TRC tengeni vyumba maalum vya wagonjwa kwenye treni

Samaki Singa

Senior Member
Nov 20, 2016
190
185
Haikuwa nia yangu kutoa hoja hii, lakini kadiri siku zinavyosonga ndivyo hali inavyozidi kuwa mbaya katika usafiri wa treni zinazoendeshwa na Shirika la Reli Nchini(TRC).

Tunatambua TRC inatoa huduma, hivyo haitakiwi kuwa na ubaguzi kwa wasafiri wanaoendelea kutumia usafiri wa shirika hilo.

Lakini lazima uongozi wa Shirika uamke sasa kwa kuzingatia haki na staha za kila abiria awapo safarini.

Wagonjwa wa viwango tofauti wamekuwa wakisafirishwa sambamba na watu wazima( wasio wagonjwa) katika mabehewa na vyumba vya abiria.

Hali hii imekuwa ikileta tafrani kubwa kwa abiria wengine na hata kuhofiwa afya zao pale ambapo mgonjwa anaweza kuwa na maradhi ya kuambukiza.

Nimeshuhudia mara tatu hali hiyo ya kuchanganya wagonjwa mahututi kwenye vyumba na watu wazima huku kukiwa hakuna huduma za kitabibu kwa wagonjwa .

Unakuta mgonjwa hawezi /hajimudu mwenyewe kwenda chooni. Hivyo haja zote anazifanyia humo humo chumbani ama kwenye behewa.
Hebu jamani fikirieni, hali namna hii inakuaje?Mazingira ya kiafya yanakuwaje hapo?Je, uongozi wa Shirika chini ya Mkurugenzi Massanja Kadogosa umefanya tathmini ya kutosha na kuzingatia afya za abiria wengine?.

Mfano ni treni ya Deluxe iliyotoka Dar es Salaam kuelekea Kigoma tarehe 6 Oktoba 2022 katika behewa namba 2232 chumba B.

Chumba hiki kilikuwa na mgonjwa asiyejiweza ambaye huduma zake zote alikuwa anazifanyia chumbani.Hali ilikuwa ngumu kwa wasafiri wengine wote (4) waliokuwa kwenye chumba hicho kuanzia mwanzo wa safari Dar es Salaam hadi Kigoma.Mgonjwa huyo alikuwa na msaidizi mmoja tu chumbani humo.

Ushauri wangu kwa TRC sio kuzuia wagonjwa wasisafirishwe, ila anayemsafirisha mgonjwa ni lazima atoe taarifa ya hali ya mgonjwa wake na namna anavyoweza kujisaidia mwenyewe huduma muhimu za kibinadamu awapo safarini.

Lakini wanaomsafirisha pia lazima wazingatie hali ya afya ya wasafiri wengine wawapo safarini. Hapa si suala la unyanyapaa, hapana, ila ni hali halisi.

TRC wanaweza kutenga chumba kimoja kwa wagonjwa na wanaowahudumia wawapo safarini, lakini na daktari endapo hali ya mgonjwa itabadilika na kuhitaji huduma ya dharura.
 
2 Reactions
Reply
Back
Top Bottom