Tatizo la Tanzania ni waziri mkuu?

Companero

Platinum Member
Jul 12, 2008
5,604
1,704


Tatizo la Tanzania ni Uwaziri Mkuu?


Sakata la Zanzibar kujiunga na OIC na G55 kudai Tanganyika irejeshwe lilisababisha Waziri Mkuu abadilishwe. Mchakato wa utoaji wa zabuni ya uzalishaji wa umeme wa dharura kwa kampuni tata ya RICHMOND ulipelekea kujiuzulu kwa Waziri Mkuu. Ugawanaji wa fedha za akaunti tete ya ESCROW unaweza kumuondoa Waziri Mkuu.

Kwa nini Tanzania ilianzisha cheo hiki cha Waziri Mkuu? Ilikianzisha ili iweje ilhali kuna Rais Mtendaji? Nini kilipelekea hilo ukizingatia kuna Katibu Mkuu Kiongozi?

Majibu ya maswali haya yanaweza kutusaidia kubaini kwa nini tunashindwa kutatua matatizo ya utendaji na ufisadi nchini. Karibu kila mara kunapokuwa na mgogoro mkubwa wa kiutendaji au kiufisadi suala la Waziri Mkuu linajitokeza. Pengine tatizo kubwa tulilo nalo ni nafasi ya Waziri Mkuu. Kama ni hivyo ‘tuutatue' Uwaziri Mkuu.

Tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu inaonesha kuwa tumekuwa na Mawaziri Wakuu 10 toka sehemu moja ya nchi yetu ilipopata uhuru mwaka 1961. Mawaziri Wakuu wawili wa kwanza – Julius Nyerere mwaka 1961 na Rashidi Kawawa mwaka 1962 – hawakuwa chini ya Rais yeyote. Wao ndio walikuwa watendaji na wawajibikaji wakuu wa Serikali.

Utaratibu wa kuwa na Rais ulipoanza baada ya kuwa na Jamhuri, nchi ilikaa kwa miaka 10 bila kuwa na Waziri Mkuu. Hivyo, kati ya mwaka 1962 na mwaka 1972 kulikuwa na Rais, makamu wake, na mawaziri pamoja na makatibu wakuu wao. Siri ya kwa nini Tanzania iliamua kuwa na Waziri Mkuu aliitoboa Rais wa kwanza wa Tanzania wakati alipokuwa akishinikiza kujiuzulu ama kufukuzwa kazi kwa Waziri Mkuu mwaka 1994.

Hivi ndivyo Nyerere alivyoitoboa siri hiyo katika kitabu cha Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania: "Narudia: kumbadili Waziri, hata Waziri Mkuu, si jambo la ajabu. Anaweza kujiuzulu, anaweza kufukuzwa na nchi isitikisike. Lakini huwezi kumtikisa Rais wa nchi bila kuitikisa nchi yenyewe." Ni dhahiri Uwaziri Mkuu ulikuwa ni wa kumkinga Rais.

Nyerere utaratibu huo ulimfaa. Japo humo anasema kuwa Kawawa hakufanya kosa lolote ila akambadili tu kwa kumweka Edward Sokoine, muktadha wa wakati huo unaonesha alifanya mabadiliko hayo kuzuia mtikisiko. Mwaka 1977 nchi ilikuwa inajiandaa kuingia vitani ikiwa katika hali ngumu ya kiuchumi – Kawawa akamhamishia Wizara ya Ulinzi kuchukua nafasi ya Sokoine. Na Sokoine huyo huyo alimtoa kwenye Uwaziri Mkuu miaka mitatu baadaye, yaani 1980, na kumweka Cleopa Msuya kisha akamrudisha tena Sokoine katika nafasi hiyo mwaka 1983 mara tu baada ya jaribio la baadhi ya watu kumpindua Rais mwaka 1982 na wakati wa operesheni dhidi ya wahujumu uchumi.

Lakini, je, nafasi hiyo bado inahitajika hasa katika kipindi hiki cha mfumo wa vyama vingi? Katika zama hizi za ufisadi nafasi ya Uwaziri Mkuu inausaidiaje Urais? Je, inausaidia katika upambanaji na ufisadi au inaukinga na uwajibikaji dhidi ya ufisadi?

Wapo wanaoona kuwa muundo huu ni kichaka cha kuficha na kukuza ufisadi. Katika mjadala wa Waking'oka na yeye ango'ke? kwenye mtandao wa kijamii, mtoa mada anasema hivi: "Kashfa ya akaunti ya Escrow ni miongoni mwa kashfa zinazotokana na watawala kuwadhania, kuwachukulia na kuwatenda Watanzania kwa ujinga. Kashfa kama hizi zinaishia mawaziri kung'oka, watu kushtakiwa na hata baraza la mawaziri kuvunjwa lakini chama kilichounda Serikali kinaendelea kwa kuruhusiwa kuingiza sura mpya. Tungekuwa na mfumo wa kumwajibisha Rais pale mawaziri wake wanapovurunda basi Baraza la Mawaziri linapovunjwa na yeye mwenyewe anaondoka nao na haruhusiwi kugombea na anapoteza mastahili yote ya ustaafu! Wangekuwa wanaogopa hata kudokoa ndotoni! Hata mawaziri wanaojiuzulu wangekuwa wananyang'anywa mafao yao na mali yote yenye utata kufilisiwa. Wangeona hela za umma chungu." Kweli zingekuwa shubiri.

Ila mtoa mada huyo, ambaye amewahi kutuhariria na kutuwekea mtandaoni chapisho lote la Nyerere lililonukuliwa hapo juu, anaonekana kusahau maneno haya yaliyomo humo: "Ni vizuri jambo hili likatamkwa wazi wazi na likaeleweka sawa sawa. Maana watu wengine wananong'onanong' ona kuwajibika kwa Rais kana kwamba ni jambo la mchezo mchezo tu. Kulazimika kumchukulia hatua Rais wa nchi ni mkasa na balaa kwa nchi yoyote ile. Ndiyo maana tunatakiwa kuwateua na kuwachagua marais wetu kwa uangalifu mkubwa; na ndiyo maana wakishakuchaguliwa, wanatakiwa wajiheshimu na kuwa waangalifu sana." Ndiyo, tuwe waangalifu mno kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.

Chapisho hilo la Nyerere linaendelea kusisitiza kuwa: "Ni jambo muhimu kabisa, kwa kweli la kufa na kupona, kufanya kila jitihada ili kujenga na kuimarisha utaratibu na mazoea ya kuchagua na kubadili Rais wa Nchi yetu kwa njia ya kupigiwa kura, baada ya Rais anayetoka kumaliza kipindi chake kimoja au viwili kwa mujibu wa Katiba. Utaratibu mwingine wowote haufai, na ni lazima tufanye kila lililo ndani ya uwezo wetu kuuzuia. Mnapolazimika kuutumia, ni jambo la kufanyaje, si jambo la kurukia."

Escrowgate inatosha kutufanya tulazimike kuutumia utaratibu huo? Bunge na wabunge wana mori na motisha wa kulirukia, achilia mbali utashi na ujasiri wa kulifanya, jambo hilo? Nchi na wananchi wapo tayari kumtua Waziri Mkuu zigo la kashfa zote za ufisadi utokanao na uzembe wa watendaji na viongozi wakuu wa Serikali na kumtwika Rais?

Au ni yale yale yaliyopelekea nchi isitikisike baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa awamu wa nne kwa miaka miwili kunena haya bungeni na kuachia ngazi bila kumwathiri Rais aliyemteua na Bunge lililompitisha: "Nadhani tatizo ni Uwaziri Mkuu. Kwamba ionekane Waziri Mkuu ndio amefanya haya, tumwondolee heshima au tumwajibishe"?

Gharama za demokrasia hakika ni kubwa. Lakini matokeo ya demokrasia yanapaswa, si kurudisha gharama hizo tu, bali pia kuzalisha faida, yaani, maendeleo yetu ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Kuwa na Serikali ambayo inalazimika kuvunja baraza la mawaziri na kubadili viongozi mara kwa mara katika kipindi kifupi cha miaka 10 tu ni demokrasia ghali. Kodi za wananchi wenzao zinawagharimia chakula, mavazi na malazi pamoja na posho za ujuzi wanaoupata katika semina elekezi na ziara za mafunzo ila hata kabla hatujaona matunda ya utendaji wao wanatoka kutokana na ufisadi wao au wa wengine.

Basi imetosha. Tusiwe na Waziri Mkuu. Rais awajibike mwenyewe. Katiba isimike hilo.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom