Tuache siasa kwenye elimu, tutambue hadhi ya walimu

Hussein J Mahenga

JF-Expert Member
Mar 5, 2012
745
633
Profesa Willy Komba, mwalimu wangu chuo kikuu cha Dodoma, aliwahi kusema, ‘walimu wanashiriki kwenye uumbaji’. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, mwalimu ndiye anayeumba taaluma zingine zote, na akasisitiza kuwa, ‘Mungu huumba binadamu, Mwalimu anaumba profession ya binadamu’. Kwa maana nyepesi, Profesa Komba anaamini umuhimu wa mwalimu kuwa ni mkubwa mno katika kutengeneza taaluma zingine, na hakuna taaluma inayokamilika bila mwalimu.

Mwl. Julius Kambarage Nyerere, akihutubia kwenye Chuo Cha Ualimu Morogo tarehe 27 Agosti 1966, aliwahi kusema, ‘shule zinatakiwa zizalishe raia wenye mwamko na wanaojitambua. Walimu wanao uwezo wa kutimilisha hili kwa namna ya tabia zao na wafundishavyo’. Mwl akaendelea kuona umuhimu wa walimu akisema, ‘…as a group, they have power which is second to none…’ akiwa na maana kwamba, walimu, kama kundi, wanao umuhimu mkubwa sana.

Ili tuweze kuwa na jamii ya watu huru nchini, kama Mwl Nyerere anavyosema, ni lazima kuwepo na watu wenye ‘mitazamo ya fikra (attitudes of mind)’; watu ambao ndiyo huunda jamii hiyo. Mitazamo mizuri ya fikra hutengenezwa angali binadamu yu mdogo, na hivyo mwenye dhamana ya kutengeneza mitazamo hii [Mwalimu], kwa kipindi hicho, ni mtu muhimu mno.

Mwalimu aingiapo darasani akiwa mnyonge, amechoka, kapauka, hana morali na wala hajivunii kuwa mwalimu, basi mtoto atakuwa na ‘mtazamo’ kuwa, ualimu ni kazi ambayo inatakiwa kukwepwa kwa namna yoyote ile; kazi ambayo haifai. Sawia kabisa na maneno ya Profesa Komba kuwa, mwalimu anaumba; anaumba kwa vitendo, maneno, tabia, maisha na namna ya ufundishaji wake.

Kwa muda mrefu, Tanzania inashindwa kuuona umuhimu huo. Utofauti wa mishahara ya walimu ukilinganisha na mishahara mingine, namna madai yao yanavyoshugulikiwa, heshima ya walimu na hata mazingira wanapofanyia kazi ni kielelezo tosha kusema kuwa, taifa bado halijatambua umuhimu wa walimu kama vile anavyoutambua Prof. Komba na Mwl. Nyeere.

Waraka wa watumishi wa serikali Na. 1 wa mwaka 2013, kwa mfano, wenye kumb. Na. CAC.205/228/01/C/14 wa Julai 2, 2013 uliosainiwa na Katibu Mkuu Utumishi, Bw. George D. Yambesi, kwa kiasi kikubwa, unaonesha ‘hadhi’ na ‘umuhimu’ wa walimu Tanzania kuwa ni mdogo sana ukilinganisha na kada zingine, na ninashukuru kuwa, walimu pia walishawahi kulijadili hiili kwenye baadhi ya Mikoa ingawa hadi sasa majibu yaliyopo ni ya kisiasa sana.

Waraka ule unabainisha kiwango cha mishahara ambacho kinaonesha utofauti mkubwa sana, na mshahara wa Mwalimu ni mdogo sana ukilinganisha na mishahara ya kada zingine. Kwa mfano, mwalimu mwenye kiwango cha elimu cha astashahada (certificate), kwa mujibu wa waraka ule, analipwa Tsh. 344,000 wakati mwenye kiwango kilekile cha elimu kwenye kada ya kilimo analipwa Tsh. 1, 060,000 na kwenye kada ya afya analipwa Tsh. 562, 000. Mwalimu mwenye kiwango cha elimu cha stashada analipwa Tsh. 432, 500, wakati mwenye kiwango kilekile kwenye kada ya kilimo analipwa 1,252,000 na kwenye afya Tsh. 821,000. Tofauti hii inaendelea kuwepo hata kwenye viwango vingine vya elimu; kada ya ualimu ikiwa na mshahara mdogo kwa kulinganisha na kada zingine.

Kikao cha walimu Mkoani Mbeya cha tarehe 3 Agost 2013, takriban mwezi mmoja baada ya waraka wa watumishi wa serikali, walikaa na kujadili tofauti ya mishahara ile, wakirejelea Sheria ya Ujira, yaani Right to just remuneration Act No. 15 of 1984, hasa ibara ya 23 (1) isemayo, ‘kila mtu, bila ya kuwapo ubaguzi wa aina yoyote, anayo haki ya kupata ujira unayolingana na kazi yake, na watu wote wanaofanya kazi kulingana na uwezo na kiasi na sifa za kazi wanazozifanya’. Walimu walikuwa na hoja nne nzito kabisa kwamba, je (i) uwezo wa walimu wa kufanya kazi haufanani na kada hizo? (ii) umuhimu wa kada ya ualimu ni mdogo tofauti na kada zingine? (iii) sifa walizonazo walimu ni tofauti kabisa na kada hizo? (iv) umuhimu wa walimu na elimu ni mdog nchini?

Ukiangalila karibu hoja zote zipo katika kuangalia ‘hadhi’ na ‘umuhimu wa walimu’ nchini, ambao kwa ushahidi huo aghalabu umekuwa hautiliwi maanani, wakati walimu ndiyo ‘creators of other professions’; kwa nini walimu hawapewi hadhi yao nchini? Je, ni kweli taifa halioni umuhimu wao?

Ufini ni nchi yenye mfumo bora wa elimu duniani kwa mujibu wa taarifa za OECD za mwaka 2012. Ubora wa elimu yao umetokana na vitu vitatu, kimojawapo ni ‘kuthamini walimu’. Pamoja na mambo mengine kwenye kuangalia thamani ya walimu nchi Ufini, mshahara wa mwalimu wa shule ya msingi (pamoja na kuwa mahitaji ya kiwango cha elimu kuwa kikubwa) kwa mwaka ni takriban dola za Kimarekani 37, 500 (takriban sh.milioni 82). Hawaishii hapo tu, heshima kwa walimu ni ya juu mno ukilinganisha na kada zingine, na kila Mfini hutamani kuwa mwalimu kuliko kada yoyote ile, na nafasi za ualimu ni za ushindani mkubwa mno. Mwalimu nchini Ufini anapewa mamlaka yote kama mwalimu bila kuingiliwa hovyohovyo kwenye kazi zake. Kazi yake ni ‘uumbaji’ wa taaluma zingine kwa uhuru mkubwa kabisa na kwenye mazingira safi, wezeshi na rafiki.

Mfumo wa elimu nchini Uchina pia umetambua hadhi ya mwalimu kitaifa, na wao kupitia mfumo wao wa Tai Pei, kila tarehe 10 ya mwezi Septemba wa mwaka ni siku ya walimu nchini. Wanachokifanya ni kuboresha hadhi ya mwalimu kijamii, kiuchumi na kitaaluma. Wanahakikisha wanakuwa na takwimu sahihi za walimu wasio na makazi na kisha kuwajengea. Wanahakikisha mwalimu anafanya kazi kwenye mazingira mazuri. Wanahakikisha mwalimu anakuwa na uwanda mpana na huru wa kujiendeleza kitaaluma. Inasadikika pia Uchina ni kati ya nchi zinazolipa walimu vizuri na kuthamini umuhimu wao.

Ukiachilia mbali suala la mishahara kama nilivyotanabaisha awali kwa rejea ya waraka wa elimu wa 2013, bado pia thamani ya mwalimu nchini ni ndogo sana ukilinganisha na kada zingine. Nitolee mfano, shule ya Sekondari Mazinge, mkoani Shinyanga hadi sasa walimu hawana ofisi. Kinachofanyika, jengo la darasa na chumba kimoja cha maabara ndivyo vinatumika kama ofisi hadi sasa. Tuseme hilo ni tatizo dogo. Sakafu ya jengo hilo linalotumika kama ofisi halina sakafu ya maana, kiatu cha mwalimu kinapigwa vumbi muda wote. Hali hiyo hiyo mwalimu wa Mazinge anakutana nayo darasani, madarasa yote hayana sakafu, hivyo yanategemea umwagiliaji maji sakafu kana kwamba mwalimu huyo anaingia bustanini. Na hii ni shule ambayo ipo katikati ya mji. Hakuna hata nyumba moja ya walimu, hakuna, na wala msingi tu haupo. Vyoo vinavyotumiwa na walimu havina tofauti na vile wanavyotumia wanafunzi. Hii ni aibu kubwa sana kwa taifa, aibu ya kushindwa kutambua thamani ya mwalimu.

Wilaya ya SIHA nako, toka walimu wasimamie mtihani mwaka 2015, hadi sasa hawajalipwa stahiki zao, yaani fedha zao za usimamizi, na wala hawajui tatizo ni nini. Mwalimu mmoja wilayani humo ananidokeza, anadai zaidi ya milioni moja, toka mwaka huo hajalipwa na hajui atalipwa lini. Iko wapi heshima ya walimu Nchini!

Kule Hai, tulisikia mwalimu katupwa ‘lock up’ kwa amri ya Mkuu wa Wilaya, kisa kashindwa kujibu maswali yake. Siku ya wafanyakazi duniani mwaka jana, walimu walipoandika mabango yao kudai haki zao za msingi, Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam siku moja tu baadaye alinukuliwa akisema alitamani sana angekuwepo karibu, angewacharaza bakora.

Matokeo mabaya mkoani Dar Es Salaam, afisa elimu, ambaye bila shaka ni mwalimu, anaandikishwa barua na Mkuu wa mkoa kwamba, kwa nini matokeo ni mabaya. Tambo zote hizi, bado taifa halijaona kabisa kuwa ni ipi ‘hadhi’ halisi ya mwalimu kwenye jamii. Mwalimu amekuwa mtu wa kunyanyaswa kila sehemu. Kila siku taifa linashuhudia askari wameboreshewa mazingira ya kufanyia kazi, wamepewa usafiri, na juu ya yote, wana posho nje ya mshahara. Mwalimu hana chochote zaidi ya mshahara wake, labda aamue kufundisha masomo ya ziada, ambapo inabidi apunguze ufanisi wa kufundisha darasani ili avutie soko lake la masomo ya ziada.

Malalamiko ya walimu nchini yamekuwa ni malalamiko yasiyofaa, na sana yamekuwa ni malalamiko yasiyo na maana, na ndiyo maana yoyote yule anaweza kujitokeza na kujibu malalamiko hayo bila kujali yeye ni nani, ili mradi tu awe mwanasiasa na ana mamlaka; yote ni kumkandamiza tu mwalimu. Pamoja na kuwa usimamizi wa walimu kwa sasa hauna mipaka tengefu baina ya vyombo vitatu; Wizara ya Elimu, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI na tume ya utumishi wa umma idara ya utumishi wa ualimu, bado haitoshi kabisa madai ya walimu, wala maadili yao kusimamiwa na mtu yoyote anayejisikia kufanya hivyo. Bado haitoshi kabisa Mkuu wa Mkoa au Wilaya kutamani ‘kucharaza bakora’ walimu ama kuwaandikisha barua hovyohovyo juu ya maadili yao, mienendo yao au hata kitu chochote kuwahusu.

Ushiriki duni wa walimu kwenye kuandaa mitaala ya elimu ni kielelezo kingine namna ambayo taifa kupitia mfumo wa elimu, halimthamini kabisa mwalimu. Kwa mfano, ukisoma sera ya elimu ya mwaka 2014 ukurasa wa 27 kwenye utangulizi, wizara inakiri kabisa kuwa, mabadiliko ya mtaala wa kutoka kwenye msingi wa maudhui na ufahamu (content and comprehension based curriculum) kwenda kwenye mtaala wa ujuzi haukushirikisha, kati ya wengine, walimu na hivyo, walimu hawafundishi vile mitaala inawafanya wafundishe. Maana yake ni kwamba, kuna mambo ambayo walimu wanayaona yanafaa kuwamo kwenye mitaala, na hawakuyawasilisha kwenye uandaaji mitaala hiyo, hivyo hayamo kabisa kwenye mtaala elekezi. Hii ni hatari na ni mwendelezo wa kudharau walimu ambao ndiyo wadau wakubwa wa elimu kwani ndiyo wanoutekeleza mtaala, wanautathmini na kuupima.

Kwa maoni yangu, ipo haja kubwa sana taifa liangalie upya na kutambua ‘umuhimu’ na ‘hadhi’ ya walimu ili kulipatia taifa wananchi wenye mitazamo mizuri ya fikra, kwa manufaa mapana ya nchi na wananchi, hasa kipindi hiki cha elimu bure. Kama anavyosoma daktari, mtaalamu wa kilimo, mwanasheria na kadhalika, mwalimu pia anakaa chuoni kupatiwa mafunzo ya ualimu, wala hajaokotwa mtaani. Juu ya yote, mwalimu anarudi mashuleni kuendeleza taaluma hizo ambazo leo hii zinaonekana kuwa na thamani kuliko mwalimu.

Nikubaliane na Profesa Komba kuwa, ‘mwalimu anashiriki kwenye uumbaji’ na Mwl.l Nyerere kuwa, walimu, kama kikundi, wanayo nguvu kubwa mno kwenye jamii. Walimu wanao uwezo wa kujenga ama kubomoa jamii kutokana na nafasi yao waliyonayo. Tukilalamika kuwa, tuna taifa la ‘vilaza’, lazima turejee ni nani huyu anayezalisha taifa la vilaza? Hadhi yake nchini ikoje? Anathaminiwaje? Kama anapewa stahiki zote bila utofauti na kada zingine, je ni kweli anaendelea kuzalisha vilaza?

Kama taifa, ni lazima lione kuwa, kuna sehemu limeshindwa kabisa kuwatendea haki walimu, na sasa ni wakati wa kurekebisha kasoro hizo hasa awamu hii ya tano ili sasa tuwe na taifa la watu wenye mitazamo ya fikra yenye tija. Serikali iboreshe mshahara wa mwalimu sawia na kazi na umuhimu wake. Iunde chombo kimoja cha kushughulikia madai yao, na zaidi waachwe wenyewe waseme, siyo kusemewa na wanasiasa wanaotumia takwimu feki kama zile za Kiufunza teachers survey ambazo hazina uhalisia.

Mwalimu aheshimike zaidi ya mwanasiasa. Inatia kinyaa mno kuona mkuu wa wilaya au mkoa anapata shauku ya kutia mwalimu ndani kwa matakwa yake binafsi, ama kucharaza mwalimu bakora kwa kudai stahiki zake, na kama kuna sheria inayowapa mamlaka hayo, basi serikali ione haja ya kuurejesha bungeni, kama muswaada, kwa ajili ya marekebisho. Inasikitisha mno kuona mwalimu anaandikishwa barua kujibu kwa nini matokeo ni mabaya wakati ana njaa, anadaiwa hela ya pango, na kama haitoshi, anafanya kazi kwenye mazingira magumu, ofisi hazilingani kabisa na hadhi yake.

Inatia uchungu mno mwalimu anayetumia muda mwingi kuandaa cha kumfundisha mtoto anakaa kilomita kadhaa kutoka aishiko hadi kituo cha kazi. Na kama haitoshi, mwalimu anahamishwa, hapewi stahiki zake za uhamisho. Taifa sasa lifikie ukomo wa kuwatumia walimu kama makalani wa mitaala kuliko waandaaji wa mitaala. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa na elimu itakayomuwezesha mwananchi kuhimili kwenye ushindani wa soko la ajira. Kupuuza hadhi na umuhimu wa walimu ni kupuuza elimu, hivyo kufanya mwanya wa kuwa na taifa la watu mambumbumbu.
 
Nilitolea mfano wa mishahara iliyoainishwa kwenye waraka wa watumishi wa serikali ambao pia nimeurejelea kwenye makala, waraka wa mwaka 2013
Article nzuri sana but hapo kwenye viwango vya mishahara umedanganya..cku nyingine usilete data ambazo huna uhakika nazo
 
NGAZI YA ELIMU UALIMU/ ELIMU KILIMO AFYA
Certificate (Cheti) Tsh 344,000/= Tsh 1,060,000/= Tsh 562,000/=
Diploma (Stashahada) Tsh 432,500/= Tsh 1,252,000/= Tsh 821,000/=
Degree (Shahada) Tsh 589,000/= Tsh 1,473,000/= Tsh 994,000/=
Jedwali hili ni kwa mujibu wa waraka huo uliotajwa hapo juu
 
Kwa hiyo watumishi ndo mishahara wanayolipwa kama ulivyoandika kwenye huo waraka wako ??
Nilitolea mfano wa mishahara iliyoainishwa kwenye waraka wa watumishi wa serikali ambao pia nimeurejelea kwenye makala, waraka wa mwaka 2013
 
NGAZI YA ELIMU UALIMU/ ELIMU KILIMO AFYA
Certificate (Cheti) Tsh 344,000/= Tsh 1,060,000/= Tsh 562,000/=
Diploma (Stashahada) Tsh 432,500/= Tsh 1,252,000/= Tsh 821,000/=
Degree (Shahada) Tsh 589,000/= Tsh 1,473,000/= Tsh 994,000/=
Jedwali hili ni kwa mujibu wa waraka huo uliotajwa hapo juu
Mkuu si umesema mwenyewe according to waraka ule analipwa...maana yake nini???
 
Okay, basi ni mistake, lakini kubwa nilitaka kuonesha namna walimu walivyo chini, na kwa mwaka huo nafikiri ndiyo yalikuwa malipo hayo, ila wacha nitatafuta ya sasa,
Yeap kweli ndo yalikuwa malipo yao...umeandika kwa usahihi malipo ya walimu but ukakosea kwenye hizo kada nyingine ume over estimate
 
Yeap kweli ndo yalikuwa malipo yao...umeandika kwa usahihi malipo ya walimu but ukakosea kwenye hizo kada nyingine ume over estimate
Oh, basi nadikiri pia waraka haukuwa sahihi, maana nimechukua kama ulivyo! Hata hivyo, nashkuru kwa kunionesha changamoto hiyo, next time nitakuwa mwandishi mzuri!
 
Andiko zuri!!Uncle M angeliona labda angejiongeza!!Anyway ngoja tuone mwezi November huu atafanya nini....maana aliahidi kitu
 
Mwalimu ni kopo LA chumvi umuhimu wake ni pale chumvi inapohitajika kwenye mboga tu! Tangu mda amebaki Kama kibao kinachoonesha direction yeye kabaki pale alipo? Nani anatambua umuhimu wake? Nani anajua pale alipo Bila Mwalimu asingefika,?
 
Sasa ongezeko la mshahara mipya ni vituko! Watumishi wako wengi ila Kama elfu tano na ushee ndio wapo kwenye mpango huu! Swali je nikada Ipi hiyo ambayo watumishi watapata bonus hiyo maaana watumishi elfu tano nikama Mkoa mmoja acheni Siasa ktk maisha ya watumishi
 
Duh! Sasa wengine itakuaje?
Sasa ongezeko la mshahara mipya ni vituko! Watumishi wako wengi ila Kama elfu tano na ushee ndio wapo kwenye mpango huu! Swali je nikada Ipi hiyo ambayo watumishi watapata bonus hiyo maaana watumishi elfu tano nikama Mkoa mmoja acheni Siasa ktk maisha ya watumishi
 
Back
Top Bottom