Timu ya uhakiki watumishi hewa ipite mikoa yote

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
RAIS John Magufuli ametangaza kutengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango na Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Abdul Dachi kwa tuhuma za kutoa taarifa ya uongo kuhusu idadi ya watumishi hewa wa mkoa huo.

Kilango amedumu katika utumishi wa umma akiwa mkuu wa mkoa huo kwa siku 28 tangu alipoapishwa Machi 15 mwaka huu. Rais alisema Kilango alitoa taarifa za kuwa mkoa huo hauna watumishi hewa.

Hivyo, alichofanya Rais ni kutuma timu ya ukaguzi iliyokwenda kufanya uchunguzi ambapo hadi kufikia Aprili 10, mwaka huu, imebaini kuwepo watumishi hewa 45 huku uhakiki ukiendelea katika wilaya mbili za Ushetu na Shinyanga Vijijini. Rais alisema watumishi hewa waliobainika walikuwa tayari wameshalipwa Sh milioni 339.9.

Aliwataka wakuu wa mikoa yote, wawafichue watumishi hewa wote ili waondolewe mara moja. Aliagiza timu iliyofanya uchunguzi mkoani Shinyanga, itumike kufanya uchunguzi katika mikoa mingine kwa lengo la kukomesha upotevu mkubwa wa fedha za umma, kwani mpaka kufikia Machi 31 mwaka huu jumla ya watumishi hewa 5,507 walibainika.

Imeelezwa kuwa Sh bilioni 583 ambazo serikali imekuwa ikitumia kila mwezi kwa ajili ya kulipa mishahara, Sh bilioni 54 zimekuwa zikipotea kutokana na kulipa mishahara ya watumishi hewa. Hatua ya Rais kutengua uteuzi huo wa Kilango, imepokewa kwa hisia tofauti na wananchi wengi.

Wengine wamepongeza na wengine wameona angepewa muda kwa kupewa onyo ili kuendelea kuhakiki. Lakini ni dhahiri kuwa uamuzi huo wa Rais una lengo la kutaka wakuu wa mikoa na watendaji wengine, kufanya kazi kwa vitendo; na siyo kusubiri kupelekewa taarifa, ambazo inakuwa rahisi kudanganywa.

Katika kuhakikisha azma ya Rais inafanikiwa kuondoa watumishi hewa serikalini na kuwa historia ni vema timu ya uhakiki, kupita mikoa yote, kama walivyoagizwa na rais kwani lililotokea Shinyanga, linaweza kutokea katika mkoa mwingine wowote.

Hata kama kuna idadi kadhaa ya watumishi hewa, kuna uwezekano wapo zaidi au kuna walioonewa kwa sababu mbalimbali, hivyo timu ya uhakiki inaweza kubaini na wakuu wa mikoa wanaweza kuwa walihakiki, lakini hawakufanikiwa katika kubaini wengine. Inawezekana ikasababisha usumbufu au kuchukua muda mrefu katika uhakiki wa mara ya pili.

Lakini, jambo lolote jema ni lazima lifanywe kwa umakini ili kusiwe na mwanya wowote, utakaosababisha watumishi hewa wajirudie wakati mwingine. Hakuna ubishi kuwa fedha nyingi zilizolipwa kwa watumishi hewa, zingeweza kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo na kuwaondolea wananchi adha mbalimbali katika jamii, kama ubovu wa barabara,madawati na mengineyo.

Hivyo umakini anaoonesha Rais katika udhibiti watumishi hewa, unapaswa kuungwa mkono na watanzania wote, hususan idara zinazohusika na malipo, kwani wao ni rahisi kujua kama mtu ameacha kazi, amekufa na mengineyo.

Napenda kuwasihi watumishi katika idara za serikali, wanaotakiwa kutoa taarifa za watumishi hewa, kutoa taarifa kabla ya timu ya uhakiki haijafika, kwani katika Serikali ya Awamu ya Tano hakuna atakayesalimika, ikiwa atabainika kutoa taarifa ambazo siyo sahihi wakati anafahamu kuwa wapo au mengineyo kwa lengo la baadaye kujinufaisha wenyewe.

Pia, katika mikoa mingine ukiwemo Shinyanga baada ya kuwajibishwa Mkuu wa Mkoa na RAS ni vema na watendaji wote waliohusika na sakata la uhakiki, wachukuliwe hatua kali, kwani lazima kuna waliodanganya huku wakifahamu ukweli.
 
Back
Top Bottom