Tu Kama Ng'ombe Kipofu Na Ng'ombe Aliyevunjika Mguu!


M

maggid

Verified Member
Joined
Dec 3, 2006
Messages
1,084
Likes
398
Points
180
M

maggid

Verified Member
Joined Dec 3, 2006
1,084 398 180
Ndugu zangu Wahehe wana msemo; Isenga imbofu na isenga indenyoofu. Kwamba ng'ombe kipofu ni sawa tu na ng'ombe aliyevunjika mguu, wote watakufa njaa. Ng'ombe kipofu hawezi kuyaona majani, na yule aliyevunjika mguu hawezi kujikokota kwenda kutafuta nyasi za kula.

Tafakuri yangu iliyopita nilimalizia kwa kuuliza swali: Je, unafikiaje uamuzi wa ama kuingia vitani, au la? Huu ni mwendelezo wa nilipoishia. Naam. Tunavyoenenda kama jamii wakati mwingine ni sawa na ng'ombe kipofu na yule aliyevunjika mguu. Unaweza kuliona hilo nyumbani kwako, katika ukoo wako na hata mahala pako pa kazi. Tumekuwa jamii ya ovyo ovyo. Tunafanya mambo ya ovyo ovyo. Ni kutoka ngazi ya familia na hata ngazi ya kitaifa.

Ona migongano ya wanasiasa wetu sasa. Ona wanavyogawanyika katika makundi yao. Hawatangulizi hata kidogo maslahi ya wengi. Wanajigawa kwenye makundi kugombania mamlaka. Nikasema huko nyuma; aliye gizani humwona aliye kwenye mwanga na aliye kwenye mwanga hamwoni aliye gizani. Na wakati mwingine, hata yule anayejiona yuko kwenye mwanga, naye pia yuko gizani. Wengi walio gizani ni watu wadogo sana. Ni wanyonge waliobakishwa gizani bila ya walio kwenye mwanga kufanya jitihada za dhati kuwatoa gizani.

Leo kuna makundi ya wanasiasa yanayopigana vita isiyo na tija kwa mtu wa kawaida. Wametafuta visingizio vya kuingia vitani. Kuna wanaodai wanapigana kuwatetea wanyonge walio gizani. Walio gizani nao wameanza kuona katika giza hilo hilo, maana wamekuwa gizani kwa muda mrefu. Wameshtuka. Wanahoji mantiki ya vita vinavyopiganwa kwa niaba yao.

Na walioamua kuingia vitani nao wanaonekana kutojiandaa vema na vita hivyo, wanaelekea kushindwa, maana wanapigana vita vya kinafiki. Na kamwe usiingie kwenye vita ambavyo hujajiandaa vema ili ushinde. Mwingine atasema vita vingine havina budi kupiganwa hata kama hujajiandaa kupigana na kushinda. Hapana, huendi vitani ili mradi tu unakwenda vitani , kama vile unakwenda harusini. Vita si lelemama.

Katika dunia hii inasemwa; chagua vita vyako. Haina maana uchague vita kama unachagua mashati ya mitumba Kariakoo. Ina maana kubwa. Pima kwanza, soma alama za nyakati. Chagua vita inayoshindika, iliyo ya muhimu kupiganwa na unayokuwa na hakika ya kuwa umejiandaa vema kulipa gharama ya ushindi.

Miaka mingi iliyopita kulikuwa na Mfalme wa Epilus aliyeitwa Pyrrhic. Mfalme huyu aliamua kuingia vitani kulikabili jeshi kubwa na lenye nguvu nyingi, ni jeshi la Warumi. Lakini kabla ya Mfalme kuingia baharini na vikosi vyake kuitafuta Italia ya Warumi, msaidizi wake wa karibu, Cineas, aliomba mazungumzo ya faragha na Mfalme. Alitaka kumwuliza maswali na kumshauri.

Cineas alimtamkia Mfalme; " E bwana Mfalme, Warumi wanasadikika kuwa na jeshi kubwa , lenye nguvu na lenye mashujaa wengi. Ndio maana wameteka nchi nyingi. Je, Mungu akitusaidia, tukaja kuwashinda Warumi, tutafanya nini na ushindi wetu?

Mfalme akajibu: " Mbona hilo ni swali jepesi sana. Mara ile tukiwashinda Warumi, hakutatokea jeshi kutoka mji wowote wa Italia litakaloweza kupambana nasi."

Cineas alitulia kidogo, kisha akamwuliza Mfalme: " Tukishaikamata Italia ya Warumi, kipi kitafuatia?"

Mfalme akajibu: Sicily ni kisiwa chenye hazina za thamani kubwa, itakuwa rahisi sana kukiteka kisiwa hicho."

Cineas aliendelea kuuliza: " Bwana Mfalme unaongea juu ya mambo ya kusadikika, lakini una maana kukitwaa kisiwa cha Sicily kutakuwa na maana ya kukoma kwa vita?"

Mfalme akajibu: " Hapo tutakuwa tumeikaribia Afrika. Na tukishaikamata Afrika ni nani hapa duniani atathubutu kutukabili kivita?"

" Hakuna" Alijibu Cineas, kisha akauliza; " Na baada ya hapo tutafanya nini?"
Mpaka hapo Mfalme hakujua Cineas alikuwa anampeleka wapi kwa lojiki ya kifikra. Mfalme akajibu:
" Baada ya hapo, tutapumzika, tutakula raha. Tutakula na kunywa . Tutabaki tukichekeshana na kucheka, siku nzima."
Kama ni hivyo, alisema Cineas; " Ni kitu gani kinachotuzuia kufanya hayo yote sasa bila kwenda vitani?

Mfalme hakuielewa mantiki ya Cineas. Akakaidi ushauri. Akavipeleka vikosi vyake kupambana na Warumi. Baada ya vita ngumu, jeshi la mfalme liliwashinda Warumi. Hata hivyo lilipata hasara kubwa ya kupoteza watu na kuwa na majeruhi wengi. Jeshi lake likadhohofika sana. Likajaribu kuitwaa Sparta, likashindwa vibaya sana. Mfalme aliwindwa na hatimaye akakakamatwa na kuawa kwa kupigwa mawe kwenye mitaa ya Argos. Isenga imbofu na isenga indenyoofu. Ng'ombe kipofu ni sawa tu na ng'ombe aliyevunjika mguu, wote watakufa njaa. Wanasema ndugu zangu Wahehe. Naendelea kutafakari, nawe tafakari pia.

Maggid ( Mwalimu Wa Zamu)
Iringa,

Februari 4, 2010
+255 788 111 765http://www.kwanzajamii.com
 
nguvumali

nguvumali

JF Bronze Member
Joined
Sep 3, 2009
Messages
4,891
Likes
198
Points
160
nguvumali

nguvumali

JF Bronze Member
Joined Sep 3, 2009
4,891 198 160
Maggid vita ya wanasiasa hasa wa chama tawala ina Tija sana, maana genge la walji sasa linaogopa kula kama halina akili nzuri, angalau wanahofu kua kundi kinzani liking'amua ulaji huo llitalipuka na kuwaacha wakiwa uchi kabisa.
 
A

August

JF-Expert Member
Joined
Jun 18, 2007
Messages
4,746
Likes
889
Points
280
A

August

JF-Expert Member
Joined Jun 18, 2007
4,746 889 280
Ni kweli umepatia ndugu yangu Viongozi wengi na waandishi wa habari ni kama ng'ombe kipofu au aliyevunjika mguu maana hawayaoni majani yaliyo mbele yao au hawawezi kuyafikia majani hayo maana miguu yao imevunjika pamoja na mashabiki wao ndio maana leo hii tupo hapa tunatumia keyboard kuuelimisha umma/baadhi ya viongozi na vibaraka wao kwamba njia sahihi sio wanayo fuata bali ni nyingine.
asante kwa makala nzuri ubarikiwe na Mwenyezi mungu akuzidishie ili uweze kutuletea maada nyingi kama hizi.
 
Mlalahoi

Mlalahoi

JF-Expert Member
Joined
Aug 31, 2006
Messages
2,124
Likes
485
Points
180
Mlalahoi

Mlalahoi

JF-Expert Member
Joined Aug 31, 2006
2,124 485 180
Pamoja na kuzunguka kote huko,kwa kifupi unajaribu kutuambia kuwa vita wanazoingia akina Muro ni maji marefu. Huu ni utetezi kwa wanaotafuna nchi yetu.

Hivi jambazi likiingia ndani ya nyumba yako utaanza kuchambua falsafa hizo au kulikabili ili uokoe familia yako? Hizi busara za kukatishana tamaa zimechangia sana kutufikisha hapa tulipo.
 
N

Ngala

Senior Member
Joined
Sep 30, 2009
Messages
160
Likes
5
Points
0
N

Ngala

Senior Member
Joined Sep 30, 2009
160 5 0
Mlalahoi tupo pamoja. Mjengwa anataka mibaka uchumi tuipigie magoti maana wana nguvu kama jeshi la warumi kwa mtazamo huo tanganyika isingedai uhuru maana mtawala alikuwa na nguvu kuliko kina Nyerere.

Nyerere pamoja na unyonge wake alisimama kidete akajenga hoja adhimu hatimaye waingereza wakaondoka. Simama kwenye haki acha kujadiliana na mwizi wako. Hao uwaonao wachache na wanyonge jua kuwa NGUVU KUU YA UMMA IPO NYUMA YAO.
 
Ludovick Mwijage

Ludovick Mwijage

Member
Joined
Jan 1, 2010
Messages
41
Likes
0
Points
0
Ludovick Mwijage

Ludovick Mwijage

Member
Joined Jan 1, 2010
41 0 0
Ndugu Maggid Mjengwa,

Nimesoma makala yako zaidi ya mara moja na kuyaelewa. Lakini sidhani msemo wa ng'ombe kipofu na aliyevunjika mguu, unaweza kulinganishwa na Mtanzania wa karne hii. Kadhalika, kauli yako kwamba 'Kamwe usiingie kwenye vita ambavyo hujajiandaa vema ili ushinde' pia sidhani ni sahihi.

Kama baadhi ya viongozi wetu kama vile Bushiri na Chifu Mkwawa, wangelishikilia mtazamo kama huu, pengine wangeliona bora kushirikiana na nguvu ambazo walijua dhahiri wasingelizishinda. Lakini badala yake, waliamua kukabiliana na nguvu hizo kishujaa, ili kutetea hadhi ya wananchi na kulinda rasilimali zao.

Kama badala ya kufanya hivi wangeliamua; kwa sababu tu ya unyonge, udhaifu wao au kutokuwa na zana bora za kivita; kushirikiana na wavamizi katika kuunda serikali ya ki-Quisling historia, hakika, ingeliwahukumu vikali.

Siyo hilo tu, lakini katika mwenendo wa kujihami dhidi ya ushambulizi wa aina yeyote (au uchokozi) inafahamika dhahiri kwamba, mshambulizi atakuwa na mkono wa juu zaidi kuliko anayeshambuliwa.

Hii ni kwa kuwa, mshambulizi kwa kawaida atakuwa amejizatiti vya kutosha kabla ya kumshutukiza mshambuliwa na shambulizi hilo. Hata hivyo, hili peke yake, halimhakikishii ushindi mshambulizi.

Kwa maneno mengine, kutojizatiti kikamilifu (au kutojizatiti kabisa) kwa upande wa mshambuliwa, siyo sababu nzuri ya kumzuia kutojibu shambulio likitokea. Aidha, udhaifu wa mshambuliwa, kamwe haumpi kisingizio cha kumkumbatia mshambulizi wake kwa mikono miwili. La hasha!

Ninahisi kutokana na mtazamo wako, inawezekana kabisa una dhana pana ya vita, inayounganisha mambo mengine mengi.

Lakini katika hali ya kawaida, mwanadamu anapodhamiria kukabiliana na kile anachoamini kuwa hakimfai katika mazingira yanayomzunguka, haya huwa ni mapambano na wala siyo vita katika tafsiri halisi ya neno.

Katika jamii yetu kuna dhana kwamba maisha ni mapambano; mapambano ambayo kama kifikra yasingelikuwapo, si ajabu thamani ya maisha ingelipungua kwa kiasi kikubwa. Hii ni kwa kuwa, ni kuwepo kwa dhana ya mapambano kinachofanya maisha yasiwe mepesi kama mwanadamu ambavyo angelipenda.

Kwa hiyo basi mapambano, yawe dhidi ya ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka ya kisiasa na nguvu za dola, ubadhilifu, uonevu wa kitaasisi, dhuluma na vitisho n.k., siyo chaguo kwa mpambanaji (au mwanaharakati).

Kwake, hili ni sukumizo linalosababishwa na ulazima wa kuthibiti uovu huo mapema, kabla ya uovu wenyewe haujamthibiti yeye na mazingira yake, na mwishowe kuathiri maendeleo yake na kukua kwa jamii.

Mtazamo huu, unaweza kueleza kwa nini ukimtaka mwanadamu achague kati ya kuishi daima amepiga magoti; akiokota vizibo vya soda na kula masalia ya watu wengine; na kusimama wima ajitegemee-licha ya ugumu atakaokumbana nao katika kupitia zoezi hili-atachagua la mwisho.

Ni ugumu mtu atakaokumbana nao kutokana na uamuzi wake huo, unaozaa dhana yenyewe ya mapambano (au 'vita' kwa mtazamo wako).

Kwa vyovyote vile, ngano ya maongezi kati ya Mfalme Pyrrhic na mlonda wake wa karibu, Cineas; uliyoitumia kujenga hoja yako; inaelekea kutowiana sana na kero ya baadhi yetu wasiopenda kuliona Taifa letu likigeuzwa kuwa kihamba cha watu tisa; au kijikundi cha watu wachache sana; wenye nia ya kujitajirisha kupindukia na kwa njia isiyo halali kabisa.

Ikiwa hili linatafsiriwa kama kuingia kwenye vita ambavyo maandalizi yake hayatoshi kuhakikisha 'ushindi', basi na iwe hivyo!

Ninakutakia wikendi njema,

Ludovick Simon Mwijage
Jagtvej 215B, 3-2
2100 Copenhagen Ø
Denmark
Tel: + 45 52 60 71 71Naam, Maggid umepata wa kukujibu kwa kirefu
 

Forum statistics

Threads 1,250,870
Members 481,514
Posts 29,748,995