabwe isipokuwa vita vya msituni vilivyoikomboa Zimbabwe miaka 28 iliyopita.

Katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa kuadhimisha miaka 28 ya uhuru, Rais Mugabe aliilaumu Uingereza ambayo ndiyo iliyoitawala Zimbabwe kwamba imekuwa ikihujumu uchumi wa Zimbabwe tangu alipowapokonya wazungu ardhi. Rais Mugabe amekuwa akidai kwamba chama cha upinzani cha MDC kinafadhiliwa na Uingereza ili kuuhujumu utawala wake.

Na kwa kuwa Morgan Tsvangirai ambaye ni mwenyekiti wa MDC hakupigana vita vya msituni kuikomboa Zimbabwe, basi anaonekana kama kibaraka wa Wazungu (Waingereza) anayetaka kuirudisha Zimbabwe kwenye ukoloni.

Umaarufu wa Tsivangirai ulitokana na kuwa kiongozi wa muungano wa vyama vya Wafanyakazi ambao baadaye uligeuka kuwa chama cha upinzani baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi.

Pamoja na kwamba Mugabe na chama chake cha ZANU PF waliikomboa Zimbabwe kutoka kwenye makucha ya mkoloni, wameshindwa kuwaletea maendeleo Wazimbabwe. Hali ya kiuchumi haitamaniki, kwani sasa mfumuko wa bei umefikia asilimia 165,000, huku asilimia 80 ya wakazi wake hawana ajira. Kutokana na matatizo hayo nusu ya wananchi wa Zimbabwe wanaishi uhamishoni.

Pamoja na hali hii mbaya ikiwemo njaa kali inayoikumba Zimbabwe, bado Rais Mugabe anadiriki kuagiza shehena ya silaha kutoka China. Kwa bahati nchi zote za Afrika zilizo na bandari zilikataa kushusha silaha hizo kwa kuhofia kutokea machafuko Zimbabwe na hatimaye meli hiyo kurudisha mzigo huo ulikotoka.

Isitoshe Rais Mugabe na washirika wake wanaishi maisha ya anasa bila kujali taabu wanayopata Wazimbabwe wengi.

Kwa Wazimbabwe maana halisi ya uhuru haionekani kwa kuwa hawaoni faida ya kuwa huru wakati hali ya maisha ni mbaya kupita kiasi.

Pamoja na kuwa tume ya uchaguzi imetangaza kurudiwa kwa uchaguzi, baada ya matokeo kuonyesha kwamba hakuna ambaye alipata kura za kumwezesha kuunda serikali, lakini hali ilionyesha kwamba Tume ilitamani kumtangaza Mugabe kuwa mshindi lakini maji yalikuwa yamewafika kooni.

Bahati mbaya ni kwamba viongozi wengi walioko madarakani wanatamani waendelee kutawala daima, mwanzo Waafrika walipambana na mfumo wa kikoloni na kifalme lakini viongozi walioshika madaraka baada ya uhuru wengi wao wanatamani nao wawe wafalme watawale milele. Wanasahau kwamba kilichokuwa kinatafutwa baada ya uhuru ni maisha bora kwa wananchi na siyo utukufu kwao.

Wanachofanya ni kujilimbikizia mali wao na marafiki zao, kutawala kwa mabavu na mwishowe hugeuka kuwa madikteta.

Katika Afrika ya leo, wapo viongozi kama Mugabe, na pia vipo vyama vinavyotumia kupatikana kwa uhuru kama kisingizio cha kutawala milele. Vyama hivi vimekuwa vikituaminisha kwamba mchawi wa matatizo ya Afrika ni wakoloni pekee. Wanasahau upande wa pili kwamba, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na fedha za serikali nalo ni tatizo.

Kwa mfano hapa Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM), tangu tumepata uhuru kinaendelea kutoa ahadi hewa za maendeleo wakati maendeleo halisi hayaonekani. Chama hiki kilichozaliwa kutokana na muungano wa TANU na ASP vilivyopigania uhuru wa nchi yetu, ingawa kilifanya kazi yake nzuri ya kuleta ukombozi, sasa kimepoteza mwelekeo wake.

Viongozi wake wamelewa madaraka, wanafanya watakavyo, hakuna wa kuwawajibisha. Kwa kweli tunakoelekea Watanzania, ndipo walipo Wazimbabwe.

Lakini tukumbuke kwamba Wazimbabwe hawakuamka tu asubuhi na kukuta nchi imeshakuwa mbaya. Hali ya Zimbabwe ilibadilika hatua wa hatua mpaka kufikia hapo ilipo. Alichofanya Mugabe ni kuwalisha kasumba Wazimbabwe kwamba maendeleo yatapatikana kwa kuipa nafasi ZANU PF itawale milele. Leo wanakuja kushtuka kumbe Mugabe waliye mwendekeza sasa amegeuka dikteta.

Hivyo ndivyo CCM inavyowalisha kasumba Watanzania kwamba ili nchi iendelee kuwa na amani ni lazima waichague CCM. Katika uchaguzi mdogo uliofanyika jimbo la Kiteto baada ya mbunge wa awali kufariki, CCM ilidiriki kutumia picha za machafuko ya Kenya ili kuwarubuni wapiga kura, kwamba wakichagua upinzani kutatokea machafuko! Huku ni kufilisika kisiasa. Ni kufilisika kwa sababu CCM siyo alfa wala omega, kuna siku mwisho wake utafika ipende isipende.

Nchi yetu sasa inaelekea kubaya hatua kwa hatua. Tusipochukua hatua mapema hakika tutajikuta yametukuta ya Wazimbabwe. Mathalani tukiangalia mfumuko wa bei ambao Rais Kikwete aliukuta ukiwa asilimia 4, leo ni miaka miwili tu umepanda hadi asilimia 10. Kwa mwendo huu ikipita miaka mitano hali itakuwaje? Na kama Rais Kikwete ataendelea kuwa madarakani kwa miaka kumi mfululizo, hali itakuwaje?

Hali za maisha za Watanzania bado hazijaboreka licha ya ahadi nyingi za maisha bora kwa kila Mtanzania. Wengi wameendelea kukosa kazi, na hata hao walioko kazini mishahara haitoshelezi.

Kwa miaka miwili na ushei tangu awamu ya nne ianze, bei za bidhaa zimepanda maradufu. Mathalani bei ya mafuta, saruji na vyakula zimepanda sana. Wakati haya yakiendelea viongozi wa CCM wanazidi kujionyesha 'live' jinsi walivyo mahiri wa kula rushwa. Wameingia mikataba mibovu na sasa tunataabika kwa maisha magumu. Wametafuna fedha za nchi hii mpaka wengine wamezihamishia nje ya nchi.

Tuhuma za rushwa na ufisadi zimeshtadi kwa viongozi wa serikali lakini wananchi bado hawajaridhishwa na kasi ya Rais Kikwete ya kuisafisha serikali yake. Kasi hii ya konokono katika kushughulikia kashfa za ufisadi inatia mashaka. Hivyo ndio kusema kwamba serikali ya CCM inafanya yale yale yanayofanywa na ZANU PF.

Katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni huko Zimbabwe, Wazimbabwe walionyesha japo hasira zao kwa kumkataa Mugabe. Japo matokeo ya urais yameonyesha kukaribiana kwa kura baina ya Tsvangirai na Mugabe, lakini chama cha upinzani MDC kimeshapata ushindi mkubwa wa viti bungeni. Lakini hatua hii ya Wazimbabwe imechelewa sana. Kama wangelijua mapema wasingejiingiza kwenye ntego uliowanasa sasa hivi.

Tunapowatazama Wazimbabwe tunapata somo kwamba Serikali dhalimu huwekwa na wananchi wenyewe kwa kupumbazwa na propaganda. Tunaweza kabisa kuilaumu serikali kwa matatizo mbalimbali yanayotupata, lakini tujue sisi ndiyo tuliowaweka madarakani watawala wabovu.

Ni vema sasa tujifunze kutoka kwa wenzetu mapema, kama Waswahili wasemavyo 'mwenzako akinyolewa, tia maji nywele zako.'Tusisubiri Nchi yetu ije kuwa kama Zimbabwe, tuanze mapema maandalizi ya kuinusuru!

Baruapepe: emsuya2001@yahoo.com

Simu:0754 897 287
 
Hii ni posti ya siku nyingi sana! Ila kwa uliyoyaeleza ni kana kwamba ya wakati huu, watanzania tulio wengi ni wagumu wa kuelewa! na ni wepesi wa kusahau, kila siku ni afadhali ya jana! Haya ulitueleza nyakati hizo za awamu hiyo ya nne na sasa kwenye hii awamu ya tano ni moto wa kuotea mbali, Jiwe ni mgumu zaidi ya R. Mugabe, sasa kibarua tunacho.NAUNGA MKONO HOJA KWA 100%
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom