Samuel Eto'o 8/3/2009 5:56:57 AM
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema litaweka utaratibu wa kuwaalika wachezaji wanaocheza soka la kulipwa Ulaya kuja Tanzania kuchezea timu za hapa kwa lengo la kuinua kiwango cha soka nchini. Rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema lengo la mpango huo ni kukuza kiwango cha soka nchini mara baada ya wachezaji hao kuja kufanya mazoezi ya pamoja na timu za hapa.
"Tunaelekea kwenye soka la kulipwa na hili nadhani ni la msingi. Mfano, tunamchukua Samuel Eto'o aliyeko Inter Milan au Kaka wa Real Madrid au hata Ronaldinho, tunamwuingiza kwenye timu kama Simba au Yanga, wanafanya mazoezi na baadaye mechi, lengo hapa ni kuona utaalamu wake, alisema Tenga.
"Hawa wenzetu wako mbali na sisi tuwatumie...najua wakati ligi zinaendelea inakuwa ngumu, tunaweza kuweka ka-program baada ya ligi zote kumalizika wachezaji hawa wakaja na inawezekana. Tuna wadhamini wengi, lakini tunasimamia palepale, tunataka kutengeneza mpira wetu," aliongeza Rais huyo wa TFF.
Akizungumzia hali ya soka Tanzania, Tenga alisema kwa sasa anafurahi kuona imepiga hatua kutokana na kuwepo kwa programu mbalimbali za vijana.
Alirejea kauli yake ya awali kuwa anamalizia kutengeneza misingi ili kwa watakaokuja baadaye waweze kuendeleza badala ya kuanza moja.
"Tanzania inao wapenzi wengi wa soka na hili ndilo naweza kusema, msingi wake ni huu, tunajenga na tunaimarisha misingi," alisema Tenga.
Source: http://www.nifahamishe.com/NewsDetails.aspx?NewsID=2716554&&Cat=6