TMA: Yatoa matarajio ya hali ya hewa kipindi cha kipupwe

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,008
9,873
MWELEKEO WA HALI YA HEWA KWA TANZANIA KIPINDI CHA JUNI – AGOSTI (JJA), 2020

Dondoo muhimu za hali ya hewa kipindi cha Julai-Agosti (JJA), 2020

Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa pamoja na hali ya hewa inayotarajiwa katika msimu wa Kipupwe kwa miezi ya Julai hadi Agosti (JJA), 2020; Ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao. Kwa kawaida, kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti (JJA), huwa ni kipindi cha baridi na kipupwe kwa maeneo mengi ya nchi.
Kwa muhtasari, mwelekeo huo na athari zake unaonesha kuwa:

a) Viwango vya joto
• Kwa ujumla katika kipindi cha JJA, 2020 hali ya joto inatarajiwa kuwa ya kawaida hadi juu kidogo ya kiwango cha kawaida katika maeneo mengi ya ukanda wa Pwani. Hali hiyo inamaanisha uwepo wa vipindi vichache vya baridi ikilinganishwa na wastani wa muda mrefu (1981-2010) kwa miezi ya Juni-Agosti katika maeneo hayo.

• Vipindi vya baridi kali vinatarajiwa kufikiwa mapema katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Juni na kuwahi kupungua katika kipindi cha kuelekea mwishoni mwa msimu.

• Kwa upande mwingine, hali ya joto la kawaida kama ilivyozoeleka inatarajiwa katika maeneo mengi ya ukanda wa Pwani (mikoa ya Lindi, Mtwara na Tanga), maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki, kanda ya ziwa Victoria, kanda ya kati, Magharibi mwa nchi, mkoa wa Iringa pamoja na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Ruvuma.

• Maeneo mengi ya nyanda za juu kusini magharibi pamoja na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Ruvuma, hali ya joto la kawaida kama ilivyozoeleka hadi chini kidogo ya joto la kawaida linatarajiwa. Hata hivyo vipindi vya baridi kali vinatarajiwa katika maeneo ya miinuko hususan nyakati za usiku na asubuhi.

b) Upepo
• Kwa ujumla vipindi vifupi vya upepo mkali wa Kusi na hali ya ukavu inatarajiwa katika maeneo mengi. Vipindi vya Upepo wa Matlai vinatarajiwa kuleta unyevunyevu kutoka katika bahari ya Hindi na kusababisha vipindi vifupi vya mvua nyepesi katika maeneo machache.

c) Athari
• Hali ya ukavu, upepo na ubaridi inaweza kusababisha athari kwa binadamu, wanyama na mazao.
• Jamii inashauriwa kuchukua hatua za tahadhari ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi mazuri ya maji na kujikinga ili kupunguza athari mbaya zinazoweza kusababishwa na hali ya hewa inayotarajiwa.

1.0 MIFUMO YA HALI YA HEWA

Katika kipindi cha msimu wa JJA, 2020, hali ya joto la bahari la wastani hadi chini ya wastani inatarajiwa katika eneo la ukanda wa kati wa kitropikali ya bahari ya Pasifiki. Hali hii inatarajiwa kusababisha ukavu katika maeneo mengi ya nchi. Hali ya joto la juu kidogo ya wastani inatarajiwa magharibi mwa baharí ya Hindi, wakati maeneo ya mashariki mwa baharí ya Hindi hali ya joto la bahari la juu zaidi ya wastani inatarajiwa. Hali hii inatarajiwa kusababisha hali ya ukavu katika maeneo ya ukanda wa Pwani na nyanda za juu kaskazini-mashariki. Hata hivyo katika eneo la mashariki mwa baharí ya Atlantiki (Pwani ya Angola), joto la baharí linatarajiwa kuwa la wastani hadi chini ya wastani. Hali hii inatarajiwa kupunguza upepo utokao magharibi kuelekea maeneo ya magharibi mwa nchi. Vile vile, joto la baharí la wastani hadi chini kidogo ya wastani katika eneo la bahari ya Hindi kusini mwa Afrika linajatajiwa kupunguza msukumo wa hewa baridi kutoka kusini hasa nyakati za usiku katika maeneo ya ukanda wa Pwani.

2.0 MATARAJIO YA VIWANGO VYA JOTO KWA MIEZI YA JULAI HADI AGOSTI, 2020

Kwa ujumla katika kipindi cha JJA, 2020 hali ya joto la kawaida hadi juu kidogo ya kiwango cha kawaida inatarajiwa katika maeneo mengi ya ukanda wa Pwani. Hali hii inaashiria uwepo wa vipindi vichache vya baridi ikilinganishwa na hali ya wastani wa muda mrefu (1981-2010) kwa miezi ya Juni-Agosti katika maeneo hayo. Kwa upande mwingine, hali ya joto la kawaida kama ilivyozoeleka inatarajiwa katika maeneo mengi ya ukanda wa Pwani (mikoa ya Lindi, Mtwara na Tanga), maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki, kanda ya ziwa Victoria, kanda ya kati, Magharibi mwa nchi, mkoa wa Iringa pamoja na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Ruvuma. Maeneo mengi ya nyanda za juu kusini magharibi pamoja na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Ruvuma, hali ya joto la kawaida kama ilivyozoeleka hadi chini kidogo ya joto la kawaida linatarajiwa. Hata hivyo vipindi vya baridi kali vinatarajiwa katika maeneo ya miinuko hususan nyakati za usiku na asubuhi. Vipindi vya baridi kali vinatarajiwa katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Juni na kupungua kuelekea mwishoni mwa msimu.

2.1 Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu):
Kiwango cha joto la chini (”minimum temperature”) kinatarajiwa kuwa cha kawaida kama ilivyozoeleka kati ya nyuzi joto 14 na 18 katika maeneo mengi.

2.2 Ukanda wa pwani ya kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba):
Joto la chini linatarajiwa kuwa la kawaida hadi juu ya kawaida katika maeneo mengi, kiwango hicho kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 18 na 22. Aidha, maeneo machache ya visiwa vya unguja na Pemba yanatarajiwa kuwa na nyuzi joto zaidi ya 22. Hata hivyo, kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 14 na 18 katika maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro. Kwa upande mwingine maeneno yenye miinuko hususan katika mkoa wa Tanga na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 14.

2.3 Kanda ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):
Katika msimu huu kwa ujumla kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa cha kawaida kati ya nyuzi joto 14 na 18 katika maeneo mengi. Aidha, katika maeneo ya miinuko kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa chini ya nyuzi joto 14.

2.4 Kanda ya magharibi (Mikoa ya Tabora, Rukwa, Katavi na Kigoma ):
Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa cha kawaida kama ilivyozoeleka, kati nyuzi joto 12 na 18 katika maeneo mengi.

2.5 Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma):
Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa cha kawaida kati ya nyuzi joto 10 na 16 katika maeneo mengi.

2.6 Ukanda wa pwani ya kusini (Mikoa ya Mtwara na Lindi):
Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa cha kawaida kati ya nyuzi joto 16 na 20 katika maeneo mengi. Hata hivyo, maeneo machache yanatarajiwa kuwa na joto la chini linalozidi viwango vya kawaida kati ya nyuzi joto 18 na 22.

2.7 Kanda ya kusini (Mkoa wa Ruvuma):
Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa cha kawaida hadi chini kidogo ya viwango vya kawaida kati ya nyuzi joto 10 na 14 katika maeneo mengi.

2.8 Kanda ya nyanda za juu kusini-magharibi (Mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe pamoja na maeneo ya kusini ya mkoa wa Morogoro):
Maeneo mengi yanatarajiwa kuwa na joto la chini la kawaida hadi chini kidogo ya viwango vya kawaida, kati ya nyuzi joto 6 na 12. Aidha, kiwango cha joto la chini katika maeneo ya miinuko kinatarajiwa kuwa chini ya nyuzi joto 6.

2020-06-08 (5).png


3.0 MWENENDO WA UPEPO KWA KIPINDI CHA JULAI HADI AGOSTI (JJA), 2020
Kwa kawaida msimu wa kipupwe hutawaliwa na upepo wa Kusi. Kutokana na matarajio ya uimarikaji wa wastani wa mgandamizo mkubwa wa hewa kusini mwa Afrika vipindi vichache vya upepo mkali vinatarajiwa kujitokeza. Hata hivyo, katika kipindi cha mwezi Juni, 2020 vipindi vya upepo mkali wa Kusi vinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Vilevile, katika msimu wa mwaka huu, vipindi vya upepo unaovuma kutoka kusini-mashariki na mashariki (Matlai) vinatarajiwa katika ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi na maeneo ya mwambao wa pwani hususan mwezi Agosti, 2020.

Vipindi vya upepo wa Matlai vinatarajiwa kuleta unyevunyevu kutoka katika bahari ya Hindi na kusababisha vipindi vifupi vya mvua nyepesi katika maeneo machache ya visiwa vya Unguja na Pemba, pamoja na ukanda wa Pwani (Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara). Aidha, katika ukanda wa ziwa Victoria pamoja na maeneo ya miinuko ya nyanda za juu kaskazini mashariki na kusini magharibi vipindi vifupi vya mvua vinatarajiwa kujitokeza katika maeneo machache.

4.0 ATHARI NA USHAURI
Hali ya baridi inayotarajiwa hususan maeneo yenye miinuko inaweza kuleta athari kwa binadamu, wanyama, samaki pamoja na ustawi wa mazao mashambani. Kutokana na hali ya joto katika bahari ya Hindi kuwa juu ya wastani, ongezeko la tija katika shughuli za uvuvi katika kipindi cha msimu huu linatarajiwa.


Hali ya ukavu na upepo inaweza kuongeza upotevu wa maji kwa njia ya mvukizo na kuathiri upatikanaji wa maji kwa mazao, mifugo na matumizi mengine. Hivyo, Jamii inashauriwa kuchukua hatua za tahadhari ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi mazuri ya maji na kujikinga ili kupunguza athari mbaya zinazoweza kusababishwa na hali ya hewa inayotarajiwa.


Mwelekeo wa hali ya hewa uliotolewa hapa umezingatia zaidi kipindi cha msimu (miezi mitatu) na hali ya hewa katika maeneo makubwa. Hivyo, viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi. Watumiaji wa taarifa za utabiri huu wanashauriwa pia kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 pamoja na mwezi kama unavyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa.

Imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania:


Dkt. Agnes L. Kijazi
Mkurugenzi Mkuu
 
Back
Top Bottom