SoC01 TEHAMA inakuza au inadumaza fikra kwa watoto?

Stories of Change - 2021 Competition

Prof Sankara

Member
Sep 17, 2021
6
10
"Mapinduzi yanaletwa na watu, watu wanaofikiri kama watu wa vitendo na kutenda kama watu wenye fikra” aliwahi kusema Rais wa Ghana Nkwame Nkuruma wakati wa uhai wake.

Maendeleo Teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) yamechukua nafasi kubwa katika maisha ya Watanzania. Fikira zetu zote tumezielekeza katika ombwe la Teknolojia ya mawasiliano.

Ni wakati ambapo binadamu hasa Waafrika kama siyo Watanzania tumebaki kuwa watumiaji wa nyezo hizi za mawasiliano pasina kuangalia kwa makini jinsi zinavyodhoofisha uwezo wa fikra zetu. Hapa lazima tukubaliane kuwa kuna faida na hasara za uwepo wa maendeleo ya sayansi ya mawasiliano ya habari.

Dhana ya uwezo wa kufikiri na kutawala mazingira hujengwa kulingana na mazingira yanayomzunguka mhusika katika eneo husika kwa wakati na muda husika. Mabadiliko yeyote yanayotekea katika mahali huwa na chanzo cha fikra za watu ambao huleta mabadiliko hayo kama sehemu ya kutatua changamoto katika jamii husika.

Hali ni mbaya zaidi kwa watoto wanaozaliwa karne hii ya 21,ni waathirika wakubwa wa maendeeleo haya. Wazazi hupenda kuwafurahisha na kuwaburudisha watoto wao, huwanunulia zawadi, kama mwanasesere (mdoli) bunduki na ndege za plastiki,magari,baiskeli, simu zenye michezo au muziki nk.

Muda wote mtoto akiwa nyumbani hujishughulisha na madubwasha haya, anajifanya anapiga risasi, anaendesha gari, kucheza michezo ya komputa, simu nk.

Michezo ya siku nzima mtoto hushinda akijifariji na midoli, ‘gemu’ gari baiskeli nk.. Sisemi kwamba hayafai, la hasha! Ni mazuri lakini swali la kujiuliza ni nchi gani Duniani iliyopata maendeleo kwa kutumia zana,fikira, utamaduni wa Taifa lingine? Hapa kidogo nigusie mambo ya asili yanayopambanua jamii moja na nyingine, Lugha ubunifu, utamaduni nk.

Ikiwa mtoto huyu hushinda kutwa kwa kubinyabinya bunduki ya kichina na kucheza michezo ya komputa , nafasi yake ya ubinifu itatoka wapi? Utamaduni wake ni upi?

Historia inaonesha kabla ya wazungu kuvamia bara la giza, waafrika walikuwa na ubunifu wa asili.Walitengeneza vifaa walivyovitumia katika maisha yao, kama mkeka, kuchonga viti, mizinga,uvuvi, kilimo, kutengeneza nguo kwa kutumia ngozi za wanyama na magome ya miti nk, swali la kujiuliza ni nani aliwafundisha haya?

Walijipambanua hivyo kulingana na mazingira ya maisha yao, baadaye jamii ilipitia mabadiliko mbalimbli ya kimaendelao mpaka wakati huu. Baada ya uhuru Serikali ilianzisha sera ya elimu ya kujitegemea na ujamaa.Ilihimiza juu ya kutafuta,kuthamini, maarifa na elimu ili mtu aweze kujitegemea,kuwa huru katika uamuzi wa mambo yake mwenyewe.

Lengo lingine lilikuwa ni Kumwezesha mwanafunzi kujivunia utaifa na utamaduni wa Taifa la Tanzania. Elimu hii ilimtaka kijana kudumisha mila na desturi za kitanzania na kuachana na mila za kigeni ambazo zilionekana kuharibu utaifa wa Tanzania.

Hivyo basi kwa kuwa tunafikiri kuwa watoto wetu watapata elimu na maarifa kwa kutukuza vitu vinavyoletwa na wazungu kama ishara ya kuwaburudisha kumbe ni kuwangamiza katika fikira na hivyo tusitarajie mabadiliko katika maisha yao baadaye.

Zamani watoto walijifunza vitu vingi utotoni na vilikangaza akili na mwili, hasa panapochagiza na kufundishwa na mzazi.

Kwa mazingira ya usasa ambao uliopo , watoto wetu Leo, hawawezi kuumba, kuunda na kujishughulisha na fikira zaidi ya kutegemea vya wazungu. Hawajiamini, magoigoi, mbumbu hali inayosababisha kumalaza darasa la saba mtu hajui hata kusoma.

Wanapofikia umri wa ujana watoto wanakumbana na janga lingine, amabalo linaua na kumaliza kabisa fikira zao. Si mtoto tena, yupo kidato cha tatu au nne. Mazingira yanayomzunguka ya kutokuwa na fikira na kutukuza ya wazungu naye huingia mzima mzima.

Kijana wa kisasa, ana simu kali, yenye programu kama facebook, twitter, instagram whats app nk.Akili na fahamu zao zimejengeka katika matumizi ya mitandao ya kijmii.

Vijana wa vyuo Sekondari na watu wengine utawaona wamebeba simu kubwa mikononi. Kazi ni kupapasa vioo vya simu zao.ukidhani wanatafuta maarifa na kujifunza mambo ya msingi unakosea! ni kusifu picha za nusu uchi wanazoweka dada zetu wazuri wa Tanzania .

Tabia hii ya kusifu picha za wasichana Mitandaoni, imetawala fikira za vijana kwa leo. Mtu anaamka asubuhi anatafuta, nyumba, jengo, au gari na alafu apige picha halafu anaiweka mtandaoni ili watu waisifu.

Wasichana wameenda mbali zaidi, wanapiga picha zinazoonesha viungo vyao,kisha kuweka mtandaoni ili watu waisifu picha yake.Kwa sababu watu walio katika mkondo huu ni wajinga, bila hiyana huisifu picha kwa maneno ya manukato. Inawezekanaje kuisifu picha ya mwanamke aliye nusu uchi,au aliyepiga picha akiwa ndani ya gari ilihali hata kupiga honi hajui?. Ni kupoteza muda bila faida.

Walimu shuleni wanapiga kelele,marufuku mwanafunzi kuwa na simu shuleni. Kwa kuwa wamejawa na ujinga hupingna na utaratibu huo. Mwishowe huishia kufukuzwa shule. Kumzuia mwnafunzi kutokuwa na simu Shuleni ni jambo la maana sana.Kumfanya mwanafunzi aweke bidii katika jambo moja tu, kusoma.

Ikiwa jamii yetu itaathiriwa hasi zaidi , hatari iliyopo ni kuwa naTaifa la watu wajinga wasiofikiri kama watu wenye fikira. Sisemi njia hizi ni mbaya la hasha! Tunazitumia kinyume. Kujidhalilisha, kuudhalilisha utu wake, hivyo hatufikiri kama watu wenye fikira kama alivyosema Nkuruma miaka mingi iliyopita

Azimio laArusha 1967 kuna kipengele kinachosema “Kuweka heshima ya mwanadamu kwa kufuata barabara kanuni za Tangazo la Ulimwengu la Haki za Binadamu” ikiwa mtu kwa utashi wake anaweka picha ya uchi mtandaoni maana yake ameshindwa kujiheshimu na hivyo anajidhalilisha yeye, utu wake, na jamii yake ambayo haina utamaduni wa namna hiyo.

Ameshindwa kuheshimu haki yake kama binadamu,hii si tabia nzuri ya kuvumilika. Ndio maana Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha mswada wa sheria ya makosa mtandaoni ambao unasubiriwa kusainiwa na Rais na kuwa sheria. Ikiwa mswada huo utasainiwa basi kutakuwa na sheria itakayoweza kuzuia matumizi hasi ya mitandao ya kijamii.

Mwalimu nyerere alisizitiza kuwa ili watu waendelee ni lazima kuweka bidii kuondoa ujinga na kujijengea uwezo,elimu,na ufahamu wa kukabilina na changamoto za maisha.kuhakikisha hilo linafanikiwa serikali iliweka juhudi kuchapisha vitabu, kujenga shule na kuanzisha taasisi mbalimbali za elimu kama elimu ya watu wazima lengo likiwa kuleta mapainduzi ya fikira kwa binadamu , kupanua, kukabiliana na kutatua matatizo ya kisiasa kiutawala na kijamii.

Bado tuna maduka machache sana ya vitabu;hatuna utamaduni wa kununua vitabu; halafu usomaji wetu unazidi kupungua. Uvivu wa kusoma uliokuwepo tangia zamani unazidi kuiva na kuota nywele, vipele na manyasi. Mmoja wa waandishi mashuhuri wa riwaya nchini William Mkufya kasema katika jarida jipya la fasihi , SOMA, kuwa idadi ya Watanzania zaidi ya milioni 44 wanaosoma imepungua kwa asilimia 50 karibuni.

Mtazamo kwa wengi unamaanisha tunasoma tu tukiwa shule, kufaulu mitihani. Tukishamaliza shule basi tena kitabu hakishikwi, kinaonekana utoto; hakuna muda. Kazi inayojitokeza ni kunyoosha mikono miwili kupokea pombe, kazi, kulea, kukaa barazani kupiga soga. Haya yote ni muhimu ndiyo; lakini ukweli mmoja.

Kusoma ni sehemu mahsusi ya maendeleo ya jamii yeyote duniani. Na kusoma si tu kwa ajili ya elimu-ufundi au elimu-taaluma bali kusoma kujifunaisha kilugha na kistarehe. Haya hupatikana ndani ya fasihi, tamthiliya, sinema, muziki na sanaa.

Moja ya matokeo ya tatizo hili kubwa la kutokusoma fasihi na hadithi za kubuni linaonekana namna leo watu wengi (wazee kwa vijana; viongozi, wanasiasa , waandishi wa habari na wataalamu) wasivyoweza kuandika au kusema sentensi chache bila kuchanganya changanya maneno ya Kiswahili na Kiingereza. Bado sisi wabovu tunadhani tutaeleweka zaidi ( na kuonekana wajanja) tukiandika Kiswahili hapa; Kiingereza (kibovu) pale; Kiingereza hapa na Kiswahili (kibovu) kule. Ulemavu huu unatokana na kukosa msamiati.

Tunapoendelea kupokea njia hizi za mawasiliano, lazima tuangalie ni kwa namna gani hazitaathiri fikira zetu kulingana na utamaduni wetu. Si busara kumnunulia mtoto ki-komputaa cha kuchezea ‘gemu’ badala yake tumnunulie kitabu. Wakizoezwa hivyo tutakuwa tunajenga Taifa lenye watu wanaofikiri kama watu wenye utu.

Watoto wakuuzwe njia za kuwafanya wawe watu wa kufiri na si u kupokea madubwasha kutoka ng’ambo na kuyashabikia kana kwamba yanazalishwa Tanda Tundale. Nafasi hiyo itawapa watot uwezo wa kufikiri, kuunda kuvumbua, kuumba. Elimu ni mchakato endelevu wa kuuondoa ujinga.
 
Back
Top Bottom