Tido: Twende kazini

kbm

JF-Expert Member
Oct 5, 2012
5,222
1,667
Nilifurahi sana kwamba zamu yangu ya kwanza ilihusiana na mambo ya muziki, kwani nilikuwa mpenzi mkubwa wa muziki, muziki wa aina mbalimbali na kwa hakika sehemu yangu ya kwanza ya maisha ya utangazaji yalijikita sana kwenye vipindi vya muziki.
Kwa muda wa miaka mingi, Tido Mhando amekuwa akifanya kazi ya utangazaji, kazi aliyojipangia kuifanya tangu akiwa mtoto. Mnamo mwaka 1969 ndoto yake hiyo ilitimia na baada ya kipindi cha miezi mitatu ya mafunzo ya ndani, siku aliyokuwa akiisubiri kwa hamu kuu ya kuanza kutangaza kwenye kituo cha Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), ikawadia. Haya ndiyo baadhi tu ya yale aliyoyahadithia Jumapili iliyopita kwenye Simulizi zake hizi za kila wiki. SASA ENDELEA…
Siku yangu ya kwanza hewani, yaani ile siku niliyokuwa nikiivizia sana, siku yangu ya kuanza kutangaza, nikiwa peke yangu kabisa, ilikuja bila ya kutegemea. Kwa nini? Maana si mimi na wala wale waliokuwa wakiniongoza kwa mafunzo walitarajia hivyo. Kwa kawaida utaratibu uliokuwapo siku hizo ni kwamba, mwanahabari mgeni alipaswa kupitia hatua kadhaa za mafunzo kabla ya kupewa nafasi ya kuanza kwenda hewani peke yake. Hilo lilikuwa ni pamoja na kupewa muda wa kipindi fulani akiwa anatangaza kwa kumsaidia mtangazaji mzoefu, kama inavyokuwa kwa mtu anayefunzwa kuendesha gari. Sasa wakati nikiwa bado katikati tu ya mafunzo, wala hata sijaanza kupewa ile nafasi ya kumsaidia mtangazaji mwingine, siku moja bila ya kutarajia, nikaona jina langu kwenye ratiba ya watangazaji wa zamu wa Idhaa ya Biashara. Nikajua kuna kosa limefanyika hapa! Kulikuwapo sababu nyingi zilizonifanya niamini kwamba mpanga ratiba ya watangazaji wa siku hiyo alikuwa kapitiwa.
Kubwa zaidi ni kwamba wale ambao walikuwa wanatangaza idhaa hiyo ya biashara walikuwa ni wateule wachache tu walioonekana kuwa na uwezo na uchangamfu wa utangazaji machachari.
Mimi nilikuwa sijaanza kutangaza, kwa hiyo nisingeweza kuwekwa kwenye kundi hilo. Na zaidi ya hilo, bado nilikuwa sijakamilisha mazoezi mengine. Kikubwa tu, labda, ni kwamba nilikuwa nashiriki sana kwenye kipindi cha watangazaji wote cha kila mwishoni mwa wiki cha “Makoroma Hall”. “Makoroma Hall” kilijipatia umaarufu mkubwa miongoni mwa wasikilizaji. Hiki kilikuwa kipindi cha shoo ya muziki ambapo ni watangazaji wenyewe tu ndiyo walikuwa wakishiriki. Watu walikuwa wanachangamka sana humo, wengine wakitaniana na kujadili mambo haya na yale huku wakipigana vijembe. Kwetu sisi, hii ilikuwa nafasi ya kuitwa na kutambulishwa kwa wasikilizaji kwamba nawe umeingia kwenye familia hiyo ya watangazaji na baadaye na wewe ukaanza kutolewa ushamba kwa njia moja ama nyingine. Nilipenda sana kushiriki kwenye “Makoroma Hall”, maana hapa napo nikuwa napata fursa ya kuzidi kufahamiana na kuchangamana kwa karibu na watangazaji wa muda mrefu. Sasa, baada ya kuliona jina langu kwenye ratiba pale ubaoni, nikaamua kumezea tu. Kwa kawaida ratiba ile ilikuwa inatayarishwa mara moja kila mwezi. Nami nilikuwa nimewekwa kwenye siku za mwishoni-mwishoni mwa mwezi huo. Nikawa na shauku iwapo kama yangefanywa masahihisho. Kila siku asubihi jambo la kwanza nililokuwa nikifanya ni kupita pale ubaoni kuangalia kama pamekuwapo mabadiliko, lakini kila siku mambo yakawa yale yale tu.
Nikaendelea kuwa kimya zaidi nikiomba kosa hilo lisigundulike. Kwa upande mwingine, nilizidi kufanya maandalizi binafsi kwa kila hali, ikiwa ni pamoja na kujipa matumaini kwamba endapo hali itaendelea hivyo hadi siku ya siku, nitamudu bila ya shaka kuliongoza jahazi.
Kwa kawaida vipindi vyote vya idhaa hii ya biashara vilikuwa ni vipindi mbalimbali vya muziki na kama kawaida kulikuwa na watu waliokuwa wakiviandaa. Lakini kile kilichokuwa kikiendelea ni kwamba kila mtangazaji aliyekuwa zamu alikuwa akiingia na aina ya muziki anaoupendelea.
Kwa maana hiyo wasikilizaji walikuwa wanaweza kuwajua mtangazaji gani anapenda muziki upi. Kwa Mfano akiingia Enock Ngombale, basi jamaa walikuwa wanajua kwamba siku hiyo ni ngoma za kutoka nchi jirani ya upande wa pili wa Ziwa Tanganyika, yaani Zaire, (siku hizi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) ndizo ambazo zingevuma. Nami basi maandamizi makubwa niliyokuwa nayafanya kimya-kimya yalikuwa ni kuandaa hazina ya muziki wa kikweli-kweli ambao nilijua ungeweza kunijengea jina barabara mara tu baada ya kuanza kusikika hewani. Naam, siku ya siku ikawadia.
Mapema asubuhi nikapita ubaoni tena, ili niweze kuona kama yamefanywa mabadiliko yoyote. La hasha, mambo ni vile vile. Moyo ukawa unanidunda kupita kiasi. Nikawa najipitisha pitisha huku na kule, ili kujichangamsha na kuzidi kujitia moyo. Hiyo ilikuwa ni zamu ya mwisho ya jioni hadi saa za kufunga matangazo, yaani saa sita usiku. Nilikuwa nampokea mwenzangu aliyefungua kituo saa kumi na moja ambaye siku hiyo alikuwa ni Dominic Chilambo. Kwa desturi nilikuwa natakiwa niwe nimerejea nyumbani mchana baadaye nichukuliwe na gari la kunileta kazini. Lakini nilimfahamisha dereva wa zamu siku hiyo ya kwamba mimi nitakuwa papo hapo ofisini, hivyo asipate shida ya kunifuata nyumbani. Ilipofika saa moja usiku nilikaingia Studio 5 kama ilivyokuwa ikifahamika na nikamwona mwenzangu Chilambo akiwa ameshangaa kidogo. Nikamwambia asiwe na wasiwasi hata kidogo, yeye arejee nyumbani kwa amani kabisa na kila kitu kitakwenda sawasawa bila shida yoyote. Nilikuwa tayari kwenda hewani na Chilambo akanitambulisha kwa wasikilizaji.
Nilipokea zamu kwa shauku kubwa, kwani nilikuwa nimejiandaa vizuri. Nilijua nini ninachotakiwa kukifanya tangu wakati huo hadi mwisho. Nilikuwa niendelee na kipindi kilichokuwa maarufu sana siku hizo - Hongera”. Kilikuwa ni kipindi cha salamu za pongezi na muziki.
Ninaamini siku hiyo wasikilizaji wangu wapya walifurahi sana, maana nilikuwa nafanya kila kitu kwa ajili yao. Muda ulikwenda mbio mbio mno na ghafla nikajikuta namalizia kipindi changu cha mwisho usiku huo, kipindi cha “Lala Salama”.
Sikuamini hata kidogo siku hiyo imepita haraka hivyo. Siku ya pili nilipofika ofisini kila mtu alikuwa ananipongeza kwa kazi nzuri niliyoitekeleza. Wengi wao hawakuamini ya kwamba ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuwa peke yangu hewani. Walishangaa kwa kile walichokiita uchangamfu na uhodari niliouonyesha usiku ule. Kuanzia hapo nikawa nimejijengea heshima.
Nilifurahi sana kwamba zamu yangu ya kwanza ilihusiana na mambo ya muziki, kwani nilikuwa mpenzi mkubwa wa muziki, muziki wa aina mbalimbali na kwa hakika sehemu yangu ya kwanza ya maisha ya utangazaji yalijikita sana kwenye vipindi vya muziki.
Idara yangu mahsusi ilikuwa hasa ni ile ya Matangazo ya Nje (External Service), iliyokuwa ikitangaza hasa kwa lugha ya Kiingereza. Kwa hiyo mara nyingi nilikuwa nikipangwa kwenye zamu ya idara hiyo iliyokuwa na vipindi kadhaa vya muziki, maarufu kilikuwa kile cha “At the Table”. Kipindi hiki kilikuwa mahsusi kwa muziki murua na mororo wa taratibu. Ndipo hapo nami nilipojifunza kuzipenda na kuzicheza nyimbo za mtindo wa jazz na nyingine maarufu kama vile “The Girl from Ipanema” wa Frank Sinatra, “Bring it Home to Me” wa Sam Cooke, “Midnight Train to Georgia” wa Gladys Knight na nyingine nyingi za waimbaji nguli wa kimataifa wa aina hii ya nyimbo kama akina Ray Charles, BB King na wengineo.
Ukiondoa ushiriki kwenye idara hii, pia nilikuwa napangwa zamu kwenye idara nyinginezo na miye binafsi nikipendelea zaidi kwenda kwenye ile Idhaa ya Biashara, maana kule ndiko kulikuwa kila kitu kuhusu mambo ya muziki. Tangu nikiwa skuli, nilikuwa nimejenga mapenzi makubwa ya muziki wa hapa nyumbani, kwani tayari bendi za nyumbani zilikuwa zimeanza kuvuma sana pote Afrika ya Mashariki kiasi cha kuanza kuutikisa sana muziki wa kutoka nchi jirani ya Congo.
Nakumbuka hata wakati mmoja aliyekuwa Waziri wa Utamaduni, Chadieli Mgonja, alizipiga marufuku bendi za Tanzania mtindo wa kuiga nyimbo zilizokuwa za ndugu zetu hao, kwani alijua ya kwamba wanamuziki wetu nao pia walikuwa na uwezo mkubwa wa kufanya vitu vya kuvutia.
Kwa kweli, uamuzi huo ukawa chachu zaidi ya maendeleo ya muziki wa Tanzania. Naam, na mimi mara tu nilipoanza kujimwaga hewani nikawa karibu mno na takriban wanamuziki wote hapa nchini. Hakuna ambaye alikuwa hanifahamu ama mimi kumfahamu. Walikuwa marafiki zangu wa karibu sana. Nilipokuwa zamu, redio ilikuwa ikichangamka bwana. Nilikuwa navurumisha vibao kama vile “Roza Nenda Shule” wa Safari Trippers. “Esta” wa Mbaraka Mwaruka, “Nimepigwa Ngwala” wa King Kiki na Orchestra Marquis, “Nasema Sina Ndugu” wa bendi hiyo hiyo na kadhalika Hali kadhalika, niliachilia vibao kama “Vigelegele” na Rosa” za Wetern Jazz, “Asha” wa Tabora Jazz Band, “Ndugu Umepotea” wa Marijani Shabani, “Harusi” wa Afro 70, “Nipeleka kwa Baba” wa Nuta pamoja na nyingine kadhaa kutoka bendi zilizokuwa zikiwika siku hizo kama vile Cuban Marimba ya Juma Kilaza, Atomic Jazz, Dar Jazz wakijulikana zaidi kama Majini ya Bahari pamoja na wapinzani wao wa jadi Kilwa Jazz Band ya Ahmed Kipande pamoja na kile cha Safari Sound cha Ndala Kasheba akijulikana zama hizo kama Freddy Supreme. Lakini siku zile, labda tofauti sana na siku hizi, muziki wa kutoka Zaire ndiyo uliokuwa juu zaidi, labda pote barani Afrika.
Mpenzi halisi wa muziki wa Kiafrika alikuwa hawezi hata kidogo kuupuuzia. Wanamuziki wa kutoka huko na nyimbo zao, japo zilikuwa kwenye lugha ya kigeni ya Kilingala, zilipendwa kupindukia.
Vikundi kadhaa vya muziki kutoka Zaire vilijijenga sana hapa Tanzania. Vikundi kama Negro Success, Bella Bella, Lipua Lipua, African Fiesta, Thu Zaina, Somo Somo, Orcehstra Bantou, Shama Shama, Vox Africa, na Trio Madjesi (Soso Liso), Zaiko Langa Langa, African Jazz na TP OK Jazz ya aliyekuwa mfalme wa wanamuziki wote wa Zaire wakati huo, Franco Lwambo Luanzao Makiadi.
Kwa maana hii kama ulitaka uonekane DJ wa kweli kweli siku hizo, ilikuwa lazima uukumbatie muziki huu na mimi sikuchelewa.

CHANZO: MWANANCHI
 
jamaa ananifurahisha sana na historia yake....biography nzuri sana..
 

Similar Discussions

2 Reactions
Reply
Back
Top Bottom