Toa utazamwe, fanya utazamwe

bigmukolo

JF-Expert Member
Mar 6, 2012
597
2,225
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na mwenyeji wake Donald Trump wa Marekani wamekutana na kuratibu majadiliano ya mkataba wa biashara huru kati ya mataifa hayo mawili.

AGOA ni kifupisho cha African Growth and Opportunity Act. Huu ni mkataba baina ya mataifa ya Africa na Marekani ambao huruhusu zaidi ya bidhaa 6500 kuingia Marekani kutoka Africa bila ushuru wowote. Mkataba huu umekuwepo tokea mwaka 2000 zamani za Mwai Kibaki akaurithi Uhuru.

So kinachoshangaza umma ni ziara ya bwana Uhuru Kenyatta nchini Marekani kwa ajiri ya uimarishaji wa huu mkataba siku mbili baada ya kifo cha mtukufu Arap Daniel Moi. Yaani ameacha maiti ndani akaenda ughaibuni. Natafuta kujiuliza ni kanuni ipi inampa ujasiri Uhuru kuiacha maiti ya mtangulizi wake sandukuni.

Kibiblia mambo mawili yamebainishwa nayo ni mosi, kuwaacha wafu wazikane. Soma hapa:-

"Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao"(Matayo 8:22).

Kauli hii ni jibu kwa watu ambao walitaka kuacha wajibu wao wa kumfuata Yesu kwa kigezo cha kwenda mazikoni. Endapo Uhuru Kenyatta ameegemea hapa ni halali ashughulikie walio hai kuliko kupoteza muda na uchumi wa taifa kubwa kungojea maziko ya mzee Moi. Akifanya hivyo anaungwa mkono katika aya hii:-

"................Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai"(Matayo22:32).

Rais Uhuru atakuwa huru kwelikweli ikiwa amekusudia kuliishi Neno na ni uamzi mgumu utakaosababisha wengi wamtazame kama dikiteta na katili. Lakini ni uduni wa maarifa kiasi gani kwa wale wajiitao viongozi wa dini ambao hupoteza muda na mali kushughulikia wafu! Kwa mfano watu wamekaidi makusudi Kweli za Mungu wakahadaika kukanyaga eti mafuta ya upako na kisha wakafia huko. Wewe n'nani hata ukawaombee wafu? Kama walishindwa kumwamini Mungu wangali hai leo maiti zitaamini? Nafuatilia ziara ya Uhuru Kenyatta.

Pili ni suala la kutazamwa. Wengi tunafanya mambo ili tutazamwe, tusifiwe na kupongezwa fullstop! Angalia hapa:-

"Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni"(Matayo6:1).

Kama kungali na mambo duniani basi ni hili la mtu kufanya jambo ili atazamwe. Atazamwe tu! Watu wengi wasingalikuwa na marobota ya nguo nyumbani na asingalikuwepo hata mhitaji mmoja. Lakini kwasababu tunapenda kutazamwa lazima tuvae very expensive apparel!!!

Bei ya chini kwa vazi moja la suti ni 150,000/=. Mtu mmoja ana sanduku lenye suti 40 mpaka 100 yaani kila siku anatoka na suti mpya! Akina mama naona kama mnarukwa akili hivi. Fikiria maisha ya familia hii wangeishi kisiwani (kisiwa cha familia moja tu)baba na mama na ofisi ikawekwa palepale na kupata mahitaji yote. Mama angevaa viwalo? Atazamwe na nani?

Kinachotufanya tubadilishe nguo mara tatu kutwa si jambo jengine bali tukatazamwe. Kinachowafanya wanawake wengi wavae vimini ni kutazamwa! Kinachowafanya vijana wengi wavae vimodo na kunyoa viduku ni kutazamwa. Naungana na usemi wa kwetu usemao, "Omgasi ni mwana" yaani mwanamke ni mtoto. Wanaotusumbua na kutukera katika jamii ni kundi la wanawake na vijana wa kiume. Ni hao tu akili zao zinafanana kufanya ya ovyo-ovyo ili maovyo-ovyo hayo yatazamwe!! Hivi kweli mwanamke atakua? Muulize jiranio, je wewe ni mwanamke au u mtoto?

Angalia nguvu ya "mob psychology". Mtu anajenga kamjengo ka kisasa msonge mbele kwa mbele na bati za kisauzi. Nyumba ambayo kama ingelijengwa bila mihemko ya wakati na lika ikatoa vyumba vitatu, sasa imejengwa kisasa ikaambulia chumba kimoja na sebule. Watoto wanalala eidha sebuleni kwa kutenganisha jinsia kwa pazia au kwa jirani. Sababu ni mjengo wa kisasa ili utazamwe!!

Huku makanisani nako hakukaliki. Wanakataa siasa za nchi lakini wanaendesha siasa za kidini kushika hatamu. Yaani nyazifa za uzee wa kanisa na uhasibu ambazo hazina posho wala takrima, zinafanyiwa kampeni na mtu akikoswa alipolenga ananyong'onyeana pengine kulisusia kanisa ama kukataa nyazifa zilizo chini yake. Sababu si utendaji bali kutazamwa tu!

Njoo kwenye hizi chaguzi za uongozi wa kijimbo. Yaani kama imani yako ni changa huko ndiko utaasi kabisa, bora usiende! Yaani wachungaji wazima wanaenda kupiga ramli? Imenistajaabisha sana! Wachungaji wanapita guest to guest house ambako wawakilishi tumefikia wakiturubuni kwa kampeni kali na zenye chuki!!! Balaa!

Yaani wachungaji walioko jimboni wanatuletea maswali ya kuwauliza wakubwa(maaskofu) yumkini waanguke kabisa!! Huwezi amini nikisemacho! Nasema hivi, wachungaji wana vijambo ila wanaogopa kuwauliza maaskofu kwa hofu ya kuhamishwa vituo vya kazi. Iko hivi, ukionekana ulimkerembesha askofu au mkuu wa idara kwa maswali mazito juu ya uhafifu wa utendaji wake, askofu/mkuu huyo wa idara akishinda uchaguzi hujilipiza kisasi kwa kuwahamishia vijijini(interior). Kwa sababu hizo maswali yatapewa wawakilishi wa makanisa wayaulize! Kutazamwa!

Kisiasa/kiutawala walio chini hufanya kwa udi na uvumba kuwasifia watawala si kwa dhati bali watazamwe! Watu wa jinsi hiyo tayari huwa malipo yao wamejilipa na wasitarajie ya baadaye kwa mjibu wa aya hapo juu. Hawakosoi wala hawaelekezi ni watu wa kuitikia kwa kila jambo Amina, kidumu, power!

Mtazamo huu unamjengea Uhuru Kenyatta upekee wa aina yake. Kwa maana watu wa kutazamwa huiangalia jamii itanisemaje badala ya Mungu atanisemaje. Wako radhi kugharimika kwa lolote wawahi maziko kwa maana mazikoni kuna wengi wa kumtazama kinyume na idadi ya wamuuguzao hospital ambao huwa kati ya wawili au watatu hivi. Atazamwe na nani?

Kwa misingi hii ya kutazamwa, maziko hufanyika kwa gharama kubwa na za kifahari. Wanyama huchinjwa, chupa tele za maji na soda na mziki mzito kumsindikiza marehemu ambaye hasikii wala haoni.

Ni katika misingi hii-hii ya kutazamwa wengi huwajengea wazazi wao nyumba si kurudisha heshima na shukrani kwa wazazi ila kuandaa msiba usiwe wa kuwafedhehesha. Wanajua wazazi wao wamo mbioni kufariki na ili kujiondolea kudharaulika siku ya msiba, wanawajengea vijumba vizuri lakini tokea wameanza kuzishika pesa imepita miaka kadha wa kadha bila kufanya lolote kwa wazazi wao. Kanuni ya aibu ni kutoa ili utazamwe na ukiisha kutazamwa aibu kwisha!

Hiyo ni tafsiri ya ziara ya Uhuru Kenyatta huko Washinton DC kiuchumi, kijamii, kisiasa na kidini. Tafsiri yake kidemokrasia ni kwamba hana haja na mwili wa marehemu Moi ijapokuwa aisomeshwa naye kwenye utawala wake. Wengi mtaikumbuka taarifa ya habari ya KBC Nairobi zamani hizo. Huu hapa ni mhutasari wa taarifa ya habari ya mwaka 1992 mchana wa jumapili tarehe 5 July iliyosomwa na Charles Omga Kabisae. Isikilize:-

"Ifuatayo ni taarifa ya habari kutoka KBC Nairobi, kwanza ni mhutasari wake msomoji ni Charles Omga Kabisae. Mtukufu rais Daniel Arap Moi leo amehudhuria ibada kanisa la Machakosi............."

Taarifa hii hunikumbusha ulivyokuwa udikiteta wa rais Sessesseko Mobutu. Kabla ya taarifa, kama ilivyo kwa ngoma za mzee Moris Nyunyusa za TBC, kwa upande wa Zaire ilishuka picha ya Mobutu kutoka juu angani na kuwaaminisha kuwa yeye ni mungu wa Zaire na malofa wengi kama ilivyo kawaida yao na huko walimtukuza sana. Mtu alihesabika adui endapo angeliukosoa utaratibu huo. Leo hii haohao waliomtukuza na kumsifia ndiyo waliokataa katakata kuupokea mwili wake kwa maziko na badala yake akazikwa kibudu!!

Nchini Kenya, mzee Moi alijifanya muungu mtu na lazima uanze na state title, "mtukufu" ndipo utaje jina lake. Kadhia hiyo iliwafanya baadhi ya viongozi wa Africa wajishebedue kutoitwa "mtukufu" ijapokuwa matendo yao yalijaa unyama na udikiteta.

Ni Daniel Moi pekee tokea nchi ya Kenya ipate uhuru ambaye amekuwa dikiteta wa kutisha. Uzuri ni kwamba Mungu huwaruhusu madikiteta waishi umri mkubwa kama Moi na Mgabe ili wajionee kwa macho mazuri ya wema katika demokrasia walau wajute waombe radhi wasameheke kabla ya umauti kuwajia. Ajabu ni kwamba madikiteta huwa hayajitambui mpaka yanakufa!

Ni huyuhuyu Moi alimfunga miaka zaidi ya sita gerezani bwana Koigi Wamwele kisa aliupinga utawala wake dhalimu. Kwa ujumla mzee Moi hakuwa na hana jema hata moja la kumkumbuka wala kumuenzi. Hana kabisa! Ukimtaja tu, papohapo ubaya wake unaibuka. Hii ni tofauti kwa Nyerere. Yeye ukimtaja tu, orodha ya mema ni ndefu kuimaliza. Yumkini kwa sababu hizi, mheshimiwa rais Uhuru Kenyatta hakuona la maana kupoteza fursa za kusaini mkataba wa AGOA jijini Washington badala yake ni waache wafu wazikane!!

Utakapokufa utakumbukwa kwa lipi? Wema au ukatili?
 
Back
Top Bottom