Tips za kuboresha Mapenzi na Mahusiano

Von Mo

JF-Expert Member
May 7, 2012
1,819
1,185
Habari Wakuu,

Naomba msome hivi vipengele viwili vinavyogusa karibu kila mtu. Ujumbe una vipengele viwili:-


KIPENGELE [ A ] - MAMBO YANAYOMFANYA MTU AYACHUKIE MAPENZI

SIJUI wewe ulikuwa una malengo gani wakati unafikiria kuwa na ambaye unaye; wapo ambao walikuwa na malengo kwamba akiwa na mwanaume, maana yake awe ndio sawa na mashine ya kutolewa fedha maarufu kama ATM.

Ikiwa ulichokuwa unatafuta ni mwanaume au mwanamke ambaye kwako atakuwa ni ATM, kwamba ndiye awe anakupa kila kitu unachotaka, ikiwa hatakuwa na fedha si rahisi mkaendelea kuwa na uhusiano mzuri, kwa kuwa mpango wako haukuwa mapenzi, bali kuchuma fedha na kula raha.
Wajinga ni wale ambao wanaingia kwenye mapenzi ili kusaidiwa tu, badala ya kusaidiana. Mwenye hekima ni yule ambaye anafahamu kwamba kuingia kwenye mapenzi, maana yake ni kuongeza timu ya kusaidiana katika maisha, si vinginevyo.

Mwanamke yeyote ambaye anafikiri yuko na mwanaume maana yake ni kwamba awe anamnunulia kila kitu, kwamba kwake mwanaume ni kila kitu, kinywaji anunuliwe, chips anunuliwe nk...kwamba yeye ni mtu wa kupewa tu ofa, maana yake ni kwamba akili yake imekufa.

Kufikiri kwamba kuoana na fulani maana yake ni sasa yeye atakuwa anakusaidia kila kitu milele na kwamba asipofanya hivyo utamdharau, si kitu sahihi.

USIWE NA MATARAJIO MAKUBWA UNAPOINGIA KWENYE NDOA

Unapoingia kwenye ndoa, usiwe na matarajio makubwa sana mazuri. Jambo unalopaswa kufahamu ni kuwa uhusiano ni suala la kawaida, kwamba unakuwa na mtu kwa lengo la kuwa nae kama timu moja kusaidiana katika kuleta maendeleo.

Kati ya mambo yanayofanya watu kutofurahia mapenzi, ni pale anapotishwa kwamba labda asipofanya hiki kwa mfano kukusaidia, basi uhusiano wenu utaharibika.

Kuna wanawake utasikia aaah sasa kuna maana gani ya kuwa na mwanaume ikiwa namwomba fedha hawezi kunisaidia? Fikra kama hii ni ya kipuuzi. Wewe kwanini huna fedha? Ndoa ni kusaidiana, sio kugeuzana ATM.

YUKO BIZE NA SIMU, KOMPYUTA NK

Kati ya mambo yenye kutiana ‘kichefuchefu' katika mapenzi ni pale kwamba uko na mwenzi wako, lakini ni kama wewe ni tambala la deki; yaani yuko bize na simu yake au kompyuta au kitu kingine chochote.

Wengine unakuta labda anawasiliana na wengine kwa mitandao ya kijamii kama vile facebook, twitter nk, kumaanisha kwamba wewe ni muhimu, walio muhimu ni wale ambao anawasiliana nao huko.



KUKOSOANA MBELE ZA WATU AU HATA KUPIGANA

Wapo watu wamekuwa na tabia ya kukosoana au hata kupigana mbele za watu. Kati ya makosa yenye kukera na huenda ukasababisha uhusiano ukabaki historia ni hii...ni vizuri ndugu yangu kujifunza namna ya kuachana na hasira kali.

MATUMIZI MABAYA YA FEDHA NA KUTOKUWA NA MIKAKATI KATIKA MAISHA

Kila mtu Duniani anataka maisha bora, kwa maana hiyo ni furaha ya kila mtu kuona mwenzi wake anakuwa mwenye mikakati imara katika kuimarisha maisha yao.
Tabia kama za ufujaji wa fedha, kutokuwa na mikakati katika maisha, ni kati ya mambo yanayochangia ndoa au uhusiano wa mapenzi kuwa mbaya.

HUDUMA KWA WATOTO NA FAMILIA


Ukiwa kama baba au mama, unapaswa kutafakari vizuri nafasi yako katika malezi ya familia. Ni furaha ya mke na mume, kuona mwenzi wake anajali watoto na familia kwa ujumla. Je, wewe ukoje? Pata muda kufakari hali ya maisha yako, chukua hatua.

UCHAFU NA KUTOWAJIBIKA 


Kuna watu wamekuwa wachafu kupindukia, hata kuoga kabla ya kulala ni shida, wengine kuvaa nguo mpya ya ndani hadi awe na ahadi ya kuonana na nesi au daktari.

Lakini zaidi ya yote, ni muhimu wanaume na wanawake wakafahamu kila upande kwa kawaida huwa na nafasi yake ya kuwajibika.

Hata kama wote mna ajira au fedha, mume anapaswa kuangalia namna ya kumfanyia mkewe mambo kama kununua nguo, chakula ndani nk...kuna wanaume hawa hawajui wake zao wamevaa nini wala hawajui ndani chakula kinanunuliwaje...hili ni kosa. Ndoa ni kusaidiana, kila upande uwajibike, ni nzuri kuwa na vikao vya namna ya kuendesha ndoa yenu.

KIPENGELE [ B ] - FAHAMU NAMNA YA KUISHI NA MPENZI ANAYEPENDA FEDHA!

HAPA tunazungumza kuhusu mapenzi kama kawaida yetu. Leo nimekuja na mada ambayo naamini itawagusa wengi. Marafiki zangu, kusaidia katika mapenzi ni jambo zuri tena lenye mantiki sana.

Suala la kusaidiana si la upande mmoja. Linaweza kuwa kwa wote, kwa mwanaume au mwanamke. Ni kati ya nguzo muhimu katika mapenzi, lakini kwa bahati mbaya kuna wale ambao wamekuwa na tabia ya kupenda sana fedha!
Unajua wenzi wanajuana kulingana na wanavyoishi, hivyo ni rahisi sana kumgundua mwenzako kama anapenda sana fedha au ni kweli ana tatizo linalohitaji msaada wako. Hii ni kasoro, lakini haimaanishi kwamba ndiyo sababu ya kuachana.

Katika mada hii ipo dawa ya namna ya kudumu katika mapenzi motomoto na mwenzi wa aina hii. Imekuwa ni kawaida kumsikia msichana akitamba mbele ya wasichana wenzake kwa kusema: "Mimi nina kibuzi changu bwana kila ninachotaka kinanipa, kinajua kisiponipa nakitosa tu, yaani nakichuna kama sina akili nzuri."

Umewahi kukutana na maneno ya aina hii? Bila shaka jibu ni ndiyo. Si hivyo tu, wapo wanaume pia ambao ni kero kwa wapenzi wao, yaani wamegeuka wanaume kama mabinti kwa tabia zao za kutegemea kupewa kila kitu na wapenzi wao hata kama wanao uwezo wa kuvipata vitu hivyo kama watajishughulisha.

Ninachotaka kusema leo ni kwamba, mapenzi ya kweli hayana uhusiano wowote na fedha, ukiona mpenzi wako anaweka fedha mbele na ukishindwa kumpatilizia anachokitaka anakasirika, jua penzi lake lina walakini, hakupendi bali anataka kukutumia kisha kukuacha.
Katika mapenzi hatukatai suala la kusaidiana, mpenzi wako akiwa na shida fulani akaomba umsaidie, kama unao uwezo msaidie na kama huna mueleze ukweli kisha muangalie namna nyingine ya kumsaidia.

Itakuwa siyo busara kama utakuwa na tatizo lakini ukaona kwamba ukimweleza mpenzi wako ataona unamchuna. Wapenzi wanaopendana kwa dhati hawachunani bali wanasaidiana na hili ni kwa pande zote mbili.

Kinachokera ni kutoishiwa na matatizo na wakati mwingine unakuta kuchuna kwingine ni kwa mambo ya starehe. Yaani sasa hivi umemuomba mpenzi wako vocha, hajakaa vizuri umemtaka akija akuletee chipsi mayai, baadaye unataka akutoe ‘out', bila kujali kwamba wakati huo mpenzi wako ana fedha au laah.

Katika mazingira hayo unadhani mpenzi wako atashindwa kukuchoka? Akikuacha kwa sababu hiyo utamlaumu? Kimsingi ukiwa na mpenzi mwenye tabia ya kutaka kukuomba fedha kila wakati tena katika matumizi mengine ambayo siyo ya msingi, mbinu zifuatazo ni muhimu kuzifuata. Twende tukaone.

MWELEZE UKWELI

Kama huna fedha wakati mpenzi wako anakuomba, mueleze wazi kuwa huna na kamwe usijaribu kutoa ahadi ambazo huenda ukashindwa kuzitimiza. Usiwe mtu wa kutoa ahadi za uongo, mara nitakununulia hiki na kile.
Mwanaume hatakiwi afahamike siku ana fedha au hana. Maana kuna wenzangu ambao siku za mishahara wanabadilisha hadi kutembea! Mwanamke akijua hilo naye ataongeza ‘mizinga' ili afaidi.

JENGENI KUSAIDIANA

Jambo la muhimu ambalo wanaume wengi wanalisahau ni kutokuwafundisha wapenzi wao wajibu wa kutoa. Utakuta kila kitu ananunua yeye, hata nauli ya basi analipa, wakati mpenzi wake ana kazi yake.

Ifike wakati kwa makusudi, mwanaume ampe majukumu ya kufanya mpenzi wake, hiyo itamsaidia mwanamke kujua namna fedha zinavyokuwa hazitoshi na ataweza kubana matumizi.

ACHA UFUJALI

Kuna wanaume wengine tangu wanatongoza wanakuwa ni wafujaji wakubwa wa fedha kwa kutoa ofa na zawadi kibao. Hii inaweza kumjengea imani mpenzi wako kuwa unazo! Unachotakiwa ni kudhibiti mapema matumizi yako hata kama fedha itakuwepo. Ifahamike kuwa kutoa hakushibishi uhitaji, kadiri unavyotoa ndivyo unavyoongeza mahitaji. Weka maisha yako katikati usijidai tajiri kumbe ni kapuku tu.

BAKI NA HILI

Katika kumalizia niseme tu kwamba, mapenzi si kukomoana, bali kusaidiana. Jenga tabia ya kumsaidia mwenzako ili siku na wewe ukiwa na tatizo akusaidie. Kitu unachotakiwa kukiepuka ni kuwa tegemezi hadi unakuwa kero. Kumbuka kumpiga mizinga mpenzi wako kila mara kunapunguza mapenzi hivyo epukana na tabia hiyo.


VM.
 
Mkuu, nakushauri uweke vipande vipande, kwani huu uzi ni mzuri, lakini kwa namna ulivyouweka napata mashaka kama utasomwa.

Ili kuwasaidia wasomaji wapate illmu hii ya bure, weka kwa topic at least kila baada ya siku mbili ili kuwapa fursa ya kusoma na kuchangia, la sivyo watu watakuwa wanapita tu hapa na kuchapa mwendo.....

Ni ushauri tu.........
 
Back
Top Bottom