Tiba ya foleni Dar katika mchakato

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
Tiba ya foleni Dar katika mchakato






Traffic%20jam.jpg

Magari yakiwa kwenye foleni katoka moja ya barabara JijiniDar es Salaam.



Mchakato wa ujenzi wa barabara za juu (fly over) jijini Dar es Salaam, unaendelea vizuri na utakapokamilika utasaidia kupunguza foleni kwenye maeneo mbalimbali.
Ujenzi huo unaotarajiwa kugharimu mabilioni ya fedha, utafadhiliwa na wahisani mbalimbali ikiwemo Japan ambayo Shirika lake la Kimataifa la Maendeleo (JICA), ndilo linaendelea kutengeneza mpango mkuu wa usafiri (Transport Masterplan).
Kwa kuanzia, kipaumbele cha ujenzi wa barabara za juu kitakuwa maeneo ya Tazara na Ubungo ambapo kumekuwa na foleni kubwa nyakati za jioni na asubuhi.
Akizungumza na Nipashe, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Mwakyusa Philip, alisema fedha za ujenzi huo bado hazijapatikana na kinachosubiriwa ni kukamilika kwa ripoti ya mpango mkuu wa usafiri Dar es Salaam.
"Serikali ya Tanzania iliomba serikali ya Japan isaidie kuandaa Masterplan ya usafiri jijini Dar es Salaam, wao waliteua kampuni kutoka kwao na ikafanya kazi hiyo na tayari wametukabidhi ripoti ya awali ya mpango huo hawakutupa fedha," alisema na kuongeza kuwa ujenzi huo unahitaji fedha nyingi sana.
Aliongeza kuwa baada ya kukabidhiwa mpango huo wa usafiri jijini, wanaendelea na mikakati ya kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo kwenye maeneo yalioyoainishwa katika mpango huo.
Alisema wanafanya kazi hiyo kwa kushirikiana na wadau wake kama Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Miundombinu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Ardhi na Manispaa za jiji la Dar es Salaam.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Dar es Salaam, James Nyabakari, aliliambia gazeti hili kuwa mpango huo ni mkubwa na utahitaji fedha nyingi sana itakapofika wakati wa utekelezaji wake.
"Mpango ule ukikamilika ndio utabainisha nini kifanyike na wapi, lakini maeneo yanayolengwa zaidi ni Tazara na Ubungo. Sisi Tanroads tunahusika zaidi na ujenzi hivyo siwezi kujua fedha za utekelezaji wa mradi zitatoka wapi ingawa najua wahisani mbalimbali watasaidia," alisema.
Pamoja na maandalizi ya mpango huo, Wizara ya Miundombinu itazifanyia matengenezo kwa kiwango cha lami barabara za vichochoroni ili kujaribu kupunguza foleni jijini Dar es Salaam.
Ripoti ya awali ya kampuni hiyo ya Japani inaonyesha matumizi ya barabara za Jiji la Dar es Salaam kuwa kwa wastani mwendo kasi wa magari ni kilomita 25.6 kwa saa na kwamba kama mfumo huo hautaboreshwa mwendo huo utapungua hadi kilomita kumi kwa saa ifikapo mwaka 2030.
Msaidizi wa Msemaji wa Wizara hiyo, Issah Mbura, ameliambia gazeti hili kuwa barabara hizo zinajengwa na mkandarasi mzalendo wa kampuni ya Estim.
Alisema barabara zinazotengenezwa kwa lami ni kutoka External kwenda Ubungo Maziwa na kutoka Maziwa, Kigogo hadi Jangwani. Alitaja barabara nyingine kuwa ni ile inayokatiza Tabata Dampo kuelekea Kigogo.
Kadhalika, alisema kuna mpango wa kuipanua barabara ya Old Bagamoyo ili magari mawili yawe yakipita mawili kwenda na mawili kurudi kwa kuwa barabara hiyo kwa sasa ni finyu na inasababisha foleni.
Alisema mazungumzo ya ujenzi wa barabara hiyo yako katika hatua za awali kabisa na utekelezaji wake si wa hivi karibuni.



CHANZO: NIPASHE http://www.ippmedia.com/
 
Back
Top Bottom