Tatizo La UKIMWI | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tatizo La UKIMWI

Discussion in 'Mahusiano, mapenzi, urafiki' started by X-PASTER, Mar 22, 2009.

 1. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #1
  Mar 22, 2009
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Mtazamo Wa Uislamu Juu Ya T
  atizo La Ukimwi


  0.0 Utangulizi

  Ubora na uzima ni asili ya mwanadamu kama alivyotufunza Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) katika hadithi yake mashuhuri ya fitra, na kutufahamisha kwamba aliyebakia katika fitra hiyo ndie aliefanikiwa. Asili ya mwanadamu ni kupendelea kheri (Nafsi zimeumbiwa kupendelea kheri). Lakini kwa sababu ya hekima za Allaah za kuwepo vita baina ya haki na batili na mivutano mikubwa baina ya kambi mbili hizi kunapelekea wakati mwengine mizani kutetereka na mambo kuharibika hasa pale ubabe wa batili unapoonekana kushika nafasi katika jamii, na kujilazimisha kwa watu na kuwaacha wachache wanaofuata haki kuwa katika njia panda wakadhania wakati mwengine kuwa hakuna njia ya kuokoka na hali mbaya ila kujisalimisha katika hali halisi. Hali hii inadhihirika wazi pale tunapoangalia masuala mbalimbali likiwemo la ukimwi na tunaporudi kuangalia nini cha kufanya, ukijaribu wakati mwengine kubainisha hatari ya vyombo vya habari na hatua za kuchukua kama vile kuondosha uchafu uliomo, unaweza ukakuta wale wanaohisi kwamba kuondosha vipindi hivyo katika TV moja sio suluhisho eti atakwenda kuangalia TV nyengine, hii ni kauli kiasi fulani ina ukweli lakini tusisahau kwamba kila mmoja ataulizwa kila alichokifanya yeye na hataulizwa ubaya wa mwenziwe, jengine wajibu kulifahamu hapa ni kwamba haki itabakia hata ikiwa wafuasi wa haki watakwisha au kubakia mmoja pekee. Kwa maana hii ni lazima kwa kila muislam anapochangia katika kutatua tatizo lolote katika jamii atoe ushauri sahihi na kwa mujibu wa dini yetu.

  Mwenyezi Mungu Ametuwekea mipaka na Akatutaka tusiichupe na mwelekeo wowote wa kuichupa mipaka hio ni kwenda kinyume cha maumbile na kujiingiza kwenye maangamizi, haya yanatupelekea kuona kwamba yote yaliyoamrishwa na Allaah ni yenye maslahi kwetu na yaliyokatazwa ni yenye madhara, iwe tunayaona au hatuyaoni. Mifano mingi ya wale waliokuwa wanatenda maovu na vipi mwisho wao ulikuwa, tunaiona katika Quran tukufu pale tunaposoma kama vile kaumu vya watu wa nabii Lut walipoangamizwa kwa kosa la liwati; kwa kutamaniana wanaume kwa wanaume na kuacha wanawake ambao ni tohara kwao kindoa, mfano mwengine ni watu wa Shu’ayb walioingia katika dhuluma ya kijamii katika vipimo, kadhalika na watu wa firaun walikita katika dhuluma za kisiasa. Jamii hizi ziliangamizwa kwa kukosa kutanabahi hadi pale maasi yalipokuwa ni sehemu ya maisha yao wakawa hawawapendi kabisa wale ambao wamekuwa wakiwakosoa. Hali hii inatuthibitishia wazi kwamba maasi yoyote ni mabaya kwa jamii nzima na sio kwa yule ayatendae tu bali hata wasiotenda. Hivyo ni lazima kutumia nguvu zetu zote kuzuia maasi yasienee katika jamii na kuwaelekeza kwenye njia ya usalama ili jamii iweze kusalimika.

  Moja kati ya aina za maasi ni suala la zinaa; nayo ni maingiliano yasiyo ya kisheria kati ya mwanamke na mwanamme pamoja na suala la liwati kati ya mwanamme kwa mwanamme. Yote haya ni mambo ya kinyume na fitra na maumbile ya mwanadamu na ndio maana kuyatenda kwake kunaletea madhara na maangamizo. Miongoni mwa athari kubwa ya zinaa na liwati ni haya maradhi ambayo hadi hivi sasa imeshindikana kupatikana tiba yake, licha ya majaribio au kupatikana kwa njia za hapa na pale zijulikanazo za kurefusha muda wa kuishi mgonjwa nayo ni maradhi ya UKIMWI. Kwa upande wa waislam tunayakinisha kwamba dawa yake lazima ipo kwa mujibu wa mafunzo ya dini yetu kama asemavyo Mtume kwamba “Kila maradhi yana dawa yake” Miongoni mwa dawa hizo ni kurudi katika fitra sahihi na kuacha uchafu na kutafuta dawa nyengine. Ama katika hali ya kuacha uchafu iwe ni kwa kukusudia hasa ndani ya nafsi zetu kwamba tumekusudia kubadilika na tunataka Allaah atubadilishie hali zetu kwenda katika hali bora.

  Ikiwa hilo silo lengo letu bali ni wenye kufanya istihizai kwamba tutafute njia nyepesi za kuzini basi Allaah hatotubadilishia hali hizo, na hata akitubadilishia kwa kutupa dawa ya maradhi hayo tutarajie kwamba maradhi mengine yatakuja na yatakuwa ni makali zaidi kuliko tuliyonayo. Ama kauli kuwa hayana dawa hivyo haitafaa kusema kuwa haya sio maradhi kwani kauli hii huenda ikampeleka mtu nje ya dini. Hakika dini ya uislamu kwa ukamilifu wa mpango kamili wa maisha unatupa suluhisho la tatizo kama hili au mfano wake, suluhisho la kudumu ikiwa watu watazingatia na kukubali na kutekeleza kwa nia na ikhlasi yale ambayo dini itakuwa imeyaeleza na hayo ndiyo ambayo waraka huu mfupi utajaribu kuyaonesha.

  Maradhi hayo kabla kutambuliwa rasmi 1981 yaliyokuwa yameshika ukali wake na kusababisha vifo vya watu kadhaa. Hesabu rasmi za Shirika la Siha la Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba mpaka kufikia kipindi cha 2000 watu 40 milioni watakuwa tayari wameshaambukizwa ukimwi, 30 milioni watu wazima, 10 milioni watoto, hali hii itazidi ikiwa bado dawa haijavumbuliwa. Utafiti vile vile unaonesha kwamba kuna ongezeko kubwa la ukimwi kuanzia mwaka 1984 hadi mwaka 1999

  0.1 Maradhi Yanaenea Kwa Kasi

  Kwa mujibu wa takwimu kwenye kiambatisho, inatosha kuwa ni dalili ya ongezeko la maradhi haya kwa kasi zaidi katika rika zote. Vile vile inasemekana kwamba asilimia 80 ya wagonjwa ni watu ambao tayari wameshafunga ndoa. Vile vile tunaweza kusema ongezeko pia liko kwa vijana ambao bado kuoa wala kuolewa, pia sababu ya ongezeko la ukimwi, katika jamii ni suala la mchanganyiko wa watu kutoka miji mbali mbali nje ya nchi pamoja na kuhamahama watu ndani ya nchi kutoka sehemu hii na kwenda sehemu nyengine. Jamii kama hii yetu ya kizanzibari yenye asili ya kiislam na urathi mkubwa wa kufunza akhlaqi na silka njema, inapaswa kwa makusudi kila wakati kurejea kwenye dini na kufaidika na mafunzo ya dini ambayo kwa hakika yamepotea kwa sababu mbali mbali kama vile:

  • Kukosekana watu wakutosha wanaoamrisha mema na wanaokataza mabaya.
  • Watu kukosa elimu sahihi ya dini yenye kuonyesha umuhimu wa kujistiri, masomo yenye kubainisha kuharamishwa zinaa, ulevi, liwati n.k ambayo ndio zaidi vinavyopelekea au kuchangia kuzuka maradhi mabaya kama haya na mengineyo.
  • Watu kukumbwa na kuburuzwa na mfumo wa maisha yaitwayo maisha ya kisasa ambayo ni zaidi yamefungua milango ijulikanayo kwa istilahi ya Ibahiya. (yaani kila kitu ni halali kukitenda) na kuwafanya watu waigize mitindo ya nje ya michanganyiko mibaya na mavazi ya maajabu.
  • Wazee kukosa mielekeo ya kuwaongoza vyema watoto.
  • Miundo mibaya ya elimu kwa kufuata mifumo ya masomo ambayo inadharau au kuiona dini haina maana sana haya tunapata katika elimu za familia nk.

  Licha ya haya uislamu unatupa nafasi kumuokoa mwanadamu ambae ndie mtengenezaji wa ustaarabu (civilization) asiangamie hasa tukizingatia kwamba jamii kuendelea inahitaji watu walio na siha na uzima wa kimwili na kiroho.

  0.2 Jee Uislamu Unazuia Starehe Ya Kimwili?
  Starehe ya kimwili (kujamii) ni ghariza (matamanio) ya kimaumbile, wala sio tabia aliyojizowesha nayo mwanadamu, ambayo anaweza akaiacha ikiwa atataka. Ni lazima ghariza hii ishibishwe kwa mujibu wa sheria za dini. Sheria ambazo hazikuiharamisha bali imeipangiwa misingi maalum. Kinyume chake itatumika mfano ya wanyama, na mtu lengo lake kuu litageuka na kuwa ni kujamii kila wakati na hapo hataweza tena kujizuia na mwishowe hatachagua njia, na ataishibisha kwa kulawiti, au kulawitiwa au kuingilia wanyama, kusagana, kuingiliana na watu watano pamoja nk. Mtu kama huyu hupoteza utu wake na kuwa zaidi ya mnyama, na kuacha uhalali uliowekwa na dini ambao ni ndoa pekee.

  0.3 Mahusiano Batili
  Kwa maana hii dini imeharamisha mahusiano yoyote ya mtu nje ya ndoa, au kukaa pamoja baina ya mwanamme na mwanamke wawezao kuoana kwani shetani atakuwa wa tatu wao na ataanza kuwapambia uchafu, na hatua ya pili atawasukuma kufanya uchafu huo.

  Mwenyezi Mungu Anasema katika Suratul Baqarah aya 36 akibainisha vipi Iblisi alimsukuma Adam kufanya makosa:

  “Basi Shetani (Iblisi adui) aliwatelezesha wote wawili (wakahalifu amri ya Mola wao)”

  Mwenyezi Mungu Anasema
  “Wala msikaribie zinaa hakika hiyo zinaa ni uchafu mkubwa na njia mbaya kabisa”
  Suratul Israa 31

  Hakika athari za zinaa ni nyingi sana katika jamii na kama ilivyo kawaida athari za mema hazibaki kwa mtendaji tuu bali huenea kwa jamii nzima vile vile athari za maasi hazibakii kwa mtendaji bali huzagaa kwa jamii nzima na miongoni mwa athari za zinaa:-
  • Vifo vya haraka kama ilivyokuja katika hadithi ya Mtume.
  • Kuvunjika familia.
  • Kupotea nasaba.
  • Kuchanganyika kwa kizazi.
  • Kupotea haki ya watoto hasa upande wa baba kama vile mirathi.
  • Mtoto huyo pia haitwi yatima.
  • Kuvunjika heshima ya familia.
  • Kupotea kwa akhlaqi njema.
  • Kuongezeka kwa maasi kwa kuondoka haya, katika hali kama hii zinaa itaonekana ni jambo la kawaida na asiezini huitwa ni mjinga na watu kumstaajabia.
  • Uislamu vile vile umetuhadharisha na vishawishi vya zinaa pale Aliposema Allaah: “Wala msiikaribie zina hakika ni jambo chafu na njia mbaya” Al-Israa: 32


  0.4 Adhabu Kwa Mwenye Kupuuza Amri
  Lakini atakaekuwa amepuuza sheria basi adhabu itamfikia kama ilivyotamkwa na uislam kwa alieoa na kuolewa kupigwa mawe hadi kufa, na alieluwa bado kuoa au kuolewa kupigwa bakora mia. Ama kwa yule ambae atakuwa anazikaribia dalili za zinaa basi adhabu ndogo kama vile kuadhiriwa itapitishwa. Allaah Anasema:

  “Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume mpigeni kila mmoja katika wao mijeledi mia wala isiwashikeni kwa ajili yao huruma katika kupitisha hukumu ya Allaah ikiwa nyinyi mnamuamini Allaah na siku ya mwisho, na lishuhudie adhabu yao hii kundi la waislamu”
  An-Nuur: 2

  Hivyo Uislamu hauruhusu hata kidogo ile hana ya “zinaa ya usalama” yaani kuzini na mwanamke mmoja tu au mwanamme mmoja tu. Pia hairuhusu biashara ya kondom kwa ajili ya kujikinga nayo, bali ni sawa na kuichochea.
  Ama utumiaji ingelikuwa kwa njia ambayo sio kama hiyo basi hilo lingelihitajia maelekezo mengine. Vile vile uislamu umeharamisha liwati na aya inathibitisha.

  “Na wakumbushe (Nabii) Luut alipowaambia watu wake je, mnaufanya uchafu na hali mnaona? Mnawaingilia wanaume kwa matamanio mabaya baada ya wanawake hakika nyinyi ni watu mfanyao ya ujinga kabisa” An-Namli: 54-55

  Pia angalia 165-166 Ashu’araa:
  “Je, mnawaingilia wanaume katika viumbe vyake Allaah na mnawaacha alichokuumbieni Mola wenu katika wanawake wenu kweli nyinyi ni watu mnaochupaa mipaka mliyowekewa”
  Ashu’araa: 165-166

  Pia kumlawiti mwanamke
  Mtume anasema: “Mwenyezi Mungu hatamuangalia mtu aliyemuingilia mkewe kwa nyuma”

  Ikiwa wanawake ni makonde yetu basi lazima kujiuliza ni mahala gani mtu akimuingilia mkewe anatarajia kuvuna? Hivyo hii haiwi dalili ya kuingiliwa mwanamke popote apendapo mwanamume, na vile vile ni ukosefu wa elimu na kwenda kinyume na fitra ya mwanadamu na Aayah tukufu za Allaah.
  Pia katika hedhi ni kosa, Allaah Anasema...

  “Niajiepusheni na wake zenu wanapokuwa katika hedhi (zao) wala msiwakaribie mpaka pale wakishajitoharisha”
  Suratul Al-Baqarah: 222

  Katika hali ya hedhi sheria imeruhusu mtu kumgusa mkewe sehemu nyengine zote zile isipokuwa baina ya kitovu na magoti.

  1.5 Nini Cha Kufanya Kuondosha Matatizo Yaliyopo
  Ni lazima kuziba njia zote zile ambazo zinapelekea katika haramu au sivyo kazi itakuwa ni ngumu, (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)a na mtu anaetapatapa baharini bila ya kujua kuogelea, hutarajiwa zaidi kufa kuliko kuokoka, na wala haitatusaidia kitu kuwasha mishumaa na kushereheka na kuomboleza waliofikwa na janga la ukimwi hasa tukizingatia kwamba haya ni kinyume cha dini. Ama Uislamu umetutaka tumzuie shetani na kuziba kila njia mfano wa haya ni kuzingatia yafuatayo:

  • Kufumba macho dhidi ya kuangalia vishawishi mbali mbali angalia Suratun-Nuur: 30-31.
  • Kukataza watu kwenda utupu kwa kuvaa nguo fupi, laini, zenye kubana zisizositiri miili ikiwa ni mwanamke au mwanamme.
  • Wanawake kutodhihirisha mapambo yao, manukato, na wanaume kuvaa mapambo ya kike kama herini nk.
  • Kuweka udhibiti katika vyombo vya habari na kutoonyesha mambo kinyume na maadili ya dini.
  • Mwanamke kutoregeza sauti anapozungumza na mwanamme awezae kumuoa.
  • Inawataka watu wawe na haya.
  • Uislamu umehimiza ndoa na Kuwa ni kinga kuu dhidi ya maasi na ni jambo la kinyume mtu awe keshaoa halafu bado azini hakika huyo anaonyesha kwamba hajaelewa umuhimu na maana ya ndoa.

  Ndoa pia ni dalili ya Qudra ya Allaah
  “Na hakika katika ishara zake za kuonyesha ihsani zake juu yenu ni kuwa amekuumbieni wake zenu katika jinsi yenu ili mpate utulivu kwao, nae amejaalia mapenzi na huruma baina yenu bila shaka katika haya kuna ishara kwa watu wenye kufikiri.”
  Suratun Ruum: 21

  Katika kutuonyesha umuhimu wa ndoa Uislamu umetoa ruhusa ya mwanamme kuoa hadi wanne.
  Jambo hili ni muhimu na wala halihusiani na ongezeko la maradhi kama wanavyodhani wengi wakasahau kwamba uzinifu ni hatari katika ongezeko la watu.


  Miongoni mwa malengo ya ndoa ni kuwalinda watu na tabia mbaya.
  Pia Uislam unahimiza maingiliano kamili ya kimwili na kuyashibisha kwa kuanza na utangulizi.

  Ni lazima watu kufahamu fiqh ya ndoa katika Uislam ili kukamilisha majukumu na haki za pande mbili na kuzuia mambo ambayo pengine yangechafua ndoa na kutokea khiyana.

  1.6 Hitimisho
  A- Ili Tupate Ari Ya Kuacha Maasi Na Kujiepusha Na Mitihani Nukta Zifuatazo Ni Lazima Kuzingatiwa.

  • Kutambua ubaya wa kosa lenyewe.
  • Kuwa ni watu wenye haya mbele ya Allaah.
  • Kuzichunga neema kwa kutambua kwamba makosa ni yenye kusababisha nakama na maangamizo.
  • Kumuogopa Allaah kwa uhakika.
  • Kumpenda Allaah mapenzi yenye utiifu.
  • Kuitukuza mtu nafsi yake.
  • Kujua mwisho mbaya wa makosa.
  • Kutojipa tamaa ya kuishi sana.
  • Kupunguza matamanio ya kula, kunywa na starehe nyenginezo zenye kupeleka kunyanyua shahawa na matamanio mabaya.

  Njia nyengine za kupambana na maradhi:
  • Kutambua wazi kwamba asili ya maradhi haya ni uzinzi.
  • Kujiepusha na mahusiano ya kimwili nje ya ndoa na aina nyengine za haramu.
  • Kujiepusha na utumiaji wa ulevi na madawa ya kulevya ambayo ni njia moja wapo ya kuenea maradhi ya ukimwi kwa kukosa nadhari kwa alielewa.
  • Kuangalia damu kabla ya ndoa.
  • Kuangalia vyema damu kabla ya kutiwa mgonjwa.
  • Maelekezo na ushauri nasaha kwa mgonjwa wa ukimwi ili isiwe ni kichocheo cha kueneza maradhi.
  • Wageni wanoingia nchini kuangaliwa nyendo zao na ikiwezekana kupimwa ifanyike hivyo
  • Kuwapa maelekezo wale wanaotoa huduma moja kwa moja kama vile vinyozi kuepuka matumizi mabaya ya viwembe.
  • Kuhimiza watumishi wa mahospitali kufanya kila tahadhari katika matumizi ya vyombo kama vile sindano n.k
  • Kutofanya istihizai kwa wale waliofikwa na mtihani na kukumbuka kwamba mtihani unaweza kumfikia yeyote na kwa njia mbali mbali (ya makusudi na bahati mbaya).


  B-Tunapopata Misiba Kutambua Kwamba:
  • Mitihani ina malipo kwa atakaeweza kuvumilia.
  • Mitihani ni sababu ya kusamehewa madhambi hivyo lazima mtu alete toba na istighfari.
  • Tambua hiyo ni qudra ya Allaah.
  • Mtihani haujaja kukuadhibisha bali ni kukukumbusha na kukujaribu subira yako.
  • Mtihani waweza kuwa ni sababu ya kupanda daraja ya imani pia ikawa ni sababu ya kupata pepo.
  • Mtihani ni haki ya Allaah kwa waja wake iwe mtihani ni katika mambo yenye madhara au mazuri.


  C- Mapendekezo Ya Kisheria

  • Kutokubali kuoa au kuolewa na yule ambae tayari ameshakumbwa na maradhi ya ukimwi
  • Inajuzu kuwalazimisha wanaotaka kuoana kuangalia kwanza siha zao ikiwa ndio kwanza wanataka kuoana na kwa wajane zaidi.
  • Inawezekana kwa waliotayari kuambukizwa maradhi kuoana baina yao pamoja na kuchukua hadhari za kitabibu ili kuweza kuzuia maradhi kwa kizazi kitakachozaliwa, au kuzuia kizazi kisikuwepo kwa kujua wazi kwamba pindipo atazaliwa tayari keshaambukizwa na kuishi katika hali ngumu, na itakuwa ni njia moja wapo ya kueneza maradhi yenyewe.
  • Ni lazima kwa alie na maradhi kumpa taarifa mwenzake kama ni mke au mume. Ama kunyamaza na kumsababishia maradhi kwa makusudi itakuwa ni kosa kubwa.
  • Ni haki ya kisheria kwa kila mmoja kuomba kuachana ikiwa mmoja wao amefikwa na maradhi hayo, ama wakiridhiana kubaki pamoja, iwe ni pasina maingiliano ya kimwili ya moja kwa moja, pamoja na kutumia njia za kinga kama vile (gloves) katika kutoa huduma.
  • Mama aliefikwa na maradhi haitakuwa vyema kunyonyesha ikiwa tunayakini kwamba kufanya hivyo kutapelekea mtoto huyo kupata maradhi.
  • Huduma za wagonjwa zifanywe na jamaa, ikiwa mgonjwa asie na jamaa basi dola au jumuiya zinazoshughulikia wagonjwa kuwapa huduma.
  • Ni kosa kubwa mtu kueneza ukimwi kwa makusudi ima kwa kuchangia damu yenye ukimwi akiwa anajua hivyo, au kumwingilia na ikiwa atakufa alieambukizwa muambukizaji atahesabiwa ameua makusudi naye anastahiki kifo.
  • Ikiwa kimakosa basi itamuwajibikia dia kama yule aliyeua kimakosa na atazuilika na mirathi
  • Wako wanaoona kwamba akiwa ni mja mzito kabla miezi minne na ikathibitika mimba kuingia maradhi anaweza kuitoa, ama baada ya miezi minne itakuwa ni haramu.

  Ni matarajio yetu kwamba waraka huu utasaidia katika suala hili la kupambana na tatizo la ukimwi ikiwa tutajaribu kuyazingatia haya.


  Wabillahi Tawfiq
   
Loading...