TTCL, ATCL kumejaa ‘vihiyo’

kbm

JF-Expert Member
Oct 5, 2012
5,224
1,676
ttcl+vihiyo.jpg

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad ametaja mambo tisa yanayoongoza kwa kuipotezea Serikali fedha huku akitaja kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na Shirika la Ndege Tanzania (ATC) kuwa yana idadi kubwa ya wafanyakazi ambao elimu yao ni darasa la saba. Alisema hayo jana wakati akitoa mafunzo kwa kamati nne za Bunge juu ya mambo ambayo wanatakiwa kuhoji wanapokuwa kwenye vikao vya bajeti yanayohusu ripoti za CAG.

Akizungumzia kuhusu ATCL na TTCL, Profesa Assad alisema mashirika hayo yamekuwa hayana faida kwa Serikali zaidi ya kuitia hasara ya kulipa wafanyakazi mishahara wakati hakuna kazi zinazofanyika. Alisema matatizo yanayokabili mashirika hayo ni ukosefu wa mitaji na kuwa na waajiriwa ambao wana uelewa mdogo hivyo kushauri yafutwe.

“Mfano hili shirika la TTCL halina faida yoyote kwenye nchi hii kwa zaidi ya miaka 10 sasa, watu wanalipwa mishahara lakini hakuna kinachofanyika, ukienda pale asilimia kubwa ya wafanyakazi ni darasa la saba” alisema na kuongeza kuwa lilitakiwa lisiwepo kabisa lakini limekuwa linavumiliwa na wakati huohuo na wabunge wapo.

“Naongea haya nikiwa ninajiamini kwa sababu ninayafahamu vizuri... ATC ina ndege mbili tu lakini ukienda pale kuna wafanyakazi zaidi ya 300 wote wanalipwa mishahara hakuna kodi inayopatikana pale.”

Profesa Assad alisema hata hizo ndege mbili zilizopo nazo hazifanyi kazi na kwamba shirika hilo lilitakiwa kuwa na wafanyakazi wachache na ofisi mbili tu.



Mambo tisa

Kuhusu mambo tisa yanayoongoza kupoteza fedha za Serikali, Profesa Assad aliyataja kuwa ni utaratibu wa utoaji wa zabuni za Serikali, bajeti zisizotekelezeka, fedha zilizomo katika bajeti kutotolewa kwa wakati, uhamishaji wa bajeti kwenye vifungu, kubadilishwa viwango vya ubadilishaji wa fedha na vikwazo vya bajeti.

Pia alitaja ukiukwaji wa utaratibu kwa wenye mamlaka (watendaji), kutochukua hatua kwa watu wanaokiuka kanuni na taratibu za matumizi ya fedha na mgongano wa masilahi.

Kuhusu zabuni, alisema baadhi ya watendaji wanaozisimamia wamekuwa wakila njama na kutozingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 hali inayosababisha malipo ya kughushi na matumizi mabaya ya fedha.

“Kumekuwa na upandishaji wa bei za bidhaa zinazonunuliwa kwa zabuni, mfano halmashauri ikitaka kununua mabati kama bei ni Sh16,000 inapandishwa na kuwa Sh17,000 lakini akienda kununua mtu wa kawaida anapewa bei iliyopo” alisema.

Profesa Assad hakuacha kuwapasulia ukweli wabunge hao akiwaambia kuwa baadhi yao wanapokuwa kwenye vikao vya kupitisha bajeti wanakuwa na masilahi binafsi

“Nitolee mfano nilikuwa na mbunge mmoja mjumbe katika bodi, tulikuwa tunajadili jambo la maana linalohusu kupitisha bajeti, lakini hakuongea chochote zaidi aliishia kuulizia posho,” alisema.

Alisema kumekuwa na vikwazo vya bajeti vinavyosababishwa na ucheleweshaji, kutotolewa na kutolewa fedha chini ya kiwango kilichopangwa, matumizi ya fedha kinyume na zilivyopangwa.

Pia, alisema suala la bajeti zisizotekelezeka limekuwa likifanyika wakati wa ukusanyaji wa fedha ili kukidhi makadirio ya matumizi ya Serikali na hii inatokana na kuwa na wigo mdogo wa kodi, kutegemea fedha za wafadhili na rushwa miongoni mwa watendaji.

Mhadhiri wa uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Haji Semboja aliwataka wabunge kutambua kuwa Tanzania siyo maskini.

“Kumekuwa na dhana mnawaambia wananchi Tanzania ni nchi maskini, nchi hii siyo maskini, tatizo lililopo ni utawala bora na ndiyo maana wananchi wengi wana hali ngumu ya maisha,” alisema.

Alisema tatizo la serikali ni kuwategemea watu wengine kutoka nje ya nchi wakiwamo wawekezaji kuja kumiliki, kuendesha na kusimamia rasilimali za nchi, Serikali ikisubiri kukusanya kodi.



Wabunge wanena

Wakizungumzia mafunzo hayo, baadhi ya wabunge walisema kuna mashirika mengi na taasisi ambazo haziridhishi katika utendaji lakini bado zinalelewa. Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Raisa Abdallah Mussa alisema mashirika hayo mara nyingi yanapohojiwa kuhusu utendaji wao yanadai kupewa bajeti ndogo na Serikali.

“Tumejaribu pia kuhoji juu ya mashirika haya likiwamo la ATC wanadai bajeti wanazopewa na Serikali kuendesha mashirika zinakuwa hazikidhi mahitaji na haziji kwa wakati ndiyo maana zinashindwa kujiendesha” alisema.

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom