Tuajiri rais wa kigeni aikomboe tanzania | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tuajiri rais wa kigeni aikomboe tanzania

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Mpiganaji tz, Sep 25, 2010.

 1. Mpiganaji tz

  Mpiganaji tz Member

  #1
  Sep 25, 2010
  Joined: Jul 22, 2010
  Messages: 21
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  TUAJIRI RAIS WA KIGENI AIKOMBOE TANZANIA
  Inashangaza kuona taifa letu likiendelea kudorola kiuchumi lakini hakuna anayejali! Nchi imeelemewa na mzigo wa viongozi wenye upeo duni wa kufikiri, wanafiki, wababe, mafisadi, na wabinafsi. Wanakumbatia mambo ya hovyohovyo ilimradi tu maslahi yao binafsi yanatimia. Ufisadi umekuwa fasheni na utamaduni kwa kila mwenye madaraka. Kwasababu ya ufisadi wao afya zetu zipo hatarini kwani wanaachia madawa bandia ya binadamu, vyakula na bidhaa nyingine bandia kufurika nchini ili hali wana uwezo wa kutokomeza uozo huo. Kila kukicha tunashuhudia maamuzi ya hovyohovyo sambamba na kusainiwa mikataba ya kipuuzi na yenye kulitia taifa aibu na gharama kubwa huku watanzania walio wengi wakiendelea kutaabika kiuchumi.

  Tumekosa viongozi wenye dhamira ya kweli ya kutusaidia tuweze kupiga hatua kielimu, kiafya na kiuchumi. Huu umaskini unaolikabili taifa kwasasa ungeweza kupatiwa ufumbuzi kwa muda mfupi lakini kwa vile hakuna kiongozi mwenye nia hiyo toka moyoni mwake watanzania tunazidi kupigika huku wateule wachache wakiendelea kula kuku kwa kodi tunazolipa na kwa kuuza rasilimali za nchi. Tanzania imekosa kitu chochote cha kujivunia mbele ya mataifa mengine hata yale ya Afrika Mashariki! Viongozi wetu wakiulizwa tuna nini cha kujivunia wanakwambia eti amani. Sidhani kama hawa viongozi wanajua maana hasa ya neno amani. Amani ipi wakati watanzania kibao wanalala njaa kila siku? Amani gani wakati kila siku walemavu wa ngozi wananyofolewa viungo vya miili yao na wengine kuuawa? Amani ipi wakati wenzetu wa kule Kigoma, Kagera, Mara na kwingineko kila kukicha wanavamiwa, kupigwa na kuporwa mifugo na mali zao na wavamizi kutoka nchi jirani?

  Viongozi tuliowategemea kulisaidia taifa wamegeuka vioja. Wanatumia muda mwingi kujisifia kuwa wameleta maendeleo makubwa katika jamii! Wanapenda wasifiwe pasipo sababu, hawataki kuambiwa ukweli wala kukosolewa! Wandishi wa habari wakiripoti kuhusu kero na shida zinazowakumba wanetu mashuleni kama vile uhaba wa vyoo wanakamatwa na kuswekwa mahabusu! Kila apandaye jukwaani anasifia ujio wa shule za kata. Wanadhani hatujui kuwa shule hizo zimejengwa kwa nguvu za wananchi? Kwanza shule zenyewe hazina sifa ya kuitwa shule! Unakuta shule ina wanafunzi mia tano lakini ina mwalimu mmoja, haina kitabu hata kimoja na watoto wanakaa mavumbini! Tena naomba wakome kuziita shule, ni bora zikaitwa vituo vya watoto wa walalahoi kupotezea muda.

  Hakuna kiongozi mwenye azma ya kweli kuboresha elimu hapa nchini. Bila elimu ya maana maendeleo yatakujaje? Watanzania watajinasua vipi kutoka lindi la umaskini? Tutashindana vipi katika soko la Afrika Mashariki? Nashawishika kuamini kuwa hawa viongozi wetu wana mkakati wa maksudi kuhakikisha kuwa watanzania hawapati elimu ya maana ili waendelee kuwa rahisi kudanganyika kwani wakielimika hawatakuwa tayari kudanganyika kirahisi kama ilivyo sasa, badala yake wataamka na kudai fursa za kuajiriwa na kupatiwa mazingira mazuri ya wao kujiajiri, afya bora, elimu ya maana kwa watoto wao nk. Hivi karibuni wabongo wakaambiwa watapatiwa maeneo maalumu, mikopo na zana bora wachimbe madini, bila kujua kuwa hiyo ni longolongo wakashangilia ahadi hiyo! Sasa subirini uchaguzi upite mtakiona cha moto. Kwasasa mwaitwa wachimbaji wadogowadogo, baada ya uchaguzi mtaitwa wachimbaji haramu na hamtaruhusiwa kuchimba hata kokoto achilia mbali dhahabu!

  Hivi majuzi tumesikia wakiahidi wanafunzi wa vyuo vikuu eti wakifungua vyuo mwezi Novemba watakuta matatizo yao ya muda mrefu yametatuliwa! Kwanini hiyo ahadi ije wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu? Hizi ni longolongo za wazi, wajinga ndio waliwao, na hapa ndipo wenye akili zetu tunasema hakuna kiongozi katika serikali ya sasa mwenye nia ya dhati ya kumkomboa mtanzania maskini. Hebu fikiria serikali kukosa sh. milioni tisa za kuleta maji Geita tangia mwaka 2005 hadi wamekuja kusaidiwa na kampuni ya kuchimba madini! Serikali inakosa milioni tisa kwa takriban miaka mitano, hiyo miradi mingine ya mabilioni itakuwaje? Wengine tu mbayuwayu tuna akili zetu, Oktoba 31 tutafanya kweli.

  Umasikini ni umasikini lakini umaskini wa maarifa ni balaa. Zamani nilikuwa nachukia tulipoambiwa watanzania ni wafu, na tuna akili baridi, kwasasa sichukii kwani naona kuna ukweli katika hilo! Hebu fikiria mgombea urais anasimama jukwaani na kuwaomba watanzania wamchague mtu ambaye anatuhumiwa na amefunguliwa mashitaka ya kukwapua mamilioni ya kodi tunazokamuliwa, badala ya wananchi kuona kinyaa wakashangilia kama mazuzu!! Hawa mafisadi wakiwa wanahutubia longolongo zao majukwaani unakuta watanzania wanashangilia wakidhihirisha kuwa hawajui watokako wala waendako ilimradi jua likitoka wanaamka likizama wanalala basi!! Ukikuta mtanzania mwenye elimu na upeo wa kutosha anashangilia hotuba za mafisadi basi ujue kuwa ni rafiki au jamaa wa karibu wa mafisadi na anafaidika na ufisadi huo kwa njia moja ama nyingine. Kama unabisha tembelea mkutano wowote wa kampeni za mafisadi angalia wale wanaoshangilia kwa nguvu huku wamejipamba rangi za chama hicho waulize kuhusu elimu yao watakwambia wazazi wao walikosa ada hivyo wakaishia darasa la pili, nne au la saba na pengine hata hawajui kuandika wala kusoma!

  Inauma kuona taifa linapata hasara mara mbili. Kwanza ni ile ya kuwasomesha hawa viongozi tulionao bure pasipo kulipa chochote na hata wengi wao wamesomeshwa nje ya nchi kwa jasho la mlipakodi ili waje kusaidia kulijenga taifa letu pendwa lakini imekuwa tofauti! Hawa jamaa wameamua kuliingiza taifa katika gharama za mara ya pili kwa kuendelea kusaini mikataba mibovu, ya kipuuzi na ya kuliingiza taifa katika aibu na hasara kubwa. Wanasaini mikataba ambayo mtu huwezi amini kama viongozi hao wamewahi kwenda shule! Viongozi wa kitaifa wanaongea upuuzi majukwaani hadi mtu mwenye akili timamu unashindwa kuamini kama wamewahikwenda shule. Wanadai haiwezekani walalahoi kusoma vyuo vikuu bila kulipia, je, mbona wao walisomeshwa bure na mwalimu Nyerere? Kama kipindi hicho iliwezekana kwanini na sasa isiwezekane?

  Wanajigamba majukwaani kuwa wametatua kero nyingi za watanzania, ni kero zipi hizo? Je, wamemaliza adha ya msongamano wa magari katika majiji kama vile jijini DSM, Arusha, Mwanza nk? Je, wamezuia vyakula, madawa ya binadamu, na bidhaa nyingine bandia zinazo hatarisha maisha ya watanzania kuingia nchini? Je, wamedhibiti uchakachuaji wa mafuta ya petroli achilia mbali bei yake inayopaa kila dakika na kufanya nauli kupanda na maisha kuwa magumu? Je, Wamezuia mgambo kuwanyanyasa wafanyabiashara ndogondogo? Je, wamedhibiti wizi wa vifaa vya magari bandarini? Je, wameshusha bei ya sementi, mabati na pembejeo za kilimo ili watanzania wote wapate kuzimudu? Je, wameacha wakulima wauze mazao yao popote wanapoona pana bei nzuri kuliko wanavyowazuia sasa na hali serikali haina uwezo wa kununua mazao hayo? Je, wamezipatia zahanati zote za vijijini magari ya kubebea wagonjwa au bado wagonjwa wanabebwa kwenye baiskeli na mikokoteni? Je, watoto wote wa walalahoi wanapatiwa mikopo ya vyuo vikuu kulingana na mahitaji yao na kwa wakati? Je, polisi wamepatiwa nyumba za maana za kuishi na familia zao? Walimu je? Je, hospitali za serikali zimepatiwa madawa na vitanda vya kutosha? Je, wamezuia wawekezaji wa kigeni kuwanyanyasa raia? Je, rushwa mahakamani, polisi, na hospitalini imekomeshwa? Je, wamewalipa wastafu wa jumuiya ya Afrika Mashariki mafao yao? Je, wastafu wengine wanaosulubika pasipo kulipwa viinua mgongo vyao? Kama haya yote yamewashinda, kero walizotatua ni zipi?

  Hali ya mambo katika serikali hii ya CCM inadhihirisha kuwa hatuna mtanzania mwenye uwezo wa kuwa rais katika nchi hii! Urais si lelemama wala sio sawa na kuongoza kikundi cha ngoma za mchiliku, mnanda ama mdundiko, urais wahitaji mtu shupavu jasiri na makini. Hebu fikiria serikali ya chama tawala imekosa mtanzania mwenye sifa ya kuwa rais wa hospitali ya Muhimbili tukaenda kutafuta mzungu, tukakosa mtanzania wa kuwa meneja Tanesco tukaenda kuazima Afrika ya Kusini, tumekosa walimu wa michezo tumeenda kukodi watu wa nje, tumekosa mameneja wa kuongoza makampuni mbalimbali hapa nchini tumeajiri wenzetu wakenya, mahausi geli wa kutumika masaki na Oyster bay tumesaidiwa na Malawi, sembuse urais wa nchi? Na hivi majuzi tumeambiwa serikali imeomba walimu toka Marekani waje kufundisha shule za sekondari hapa nchini. Aibu gani hii?! Yaani taifa linashindwa hata kuzalisha walimu wa kufundisha sekondari tunaomba msaada toka Marekani?!

  Kwa mtaji huu tumekwisha! Kama tutashindwa kutafuta rais kutoka nje ya chama tawala ni bora tutafute mjapani au mchina makini aje tumpe urais atunyoshee mambo. Tukipata rais wa kigeni naamini hatamwangalia nyani usoni, atawanyonga mafisadi wote, pesa tunazokamuliwa kulipia kodi hazitaenda kununulia magari ya kifahari, ndege mbovu wala samani za mamilioni za maofisini na majumbani kila mwaka ilihali hatujui zinakopelekwa samani zilizochakaa! Rais wa kigeni ataboresha miundombinu, longolongo na adha za reli ya kati zitakomeshwa, atawainua wakulima kikwelikweli na sio longolongo za majukwaani, sementi na bati zitauzwa kwa sh.5,000/=, atawathamini wafanyakazi atawalipa mishahara minono, ataboresha elimu na atatuwezesha wazalendo kuwa na viwanda, hata kama tutakosa kuwa na viwanda vya teknolojia ya hali ya juu lakini tutamudu japo kufuta aibu ya kuagiza hata vijiti vya kutolea nyama kwenye meno (tooth picks) toka China!

  Mungu ibariki Tanzania
  Mpiganaji Mzalendo


   
 2. J

  Jembejipya Member

  #2
  Sep 25, 2010
  Joined: Sep 23, 2010
  Messages: 8
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Maendeleo ni mabadiliko kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine au Lenin alisema two steps forward and one step backward, na hayo mabadiliko huchukua sura nyingi (phases) kama vile nyanja ya siasa,uchumi,jamii, na kadhalika. Aliyekuwepo Tanzania 1885 wakati wa Berlin conference ataona ni tofauti na Tanzania ya 1961 na aliyekuwepo muda huo na leo ambapo mtanzania anatoka kwa teksi Mwanza hadi Dar es salaam ni miujiza.


  Ebu nenda kwenye Elimu 1961 Tanzania ilikuwa na graduates wangapi katika fani ya Sheria, Uhandisi, Ualimu , Uhuasibu nk. Leo hali bi tofauti kabisa wasom,i ni wengi ebu nenda kwnye nyanja ya kidini 1961 hata Mungu wako ulikuwa humjui leo ukimkosa ni kiburi chako tu. Hiyo ni mifano michache, hayo yote yamefanywa na Baba wa Taifa Mwalimu JK Nyerere, Alhaji Ali hassan Mwinyi, Mh. Benjamin Mkapa na leo kwa ari zaidi, kasi zaidi, na nguvu zaidi na DK. Jakaya Kikwete unataka tena Rais gani wa kigeni, hakuna anayeweza kuvunja rekodi za watu hao . Iwe utawala bora, Uongozi uliotukuka, Amani na utulivu kwa watanzania ,upendo unaovunjavunja kila aina ya ukabila ,udini, na ueneo.

  kwa kukusaidia zaidi soma gazeti lamkakati tarehe 24 - 30 Septemba 2010 UK. 5

  Ndugu yangu chagua Kikwete 31 Oktoba 2010 kataa RAIS wa kigeni
   
 3. T

  Tafakari New Member

  #3
  Sep 25, 2010
  Joined: Sep 23, 2010
  Messages: 3
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Hongera sana jembe jipya sasa JF inapata watu wenye akili nilianza kuona kichefuchefu kusoma JF kwa sababu niliona nusu ya wachangiaji ni mentali cases kiasi ambacho hawajaona na hawaelewi jinsi nchi yetu ilivyobahatika kupata viongozi wenye hekima , na waadilifu sasa nimefurahi kuona wenye vichwa vizuri wanachangia hoja zilizo kwenda shule. Lazima wajue kiongozi bora anatoka CCM na hilo ni agizo, unabii, maono, muongozo wa Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere , na Jakaya Kikwete ni chaguo la CCM, ni chaguo la Taifa la Tanzania. Ni sauti ya watanzania, jamani tafakari kura yako iende kwa Jakaya Kikwete 31, Oktoba
   
Loading...