Story of Change Thamani ya Huduma Bora za Uzazi wa Mpango Katika Uwezeshaji Wanawake Kielimu na Kiuchumi

Azathioprine

JF-Expert Member
Sep 16, 2013
483
250
UTANGULIZI:
Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania 2015-2016, umebaini kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya utafiti huo, wanawake wa Tanzania wanazaa wastani wa Watoto 5.2. Vilevile, uwezo wa kuzaa kati ya wanawake unatofautiana kwa makazi yao, viwango vya elimu na uwezo wa kiuchumi. Kwa Tanzania Bara, wanawake wanaoishi katika maeneo ya vijijini ilibainika kuwa kwa wastani wanazaa Watoto 6.0, ikilinganishwa na Watoto 3.8 miongoni mwa wanawake wa maeneo ya mijini.

Kwa upande wa viwango vya elimu, wanawake wasio na elimu wanazaa kiasi cha watoto 3.3 zaidi kuliko wanawake wenye elimu ya sekondari au zaidi. Tofauti na Imani ya wengi kwenye jamii zetu, utafiti ulibaini kuwa uwezo wa kuzaa unapungua sambamba na kuongezeka kwa utajiri wa kaya ya mhojiwa. Wanawake wanaoishi katika kaya maskini sana wana idadi kubwa zaidi ya Watoto. Wastani wa Watoto 7.5 ikilinganishwa na wastani wa Watoto 3.1 kwa wanawake wanaoishi katika kaya Tajiri sana.

Ingawa ni kweli kuwa uzazi ni suala binafsi kwa wenzi, kwa kuwa wao ndio wenye mamlaka ya kupanga na kufanya maamuzi kuhusu idadi ya watoto, muda na mpangilio wa uzazi wao. Lakini, suala hili pia linaigusa jamii nzima inayowazunguka kwa sababu ni suala ambalo linaweza kukwamisha au kusukuma maendeleo ya jamii hiyo.

Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa kiwango cha juu cha uzazi kama hivi ambavyo vimebainika Tanzania, vinaweza kusababisha madhara ya kiafya kwa mama na kwa mtoto. Hivyo basi, kwa mtazamo huu, viwango vya juu vya uzazi sio tu vinaleta changamoto kwa watu binafsi, bali pia vinaleta athari za kiafya na kiuchumi kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Je, Tatizo ni nini?
Taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNPFA) ya mwaka 2018 imeeleza kuwa wanawake wengi wanakuwa na watoto wengi kuliko mahitaji yao kwa sababu ya uwezo finyu wa kupata huduma waitakayo ya kuzuia mimba, hali inayosababisha mimba zisizopangwa. Pia, taarifa mbalimbali za shirika la afya ulimwenguni WHO, zinabainisha kuwa Mimba zisizopangwa zinaweza kusababisha kiwango kikubwa cha kuwa na watoto wengi, kiwango kidogo cha elimu, ukosefu wa ajira na umaskini, changamoto ambazo zinaweza kukumba kizazi na kizazi”.

Hivyo basi, moja ya suluhisho lake ni utolewaji wa huduma bora za uzazi wa mpango sambamba na elimu ya kutosha kwa jamii kuhusu matumizi na manufaa ya uzazi wa mpango. Katika Makala hii, tutajikita katika ufanunuzi wa njia mbalimbali za uzazi wa mpango za hiari na namna zinavyoweza kuwawezesha wanawake kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi kikamilifu.

Uzazi wa Mpango.
Uzazi wa Mpango ni uamuzi wa hiari wa mtu binafsi au wenzi wa kuamua waanze lini kuzaa, wazae watoto wangapi na wapishane kwa muda gani. Jambo zuri ni kwamba nchini Tanzania huduma hii, inatambulika kama ni haki yamsingi ya kila mtu bila kujali kama ameoa au kuolewa na kama amezaa au hajazaa. Zipo sera na miongozo mbalimbali ambayo inasimamia utoaji wa huduma za uzazi wa mpango ikiwa na pamoja na kuweka msisitizo katika kuwaelimisha wanawake kuhusu manufaa ya uzazi wa mpango hivyo kuongeza matumizi ya njia zote za uzazi wa mpango Tanzania.

Manufaa ya Huduma za Uzazi wa Mpango.
Uzoefu unaonesha kwamba uwekezaji katika huduma bora za Uzazi wa mpango una manufaa makubwa katika jamii. Ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vya wanawake na watoto, kudumisha afya ya mama na mtoto, uchumi na maendeleo ya familia.
  • Kupunguza vifo vya wanawake na watoto, kudumisha afya ya mama na mtoto: Iwapo mtoto mmoja na mwingine watapishana kwa miaka 2 au zaidi, Uzazi wa mpango husaidia kurudisha afya ya mama kabla yakubeba ujauzito mwingine. Husaidia kupunguza vifo vya wanawake vinavyotokana na ujauzito na uzazi na pia hupunguza vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka 5.
  • Uzazi wa mpango unachangia kudumisha uchumi na maendeleo ya familia: Hii ni kwa sababu; uzazi wa mpango unasaidia wazazi kuwa na idadi ya watoto ambao wanamudu gharama za elimu, afya, chakula na malazi bora nakupata muda wa kutosha kujishughulisha na kazi za maendeleo na hivyo kukuza pato la familia na uchumi wa taifa.

Njia za uzazi wa mpango:
Njia za uzazi wa mpango zimegawanyika katika makundi makuu manne ambayo ni: Njia za muda mfupi za uzazi wa mpango, njia za muda mrefu za uzazi wa mpango, njia za asili za uzazi mpango na njia za kudumu za uzazi wa mpango.

1. Njia za Muda Mfupi za Uzazi wa Mpango: Njia za muda mfupi ni pamoja na;- vidonge vya uzazi wa mpango, sindano za uzazi wa mpango na kondomu. Vidonge vya uzazi wa mpango ni vidonge ambavyo mwanamke anameza kidonge kimoja kila siku ili kuzuia ujauzito. Vidonge hivi vinakuwa na vichocheo (hormones) vinavyofanana na vile vya asili vya mwili wa mwanamke. Sindano za uzazi wa mpango, pia zina kichochea kimoja cha progestin ambacho hutolewa na mtaalam wa afya kwa sindano kwenye msuli wa bega au tako la mwanamke kila baada ya miezi mitatu. Kondomu ni njia mojawapo ya muda mfupi ya uzazi wa mpango ambayo hutumika ili kuzuia ujauzito na pia husaidia kuzuia maambukizi ya magonjwa yaenezwayo kwa njia ya kujamiiana. .
2. Njia za Muda Mrefu za Uzazi wa Mpango: Njia za muda mrefu za uzazi wa mpango ni pamoja na matumizi ya kitanzi na Kipandikizi. Kitanzi ni njia ya uzazi wa mpango inayowekwa kwenye kizazi ili kuzuia mwanamke kushika mimba. Huduma ya uwekaji wa kitanzi hutolewa na mhudumu wa afya mwenye utaalamu wa jinsi ya kuweka kitanzi. Njia hii inaweza kukulinda kwa muda wa miaka kumi lakini kinaweza kutolewa muda wowote ukitaka kupata mtoto au kwa sababu nyingine yoyote. Kipandikizi ni aina nyingine ya njia ya muda mrefu ya uzazi wa mpango, ambayo huweka chini ya ngozi sehemu ya ndani ya mkono chini kidogo ya kwapa kwa ajili ya kuzuia mimba. Hiki ni kifaa kidogo cha plastiki mfano wa njiti ya kiberiti ambacho kina vichocheo. Kipandikizi huzuia kupata ujauzito kwa muda kati ya miaka mitatu hadi mitano.
3. Njia za Kudumu za Uzazi wa Mpango: Njia za kudumu za uzazi wa mpango ni pamoja na kufunga kizazi kwa mwanamke na kufunga uzazi kwa mwanaume kwa kufanyiwa upasuaji mdogo wa kufunga miriji ya uzazi. Njia hii hufanywa kwa hiari na wale walioridhika na idadi ya watoto walionao. Kwa kawaida ufungaji huu hufanywa kwa muda mfupi tu, pia mteja hahitaji kulazwa hospitalini.
4. Njia za Asili za Uzazi wa Mpango: Njia za asili za uzazi wa mpango ni pamoja na kunyonyesha, Kuchunguza ute wa ukeni pamoja na matumizi ya kalenda ya hedhi. Mfano, njia ya kunyonyesha ni ya uhakika zaidi katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo baada ya kujifungua, Inatakiwa mama awe hujapata hedhi tangu kujifungua na iwapo atamnyonyeha mtoto maziwa pekee kikamilifu pia inashauriwa muda wa kunyonyesha usipite masaa manne mchana na masaa sita usiku.

Je, Njia Ipi ya Uzazi wa Mpango ni Bora?
Shirika la afya ulimwenguni, limeandaa muongozo unaosaidia watoa huduma za uzazi wa mpango kupendekeza njia salama na bora kulingana na hali ya matibabu au sifa zinazohusiana na matibabu yaani Medical Eligibility Criteria for Contraceptive Use 2015. Hivyo ni muhimu, kabla ya kuanza kutumia njia yoyote ya uzazi wa mpango ukakutana na watoa huduma ili waweze kukushauri njia bora zaidi inayokufaa wewe binafsi ili kupunguza uwezekano wa kupata athari za kiafya.

Katika kuleta tija zaidi katika huduma hizi, nina mapendekezo kadhaa kwa mamlaka husika na jamii kwa ujumla:-
  • Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wengine ifanye jitihada zaidi ya kuwaelimisha wanawake na jamii kwa ujumla kuhusu manufaa ya uzazi wa mpango ikiwa ni pamoja na kuelezea njia zote za uzazi wa mpango. Changamoto kubwa ni ufahamu mdogo sana juu za njia zilizopo za uzazi wa mpango.
  • Wizara ya Afya ihakikishe inaendelea kuboresha zaidi huduma za uzazi wa mpango pamoja na upatikanaji wa bidhaa zote za uzazi wa mpango bure ili wateja waweze kuwa na uwanda mpana zaidi wa kuchagua bidhaa wanayoipenda kulingana na miongozo iliyopo.
  • Ni vizuri kwa wenzi kuzungumzia uzazi kwa pamoja lakini pia, ni busara kwa jamii yetu tuanze kujitahidi kuwapa wanawake ridhaa ya kuamua idadi ya watoto wanaotaka kuzaa.
  • Watoa huduma za afya kutokua na mitazamo hasi kwa wasichana wa shule wanaofika kupata huduma za uzazi wa mpango. Kwa sababu kama kutakua na masimango katika utoaji wa huduma hiyo, itasababisha asiwe balozi mzuri kwa wasichana wengine kufika kupata huduma hizo. Hivyo kurudisha nyuma jitihada za serikali.
HITIMISHO:
Ushahidi wa kitafiti una onesha wazi kuwa hali ya wanawake kuwa na watoto wengi, inawanyima fursa ya kushiriki kikamlifu kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi, hivyo kufifisha jitihada za ukombozi wao kimaendeleo. Pia ni dhahiri kuwa upatikanaji wa taarifa sahihi pamoja na huduma bora za uzazi wa mpango kwa wasichana wa shule itasaidia kupunguza idadi ya wasichana wanaoshindwa kuendelea na masomo kutokana na mimba zisizotarajiwa. Sambamba na hilo, itasaidia kupunguza uhitaji wa utoaji mimba usio salama unaoweza kuleta madhara zaidi ya kiafya.

Hivyo basi, huduma bora za uzazi wa mpango ni nyenzo mojawapo inayoweza kusaidia kuleta ukombozi wa kielimu na kiuchumi kwa wanawake nchini.

Asante!
 
Upvote 1

Abrianna

JF-Expert Member
Mar 30, 2021
4,691
2,000
Makala nzuri sana hii, jamii kwa kiasi kikubwa haina elimu ya kutosha kuhusu njia bora na salama za uzazi wa mpango, pia jamii yetu kwa kiasi kikubwa ina imani potofu kuhusu suala zima la uzazi wa mpango, viongozi wetu pia wamechangia kwa kiasi fulani kupotosha umma juu ya njia za uzazi wa mpango

Kuna mmoja alisema zaeni maana matiti mnayo ya kunyonyesha na elimu ni bure
 

Azathioprine

JF-Expert Member
Sep 16, 2013
483
250
Makala nzuri sana hii, jamii kwa kiasi kikubwa haina elimu ya kutosha kuhusu njia bora na salama za uzazi wa mpango, pia jamii yetu kwa kiasi kikubwa ina imani potofu kuhusu suala zima la uzazi wa mpango, viongozi wetu pia wamechangia kwa kiasi fulani kupotosha umma juu ya njia za uzazi wa mpango

Kuna mmoja alisema zaeni maana matiti mnayo ya kunyonyesha na elimu ni bure
Asante Abrianna kwa mchango wako.

Ni kweli elimu imekua ni kikwazo kikubwa sana nchini kwa suala la uzazi wa mpango, ndio maana unaweza kuwa na kiongozi ambaye anaweza kutoa matamko kama hayo hadharani. Wakati sisi kama Taifa ni wanachama wa Umoja wa Mataifa na pia tume saini utekelezaji wa Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030, wenye lengo mojawapo kutokomeza umasikini kwa watu wote.
 

Abrianna

JF-Expert Member
Mar 30, 2021
4,691
2,000
Asante Abrianna kwa mchango wako.

Ni kweli elimu imekua ni kikwazo kikubwa sana nchini kwa suala la uzazi wa mpango, ndio maana unaweza kuwa na kiongozi ambaye anaweza kutoa matamko kama hayo hadharani. Wakati sisi kama Taifa ni wanachama wa Umoja wa Mataifa na pia tume saini utekelezaji wa Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030, wenye lengo mojawapo kutokomeza umasikini kwa watu wote.
Tatizo hizi ajenda huwa hawazitilii maanani badala yake wanaongoza kwa matamshi na vipaumbele vyao binafsi pasipo kuweka maslahi ya wananchi mbele, kwa sasa wanawake wengi waliacha kutumia njia za uzazi wa mpango baada ya lile tamko
 

Azathioprine

JF-Expert Member
Sep 16, 2013
483
250
Tatizo hizi ajenda huwa hawazitilii maanani badala yake wanaongoza kwa matamshi na vipaumbele vyao binafsi pasipo kuweka maslahi ya wananchi mbele, kwa sasa wanawake wengi waliacha kutumia njia za uzazi wa mpango baada ya lile tamko
Kweli Kabisa, ni vizuri kwa wanaopata nafasi za uongozi kuzingatia dira na ajenda za nchi kwa kipindi husika. Naamini bado tuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi katika uboreshaji wa huduma hizi.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom