TTCL Yazindua huduma ya 4G, Tunguu, Mkoa wa Kusini, Zanzibar

PendoLyimo

JF-Expert Member
Sep 30, 2014
877
955
Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Mhandisi Zena Ahmed Said amezitaka Taasisi na Mashirika yaliyopo Mkoa wa Kusini Zanzibar kutumia fursa za uwepo wa mawasiliano kwa ajili ya kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kidijitali.

Katibu Mkuu Kiongozi amesema hayo baada ya kuzindua huduma ya mawasiliano ya 4G ya TTCL Corporation katika hafla iliyofanyika jana Tunguu, Mkoa wa Kusini katika viwanja vya Afisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini, Zanzibar.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Usafirishaji na Uchukuzi, Mhe. Amour Hamil Bakari, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Mhe. Rashid Hadid Rashid, Mhe. Marina Joel Thomas Mkuu wa Wilaya ya Kati, Mkuu wa Wilaya Kusini Mhe. Rashid Makame Shams, Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL Bw. Mohammed Khamis, na Bw. Yakoub Uweje, Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka Wizara ya Habari na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Bi. Clarence Ichwekeleza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano, TTCL Bw. Waziri Waziri Kindamba.

Akizindua huduma hizo, Katibu Mkuu Kiongozi amezitaka Taasisi na Mashirika kutumia zaidi huduma za intaneti ili kukuza matumuzi ya TEHAMA nchini na kuongeza kasi ya kutoa huduma kwa wananchi zenye tija na kiwango.

“Tunajua umuhimu wa intaneti yenye kasi katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA hivyo natoa rai kwa Taasisi za Umma na binafsi zilizopo katika eneo hili la Tunguu, haswa Idara za Serikali zilizopo hapa zikiwemo Idara ya Uhamiaji, Afisi za Polisi Mkoa, Afisi ya Mkuu wa Mkoa Kusini, Afisi ya Muungano, na Halmashauri za Mkoa kutumia huduma hizo kwa malengo ya kufanikisha mipango ya Serikali” amesema Mhe.Mhandisi Zena Ahmed Said.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Usafirishaji na Uchukuzi, Mhe. Amour Hamil Bakari ameipongeza TTCL kwa kuendeleza dhamira yake ya kujenga minara ya mawasiliano Zanzibar katika maeneo ya Kizimkazi, Makunduchi, Paje, Chwaka na maeneo mengine ya Pemba ili kuondoa changamoto za mawasiliano kwa wananchi.

“Napenda kuwapongeza TTCL Corporation kwa maamuzi na mkakati wa kujenga minara ya 4G hapa Zanzibar, Unguja na Pemba. Hii itasaidia katika kuimarisha Mawasiliano na kukuza fursa za kiuchumi na ajira” amesema Katibu Mkuu

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Waziri Kindamba amesema kuwa TTCL Corporation inaendelea kutekeleza mpango wake wa kujenga minara ya 4G Unguja na Pemba ili kutoa fursa kubwa kwa Watanzania na Taasisi kupata mawasiliano yenye usalama, ubora na uhakika.

Bw. Kindamba amesema ujenzi wa mnara huo wa hapa Tunguu, utawezesha wananchi na Taasisi zilizopo maeneo hayo kuwasiliana kwa ufanisi na kwa gharama nafuu zaidi na hivyo kufanikisha shughuli za kiuchumi na kijamii katika kuongeza kasi ya maendeleo ya hapa Zanzibar.
Pia Bw. Kindamba amewataka wananchi wanaozunguka maeneo ya Tunguu kupata fursa za kuboresha zaidi hali zao za kiuchumi kwa kuchangamkia fursa za kuongeza kipato kwa kuwa Mawakala wa kusajili laini, kuuza Vocha na Wakala wa T-PESA.

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Clarence Ichwekeleza amesema Serikali imeendelea kusimamia ujenzi wa minara ya mawasiliano nchini ili kutoa fursa kwa wananchi wote kupata fursa ya kupata mawasiliano kwa gharama nafuu na yenye uhakika.
“Mnara huu wa Tunguu, ni mnara wa mawasiliano wa 324 katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa Unguja na Pemba kati ya minara 8,676 kwa Tanzania nzima, lengo ni kuona wananchi wanafikiwa na mawasiliano yenye kasi” amesema Bi. Clarence Ichwekeleza.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini, Mhe. Rashid Hadid Rashid amesema ujenzi wa mnara huu wa mawasiliano eneo la Tunguu Mkoa wa Kusini kutaimarisha mawasiliano na kufungua fursa kwa vijana kupata elimu na ajira sambamba na Taasisi mbalimbali kutumia mawasiliano ya intaneti kuboresha utendaji.

“Ujenzi wa Mnara huu wa mawasiliano ya 4G ni fursa pekee kwa Mkoa wa Kusini, na utasaidia kurahisisha mawasiliano kwa kiwango kikubwa katika kuondoa changamoto za mawasiliano katika Mkoa huu” amesema Mkuu wa Mkoa wa Kusini.

Aidha, Mhe. Rashid Hadid Rashid amepongeza mpango wa Shirika wa kutaka kujenga minara ya mawasiliano katika maeneo ya Kizimkazi, Paje,Chwaka na maeneo mengine katika Mkoa huu na minara hiyo itaondoa changamoto za mawasiliano kwa wakazi wa Zanzibar.
 
Back
Top Bottom