Tendwa awaelimisha polisi kuhusu haki za vyama

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
219,422
911,172
Tendwa awaelimishe polisi kuhusu haki za vyama Send to a friend Tuesday, 30 November 2010 20:41 0diggsdigg

tendwa%20anywea.jpg
John Tendwa.

Siku kadhaa baada ya Jeshi la Polisi nchini kuzuia vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara na maandamano ya kuwapongeza walioshinda viti vya ubunge katika majimbo mbalimbali nchini, jeshi hilo juzi liliondoa amri hiyo kimya kimya. Kaimu mkuu wa jeshi hilo, Kamishna Clodwig Mtweve, aliviambia vyombo vya habari kwa nyakati tofauti juzi kuwa uzuiaji huo haukukilenga chama chochote cha siasa, bali ulikuwa ukizingatia hali halisi baada ya uchaguzi.

Kamishna Mtweve alidai kuwa zuio hilo lilikuwa muhimu kwa sababu serikali ilikuwa haijaundwa na mawaziri walikuwa hawajateuliwa na kuongeza kuwa ndio maana jeshi hilo limeondoa zuio hilo baada ya rais kuunda serikali mwishoni mwa wiki. Alisema jeshi hilo liliona hakuna ulazima wa watu kupongezana kwa kukusanyika viwanjani, bali wangeweza tu kufanya hivyo ukumbini au hotelini. Hata hivyo, wiki iliyopita kamishna huyo wa polisi alikuwa amenukuliwa akisema kuwa alikuwa hajui lini amri hiyo ingeondolewa.

Kauli hiyo ya Kamishna Mtweve inatudhihirishia mambo mawili makubwa. Kwanza, kwamba jeshi hilo pengine halijui mipaka yake kisheria na kiutendaji. Kwa kujipachika mamlaka ya kuamua vyama hivyo viruhusiwe au visiruhusiwe kufanya maandamano au mikutano, na kwa kudhani linayo mamlaka ya kuamua wapi na lini mikutano hiyo ifanyike, jeshi hilo sio tu linapora mamlaka ya vyama hivyo, bali pia linavunja sheria iliyovianzisha vyama hivyo. Pili, jeshi hilo lina dhana potofu kwamba kabla rais hajatangaza baraza lake la mawaziri na kuliapisha, serikali inakuwa haipo na kwa tafsiri ya kauli ya kamishna huyo, jeshi hilo linadhani kuwa wakati huo ndilo linakuwa limeshika nafasi ya serikali.

Inawezekana kabisa kwamba kuondoshwa ghafla kwa amri hiyo, kwa namna moja ama nyingine, kumetokana na kukakamaa kwa baadhi ya vyama vya siasa ambavyo chama kimojawapo kimetishia kwenda mahakamani dhidi ya jeshi hilo kwa kuvunja Sheria ya Kinga, Mamlaka na Haki za Bunge ya mwaka 1988, chini ya kifungu cha nne cha sheria hiyo, ambacho kinampa mbunge haki ya kufanya mikutano ya hadhara na ambayo inazitaka mamlaka zote husika kuwezesha mikutano hiyo kadri itakavyomfaa mbunge na kadri inavyowezekana kwa mazingira yaliyopo. Hivyo, kwa tafsiri yoyote ya sheria hiyo, yeyote anayezuia mikutano ya wabunge anavunja sheria.

Tulisema mwishoni mwa wiki kupitia safu hii kuwa mojawapo ya sababu za migogoro kati ya vyama vya siasa na jeshi hilo ni uelewa mdogo na tafsiri finyu ya viongozi wa jeshi hilo kuhusu Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992, ambayo haina kifungu chochote kinacholipa jeshi hilo mamlaka ya kudhibiti au kuratibu shughuli za vyama vya siasa. Sheria inatamka kuwa vyama hivyo vitoe taarifa polisi ndani ya muda uliowekwa kisheria ili vipewe ulinzi na kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinakuwapo.

Ndio maana tunalishauri jeshi hilo kuanzia sasa litambue na kuheshimu mipaka yake katika muktadha wa sheria zilizopo. Jeshi hilo litafanikiwa tu iwapo litafanya kazi yake bila kushinikizwa na chombo chochote na kwa kutambua ukweli kwamba chini ya sheria hiyo, vyama vyote vya siasa ni sawa. Pengine msajili wa vyama hivyo, John Tendwa, atakuwa ametimiza wajibu wake vilivyo iwapo atawaelimisha viongozi wa juu wa jeshi hilo kuhusu sheria hiyo ili vyama vyote vya siasa viachwe vifanye siasa ambayo vilianzishwa kufanya.

Ni matumaini yetu kwamba jeshi letu hilo litapokea changamoto hizo kwa moyo mkunjufu na kwa kutambua kuwa Watanzania wanayo imani kubwa na jeshi hilo, hasa wakati huu ambapo chini ya uongozi wa Inspekta Jenerali Said Mwema, limewapa wananchi matumaini makubwa kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi yetu.
 
Tatizo kubwa la Viongozi wa Tanzania ni kutojua sheria na taratibu katika mambo mbalimbali.Haiwezekani kuwa Viongozi wa kufanya mambo wanayoyataka wao.Lakini huko nyuma waliweza kutuburuza watakavyo lakini watanzania wa leo wameamka sasa na kujua wapi wanakwenda na wapi wametoka.
Idara ya polisi na vyombo vingine vya Dora pamoja na Viongozi wake wajue kuwa Tanzania ya leo si ile ya Jana. Sioni hata kama Tendwa mwenyewe anaweza kuvielimisha vyama vya Siasa zaidi ya yeye kueleimishwa.

Tabia ya Viongozi kufanya kazi kwa mazoea imepitwa sasa kila mtu ajue nini cha kufanya ili tuweze kuondokana na migogoro ya kijinga.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom