Thamani ya Gavana wa Benki Kuu Tanzania sawa na wakulima 12,700 | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Thamani ya Gavana wa Benki Kuu Tanzania sawa na wakulima 12,700

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Pdidy, Jan 26, 2010.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Jan 26, 2010
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,473
  Likes Received: 5,708
  Trophy Points: 280
  Thamani ya Gavana wa Benki Kuu Tanzania sawa na wakulima 12,700

  KUNA mjadala ulianzishwa katika moja ya mitandao ambamo Watanzania kokote walipo ulimwenguni hukutana kubadilishana mawazo. Mjadala wenyewe ulianzishwa na mchangiaji ambaye aliweka angalizo kuhusu mada nyingi zilizokuwa zikijadiliwa.


  Kwa mawazo yake, mijadala mingi ilikuwa hasi, ikijadili kero, kulaumu, kulaani, kutukana, na kukata tamaa. Akajaribu kuonyesha kuwa yapo mambo mazuri tu yanatokea hapa nchini na kwamba yanapaswa kujadiliwa pia.


  Kwamba zipo takwimu zinazoonyesha kuwa Tanzania imekuwa ikifanya vizuri sana -ikiwamo kuwa ya kwanza -katika masuala kadha wa kadha. Niliufuatilia kwa karibu mjadala ule huku nikitafakari kwa kina maoni kutoka kwa wachangiaji mbalimbali nikabaini ipo haja ya kudadisi zaidi.


  Nimekwishaeleza katika makala zangu huko nyuma kwamba tatizo la mijadala yetu mingi haijatulia. Tumekuwa na hulka ya kurukia tukio, tukalijadili, tukalizunguka, tukawajadili watu halafu tukadhani tumefanikiwa kulichambua na kulielewa kwa ufasaha.


  Nikasema inawezekana kabisa tunachokijadili ni matokeo tu ya tatizo, lakini kiini chenyewe cha tatizo ama hatujakibaini, au hatujakikabili barabara.


  Leo nitajaribu kutazama suala moja ambalo limezusha mjadala mkali sana katika mitandao, vyombo vya habari na katika majadiliano ya kawaida mitaani. Nitajaribu kulitazama kwa sura tofauti kidogo na namna mijadala ilivyolichambua.


  Ni suala la nyumba ya Gavana. Umeibuka mjadala mkubwa kuhusu gharama za ujenzi wa makazi ya Gavana wa Benki Kuu, ambayo yamegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.27. Je, hizi ni fedha nyingi mno kujengea nyumba moja tu?


  Mjadala uliopo unazunguka katika kiasi cha fedha zilizotumika katika ujenzi na madoido ya nyumba yenyewe. Ile nyumba ina bwawa la kuogelea ambalo maji yake yanaweza kupashwa joto analohitaji muogeleaji. Nyumba ina kamera karibu kila kona. Ina ofisi.


  Ina chumba cha kupokelea wageni. Ina vyumba vya kulala vitano. Ina nyenzo zingine za usalama n.k. Kwa kifupi tu haitofautiani na ile ya Big Brother kule Afrika Kusini.


  Nitawaomba wasomaji tusafiri hadi vijijini tulikozaliwa (wale ambao walizaliwa mijini twendeni tu mkajifunze kijijini kulivyo). Kule vijijini ujenzi wa nyumba ya kuishi ni jambo la fahari mno kuliko mengine mengi.


  Unaweza kujijengea mwenyewe au ukaomba majirani wakuongezee nguvu. Hakuna tenda. Hakuna bajeti. Hakuna misururu ya wataalamu wa ushauri wa hiki au kile. Hakuna mtu anataka kukata cha juu, n.k.


  Shughuli ya kujenga nyumba ya kuishi inaanza hivi. Anayetaka kujenga nyumba anamtuma mtoto kwenda kwa majirani na marafiki kama kumi hivi kuwaalika waje kusaidia ujenzi wa nyumba siku inayofuata. Kesho yake asubuhi na mapema shughuli inaanza hivi:


  Wanawake wanaenda kisimani au mtoni kuteka maji na kuja kuandaa udongo na tope litakalotumika kukandikia ukuta. Kwa upande wao, wanaume wanaondoka mapema kuelekea porini kukata miti, fito, kamba za kufungia na nyasi za kuezekea.


  Baadaye kama saa nne asubuhi hivi kazi ya ujenzi inaanza kwa kasi ya ajabu. Hawa wanaanza kwa kuchimbia nguzo chini. Wale wanaketi kufunga nyasi katika mafungu ya kuezekea. Wengine wanaanza kupachika fito na kuzifunga kwa kamba. Akina mama kule tayari wanachanganya tope. inapofika saa saba mchana kazi inasimama.


  Wajenzi wote wanaenda kula chakula ambacho kiliandaliwa rasmi kama malipo kwa wale waliofanya kazi ya ujenzi toka asubuhi. Mara nyingi inakuwa ni ugali wa kutosha na kuku kadhaa au mbuzi.


  Lakini wakati wa ujenzi kunakuwa na kiburudisho kama uji, togwa au maziwa. Baada ya lanchi wajenzi wanarejea katika shughuli.


  Kufikia saa kumi na mbili jioni ya siku hiyo hiyo, nyumba inakuwa tayari kwa mtu kuhamia. Kasoro inakuwa ni unyevunyevu ambao waweza kumuathiri anayelala mle.


  Labda tuangalie gharama za ujenzi ule ili tubaini thamani ya nyumba yenyewe. Maji waliyoteka akina mama kwa ajili ya kujengea yalikuwa bure. Ila tunaweza kuthamanisha kazi waliyoifanya. Tuchukue ndoo 80 x Sh100 inakuwa Sh8,000 ukiongeza na nguvu kazi ya kuchimba udongo inakuwa Sh5,000. Gharama ya miti 30 x Sh1,000 inakuwa 30,000.


  Tuweke gharama za fito 200 x 100 inakuwa Sh 20,000. Pia tuweke gharama za nyasi za kuezekea tuchukulie kwa jumla tu Sh10,000, halafu tuongeze na gharama za kamba za kufungia Sh5,000.


  Mwisho tuweke gharama za kuku watatu, ugali, togwa na maji ya kunywa jumla kiasi cha Sh20,000, kisha tuongeze Sh2,000/- kama gharama tulizopitiwa na hatukuziweka.


  Jumla ya gharama za ujenzi wa asilimia kubwa ya nyumba za kijijini ambazo hukaliwa na wanakijiji wa Tanzania ambao ni karibu asilimia 70 ya wananchi wote wa nchi hii ni Sh100,000 tu.


  Ni katika mantiki hiyo hiyo wapo watu wanashangaa kwamba inakuwaje nyumba moja tu igharimu Sh1.27 bilioni wakati fedha hizo zingetosha kujenga nyumba zile za kijijini kama 12,700. Kwa hiyo kinachotazamwa hapa ni thamani ya nyumba za kijijini 12,700 kwa nyumba moja ya Gavana.


  Kwa maneno mengine, kwa mantiki ya umuhimu wa nyumba ya kuishi, inabidi ukusanye wakulima wa kijijini 12,700 ndiyo wafikie thamani ya Gavana mmoja tu wa Benki Kuu ya Tanzania.
   
 2. r

  ral Senior Member

  #2
  Jan 26, 2010
  Joined: Dec 30, 2009
  Messages: 126
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Nimeipenda sana mkuu! wadau mnasemaje?
   
 3. JoJiPoJi

  JoJiPoJi JF-Expert Member

  #3
  Jan 26, 2010
  Joined: Aug 8, 2009
  Messages: 2,464
  Likes Received: 1,411
  Trophy Points: 280
  imetulia
   
 4. Relief

  Relief JF-Expert Member

  #4
  Nov 20, 2010
  Joined: Aug 6, 2010
  Messages: 255
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Mwanajamii, this is it!! The income inequality range is toooooooooooo biiiiiiiiiig, hapa ndo unapotambua je ni maisha bora kwa kila mtanzania au bora maisha kwa mtanzania.
  I feel this man, but wats the way forward??
   
Loading...