TOURE: Daktari wa mkoa aliyepania kumtoa jasho Lowassa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

TOURE: Daktari wa mkoa aliyepania kumtoa jasho Lowassa

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Msharika, Apr 14, 2010.

 1. M

  Msharika JF-Expert Member

  #1
  Apr 14, 2010
  Joined: May 15, 2009
  Messages: 936
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 35
  Aliwahi kuishi Ikulu ya Guinea kwa?miaka 20

  MAISHA ya binadamu yamejaa mshangao. Mnamo mwaka 1951 alizaliwa mtoto wa kiume katika familia ya wafugaji wa Kimasai iliyokuwa ikiishi katika Savanna ya Lesimingori wilayani Monduli, Mkoani Arusha.
  Mtoto huyo - Salash Ole Mokosyo kama walivyo wengine alikuwa wa kawaida na hivyo wazazi wake waliamini kuwa wamepata ‘morani’ wa kusimamia shughuli za ufugaji zilizokuwa zikifanywa na familia yao.
  Lakini mambo hayakuwa hivyo. Miaka 12 baadaye historia ya mtoto huyo ilibadilika kabisa kutoka “zizini” hadi kwenda kuishi ndani ya Ikulu ya Conakry ya Rais Ahmed Sekou Toure wa Jamhuri ya Guinea.
  Na si kuishi Ikulu ya nchi tu kwa miaka zaidi ya 20, lakini kijana huyo wa Kimasai pia alibahatika kutumia ubini wa Rais Toure na baadaye alifahamika kama Salash ole Mokosyo Toure; maarufu zaidi kama Dk.Toure baada ya kuhitimu masomo yake ya utabibu nchini humo.
  Katika miaka hiyo ambayo harakati za kutafuta uhuru zilikuwa zimepamba moto nchini, kijana huyo akiwa na umri wa miaka minane, alipata nafasi ya kujiunga na Shule ya Msingi Monduli (Monduli Upper Primary School).
  Akiwa katika shule hiyo, akiendelea na masomo, ndipo mwaka 1963, nyota njema ya Salash iliwaka ambapo alijikuta akichaguliwa kama mtoto pekee kutoka katika jamii ya wafugaji wa Kimasai kushinda nafasi ya kwenda kusoma bure nchini Guinea iliyokuwa ikiongozwa na Rais mzalendo, hayati Ahmed Sekou Toure.
  Sekou Toure, Rais Mjamaa na rafiki kipenzi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitembelea Tanzania mwishoni mwa mwaka 1963. Ziara yake ilimfikisha hadi Kaskazini mwa nchi; hususan mkoani Arusha.
  Alipofika Arusha, Rais Sekou Toure alipokelewa kwa heshima zote na wenyeji wake na alivutiwa sana na mila na tamaduni za kabila la Wamasai, na baada ya ziara yake Rais huyo aliamua kulipa fadhila kwa jamii hiyo.
  Mkuu huyo wa nchi ndogo ya Afrika Magharibi aliomba apatiwe mtoto mmoja wa Kimasai kwa nia ya kwenda kumlea na kumsomesha nchini kwake.
  Mchakato wa kumtafuta mtoto huyo ulianza mara moja. Walitafutwa wanafunzi waliokuwa wanasoma katika shule mbalimbali za Umasaini na kupewa mtihani ambapo Salash aliibuka kidedea na kumfanya achaguliwe kwenda kuishi nchini Guinea .
  Mtihani wa mchujo kutafuta mtoto wa kwenda nchini Guinea ulifanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Theresia lililopo katikati ya mji wa Arusha na ulihusisha watoto wa jamii ya wafugaji kutoka shule kadhaa za mkoa wa Arusha.
  “Watoto waliojitokeza kufanya mtihani huo walikuwa wengi kiasi na baada ya matokeo kutolewa mimi nilikuwa nimebahatika kuwa wa kwanza, na hivyo kupata nafasi hiyo”, alisema Salash katika mahojiano maalumu na Raia Mwema wiki iliyopita nyumbani kwake mjini Arusha.
  Mahojinao hayo yalifanyika baada ya Salash, ambaye sasa ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, kutangaza nia yake ya kutaka kugombea ubunge katika jimbo la Monduli ambalo kwa sasa mbunge wake ni Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa.
  Baada ya kufanikiwa kufaulu mtihani, taratibu za safari kwenda nchini Guinea ziliandaliwa na Serikali na mwaka 1964 aliondoka nchini akiwa chini ya usimamizi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo Nje wa Tanganyika wakati huo, Oscar Kambona (hayati) kwenda kuanza maisha mapya ya kuishi Ikulu.
  “Ilikuwa ni kitu cha ajabu kwangu kuondoka na kuacha familia yangu ya kifugaji na kupanda ndege nikisindikizwa na Waziri wa Mambo ya nje wakati huo, Oscar Kambona hadi Ikulu ya Conakry-Guinea” anakumbuka Salash.
  Salash, ambaye wakati huo alikuwa darasa la nne alipofika nchini Guinea alilazimika kurudia darasa la tatu, ili apate muda wa kujifunza Kifaransa —lugha kuu ya mawasiliano na kufundishia nchini humo.
  “Nilijifunza Kifaransa na nikakijua kuliko hata Kimasai” alisema Dk. Toure huku akicheka wakati wa mahojiano hayo na Raia Mwema.
  Baada ya kumaliza elimu ya sekondari nchini humo, alichaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha masuala ya tiba za binadamu —Institut Polytechnique G.A.N de Conakry ambapo alihitimu mwaka 1977 na kutunukiwa shahada kwanza ya utabibu.
  Anasema maisha katika Ikulu ya Conakry yalikuwa mazuri kiasi cha kuamini kuwa alikuwa ni mtoto wa kuzaliwa na Rais Sekou Toure.
  Alikulia na kusoma hadi kuwa daktari wa binadamu akiwa mikononi mwa mkuu huyo wa nchi akitumia ubini wa Toure katika vyeti vyake.
  “Wakati wa likizo tulikuwa tunapelekwa nchi mbalimbali kwenda kupumzika. Kusema kweli robo tatu ya Ikulu za nchi za Kiafrika nimefika aidha wakati wa likizo ama wakati wa ziara ya Rais”, anakumbukia Dk. Toure.
  Dk.Toure anaongeza: “Katika kipindi hicho pia nilipata nafasi ya kukutana na viongozi mashuhuri duniani kama Mao Tse Dong wa China, Rais Tito wa Yugoslavia, na marais wengi tu wa nchi za Kiafrika waliokuja kuitembelea Guinea wakati huo kwa ziara za kiserikali”.
  “Baada ya kumaliza mafunzo na kuwa daktari kamili wa tiba ya binadamu, nilifanya kazi katika hospitali kuu ya serikali mjini Conakry hadi mwaka 1981 ambapo Rais Toure aliniruhusu nirudi nyumbani nikatumikie Taifa langu”, alieleza mganga huyo.
  Tangu mwaka 1981 baada ya kurudi nchini, Dk. Toure, kwa vipindi tofauti, amefanya kazi katika hospitali mbalimbali hapa nchini ikiwemo Muhimbili, Wizara ya Afya, Hospitali ya Wilaya Monduli, Hospitali ya Mkoa wa Manyara na Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.
  Lakini sasa anataka kuwatumikia zaidi wananchi wa jimbo lake la Monduli kama mbunge wao iwapo atashinda mchakato wa kura za maoni ndani ya chama chake cha CCM, na baadaye katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
  “Nimeweka nia ya dhati ya kuwa mwakilishi wa wananchi wangu wa Monduli katika Bunge la mwaka ujao….hii itanipa fursa ya kushiriki kikamilifui katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii na pia kurudisha mshikamano miongoni mwa wananchi wa jimbo hilo”, alisema.
  Jimbo hilo kwa sasa linawakilishwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa ambaye ameliongoza tangu mwaka 1995. Katika chaguzi zote alipita bila kupingwa. DK.Toure anakuwa mwanachama wa pili wa CCM kutangaza kuchuana na Lowassa katika jimbo hilo. Wa kwanza ni aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana, Daniel Porokwa ambaye alitangaza kuwania ubunge wa jimbo hilo mapema mwezi uliopita.
  “Napenda kuchukua fursa hii kuwaambia wananchi wa jimbo la Monduli kuwa natarajia kugombea nafasi ya ubunge katika uchaguzi wa mwaka huu kupitia chama cha changu cha CCM”, alisema Dk. Toure wakati akitangaza nia yake hiyo hivi karibuni.
  Alisema lengo la kutangaza nia yake hiyo ni kuleta changamoto ya uongozi katika jimbo lake na pia kuwaunganisha wananchi kuwa na umoja kufuatia kuwepo kwa migogoro ya kisiasa ambayo imekuwa chanzo cha kuzorota kwa baadhi ya shughuli za maendeleo.
  “Tatizo kubwa la jimbo la Monduli ni kuwepo kwa migogoro ya kisiasa na viongozi kuwa na makundi ambayo pia yamewagawa wananchi wa kawaida, na hivyo hivyo kuzorotesha baadhi ya shughuli za maendeleo…..lengo langu ni kuwaunganisha kwanza wananchi na viongozi ili kuondoa tofauti na kushirikiana kwa pamoja kutekeleza miradi ya mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao”, alisema daktari huyo wa tiba.
  Alisema kihistoria wilaya ya Monduli ilikuwa mfano wa kuigwa katika miaka ya nyuma kutokana na kutoa viongozi ambao wamejenga taswira na heshima kubwa mbele ya jamii ya Watanzania akiwemo Waziri Mkuu wa zamani marehemu Edward Moringe Sokoine.
  “ Kama mnavyofahamu kipindi cha mtu yoyote kuwa mbunge ni miaka mitano kikatiba; hivyo basi muda wa miaka mitano umepita na kila Mtanzania sasa anayo haki ya kuwania nafasi hiyo ili kuwa mwakilishi wa wananchi wake”, aliongeza Dk.Toure.
  “Najua kazi iliyopo mbele yangu ni kubwa lakini nimejiandaa kikamilifu na wananchi wa Monduli ndiyo watakuwa wenye maamuzi ya mwisho kuamua nani awe mwakilishi wao bungeni”, alihitimisha Dk.Toure. Guinea ni nchi iliyoko Afrika Magharibi. Ilipata uhuru wake mwaka 1958 na ina ukubwa wa Kilomita za mraba 245,857 ikiwa na idadi ya watu wanaokadiriwa kufikia milioni 8,382,000 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2002 kutoka World Encyclopedia.
   
 2. Mag3

  Mag3 JF-Expert Member

  #2
  Apr 14, 2010
  Joined: May 31, 2008
  Messages: 9,094
  Likes Received: 6,187
  Trophy Points: 280

  Huu ni uwongo wa mchana, toka lini mbunge wa CCM akatetea maslahi ya waliomchagua. Watu makini na wenye uchungu wa kweli wanaikimbia CCM, yeye anakimbilia huko huko kufuata nini ? Yaani kapanda mbaazi anategemea kuvuna mpunga, ya rabi ! huo udaktari wake una mushkeli kweli kweli.
   
Loading...