Tofauti Zakwamisha Umoja Wa Afrika ~ Kikwete

Ipole

JF-Expert Member
Apr 15, 2008
294
10
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Kikwete amesema nchi za Afrika zina utashi wa kuwa na serikali moja lakini zinatofautiana katika masuala machache ambayo yanaweza kutatuliwa.

Akifungua mkutano wa siku mbili wa marais na viongozi wa nchi 12 za Afrika zinazounda Kamati ya Kushughulikia Serikali Moja ya Afrika mjini hapa jana, Rais Kikwete alisema tofauti hizo zipo katika muundo na muda wa kuanzishwa kwa serikali hiyo.

“Kimsingi nchi za Afrika zina azma ya kutimiza mchakato wa kuwa na serikali moja ulioanza tangu miaka ya 1960 na dalili zinaonyesha kuwa tunaweza kutimiza nia ya kuwa na serikali moja katika muda mfupi ujao,” alisema.

Alisema ili kutimiza lengo hilo, AU imekuwa ikiunda kamati mbalimbali za kutafuta maoni ya wadau kama vile azimio la Accra ambako walikubaliana kuunda kamati itakayopitia muundo wa AU na vyombo vyake kwa nia ya kuimarisha utendaji wake katika kuelekea serikali moja.

Kamati hiyo iliyokuwa chini ya mchumi maarufu, Profesa Adedeji Adebayo wa Nigeria iliwasilisha mapendekezo 159 kwa mawaziri wa nchi za nje wa umoja huo waliokutana mjini hapa mapema mwezi huu.

Awali, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU,Dk. Jean Ping alisema mapendekezo ya mawaziri wa Mambo ya Nchi za Nje yaligusia masuala muhimu katika kuelekea katika umoja kama vile kuwaelimisha zaidi wananchi wa Afrika juu ya AU na kuangalia vyanzo zaidi vya mapato kwa umoja huo.

Alisema mawaziri hao walitoa mapendekezo yaliyoweka msingi wa kuanzishwa kwa serikali moja ya Afrika katika misingi inayokubalika katika bara hilo masikini zaidi duniani ingawa lina rasilimali nyingi za asili.

Mkutano huo unaomalizika leo utapitia mapendekezo ya mawaziri wa Mambo ya Nchi za Nje na kuandaa mapendekezo yake yatakayopelekwa katika kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa AU kitakachofanyika nchini Misri Julai, mwaka huu.

Hata hivyo, kati ya marais 12 wanaounda Kamati hiyo, ni watano tu waliohudhuria mkutano wa jana huku wengine saba wakiwakilishwa na mawaziri wao wa Mambo ya Nchi za Nje.

Marais waliohudhuria mkutano ni Yoweri Museveni wa Uganda,Thabo Mbeki wa Afrika Kusini,Umaru Yaar’dua wa Nigeria,Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zanawi na mwenyeji wao, Rais Kikwete.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu,Salva Rweyemamu alipoulizwa juu ya marais wengi kushindwa kuhudhuria mkutano huo, alisema kuwa mawaziri wa Mambo ya Nchi za Nje wanawakilisha marais wao hivyo wana mamlaka ya kutoa uamuzi.

Marais walioshindwa kuhudhuria mkutano huo ni Muamar Gaddafi wa Libya, John Kuffour wa Ghana, Abdoulaye Wade wa Senegal, Paul Biya wa Cameroun, Omar Bongo wa Gabon, Hosni Mubarak wa Misri na Ian Khama wa Botswana.
 
Back
Top Bottom