TCU yafungua dirisha la udahili kwa waombaji wa vyuo vikuu kwa Mwaka 2024/25

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
3,331
12,952
1.0 UTANGULIZI
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) inapenda kufahamisha umma, Taasisi za Elimu ya Juu na Wadau wote wa Elimu ya juu ndani na nje ya nchi kuwa dirisha la maombi ya udahili kwa waombaji wa Shahada ya Kwanza kwa mwaka wa masomo 2024/2025 limefunguliwa kuanzia leo tarehe 15/7/2024. Dirisha hili litakuwa wazi hadi tarehe 10/8/2024.

2.0 UTARATIBU WA MAOMBI YA UDAHILI KWA MWAKA WA MASOMO 2024/2025
2.1 Makundi ya Waombaji wa Udahili
Maombi ya udahili wa kujiunga na Shahada ya Kwanza yanahusu makundi matatu ya waombaji:

a) Wenye sifa stahiki za Kidato cha Sita;
b) Wenye sifa stahilki za Stashahada (Ordinary Diploma), au sifa linganifu; na
c) Wenye sifa stahiki za Cheti cha Awali (Foundation Certificate) cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Ili kufahamu sifa stahiki kwa makundi matatu yaliyotajwa hapo juu, vyuo na programu zilizoruhusiwa kudahili, waombaji wanapaswa kusoma vigezo vilivyooneshwa katika vitabu vya mwongozo wa maombi ya udahili vinavyotolewa na TCU (Bachelor's Degree Admission Guidebooks for 2024/2025 Academic Year) vinavyopatikana katika tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz).

Utaratibu wa Kutuma Maombi ya Udahili
2.2
a) Maombi yatumwe moja kwa moja kwenye vyuo ambavyo mwombaji amevichagua na kuchagua programu za masomo anazozipenda.
b) Maelekezo mahususi ya jinsi ya kutuma maombi yanatolewa na vyuo husika.
2.3 Vigezo na Sifa za Waombaji Udahili Vigezo na sifa katika programu mbalimbali za masomo vinapatikana katika tovuti za vyuo husika na katika vitabu vya mwongozo wa maombi ya udahili vinavyopatikana katika tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz)
2.4 Masuala Muhimu ya Kuzingatiwa na Waombaji
a) Kusoma kwa makini na kuelewa mwongozo wa udahili uliotolewa na TCU pamoja na maelekezo mahususi ya vyuo kabla ya kuanza kutuma maombi ya udahili.
b) Kuingia katika tovuti za vyuo na kuwasiliana na vyuo moja kwa moja ili kujua taratibu za kutuma maombi na kupata taarifa za kina kuhusu programu za masomo ili kujiridhisha kabla ya kutuma maombi.

c) Kutuma maombi moja kwa moja vyuoni kupitia mifumo ya kielekroniki iliyowekwa na vyuo husika.

d) Waombaji wenye vyeti vilivyotolewa na mabaraza ya mitihani nje ya nchi wanapaswa kuwasilisha vyeti vyao katika Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kwa vyeti vya Elimu ya Sekondari au Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa vyeti vya Stashahada ili kupata ithibati ya ulinganifu wa sifa zao kabla ya kutuma maombi ya udahili.

Tume inawahimiza waombaji wote wa udahili kuendelea kupata taarifa sahihi kupitia tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz), tovuti za vyuo vilivyoruhusiwa kudahili wanafunzi wa Shahada ya Kwanza, pamoja na taarifa mbalimbali zinazotolewa na TCU kupitia vyombo vya habari.

3.0 TAHADHARI
Tume inatoa wito kwa waombaji wote wa Shahada ya Kwanza, endapo watahitaji kupata ufafanuzi wa suala lolote linalohusu udahili, wawasiliane moja kwa moja na vyuo husika. Aidha, iwapo watahitaji maelezo ya jumla wanaweza kuwasiliana na TCU kwa kutumia barua pepe es@tcu.go.tz.

Pia, TCU inawaasa wananchi kuepuka kutapeliwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini.

Imetolewa na:
Prof. Charles D. Kihampa
KATIBU MTENDAJI
TUME YA VYUO VIKUU TANZANIA


1000086754.jpg

IMG_20240715_170403_395.jpg

Pia soma: Matokeo Kidato cha Sita 2024 yatoka. Ufaulu wapanda kwa asilimia 0.26

 
Back
Top Bottom