SoC02 Teknolojia chanya juu ya matumizi ya gesi majumbani, maofisini na migahawani

Stories of Change - 2022 Competition

solomon_bandio

New Member
Jul 19, 2022
1
0
TEKNOLOJIA JUU YA MATUMIZI YA GESI MAJUMBANI, OFISINI NA MIGAHAWANI

Naitwa Solomon Bandio ni kijana wa miaka 25 mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nikitunukiwa digrii ya sanaa katika sosholojia. Ni mtanzania na ninaishi Dar es Salaam kama makazi yangu ya kudumu. Napenda kuwasilisha andiko langu juu ya matumizi chanya ya teknolojia katika matumizi ya gesi tukiwa majumbani, maofisini na hata kwa wenye biashara za migahawa.

Matumizi ya gesi ya kupikia yamezidi kukua siku hadi siku iwe majumbani au maofisini kwetu. Na hii imechagizwa na ukweli kwamba gesi imekua ikiokoa muda na kurahisisha mahitaji yetu kwa haraka sana kuliko kutumia mkaa ama kuni katika kuandaa vyakula vyetu vya kila siku.

Kwa Tanzania, Kuna makampuni kadhaa yanayojihusisha na uuzaji na usambazaji wa gesi kwa wateja wake. Makampuni kama Oryx Gas, Taifa Gas na Lake Gas ni baadhi tu kati ya kampuni nyingi zilizopo Tanzania ambazo zinajihusisha na uuzaji na usambazaji wa mitungi ya gesi kwa ajili ya matumizi mbalimbali majumbani, maofisini na hata migahawani.

Katika tafiti fupi niliyofanya watumiaji 9/10 wa gesi hawana uhakika au hawajui ni lini gesi yake itaisha aidha iwe majumbani au sehemu za biashara za chakula (migahawa). Wengi wa watumiaji wa gesi hukadiria tu kwamba kwa matumizi yake ya gesi, Gesi yake inaweza kudumu kwa muda gani pasi na kuisha. Na katika kuwadadisi zaidi wengi wao walisema ni mara nyingi gesi huwaishia pasipo wao kujua na hivyo kupelekea aidha usumbufu kwa wateja kama ni mgahawani hivyo kuleta hasara kibiashara na kupoteza wateja na kuleta usumbufu na aibu kwa wageni ikiwa ni mazingira ya nyumbani.

Hii yote inatokana na kwamba hawana kifaa maalumu au teknolojia maalumu ambayo itakuwa rafiki kwao yenye uwezo wa kuonesha matumizi ya gesi yake na kuonesha ni kiasi gani cha gesi kimebakia kwenye mtungi wake. Hali hii ya kutojua kiwango cha gesi kilichobakia na matumizi ya gesi yanaendaje ndio changamoto ya pili ya matumizi ya gesi ikiongozwa na changamoto ya kwanza ambayo ni kusababisha milipuko majumbani, madukani na hata migahawani.

Watumiaji wengi wanatamani kuwe na kifaa maalumu cha kuonesha matumizi ya gesi na kiwango cha gesi kinachobakia kila baada ya matumizi ili kuwasaidia kujua bajeti ya matumizi yao lakini pia kujua ni lini gesi yake inaweza kuisha ili aweze kujipanga kununua mtungi mpya wa gesi na kuepuka fedheha ambayo ingeweza kumkuta kwa kuishiwa gesi.

Katika kutatua tatizo hilo, Kampuni tajwa hapo juu zinazojihusisha na maswala ya uuzaji na usambazaji wa gesi wanaweza kuja na teknolojia ambayo itawawezesha watumiaji wa gesi kujua matumizi yao ya gesi sambamba na akiba ya gesi iliyobakia kwenye mitungi yao. Lakini kuweka kifaa pekee inaweza isiwe suluhisho la tatizo hilo la kutokujua gesi inaisha lini au imebaki kiasi gani. Kampuni hizi zinaweza kwenda mbali zaidi na kujenga uhusiano na makampuni ya simu ili kuwezesha kuwatumia ujumbe wa maneno kwa wateja wao kwenye simu ili kuwakumbusha kuhusu matumizi na akiba ya mitungi yao ya gesi.

Kushirikiana na kampuni za simu ni njia nzuri zaidi ya kumkumbusha mteja juu ya matumizi ya gesi yake pamoja na salio la gesi yake. Sababu Watanzania wengi wana simu za mkononi na aghalabu wengi wao hutumia muda wao mwingi pia kwenye simu zao za mkononi hivyo ni rahisi kuona ujumbe wa maandishi ukitumwa kama kuwakumbusha matumizi ya gesi yake na kiwango kilichobakia kwenye mtungi wa gesi yake.

Teknolojia hio inaweza kurahisisha mambo mengi ikiwemo pia ununuzi wa gesi husika na kwa wakati muafaka. Mfano; Ujumbe unasomeka kama "Ndugu mteja Solomon matumizi ya gesi yako ni asilimia 90% umebakiwa na asilimia 10% tunakukumbusha uweze kununua gesi nyingine kuepuka usumbufu. Asante". Hii itaondoa kadhia kubwa ambayo watumiaji wengi wa gesi hukutana nayo katika majukumu yao ya kila siku ya kujitaftia riziki au pia majumbani. Mtu anataka kutumia gesi lakini imeisha na pengine ni usiku wa manane na maduka yashafungwa hivyo kupelekea usumbufu na kadhia.

Faida ya teknolojia hii kwa watumiaji wa gesi ni kubwa sana; Sababu kwanza mteja anakua anajua ni kiwango gani cha gesi kinakuwa kimebakia kwenye mtungi wake, Pili anaweza kuweka bajeti ya matumizi yake kulingana na hali yake ya kiuchumi na kipato chake na faida ya mwisho ni kumtaarifu mteja juu ya kiwango kilichobaki cha gesi hivyo kumwondolea kadhia ya kuishiwa na gesi ghafla pasipo yeye kujiandaa.

Lakini pia teknolojia hii itaondoa ukakasi na ile dhana kwamba wakati mwingine wateja hulalamika kuibiwa gesi kwa kupewa ujazo ambao sio sahihi kulingana na ukubwa wa mtungi. Baadhi ya watumiaji wa gesi huwa na mashaka kama ujazo wa gesi ni sawa na kipimo cha mtungi wenyewe. Hivyo kwa kuwezesha teknolojia hii ya kumpa mteja uwezo wa kuona kiwango cha gesi kilichopo kwenye mtungi husika pia itamuongezea uaminifu na thamani halisi ya pesa yake.

Mwisho kabisa jitihada za makusudi kabisa zinaweza kufanyika ili kumuwezesha mteja wa gesi awe na uwezo wa kujua kiwango cha gesi yake kilichobakia na matumizi yake ya gesi kwa ujumla sambamba na kumkumbusha kupitia ujumbe wa simu za mikononi.

Napenda kuwasilisha andiko langu.
 
Back
Top Bottom