Top Secret: Nyaraka Namba 12333 kutoka Whitehouse

Status
Not open for further replies.

Habibu B. Anga

Verified Member
May 7, 2013
6,656
2,000
"Deception is a state of mind and mind of the State."
- James Angleton
CIA Chief of Counterintelligence (1954 - 1975)

Alhamisi March 13, 1953 Washington D.C

"Put that away." Hiyo ndiyo ilikuwa sentesi ya kwanza Rais Dwight Eisenhower kuitamka mara baada ya kuingia ndani ya Oval Office katika makazi yake ya White house.

Alitamka maneno hayo mara baada ya kumuona moja ya wageni wake waliokuja ofisini kwake anatoa makaratasi kutoka kwenye briefcase.

Huu ulikuwa mtindo wa Rais Eisenhower pale anapotaka kuongea na mtu mambo ya siri nzito na akiwa hana mpango wa kuwashirikisha Baraza la Mawaziri au Baraza la Ulinzi.

Kikao hiki kilikuwa ni kikao cha siri kubwa na kilihusisha washiriki watatu tu. Rais Dwight Eisenhower na wageni wawili ambao walikuwa ni ndugu. Mtu na kaka yake.
Mmoja aliitwa John Foster Dulles ambaye alikuwa ni Waziri wa mambo ya nje wa Marekani na Wapili aliitwa Allen Dulles ambaye alikuwa ni Mkurugenzi wa Shirika ka kijasusi la Marekani, CIA.

Eisenhower alikuwa na utaratibu wa kutotaka kuwepo na aina yoyote ya nyaraka inaweza kuihusisha ofisi ya Rais pale ambapo akitaka kuamuru ifanyike jambo amblo alihisi linaweza lisiungwe mkono na jamii ya kimataifa. Na hii ndio ilikuwa sababu ya kumuamuru Allen Dulles arudishe makaratasi yake kwenye briefcase.

Wiki tatu zilizopita kilifanyika kikao kama hiki kati ya watatu hawa na katika kikao hicho walizungumza juu ya changamoto kubwa iliyokuwa mbele yao.
Changamoto yenyewe ilikuwa ni Mohammad Mosaddegh, Waziri Mkuu wa Iran.

Miaka miwili iliyopita serikali ya uingereza walituma ombi Marekani kuwaomba wawasaidie kuandaa mpango kumuondoa madarakani Waziri Mkuu Mosaddegh mara baada ya kufanikiwa kushinda uchaguzi wa mwaka 1951. Kipindi hicho Rais wa Marekani alikuwa na Harry Truman na akakataa kuihusisha marekani katika suala hilo.

Baada ya Rais Truman kuondoka madarakani na Dwight Eisenhower kuchukua madaraka, Serikali ya Uingereza chini ya waziri mkuu Winston Churchhill wakajaribu tena kushawishi serikali mpya ya Marekani kuwaunga mkono kumuondoa madarakani Waziri Mkuu Mosaddegh.

Wasiwasi mkubwa wa Uingereza dhidi ya Mosaddegh ulikiwa ni mwenendo wa wake dhidi ya kampuni za kimagharibi na hasa hasa namna ambavyo aliiandama kamupuni ya AIOC (Anglo-Persian Oil Company (kwasasa kampuni hii ni sehemu ya kampuni ya BP)).

Kampuni hii ambayo ilikuwa inamilikiwa kwa pamoja kati ya serikali ya Uingereza na serikali ya Iran. Lakini kwa mujibu wa mkataba mapato yote yalikuwa yanaenda kwa serikali ya uingereza na serikali ya Iran ingeanza kupewa mapato mara tu kampuni ikianza "kujiendesha kwa faida" ambapo serikali ya Iran itapatiwa 16% ya mapato.

Lakini kwa miaka yote Waingereza walihakikisha rekodi za kampuni zinaonyesha kuwa kampuni inaendeshwa kwa hasara ili wasiwe wanalipa 16% kwa serikali ya Iran.

Baada ya Waziri Mkuu Mohammad Mosaddegh kushinda uchaguzi mkuu wa kwanza wa kidemokrasia nchini humo mwaka 1953 akatoa pendekezo kuwa vitabu vya uhasibu vya kampuni ya AIOC vifanyiwe ukaguzi kujiridhisha kama kweli kampuni inaendeshwa kwa harasa. Waingereza wakakataa.

Mosaddegh akatoa ofa nyingine kuwa mkataba uandikwe upya na uwape serikali zote mbili umiliki wa 50/50 wa kampuni ya AIOC. Waingereza wakakataa pia.

Ikumbukwe kuwa kutokana na mkataba huo visima vyote vya mafuta ndani ya nchi ya Iran vilikuwa chini ya kampuni ya AIOC.

Katika kipindi hiki Iran ilikuwa ni moja ya nchi masikini zaidi duniani.
Hii ilimaanisha kuwa wananchi wa Iran walikuwa wanaishi kwenye moja ya nchi yenye utajiri mkubwa wa mafuta lakini wenyewe wapo kwenye lindi la umasikini.

Ndipo hapa ambapo baada ya juhudi zake zote za kwanza kuleta uwiano juu ya unufaikaji wa mapato ya kampuni ya AIOC kushindikana, Waziri Mkuu Mosaddegh akapeleka muswada bungeni wa kuitaifisha kampuni ya AIOC.

Hapa ndipo akaamsha hasira za Uingereza na wakaweka nia kwamba ni lazima Mosaddegh aondoke madarakani. Kikwazo kikubwa kilikuwa ni kwamba Mossadegh alikuwa amechaguliwa kidemokrasia kwa kupigiwa kura na alikuwa anakubalika mno na wananchi wa Iran.

Ndipo hapa wakaona umuhimu wa kuwaomba 'kaka zao' wamarekani wawasaidie kutimiza amza yao.
Kipindi Marekani ilikuwa iko kwenye vita nchini Korea na Uingereza ilikuwa inawaunga mkono katika vita hiyo kwa kuchangia wanajeshi. Hivyo Uingereza waliamni ombi lao hili kwa Marekani litapata kibali safari hii.

Turejee kwenye kikao Whitehouse..

Wiki tatu nyuma katika kikao chao cha kwanza Rais Eisenhower alikuwa amewapa 'homework' wakaandae mkakati ambao watakuja kuuwasilisha leo hii.

Ndipo hapa ambapo Mkurugenzi wa CIA Allan Dulles akaanza kumpa mkakati alioufikiria.

Kwanza akaanza kumpa tahadhari kadhaa za kuzingatia kuhusu mpangi ambao watauweka.

- mpango huo ni vyema usijadiliwe kwenye Baraza la Mawaziri au Baraza la Usalama wa Taifa, kwasababu lazima utazua mtafaruku mkubwa kwasababu ni dhahiri baadhi ya watu wataupinga.

- pia kama ni watu wachache wataufahamu hii ina maana uwezekano wa siri kuvuja utakuwa ni mdogo.

- Pia Allan Dulles akashauri ni lazima oparesheni hii itekelezwa pasipo watu kujua kuna uhusika wa marekani ili kufanya wananchi wa marekani kukubaliana na serikali mpya itakayo wekwa kama ikitokea oparwsheni ikafanikiwa.

Kwa kuzingatia hayo basi, Allan Dulles akamshauri Rais Eisenhower atumie mamlaka yake aliyopewa na sheria ya usalama wa taifa ya mwaka 1947 (U.S. National Security Act, 1947), kuidhinisha operation ya usiri mkubwa zaidi (Covert operation) kumpindua Rais Mohammad Mosaddegh.

Sheria hii inampa mamlaka Rais wa Marekani kuamuru kufanyika kwa "covert operation" pasipo kumuweka Rais kutambuliwa uhusika wake kwenye hilo ikitokea siri ya operation hiyo imevuja.

Kwa maneno mengine Sheria hii inampa uwezo Rais kukana kuhusika kuamuru oparesheni kufanyika au kufahamu chochote juu ya kufanyika kw oparesheni hiyo ikitokea siri imevuja kuhusu oparesheni hiyo. Hii ndio inajulikana kama 'Plausible Denialbility'.

Kwahiyo; kwa kuzingatia vigezo vyote hivi ambavyo Allan Dulles mkurugenzi wa CIA aliviainisha, akawaeleza Rais Eisenhower na kaka yake John Dulles waziri wa mambo ya nje kuwa ni idara moja tu katika vyombo vyote vya ulinzi na usalama ndani ya Marwkeani yenye weledi, uwezo, watu, ufanisi na ruhusa ya kisheria kutekeleza mkakati wa dizaini hii.

Idara hiyo ni kitengo maalumu ndani ya CIA kinachojulikana kama SAD (Special activities Divisio).
Special Activities Division ni kitu gani??Kutokana kuongezeka kwa changamoto za kimataifa , ambazo nyingine zinatishia usalama au maslahi ya mrekani lakini marekani haiwezi kuchukua hatua zozote kutokana kujiepusha na lawama kutoka jamii ya kimataifa ndipo hapo ikaonekana kuna umuhimu wa kuwa na kitengo maalumu kwa ajili ya suala hili.

Ndipo hapa ambapo serikali ya marekani ikaagiza shirika la kijasusi la CIA kuanzisha kitengo maalumu ndani yake ambacho kitakuwa na maafisa (wanajeshi) ambao wanaweza kutekeleza oparesheni yoyote ya kijeshi kwa kujitegemea pasipo kuhusisha serikali ya marekani.

CIA wakaanzisha idara maalumu ndani yake na kuuita Special Activities Division au kwa kifupi SAD ambayo idara yenyewe ilikuwa na maafisa wa siri ambao hawabebi vitambulisho na majina yao ni siri kubwa hayawezi kupatikana hata kwenye orodha ya maafisa wa CIA.

Lengo kubwa la kuanzishwa kwa idara hii ni kutekeleza oparesheni maalumu za kijeshi au proaganda na iikitokea wakakamatwa au kushitukiwa basi serikali ya marekani wanawakana kuwa si maafisa wao.

Kwahiyo kitengo hiki kilikuwa kinafanya kazi kwa niaba ya serikali ya marekani lakini kulikuwa hakuna uwezekano wowote wa adui kuunganisha uhusika wa kikosi hiki na serkali ya marekani.

Ndani ya Idara hii ya SAD kuna vitengo vidogo viwili;

Kitengo cha kwanza kinaitwa Political Action Group: kitengo hiki kazi yake kubwa ni kufanya ushawishi wa kisiasa (political influence), oparesheni za kisaikolojia (psychological operations) na vita za kiuchumi (Economic Warfares). Pia kutokana na maendeleo ya kiteknolojia, kitengo hiki kimeongezewa jukumu la vita za kimtandao (cyberwarfares).

Tuchukulie kwa mfano; katika nchi fulani kuna serikali au mwenendo wa serikalin unatishia maslahi ya Marekani basi kitengo hiki kinaingia kwa siri kubwa na kufanya mojawapo ya mambo ambayo nimeyaorodhesha hapo juu.

Moja ya matukio ambayo kitengo hiki kimehusika sana na CIA wamekiri kwenye nyaraka zilizowekwa wazi mwaka 2013 ilikuwa ni kueneza propaganda ambayo ilichangia kupinduliwa kwa Rais wa Iran mwaka 1953 ambapo kisa hiki nitakieleza kwa kina katika makala hii.

Pia kitengo hiki kilitumika kuzuia chama cha kikomunisti cha Italia kushinda uchaguzi mwaka 1960.

Pia kitengo hiki kimewahi kufanya oparesheni ya siri iliyoitwa Operation Mockingbird katika taifa la marekani. Oparesheni hii ilikuwa na lengo la 'kucontrol' habari zinazoandikwa na Vyombo vya habari nchini humo.
Oparesheni hii imekuja kupingwa vikali siku za karibuni na baraza la seneti kwa kuwa sheria hairuhusi CIA kufanya oparesheni yeyote ndani ya ardhi ya marekani.


Kitengo cha Pili kinaitwa Special Oparatins Group (SAG); na kazi yake ni kama ifuatavyo;

Kitengo hiki kinajumuisha wanajeshi wenye weledi wa hali ya juu kutekeleza malengo ya kivita pasipo kujulikana uhusika wa serikali ya marekani.

Ili kulinda utambulisho wao, wanajeshi wa kikosi hiki maalumu hawavai sare za jeshi wala kubeba vitambulisho.

Inaelezwa kuwa hiki ndio kikosi maalumu cha oparesheni za kijeshi chenye usiri mkubwa nchini marekani.

Maafisa wa kitengo hiki wanapatikanaje??

Maafisa wote wanaojiunga katika kitengo hiki maalumu cha SAD wanachaguliwa kutoka katika vikosi vingine vya weledi vya jeshi la marekani mfano Army Rangers, Combat controllers, Delta Force, 24TH STS, US Army Special Forces, SEALs, Force Recon n.k.

Wakishakuchaguliwa wanapelekwa katika kituo maalumu cha mafunzo ya CIA kilichopo Virginia kinachojulikana kama Camp Peary (au maarufu kama 'The Farm') ambapo miezi 18 ya kwanza wanafundisha kuhusu intelijensia na ushushushu.

Baada ya miezi 18 hiyo wanapelekwa kwenye kituo kingine cha CIA kilichopo California ambacho kinajulikana kama 'The Point'.
Hapa wanafundishwa mafunzo ya hali ya juu ya kijeshi ambayo hayapatikani kwa kiwango hicho katika vikosi vingine vya marekani.

Mfano wanafundishwa; mapigano ya ana kwa ana ya kiwango cha juu zaidi (special hand to hand combat), kutumia karibia aina zote za silaha na milipuko ya jeshi la marekani na nchi za kigeni, ufuatiliaji adui (tracking), Kukabiliana na hali ngumu kwenye mazingira ya kawaida na nyikani ( extreme survival and wilderness train ing), Kumkwepa aduia, kuzuia adui na kutoroka adui (evasion, Resistance and escape - SERE) na pamoja na mafunzo hayo anaongezewa kozi maalumu ya kutambua fiziolojia ya binadamu (Udaktari).

Afisa ambaye anafuzu mafunzo haya kwa muda wa miezi 36 anakabidhiwa katika idara ya SAD ndani ya CIA na anatambulika kama "Afisa Mwenye Mbinu Maalumu" (Specialized Skills Officer).

Katika oparesheni zao maafisa hawa huwa wanazitekeleza katika vikundi vya watu wachache sana wasiozidi sita na oparesheni nyingine zinatekelezwa na Afisa mmoja pekee.

Katika Ofisi za CIA zilizopo kitongoji cha Langley jijini Virginia kuna ukuta wa majina ya Maafisa wa CIA waliotunikiwa tuzo za heshima kutoka na utumishi wao uliotukuka ( Distinguished Intelligance Cross na Intelligence Star). Majina ya maafisa wengi kwenye ukuta huo ni ya wale waliotumikia kitengo cha SAD ndani ya CIA.


Kwa kuzingatia kwamba makala hii inalenga kuzungumzia uhusika wa CIA katika mapinduzi ya serikali ya Iran. Hivyo basi nitatoa mifano michache sana ya oparesheni zilizotekelezwa na kitengo hiki cha SAD ndani ya CIA. Nitaeleza kwa ufupi ili tusitoke nje ya lengo kuu (mapinduzi ya Iran).

Ni idara hii maalumu ya CIA ambayo ilikabidhiwa raia wanne wa Tibet kutoka kwa kaka mkubwa wa kiongozi wa kiroho wa Tibet Mtukufu Dalai Lama ambapo idara ya SAD iliwapa mafunzo ya kikomando watibeti hao kisha wakawarudisha Tibet kutafuta raia wengine 300 ambao SAD iliwapa mafunzo ya kijeshi kwa siri katika kisiwa cha Saipan na mwezi oktoba SAD ikawaongoza wanajeshi hawa mpaka Tibet kuanzisha vuguvugi la kudai kujitenga na China.

Pia ni kikosi maalumu hiki cha idara ya SAD ambacho kilimtorosha kwa siri mtukufu Dalai Lama kwa kupita katikati ya majeshi ya China yaliyokuwa mpakani na kumpeleka India.
Mpaka leo haijulikani ni namna gani waliweza kufanya tukio hili.

Ni idara hii ya SAD ndani ya CIA ambayo ilihusika kuwapatia mafunzo ya kijeshi raia wa Cuba waliokuwa wanaishi uhamishoni na kuwaongoza katika jaribio la kumpindua Fidel Castro. Mapigano haya yakihistoria yalidumu kwa siku tatu na yanajulikana kwa jina maarufu la 'Bay Of Pigs Invasion'.
Jaribio hili la mapinduzi halikuwezekana na ndilo lililochangia kudorara kwa mahusiano kati ya Marekani na Cuba mpaka leo hii.

Kwa mujibu wa nyaraka za siri za CIA zikizowekwa wazi mwaka 2004. Amri ya kumpiga risasi Che Guevara katikakati mwa miaka ya 1960 ilitoka kwa makomado wa SAD.

Ilikuwaje; Jeshi la msituni lililojiita Jeshi la Ukombozi la Bolivia (National Liberation Army of Bolivia) lilianzisha vita dhidi ya serikali ya Bolivia ambayo ilikuwa inaungwa mkono na Marekani. Jeshi hili likuwa na vifaa vya kisasa na liliungwa mkono na mwanamapinduzi Che Guevara.

Katika hatua za mwanzo za mapigano jeshi hili la waasi lilionekana kushinda dhidi ya majeshi ya serikali.
Ndipo hapo CIA wakatuma makomando wa kitengo cha SAD ambao walienda kutoa mafunzo kwa majeshi ya Bolivia katika milima Camiri. Na baada ya hapo wakawaongoza kupigana na waasi na kufanikiwa kuwashinda. Kisha makomando wa SAD wakawaongoza makomando wa jeshi la Bolivia (Bolivia Special Forces) kumkamata Che Guevara ambapo Mara tu baada ya kukamatwa komando wa SAD aliyeitwa Felix Rodriguez akaamuru auwawe.

Hii ni mifano michache kati ya mifano mingi amabayo CIA kwa kutumia kitengo cha SAD wameendesha opesheni maalumu za kijeshi katika nchi nyingi.

Ingawa Rais wa marekani ndiye anayetoa amri ya kufanyika kwa operesheni hizi za kuvamia kijeshi nchi nyingine au kuongoza mapinduzi ya serikali halali duniani kote lakini analindwa na sheria ya Marekani ambayo inampa Rais uwezo wa kukana uhusika wa Rais wa marekani kutoa amri au kufahamu kinachofanywa na kitengo hiki. (Plausible Deniability).

Sheria hii ilitingwa mwaka 1947 inajulikana kama National Security Act. Pia Sheria hii ilitiliwa mkazo na tamko la rais namba 12333 (Executive Order 12333) lenye kichwa cha habari National Intelligence Activities.


Kikaoni Whitehouse..

Rais Eisenhower akakubaliana na mapendekezo ya Mkurugenzi wa CIA Allan Dulles na kumtaka awasiliane na wenzao Idara ya Ujasusi ya Uinhereza MI6 na waanze mikakati Mara moja pasipo kuchelewa.

Lakini kabla hatujazungumza zaidi kuhusu Oparesheni ya kijasusi iloyofuata ambayo ilitekelezwa na Maafisa wa CIA Idara ya SAD ni vyema kujiuliza. Iliwezekana vipi kwa Uingireza kujimilikisha visima vyote vya mafuta nchini Iran.??

Ili kulielewa swali hili ni vyema kuangalia historia ifuatayo kwa ufupi sana..

Miaka ta nyuma, yaani karne ya 18 hadi mwishoni mwa Karne ya 20 Iran ilikuwa inatumia mfumo wa uongozi ambapo viongozi wa juu kabisa wa nchi walitoka katika koo moja (Dynasty) na aliyekuwa na madaraka ya juu kabisa cheo chake kiliitwa 'Shah'. Cheo hiki kilikuwa ni sawa sawa kabisa na cheo cha mfalme katika nchi nyingine.

Mwaka 1901 Shah aliyekuwa anatawala aliitwa Mozzafar al-Din Shah Qajar kutoka koo ya Qajar (Qajar Dynasty). Kipindi Iran bado ilikuwa ni nchi masikini sana na hakukuwa na uzalishaji mkubwa wa mafuta.

Mwaka huo kuna shushushu wa Uingereza aliyeitwa William Knox D'Arcy alifunga safari mpaka nchini Iran kukutana na Shah.

Bw. D'Arcy alijitambulisha kama mwekezaji na alienda na ofa kwa ajili ya Shah. Waingereza walisikoa taarifa kuhusu matamanio ya Shah kutembelea nchi za Ulaya lakini kikwazo chake kikubwa ilikuwa ni uwezo mdogo wa nchi hiyo kugharamia safari hiyo kubwa kwa kiongozi wa nchi na msafara wake.

Hivyo basi D'Arcy alimueleza Shah wa Iran kuwa yeye kama mwekezaji anauwezo wa kugharamia Safari ya Shah pamoja na msafara wake kwenye nchi zote muhimu barani Ulaya ambazo Shah angependa kuzitembelea na akamuahidi kuwa atahakikisha safari hiyo ya Shah inakuwa ni ya kifahari kuakisi cheo chake cha Shah na atatumia ushawishibwake kuhakikisha kuwa kila nchi ambayo Shah ataitembelea basi atapewa mapokezi ya kitaifa kwa kulakiwa na viongozi wa juu kabisa wa nchi husika. Na akamueleza kuwa ametenga kiasi cha Paundi za Uingereza elfu 20 (sawa na Paundi Milioni 10 kwa viwango vya sasa) kwa ajili ya Safari hiyo ya Shah.

Alipoulizwa atahitaji nini kwa kugharamia Safari hiyo ya Shah, akamjibu kuwa anahitaji wampe kibali cha Kutafuta Mafuta katika pwani za bahari pamoja na baharini kwenye kina kirefu.

Na endapo mafuta yakipatikana basi ataleta wataalamu pamoja vitendea kazi ili kuanza shughuli za uchimbaji.

Ndipo hapa ambapo alifanikiwa kumsainisha Shah mkataba ambao unaipa Iran 16% ya faida (pindi kampuni "ikianza kutengeneza faida).

Miezi michache iliyofuata kwa kugharamiwa na shushushu D'Arcy, Mozzafar al-Din Shah Qajar alifanya ziara ya kifahari katika nchi za Ulaya na kukata kiu yake ya miaka mingi.

Baada ya kurejea Iran D'Arcy akaingia na watu wake na mitambo na kuanza kutafuta mafuta katika kina kirefu cha bahari ya Iran.

Si miezi mingi wakagundua kowango kikubwa cha mafuta kwenye kina kirefu na baadae mitambo mizito ya uchimbaji mafuta pamoja na wataalamu wakapelekwa Iran na kazi ya uchimbaji ikaanza.

Siku si nyingi Bw. D'Arcy "akauza" hisa zake zote kwa kampuni ya Kiingereza ya Burmah Oil Company.
Mwaka 1908 hisa zote za Burmah Oil Company nchini Iran "zikanunuliwa" na serikali ya Uingereza na ndipo hapo ikaundwa kampuni mpya ya kiserikali AIOC (Anglo-Iran Oil Company).

Mwaka 1923 Mozzafar al-Din Shah Qajar alifariki na nafasi yake akarithiwa na mtoto wake Ahmad Shah Qajar.
Tofauti na baba yake aliyekuwa ni nguli wa siasa na utawali, Ahmad Shah Qajar alikuwa ni mtu dhaifu na muoga.

Hii ilimfanya apelekeshwe na wanasiasa wakongwe nchini Iran pia alishindwa kustahimili malalamiko ya wananchi kwani ilikuwa kila wananchi walipo lalamika kihusu chochote alikitekeleza.

Mojawapo ya masuala makubwa aliyo yafanya ilikuwa ni kubadili mfumo wa uongozi wa nchi hiyo.
Wananchi walikuwa wanalalamika juu ya ukoo mmoja tu kuongoza nchi na walitaka kama mfumo huo unaendelea basi kuwa na namna ambayo kutakuwa na chombo na viongozi wengine wa kusimamia shugjuli za kiserikali.

Ndipo hapa Shah mpya akaanzisha mfumo wa Majlis.
Majlis lilijuwa ni baraza la Bunge la Iran lililoundwa na Wabunge waliochaguliwa na wananchi.

Pia kwa mujibu wa mfumo huu, wabunge hao walimpigia kura mbunge mwenzao mmoja ambaye anakuwa Waziri Mkuu ambaye ndiye aliongoza shughuli za kila siku za serikali lakini Shah alibakia kuwa kiongozi mwenye mamlaka makuu ya nchi.

Kitendo hiki kilikuwa ni suala chanya kwa siasa za kidemokrasia nchini Iran lakini hakikuwapendeza waingereza kwani walimuhisi Shah mpya kama kiongozi dhaifu.

Pia waingereza hawakupenda mfumo huu mpya wa bunge la Majlis kwani kulianza kuliizwa maswali kuhusu mikataba ya uchimbaji mafuta nchini humo.

Waingereza wakaingiza maafisa wao wa ujasusi na wakaanza npango wa kushawishi na kuwahonga wabunge wa Bunge la Majlis wamuondoe madarakani Waziri Mkuu aliye chaguliwa na Shah na kumuingiza madarakani mwanasiasa machacjari aliyeitwa Reza Khan.

Mpango huu ulifanikiwa na mwaka 1925 Waziri Mkuu wa kwanza wa Iran akaondolewa madarakani na kuingizwa madarakani waziri Mkuu mpya Reza Khan.

Kitendo hiki pia kilimchukiza Ahmad Shah Qajar na kukaanza kutokea sintogahamu ya chini kwa chini kati yake na serikali ya Uingereza.
Wanasema ukidharau mwiba mguu huota tende, na Waingereza hawakutaka madhara yatokee waanze kujilaumu baadae hivyo wakaanzisha mpango wa kumuondoa Shah katika kiti cha Ufalme.

Wakamtumia Waziri Mkuu mpya waliyemuingiza Bw. Reza Khan kulishawishi Binge la Majlis kumpigia kura ya kumuondoa kwenye kiti cha ufalme Ahmad Shah Qajar.

Mpango huu ukafanikiwa na Ahmad akaondokeqa kwenye Ufalme na Waziri Mkuu mpya Bw. Reza Khan akajivika yeye cheo hicho na kuwa Reza Khan Shah Pahlavi.

Huu ndio ukawa mwisho wa koo ya Qajar (Qajar Dynasty) kukalia kiti cha kifalme cha Shah na mwanzo wa koo ya Pahlavi (Pahlavi Dynasty) kukalia kiti hicho cha Shah.

Mwanzoni mwa utawala wake Reza Khan Shah Pahlavi akipendwa sana na wananchi kwani kwa kushirikiana na serikali ya Uingereza alifanya Nazi kubwa ya kuboresha huduma za kijamii.

Lakini kadiri siku zilivyo songa Shah Pahlavi alibadilika na kuwa zaidi ya mfalme, alianza kuwa na chembe chembe za udikteta.

Hakuwa mtu mwenye kusikiliza maoni ya Bunge lake la Majlis na aliukandamiza upande wa Upinzani kwa mabavu makubwa. Watu wote ambao walipingana nao walitiwa gerezani na wengine kuuwawa.

Katika miaka ya kati kati vugu vugu la upinzani lilikuwa limepamba moto na hoja kubwa ilikuwa ni kuishinikiza serikali ijiondoe kwenye mikataba kandamizi ya uchimbaji mafuta kati yake na serikali ya Uingereza.

Moja ya vinara wa vugu vugu hili alikuwa ni kijana aliyeitwa Mohammad Mosaddegh.
Kijana huyu alijitengenezea umaarufu mkubwa kutokana na uwezo wake wa kujenga hoja na kuliteyea taifa la Iran.

Shah Pahlavi aliona tishio la kijana huyu Mosaddegh na mwaka 1940 akamtupa gerezani.

Mwaka 1941 Reza Khan Shah Pahlavi akarothiwa kiti cha Ufalme na mtoto wake wa kiume kijana wa miaka 22 aliyeitwa Mohammad Reza Khan.

Baada ya kuchukua madaraka Mohammad Reza Shah Pahlavi pia kama watoto wengine wengi wanaorithi Ufalme hakuwa na kiongozi imara kama baba yake Reza Khan. Lakini Uingereza walimpenda kwakuwa alikuwa kibaraka wao aliyefanya kila kitu walichohitaji.

Baada ya upande wa upinzani kugundua udhaifu wa Shah mpya, wakarudisha tena vugu vugu lao.
Kwanza kabisa wakaanza kumshinikiza Shah mpya awaachilie wafungwa wa kisiasa waliofungwa na baba yake.

Mohammad Shah Pahlavi kutokana na uchanga wake wa kiuongozi akafanya 'kosa' kubwa la kuwaachia wafungwa wa kisiasa akiwepo Mohammad Mosaddegh.

Mara tu baada ya Mosaddegh kuachiliwa gerezani akaanzisha tena vugu vugu la kudai visima vya mafuta viwe chini ya Iran peke yake pasipo umiliki wa pamoja na serikali ya Uingereza.

Ili kufanikisha lengo hili, Mohammad Mossadegh aliviunganisha vyama vyote vya upinzani na kuunda 'Ukawa' yao iliyoitwa National Front.
Hoja yao kuu ikiwa ni kurudisha visima vya mafuta kwa taifa la Iran kutoka kwa wanyojani.

Mtaani kulikuwa na kikundi kilichojiita Fadaiyan e-Islam ambacho kiliongozwa Ayatollah Kashani (huyu ndiye mlezi wa kiroho wa Ayatollah Khomeini aliyekuja kuwa kiongozi Mkuu wa kiroho wa Iran (Iran Supreme Leader)).
Kikundi hiki kilimuunga mkono Mosaddegh wakimuona ni mzalendo.

Wakaenda mbali zaidi na kufanya shambulizi lililomuua Waziri Mkuu wa kipindi hicho aliyeitwa Haj Ali Razmara.

Hii ikapelekea kuitishwa upya kwa uchaguzi mkuu mwaka 1951. Mosaddegh na 'Ukawa' yake ya National Fron wakashiriki na kupata ushindi wa kishindo kwa kuingiza wabunge wengi kwenye Bunge la Majlis.

Baadae Bunge likapiga kura kumchagua Mohammad Mosaddegh.

Hii inaitwa, "usiyempenda kaja".
Mohammad Mosaddegg mpinzani anayechukiwa zaidi na Shah wa Iran na mwanasiasa mwenye Sera zinazopingwa vikali na Uingereza sasa ndio Waziri Mkuu wa Iran.

Haikumchukua mda mrefu baada ya kuapishwa akaanza 'kuwasomesha namba'.

Kwanza akaanza na Shah. Akapeleka Bungeni hoja kwamba Shah apunguziwe madaraka kwani hakuna maana katika nchi ya kidemokrasia kuwe na "mfalme mwenye mamlaka". Hoja yake aliwaeleza kwamba anataka Shah abakie lakini cheo chake kiwe ni alama tu (Ceremonial) lakini asiwe na mamlaka ya kuamuru uendeshaji wa serikali.

Mwenyewe Mosaddegh katika waraka aliouwalisha bungeni alitumia sentesi tamu zaidi, "Shah anatakiwa kutawala, lakini sio kuwa na malaka" ("reign, but not rule")
Bunge likakubaliana na hoja hiyo. Mohammad Shah Pahlavi akaondolewa madaraka yote ya kiserikali, akabakishwa kama Picha ya kikaragosi, mtawala asiye na mamlaka. Mamlaka yote ya kiserikali yakaamishiwa kwa Waziri Mkuu.

Baada ya kumsomesha namba Shah kwa uzuri kabisa akawageukia wazungu wa Uingereza. Tena akataka kuwasomesha namba kwa staha na ustaarabu kabisa.

Akawapa 'ofa' kuwa hataki kuwanyang'anya visima bali anawaomba waboreshe mikataba.
Kwanza kabisa akataka mgawanyo wa fedha usiwe kwenye "faida" pekee bali mgawanyo uhusu mapato yote. Pia akawaambia si sahihi wao wenye mafuta wapewe asilimia kiduchu (16%) hivyo akapendekeza iwe 50%.

Waingereza wakakataa kataka kata.
Mosaddegh hakuangaika nao, wanasema "ukisusa wenzio twala".
Akapeleka muswada bungeni wa kutaifisha visima vyote vya mafuta nchini Iran.

Waingereza wakashikwa na bumbuwazi, bumbuwazi likageuka kihoro, kihoro kikazaa chuki na vichwani mwao likatawala wazo moja tu. Mohammad Mosaddegh lazima ang'oke madarakani.

Lakini huyu alikuwa ni "heavyweight" tofauti na viongozi wengine wa Iran waliofanikiwa kuwang'oa.
Nchi nzima nzima mpaka ngamia walimuunga mkono Mosaddegh. Hata wakundi ambayo ilikuwa ni ngumu kwao kuunga mkono wanasiasa kwa mfano kikundi cha msimamo mkali cha Fadaiyan e-Islam na kiongozi wao Ayatollah walimuunga mkono Mosaddegh.

Mosaddegh alionekana ni shujaa wa Taifa. Mosaddegh alionekana ni "Musa" mwenye maono wa kuipeleka Iran kwenye "maziwa na asali".

Uingereza wakang'amua mapema 'ligi' hii hawaiwezi.. Hili ni zigo ambalo hakuna 'mnyamwezi' wao wowote mwenye uwezo wa kuliinua, au kama ni fupa bado hajazaliwa fisi uingere,a mwenye uwezo wa kuliuma.

Ni hapa wakaona umuhimu wa kuwageukia na kuomba msaada kwa 'kaka zao' na maswahiba wao U.S.A. wazee wa "fitna za daraja la kwanza".

Walichowaahidi ni kuendelea kuwaunga mkono kwenye vita vya Korea. Pia wakawaonyesha data za 'reserve' za mafuta chini ya bahari ya Iran na wakawaahidi kuyaruhusu makampuni ya kimarekani kwenda kumiliki baadhi ya visima vipya vya mafuta.

Ndio hii inatupeleka kwenye kikao cha tarehe 13 march 1953 ndani ya Oval Office, whitehouse. Kikaoni kati Rais Eisenhower, waziri wa mambo ya nje John Dulles na Mkurugenzi wa CIA Allan Dulles.

Ambapo Rais akatoa agizo CIA kuandaa mpango kabambe wa kumuondoa madarakani Mohammad Mosaddegh.

Na CIA kupitia Idara yake maalumu ya SAD ikaja na mpango mwanana kabisa…
TPAJAX PROJECT (OPERATION AJAX).

Ili kutekeleza agizo la Rais Eisenhower kuhakikisha serikali ya Iran inayoongozwa na Waziri Mkuu Mohammad Mosadegh inaondoka madarakani, CIA kupitia idara yake ya SAD (Special Activities Division) wakaja na mango kabambe waliouita TPAJAX PROJECT (au kwa jina linvine Operation Ajax).

Katika kipindi hiki kitengo maalumu cha SAD kilikuwa kinasimamiwa na Kermit Roosevelt Jr. (Mjukuu wa Rais wa zamani wa Marekani Theodore Roosevelt).

Hivyo basi Kermit akasafiri mpaka Iran kuungana na Donald Wilber shushushu wa CIA aliyepandikizwa Iran Siku nyingi nchini Iran akiwa kama Mwanaikolojia na mtafiti wa mambo ya kale yahusuyo milki ya Persia.

Katika kipindi hiki kikundi cha msimamo mkali cha Fadaiyan e-Islam kilikuwa kimeacha kumuunga mkono Mosaddegh kutokana na Waziri Mkuu huyo kushikilia msimamo wankutenganisha Dini na serikali.

Hivyo basi Mara baada ya Kermit kutua Iran kwa siri na kuungana na afisa mwenzake Wilber wakaenda kuonana na viongozi wa kikundi cha Fadaiyan e-Islam na kiongozi Mkuu wa kikundi kwa kipindi hiki alikuwa ni Mohammad Behbahani na kumueleza shida yao.

Kikundi cha Fadaiyan e-Islam kilokuwa na 'connection' nchi nzima na viongozi wa serikali za mitaa. Hivyo maafisa hawa wa CIA walimuomba Behbahani awasaidie kusambaza fedha kwa viongozi hao ili wasaidie kupotisha viongozi wanaowataka wao (CIA) katika uchaguzi mdofo wa wawaoilishi wa Bunge la Majlis utakaofanyika katikati ya mwaka huo.

CIA wakamuahidi Behbahani kuwa kama atashirikiana nao watahakikisha kuwa Waziri Mkuu Mosaddegh akiondoka madarakani, kiongozi atakayerithi cheo hicho anaifanya Iran kuwa nchi ya kiislamu rasmi na kutimiza matamanio ya kikundi cha Fadaiyan e-Islam.

Behbahani na wafuasi wake wa Fadaiyan e-Islam wakakubaliana na ombi hili na akaanza kazi ya kugawa fedha kwa siri nchi nzima kwa viongozi wa serikali za mitaa.

Wakati zoezi hilo linaendelea wakawasiliana na serikali ya Uingereza watume jeshi lao la Wana maji (Royal Navy) katika pwani ya Iran ili kuzuia njia kwa meli yoyote kutoka Iran iliyobena mafuta isitoke.

Uingereza ikatekeleza agizo hili kwa kusimamia kigezo kuwa, mafuta hayo yanamilikiwa na kampuni ya Ango-Iran Oil Company ambayo serikali ya uingereza ni mmiliki Mkuu wa kampuni. Kwahiyo kitendo cha Iran kuchimba mafuta hayo na kutaka kuyauza kilikuwa ni kiyendo cha "wizi".

Na hili kilifanikiwa, mafuta yalikuwa yanachimbwa lakini hayatoki ndani ya Iran kutokana na kuzibwa njia ya baharini na Royal Navy.

Taratibu uchumi ukaanza kutikisika na ajira zikaanza kuyeyuka kitokana na kutokuuzwa kwa mafuta kwenye soko la kimataifa.

Wakati haya yanafanyika maafisa wa CIA wakakutana na viongozi moja ya kikundi wapinzani wa Waziri Mkuu Mosaddegh, kilichoitwa Tudeh Party.
Hiki kilikuwa ni kikundi cha kikomunisti.

CIA wakawahonga kiasi kikubwa cha fedha na kuwaomba waache kumpinga Mosaddegh na badala yake waanze kumuunga mkono.
Wakapewa hela ya kutosha na wakabadili msimamo na kuanza "kumuunga" mkono Waziri Mkuu Mosaddegh.

Walianzisha maamndamani mitaani kumsifu Mosaddegh na kila Waziri Mkuu alipoitisha mikutano, maelfu ya wanachama wa Tudeh Party walijitokeza.

Hili lilimshangaza hata Mosaddegh mwenyewe kakini hakufikiria mbali, yeye alidhani kuwa labda sera zake zimewakuna wapinzanibwake hao na wameamua waanze kumuunga mkono.

Hakufahamu kuwa suala hili lilikuwa ni mkakati wa kipropaganda kumuangusha.

Ni kwamba; nchi ya Iran ina waisilamu wengi na wengi wao hawapendelei sera za kikomunisti kwa kuhisi kwamba ukomunisti una chembe chembe za kumpinga Mwenyezi Mungu.

Sasa kitendo cha Mosaddegh kutaifisha visima vya mafuta, zilianza kuenezwa propaganda na wapinzani wake kuwa anataka kuifanya Irani kuwa nchi ya kikomunisti. Wananchi walipuuza pripaganda hizi kwa kuwa walimuona Mosaddegh kama shujaa kurudisha visima vya mafuta kwa taifa la Iran.

Lakini kitendo cha Tudeh Party kumuunga mkono na Mosaddegh kushindwa kuwakemea au kujitenga nao, kikaanza kypandikiza hisia kwenye fikra za wananchi kuwa huenda ni kweli Mosaddegh anataka kuitumbukiza Iran kwenye ukomunisti.

Taharatuki ikazidi kuongezeka.
Mafuta hayauzwi.
Ajira zinayeyuka.
Mosadeggh anungwa mkono na makomunisti.

Balaa kubwa zaidi lililokuja kumuwehusha Mossadeggh ni baada ya matokeo ya uchaguzi wa Wawakilishi wa Bunge la Majlis kutangazwa. Chama chake kilikuwa kimeshindwa vibaya. (Kumbuka CIA waligawa fedha kwa kumtumia Behbahani kwa viongozi wengi wa serikali za mitaa wawapendelee wapinzani wa Mosaddegh).

Baada ya kikao cha kwanza cha Bunge jipya kuitishwa, vikaanza kuibuka hoja za kumpigia kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Mosaddegh.

Mosaddegh akalisitisha Binge kwa muda na kuitisha kura ya maoni kuomba wananchi wamruhusu kulivja Binge hilo.
Wananchi wakapiga kura lakini Mosaddegh akafanya kosa kubwa la kupika matokeo.

Alitangaza matokeo kwamba 99.9% ya wananchi wamekubali ombi lake la kuvunja Bunge. Hii ilikuwa tofauti kabisa na maoni halisi ya wananchi kwani wengi walitaka Bunge liendelee kuwepo ili limsimamie zaidi Mosaddegh kwani wameanza kukosa imani nae.

Kitendo cha kupika matokeo ya kura ya maoni na kulivunja Bunge na kubaki yeye pekee na baraza lake la mawaziri kuongoza nchi kilipingwa vikali wananchi na wengi walimuona kama amegeuka kuwa Dikteta.

Wapinzani wake wakaanza kuandamana mitaani na Mosaddegh akaamuru wakamatwe na kuswekwa rumande. Hii ilizidi kuchochea hasira za wananchi.

Wakati haya yote yanaendelea, mafisa wa CIA Kermit Roosevelt na Donald Wilber waliagiza makomando kutoka CIA kitengo cha SAD.
Makomando hawa wakachukua mamia ya vijana kutoka Tudeh Party na kuwaingiza kwenye msitu maeneo ya Abadan na kuwapa mafunzo ya kijeshi kwa siri kubwa.

Huko mtaani taharuki iliendelea kuwa kubwa zaidi, na umaarufu wa Waziri Mkuu Mosaddegh ulikuwa umeshuka kwa kiwango kikubwa na uhusiano wake na wananchi wake ulizorotota kupitiliza.

Mafuta yalikuwa hayauzwi kutokana na meli kuzuiwa zisitoke na Royal Navy.
Bunge la Majlis limevunjwa.
Wakomunisti wanamuunga mkono Waziri mkuu Mosaddegh.
Wapinzani wanatupwa gerezani.

Hapa ndipo ambapo CIA wakamuamuru kibaraka wao mtawala Shah Pahlavi kuingilia kati.

Ingawa Mosadeggh alikuwa amefanikiwa kulishawishi Bunge kumpunguzia madaraka Shah wa Iran lakini aliachiwa jukumu la kikatiba la kumuapisha Waziri Mkuu. Hii pia ilimpa uwezo wa kikatiba wa kumuondoa madarakani.

Ndipo hapa katika kipindi ambacho wananchi wengi wa Iran walitamani Mosaddegh kutoka madarakani, Mfalme Mohammad Reza Shah Pahlavi akaandika waraka wa kumuondoa madarakani Waziri Mkuu Mohammad Mosaddegh na kumteua Generali Fezlollah Zahedi.

Waraka huu alikabidhiwa Kanali wa Jeshi la mfalme aliyeitwa Nemattolah Nassiri. Na yeye mwenyewe mfalme akapanda ndege kwenda Uingereza akijua wazi kitakachofuata.
Baada ya kanali Nematollah kufika katika makazi ya Waziri mkuu na kumkabidhi waraka.
Mosaddegh akauchana mbele yake na kuamuru Kanali Nassiri awekwe rumande.

Sikh ya Tarehw 19 August 1953 CIA ikawachukua vijana waliokuwa wanapewa mafunzo ya siri msituni na kuwagawanya katika makundi mawili.

Kundi la kwanza liliingia mtaani asubuhi likiwa na sare za Tudeh Party na kutangaza kuwa linafanya mapinduzi ya kikomunisti kwa kumuunga mkono Waziri Mkuu Mosaddegh.

Walichokifanya walipita mitaani wakiharibu “alama zote za ubepari”.
Hii ilimaanisha kuwa waliharibu kila aina ya biashara waliyoikuta mbele yao.
Mji mkuu wa Tehran ukashikwa na tahatuki kuu.

Ilipofika mchana, CIA wakaruhusu kundi la pili kuingia mtaani.

Kundi hili la pili lenyewe, lilipita nyumba hadi nyumba kuhamasisha wananchi wasikubali kubaki majumbani wakati wanachama wa Tudeh Party wakiharibu mali zao.

Wananchi wengi wakajitokeza na silaha za jadi nabkuandamana mitaani kupambana na "wanachama" wa Tudeh Party.

Mji mzima ukaingia katika machafuko.

Ndipo hapa CIA wakampa maelekezo ya mwisho Generali Fezlollah Zahedi.
Wakamuru huo ndio ulikuwa muda muafaka wa mapinduzi.

Generali akakusanya vikosi vyake, wakaingia mtaani na vifaru na silaha nzito. Wakaelekea kwenye makazi ya Waziri Mkuu.
Hawakumkuta Waziri Mkuu, hivyo ikawalzimu kuwakamata Mawaziri wake. Masaa machache baadae Waziri Mkuu Mohammad Mosaddegh akajitokeza na kujisalimisha.

Mapinduzi yalikuwa yamekamilika.

Siku mbili baadae mfalme, Mohammad Reza Shah Pahlavi alirejea Iran akiwa kwenye ndege binafsi ya kifahari akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa CIA, Allan Dulles.

Tarehe 21 August 1953, akamuapisha Genetali Fezlollah Zahedi kuwa Waziri mkuu mpya na yakafanyika mabadiliko ya kikatiba kumrudishia Shah wa Iran nguvu kubwa zaidi kuamua kuhusu mwenendo wa nchi.

Kutokana na nchi kutokuwa na akiba yoyote ya fedha, serikali ya Marekani wakampatia Shah wa Iran Dola Milioni 5.

Mohammad Mosaddegh akahukumiwa kifungo cha maisha gerezani lakini Shah wa Iran Mfalme Mohammad Reza Shah Pahlavi akampunguzia adhabu kuwa kifungo cha miaka mitatu jela.

Ingawa tukio hili la serikali ya Marekani kwa kutumia CIA, kitengo cha SAD kuongoza mpango wa kuipindui serikali halali ya kidemokrasia kutokea mwaka 1953 lakini ndilo lililofanya kuzorota kwa mahusiano kati yake na Iran mpaka Leo.

Mpaka leo hii tunapojadili hapa, kitengo hiki cha SAD ndani ya CIA kinaendelea na shughuli mbali mbali za siri ulimwenguni kote na ni Tamko/Nyaraka namba PTU12333 kutoka Ikulu ya marekani inayowapa ruhusa ya kutekeleza shughuli hizo.Mwisho.

The Bold.


Join my exclusive whatsapp group kusoma makala na simulizikila siku – 0718 096 811 (kuna “subscription fee")Shukrani: Makala hii imeandikwa kwa kuzingatia (reference) Nyaraka za CIA zilizokadhiwa kwa Idara ya Kumbukumbu za Usalama wa Taifa nchini Marekani (U.S. National Secirity Archives) iliyopo Chuo Kikuu Cha George Washington, nchini Marekani.

Tafadhali, hairuhusiwi kutumia makala hii mahali popote pasipo ruhusa ya mwandishi H.B.A alias The Bold.
=================


Nyongeza...

Nifah

Naam,nimemaliza sasa kuisoma makala hii ya aina yake.


SWALI

Nimeona mwisho wa makala hii Waingereza walishinda 'vita' dhidi ya Mohammad Mosaddegh ambaye alikuwa kawabana mbavu katika dili la mafuta.

Na kiongozi aliyefuata alikuwa kibaraka wao aliyekuwa anafuata kila wamuambialo.

Je,Iran waliweza vipi kujikwamua kutoka katika utumwa huu dhidi ya Uingereza?

Ni nani aliyeongoza mapambano hayo ya kurejesha visima vyao vya mafuta?

Je alitumia mbinu gani?


MIAKA 26 BAADAE


Swali zuri sana mama, ingawa jibu lake nahisi linastahili niandike uzi mwingine but ngoja nigusie walau kidogo naona pia The Boss, Adharusi na gwijimimi wameshauri ningegusia hilo pia..

Kwanza ni muhimu kufahamu baada ya Mosaddegh kuondolewa madarakani na Shah kurudishiwa mamlaka yake na Marekani kuanza kuhusika na uchimbaji wa mafuta Iran ikaanza kupata maendeleo ya kasi mno.

Huduma za kijamii zikaboreka sana na vipato vya wananchi vikakua maradufu.

Lakini Shah Mohammad Reza Pahlavi alifanya makosa haya makubwa;

1. Alikataa kuifanya Iran kuwa nchi ya Kiislamu tofauti na matamanio ya wananchi wengi.
Badala yake Shah Pahlavi akawa anaifanya Iran kuwa ya nchi ya kimagharibi zaidi kiutamaduni.

2. Aliishi maisha ya kifahari kupitiliza kiasi wananchi wakaanza kukwazika.

3. Akaingia kwenye mgogoro na Marekani kwa 'kusapoti' mkataba wa nchi za OPEC kuhusu kuongeza bei ya mafuta.

Makosa haya yakazaa yafuatayo;

=> likaanza vugu vugu la kiislamu la kudai Iran kuwa Jamuhuri ya kiislamu na kupinga umagharibi ndani ya Iran.
Vugu vugu hili liliongozwa na waislamu wa madhehebu ya Shia chini ya kiongozi wao Ayatollah Khomeini.

=> Marekani wakatangaza kuwa hawatakuwa bega kwa bega wala kuwauzia silaha nchi zisizo heshimu haki za binadamu.

=> Baada ya wapinzani wa kisiasa wa Shah kugundua uhusiano wa Shah na marekani umedorora nao wakaanzisha vugu vugu la kupinga Iran kutawaliwa na koo moja (Dynasty).

Baada ya mambo hayo kutokea, Shah Pahlavi akishikwa na kitete na kufanya makosa zaidi;

Mfano;

- akaamuru Ayatollah Khomeini akamatwe. Hii ikamlazimu Ayatollah khomeini kukimbia Iran na kwenda kuishi uhamishoni nchini Uingereza.

- Shah akasimamia kuuwawa kwa sumu kwa Mostafa Khomeini, mtoto mkubwa wa kiume wa Ayatollah Khomeini.

- Shah akasimamia pia kuuwawa kwa sumu kwa moja wa wanafalsafa nguli wa nchi hiyo aliyeitwa Ali Shariat ambaye kwa kipindi hicho alikuwa anaandika makala za kufikirisha mno lakini zikimpinga Shah na mawaziri wake.

- Shah akaamuri kuwekwa vizuizini na gerezani kwa wanasiasa wengi wa upinzani.

- Pia Shah akaanzisha mkakati wa kipumbavu kabisa, ambapo kupitia magazeti ya nchi hiyo zikawa zinaandikwa makala za kumkashifu Ayatollah Khomeini kuwa ni kibaraka wa Uingereza anayetumiwa kuivuruga Iran. Hii iliwaudhi wananchi wake ambao walikuwa wanamuheshimu sana Ayatollah na pia liliwaudhi mabwana wakubwa nchi za magharibi kwa kupewa tuhuma mbaya namna hiyo.

Mambo haya yote yakaifanya Iran kuwa katika 'tension' kubwa. Na hatimae mwaka 1977 waislamu wote wa madhehebu Shia nchi nzima wakaanzisha maandamano ya kupinga Shah Pahlavi na uongozi wake.

Mwishoni mwa mwaka huo pia kukatokea mdodororo wa kiuchumi na mfumuko wa bei kutokana na nchi za magharibi kugoma kununua mafuta ya Iran kutokana na kutoridhishwa na muonendo wa uongozi wa Shah Pahlavi.

Hii ikasababisha wafanyakazi wote kugoma nchi nzima na kuingia mitaani kuungana na wananchi wengine kumpinga Shah na uongozi wake.

Maandamano haya yalikuwa ni yale "maandamano yasiyo na kikomo" na yalifanyika nchi nzima.

Shughuli za kiuchumi zote zikasimama. Wananchi wote wako mitaani wanaandamana.

Shah Pahlavi alishindwa kulihusisha jeshi kwasababu alijua fika ingembidi kuuwa wananchi wote na ni wazi kama angeliamuru jeshi kufanya hivyo wangemgeuzia kibao na kumkataa.

Kwahiyo suluhisho aliloliona, mwezi Febeuary 1979 akaondoka kwa siri nchini Iran na kwenda uhamishoni.

Baadae mwezi machi Jeshi likatangaza kutokumuunga mkono Shah.

Taarifa za jeshi kuunga mkono juhudi za wananchi na kwamba Shah Pahlavi amekimbia Iran zikamfikia Ayatollah Khomeini aliyeko uhamishoni Uingereza.

Kwahiyo, mwezi April 1979 Ayatollah Khomeini akarejea Iran na kuchukua Uongozi wa nchi na kuitangaza Iran kuwa ni Jamuhuri ya Kiislamu na yeye Ayatollah akiwa kama "Supreme leader".

Huu ndio ukawa mwanzo wa historia ya Iran hii ya sasa tuliyonayo.

Nikipata wasaa huko mbeleni nitaweka Uzi kueleza kwa kina kuhusu Iran hii ya sasa ilivyanza.


Join my exclusive whatsapp group kusoma makala na simulizikila siku – 0718 096 811 (kuna “subscription fee")
 

Tyta

JF-Expert Member
May 21, 2011
12,799
2,000
CIA -Kitengo cha Fitna na Figisu Figisu Ainati....They got millions of classified information.They often tend to get away with most of their failed/successful missions/operations that reach the general public.Too much power to be accountable to average joe.
 
Status
Not open for further replies.

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom