Tatizo la Mimba Kutunga Nje ya Mfuko wa Uzazi (Ectopic Pregnancy)

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,299
33,080
Mimba kutunga nje ya mfuko wa uzazi wa mwanamke au ectopic pregnancy ni tatizo ambalo limetokea kuathiri wanawake mbalimbali. Kwa kawaida, isipokuwa mara chache sana, mimba zitungazo nje ya mfuko wa uzazi hazina uwezo wa kukua kuwa mtoto kamili. Aidha, mimba hizi ni hatari kwa afya ya mama mjamzito kwa vile humfanya kupoteza damu nyingi na hatimaye kusababisha kifo.

Kazi za mirija ya fallopian ni kusafirisha mayai kutoka katika kiwanda chake cha uzalishaji (ovary) mpaka kwenye mfuko wa uzazi (uterus). Utungisho wa yai la kike (ovum) na mbegu ya kiume (sperm) hufanyika kwenye mirija hii.

Mara baada ya utungisho, misuli inayozunguka mirija ya fallopian ikishirikiana na vinyweleo vilivyopo ndani ya mirija hii husukuma kiinitete au yai lililorutubishwa kulipeleka kwenye uterus. Yai lililorutubishwa, au kiinitete, lifikapo kwenye uterus hujipachika katika mojawapo ya kuta zake kwa ajili ya kuendelea kurutubishwa, kukua taratibu na hatimaye kufanya mtoto.
Inapotokea misuli hii kushindwa kufanya kazi au vinyweleo hivi kukosekana, kiinitete hushindwa kusafirishwa kuingia kwenye uterus na hivyo hujitunga nje ya uterus kusababisha ectopic pregnancy. Karibu asilimia 1-2% ya mayai yaliyorutubishwa hutunga nje ya mfuko wa uzazi wa mwanamke.
Aidha, zaidi ya asilimia 95% ya mimba zinazotunga nje ya uterus hutokea kwenye mrija wa fallopian. Mimba zinazotunga kwenye mrija wa fallopian husababisha kiinitete (embryo) kujipachika katika kuta zake na hivyo kusababisha mishipa ya damu inayopita karibu na mrija wa fallopian kupasuka na damu kutoka kwa wingi hali ambayo isiposhughulikiwa mapema husababisha madhara zaidi na hata kifo.

Kuna aina kuu nne za mimba zinazotunga nje ya mfuko wa uzazi, nazo ni
1. Mimba zinazotunga kwenye mirija ya fallopian
2. Mimba zinazotunga nje ya uterus na nje mirija ya fallopian
3. Mimba zinazotunga ndani na nje ya uterus kwa wakati mmoja
4. Mimba zinazojirudia kutunga nje ya mfuko wa Uzazi

Mimba zinazotunga kwenye mirija ya fallopian

Sababu kubwa inayopelekea mimba kutunga kwenye mirija ya fallopian ni kushindwa kusafirishwa kwa kiinitete katika mirija hii hali inayotokana na mabadiliko katika hali ya mirija au uwezo duni wa mirija hiyo katika kusukuma kiinitete kuingia kwenye uterus kwa sababu ya ukosefu wa vinyweleo kutokana na magonjwa mbalimbali yanayoathiri muundo na maumbile ya mirija ya fallopian.
Mimba zinazotunga kwenye mirija ya fallopian huwa zina madhara makubwa zaidi kwa sababu eneo hili ni jembamba mno kuweza kuhimili ukuaji wa mimba na pia lina mishipa mingi ya damu inayopita karibu ambayo ipo hatarini kupasuka hivyo kupelekea mgonjwa kupoteza damu nyingi sana.

Mimba zinazotunga nje ya uterus na nje mirija ya fallopian

Baadhi ya mimba huweza kutunga kwenye kiwanda cha kuzalisha mayai (ovary), kwenye shingo ya uzazi (cervix) au ndani ya tumbo (intra-abdominal). Aina hii ya mimba ni chini ya asilimia tano ya mimba zote zinazotunga nje ya mfuko wa uzazi.
Mimba inayotungwa ndani ya tumbo (intra-abdominal) wakati fulani huweza kutoa mtoto aliye hai tofauti na aina nyingine za mimba zinazotunga nje ya uterus. Hata hivyo uzalishaji wake hufanywa kwa operesheni ingawa hakuna ushahidi wa kitabibu kuhusu suala hili mpaka sasa.
Madhara ya kutokea kwa upotezaji wa damu pamoja na maambukizi ni makubwa hivyo mara nyingi mimba za namna hii huitaji kushughulikiwa haraka ili kumuepushia madhara makubwa mama mjamzito.

Mimba zinazotunga ndani na nje ya uterus kwa wakati mmoja

Wakati fulani, mayai mawili yaliyorutubishwa kwa wakati mmoja hutokea kupandikizwa sehemu mbili tofauti. Moja likipandikizwa nje ya uterus na jingine ndani ya uterus. Katika aina hii ya ectopic pregnancy, uwezekano wa yai lililotungwa ndani ya uterus kukua na kutoa mtoto ni mkubwa sana.

Mimba zinazojirudia kutunga nje ya mfuko wa Uzazi

Wakati fulani hutokea kuwa, hata baada ya operesheni ya kuondoa mimba iliyotunga nje ya kizazi kufanyika, baada ya muda fulani seli za kiinitete huendelea kukua na kujitengeneza tena kufanya kusanyiko la seli kama mimba nyingine. Hali hii huitwa mimba zinazoendelea kutunga nje ya mfuko wa uzazi au persistent ectopic pregnancy.

Nini husababisha mimba kutunga nje ya kizazi?

Katika mimba nyingi zinazotunga nje ya uterus, chanzo chake huwa hakijulikani. Hata hivyo kuna vihatarishi ambavyo humfanya mwanamke kuwa katika hatari ya kupata tatizo hili. Vihatarishi hivi ni pamoja na
1. Matatizo katika mirija ya fallopian
Magonjwa yanayoweza kusababisha hali hii ni pamoja na

  • Maambukizi katika mfumo wa uzazi wa mwanamke (PID)
  • Matumizi ya vitanzi vya kuzuia mimba (Intra-uterine contraceptive devices)
  • Kuoteana kwa tishu za uterus kwenye viungo vingine vya uzazi au endometriosis.
2. Uvutaji sigara
Uvutaji sigara kwa mwanamke una uhusiano mkubwa na utungaji wa mimba nje ya kizazi. Imeonekana kwamba wanaowake wanaopendelea kuvuta sigara mara kwa mara wana hatari ya kupatwa na tatizo hili mara tano zaidi ya wale wasiovuta kabisa. Hali hii husababishwa na nicotini iliyomo ndani ya tumbaku. Kwa kawaida nicotini huchochea kusinyaa kwa mirija ya fallopian hali iletayo kuziba kwa mirija hiyo na hivyo kufanya kiinitete kushindwa kupita kwenye mirija kuingia kwenye uterus na kufanya mimba kutunga kwenye mirija ya fallopian.
3. Upasuaji wa tumbo uliofanyika zamani
Operesheni yeyote inayohusu mirija ya fallopian inaongeza uwezekano wa mwanamke kutunga mimba nje ya uterus kwa vile mirija ya fallopian huwa imesinyaa kutokana na operesheni hiyo.
4. Matumizi holela ya baadhi ya dawa
Matumizi ya baadhi ya dawa zenye homoni husababisha kupungua kwa uwezo wa mirija ya fallopian kusukuma kiinitete kuelekea kwenye uterus na hivyo kuleta uwezekano wa utungaji wa mimba nje ya kizazi. Dawa hizo ni kama dawa za kuzuia mimba zenye homoni za kike za progesterone, na dawa za kusaidia uzazi aina ya clomiphene.
Dalili za ectopic pregnancy
Katika wiki za mwanzo za ujauzito, mimba iliyotunga nje ya uterus huwa na dalili sawa na za mimba ya kawaida. Dalili hizi ni pamoja na mwanamke kukosa hedhi, kujaa kwa matiti, kichefuchefu, na uchovu wa mwili. Hali hii hufanya ugunduzi wa mimba iliyotunga nje ya uterus kuwa mgumu katika hatua zake za awali.
Hata hivyo dalili ya awali ya kuonesha kuwa mimba imetunga nje ya kizazi ni kuwepo kwa maumivu makali na damu kutoka ukeni. Maumivu yanaweza kuwa kwenye nyonga, tumbo au wakati mwingine kwenye mabega au shingo (iwapo kiwango cha damu inayotoka kwenye mirija iliyopasuka ni kingi sana mpaka kugusa kiwambo cha hewa).
Maumivu haya huweza kuwa makali na yanayokata kama kisu, na yanaweza kuwa upande mmoja zaidi wa nyonga ingawa si lazima yawe upande ulio na mimba.
Dalili nyingine ni pamoja na

  • Kizunguzungu na kuzimia kwa sababu ya kupoteza damu kwa wingi
  • Shinikizo la damu kuwa chini, na
  • Maumivu ya chini ya mgongo
Ugunduzi wa ectopic pregnancy
Mimba iliyotungwa nje ya kizazi huweza kugunduliwa kwa

  • Daktari kusikiliza historia ya mgonjwa na kufahamu dalili zake na kumfanyia uchunguzi wa mwili (physical examination).
  • Kufanya vipimo kadhaa vinavyoonesha kuwepo kwa tatizo hilo. Vipimo hivyo ni pamoja na
    • Kupima damu kwa ajili ya kuangalia kiwango cha homoni ya HCG
    • Kupima kiwango cha homoni ya progesterone ambayo kwa mama mwenye ectopic pregnancy huwa chini (chini ya 15ng/mls) zaidi ya mwenye mimba ya kawaida.
    • Ultrasound ambayo husaidia kutambua mimba ilipotungwa.
Matibabu ya Ectopic pregnancy
Matibabu ya mimba iliyotunga nje ya kizazi yaweza kuwa ya aina mbili, yale yasiyohitaji upasuaji, au yanayohitaji uangalizi na dawa na yale yanayohitaji upasuaji.
1. Matibabu kwa kutumia dawa:
Faida kubwa ya kufanya uchunguzi mapema ni kuwa inaongeza uwezekano wa kuokoa maisha ya mama, kuokoa mirija isipasuke na hivyo kuongeza uwezekano wa kupata mimba kwa njia ya kawaida siku za usoni. Iwapo, mimba bado ni ndogo sana na kiwango cha HCG bado kipo chini mno, daktari anaweza kushauri kusubiri huku akimfuatilia mgonjwa kwa ukaribu sana. Wakati mwingine, mwili huwa na uwezo wa kuifyonza mimba changa ndani kwa ndani na hivyo kuondoa hatari ya kuwepo kwa ectopic pregnancy.
Hali kadhalika, mama anaweza kupewa dawa aina ya methotrexate, ambayo ina uwezo wa kuzuia mimba kukua zaidi. Wakati dawa hii inapotolewa, ni muhimu pia kufuatilia kiwango cha HCG ili kujiridhisha kuwa kimeshuka mpaka kufikia sifuri ili kuwa na uhakika kuwa mimba haipo tena.
Baadhi ya madaktari pia hutumia njia ya kuchoma dawa ya sumu ya potassium chloride kwenye mimba ili kuifanya isinyae na hatamaye kufyonzwa na mwili. Matibabu haya hufanyika chini ya uangalizi wa kipimo cha ultrasound.
2. Matibabu kwa kutumia upasuaji
Iwapo mrija tayari umepasuka, upasuaji wa dharura hufanyika kwa ajili ya kuzuia kupotea zaidi kwa damu. Sehemu ya mrija iliyopasuka huondolewa na mshipa wa damu uliopasuka hufungwa. Athari za matibabu kwa njia hii ni kuwa, huondoa uwezo wa mrija ulioathirika kupitisha yai tena maishani na hivyo kupunguza uwezekano wa mama kupata mimba siku za usoni.

Njia za kuzuia mimba kutunga nje ya kizazi

Yawezekana kupunguza uwezekano wa mimba kutunga nje ya kizazi kwa kuzuia na kujiepusha na vihatarishi vinavyosababisha hali hiyo. Njia hizo ni kama

  • Kujikinga na maambukizi katika mfumo wa uzazi wa mwanamke kwa kujiepusha na ngono zembe, au kupunguza idadi ya wapenzi wa kufanya nao ngono.
  • Kuacha kutumia holela dawa za homoni bila kupata ushauri wa daktari, na
  • Kujiepusha na uvutaji wa sigara.

Mimba Kutunga Nje ya Kizazi.jpg
 
hii nzuri sana, hata wanaume inawahusu maana si ndio wanowapatia wanawake hizo mimba? sasa mimi MiziMkavu swli langu ni kuhusu placenta previa...inasababishwa na nini? ina uhusiano wowote na utoaji wa mimba wa awali kwa mwanamke? naomba msaada tafadhali..
 
hii nzuri sana, hata wanaume inawahusu maana si ndio wanowapatia wanawake hizo mimba? sasa mimi MiziMkavu swli langu ni kuhusu placenta previa...inasababishwa na nini? ina uhusiano wowote na utoaji wa mimba wa awali kwa mwanamke? naomba msaada tafadhali..
Placenta previa (pluh-SEN-tuh PREH-vee-uh) occurs when a baby's placenta partially or totally covers the mother's cervix - the doorway between the uterus and the vagina. Placenta previa can cause severe bleeding before or during delivery.


The placenta provides oxygen and nutrients to your growing baby and removes waste products from your baby's blood. It attaches to the wall of your uterus, and your baby's umbilical cord arises from it. In most pregnancies, the placenta attaches at the top or side of the uterus. In placenta previa, the placenta attaches to the lower area of the uterus.


If you have placenta previa, you'll probably be restricted to bed rest for a portion of your pregnancy and you'll likely require a caesarean section (C-section) to safely deliver your baby Mkuu.@Ye Soya
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom