Tatizo la maendeleo ya Tanzania ni Watanzania wenyewe - na wewe pia!

Synthesizer

JF-Expert Member
Feb 15, 2010
11,143
18,774
Mara nyingi swali limeulizwa; kwa nini Tanzania ni masikini - na majibu mbali mbali yakatolewa. JK aliwahi kusema yeye hajui kwa nini Tanzania ni masikini! Balozi mmoja wa Germany hapa nchini , Guido Hertz, alisema yafuatayo;

"Tanzanians would do themselves and their country a lot of good by more vigorously tackling the factors that make some of them live in abject poverty in the midst of an abundance of economic and other resources"

Nadhani mheshimiwa huyu balozi alikuwa karibu sana na ukweli, na kuna jambo kubwa sana ambalo alilisema huenda bila hata kujua "Tanzanians themselves".

Ukirudi kwenye philosophy za Nyerere, ili tuendelee tunahitaji vitu vinne, ambavyo kama sikosei alivitaja kama ifuatavyo;

- Ardhi (inayotia ndani natural resources, madini, mbuga za utalii, maji nk)
- Uongozi bora (uwepo wa viongozi makini nchini)
- Watu (nguvu kazi)
- Siasa safi (development condusive policies, kutia ndani mazingira ya uwekezaji toka kwa wazalendo na wageni)


Baadhi ya watu walisema Nyerere alipaswa kuongeza mtaji (capital), katika mambo makuu manne ya maendeleo. Labda kweli, lakini ukiwa na Ardhi na vipengele vyake (madini nk) suala la capital litakuja lenyewe tu! Hatukuhitaji capital yetu wenyewe ili kuanzisha miradi kama Bulyankulu na Songo Songo.

Sasa Katika hayo hapo juu Tanzania tuna matatizo hasa katika uongozi bora, watu na labda kidogo siasa safi (policies). Ardhi (natural resources) sio tatizo, tuna ardhi kubwa sana nzuri ya kulima - wakati fulani Raisi mmojawapo wa Marekani, Ford kama sikosei, alimwambia Nyerere ninaweza kukupa wakulima wa Marekani watano tu na hao wakaibadilisha Tanzania toka kuwa nchi yenye kuomba misaada ya chakula na kuwa nchi yenye ku-export chakula. Raisi huyo alijua Tanzania ina ardhi ya namna gani. Tanzania sio Libya bwana, ambayo ni jangwa tupu.

Na pia katika ardhi - tuna mbuga za wanyawa zilizo classic, madini - tanzanite, dhahabu, almasi, uranium, nickel, nk! Maji - ukiangalia ramani ya Africa utaona Tanzania ni mojawapo ya nchi zinazoongoza kwa wingi wa fresh water bodies, tumezungukwa na rangi za blue zenye kuonyesha maji katika ramani ya Africa!

Upande wa policies - si mbaya sana kwa kweli, ni kweli kulikuwa na vipengele kadhaa kwenye policies za ujamaa na kujitegemea ambazo vilikuwa ni tatizo, lakini kwa sasa policies si kikwazo kikubwa cha kutuzuia kuendelea.

Sasa tunapokuja kwenye mambo yanayohusu watu - Watanzania wenyewe, (nguvu kazi na uongozi bora) - hapa ndipo kwenye madudu mengi ya ajabu kabisa!

Kwanza uongozi bora - wengi wa viongozi wetu ni wabinafsi (selfish) na wengi hawana uzalendo (patriotism). Viongozi wengi wanapopewa daraka fulani wanaona ni kwa manufaa yao binafsi na sio kwa ajili ya Tanzania. Suala kubwa kwao linakuwa hii nafasi niliyopata itanisaidiaje kijiimarisha kiuchumi na sio nafasi niliyopata nitaitumiaje kutumikia taifa langu la Tanzania. Sasa hili ni tatizo kubwa sana, the worst mind set one can ever have! Hapa ndipo utaona tofauti kati yetu na Wajerumani, Wa-Norway, Wa-Denmark, Waingereza, Wajapan nk.

Tuna tatizo hilo hata kwa ngazi ya baadhi ya wanaogombea uraisi - hawaangalii uwezo wao wa kuwa maraisi, bali ni hali ya "kuukata" watakaupata uraisi wa nchi!

Na ajabu hata watu tulio wengi huku chini tuna huu mtazamo mbovu sana! Mtu akisikia umepewa kazi Customs au TRA, wazo la kwanza kuja kichwani au hata kukuambia ni kwamba "eeh, hapo umeula rafiki yangu, ulishaukata wewe!" Je hujasikia mtu anakwambia fulani kaula kapewa kazi fulani?

Sasa ujinga gani huu tulio nao; napata kazi TRA, Customs, Bandari unaniambia nimeukata, unatarajia nini toka kwangu, au jamii inataka nifanye nini? Kumbuka kwamba mtu anasema umeula si kwa sababu anajua utakuwa na mshahara mkubwa sana, bali kwa kuwa anaona una mwanya mzuri wa kuihujumu nchii hii, wa kuifisadi nchi yetu.

Na zaidi, nikistaafu toka sehemu kama hizo za TRA, Customs na hali ya kawaida tu kiuchumi, labda na nyumba yangu moja ya kawaida, jamii inanihukumu! Unakuta watu wananisema, kwamba "yule jamaa alikuwa mzembe sana, hebu fikiria kafanya kazi Customs miaka ishirini anastaafu hana kitu!"

Tunatangaziwa baraza la mawaziri; waziri wa fedha, au nishati na madini, au usafirishaji na miundo mbinu tunaona ameula, wa kilimo na sayansi na teknolojia tunasema hajapata kitu!

Sasa je, tunalalamikia ufisadi katika jamii ya Watanzania iliyoidhinisha ufisadi kuwa halali?

Polisi akihamishwa kutoka kitengo cha usalama wa raia kwenda traffic anaambiwa na watu kaukata! Akitolewa toka traffic kwenda FFU yeye na watu wengine wanaona kaadhibiwa! Hata nimesikia askari wa FFU wanapiga sana watu kwa ajili ya hasira za kuwekwa sehemu isiyo na ulaji, na kwamba kufanywa FFU ni namna ya kupewa adhabu ndani ya jeshi letu la Polisi!

Kwa hiyo utaona sisi Watanzania wenyewe, tunatengeneza aina ya watu katika uongozi tulio nao. Na hii ni kuanzia yule mlala hoi wa kawaida mtaani hadi wanachama wa NEC wa CCM kule, ambao kabisa wanapotaka kupitisha jina la mgombea uraisi wanasahau kabisa kwamba lengo ni manufaa ya nchi, na sio ya kundi lao ndani ya CCM (maana kuna makundi ndani ya vyama), au nani atawalinda na kuwaendeleza kiuchumi na kisiasa. Unakuta CCM wanapomlinganisha Lowasa na Membe, Sitta au Mwandosya, si suala la nani atatusaidia kuendeleza nchi, bali nani atakuwa na manufaa kwetu binafsi, bila kujali uwezo wake au capability ya kutuvusha kutoka lindi la umasikini tulio nao!

Hata Chadema wameanza kuingiliwa na mdudu huyu huyo; masuala ya Zitto, au Slaa, au Mbowe sijui, je ni kweli hapa kilichoko akilini katika makundi yanayoanza kujitokeza ni suala la uwezo wa mtu au nani anaweza kusimamia maslahi yetu binafsi?

Kwa upande wa watu (nguvu kazi), hapa kuna jambo jingine muhimu tu. Sisi watanzania ni watu wa ajabu kabisa. Tunaona uzalendo (patriotism) ni kwa ajili ya viogozi wetu tu, halituhusu sisi mtu mmoja mmoja. Je kweli, kuna siku tunaamka, tunaenda shule au kazini tukiwa na uchu wa kuendeleza taifa kama ilivyokuwa kipindi fulani kwa Wajerumani, Wajapan? Kufikiri kwetu ni tofauti kiasi gani na wale wanaotuongoza, juu ya kujinufaisha kibinafsi?

Angalia jambo moja juu ya tatizo letu kama kama watu wa nguvu kazi ya nchi hii. Leo hii, tumekuwa na viongozi ambao kweli kweli wamejitahidi kupigania maendeleo ya nchi bungeni pale, wamejitahidi sana. Na pia wamekuwapo viongozi wengi tu ambao tumeona wakituhumiwa na mengi sana juu ya kukosa maadili ya uongozi, rushwa na ufisadi.

Sasa hawa watu wanaporudishwa tena kwetu, tuwachague kama viongozi, tuwapigie kura, ni suala gani linakuwa akilini mwetu? Ni ajabu sana kinachotokea hapa, kwamba wale waliopigania sana haki zetu bungeni nk, wana tatizo kubwa na kukubalika na watu na mara nyingi hata wanakosa uongozi wanaopigania! Na wale wanye tuhuma nyingi nzito nzito, watoa rushwa, ndio utakuta mara nyingine wamepita hata bila kupingwa!

Sasa sisi ni watu wa namna gani, ni watu ambao kweli tunaweza kuwa chachu ya maendeleo ya nchi yetu? Inaonekana sisi ni watu ambao tunaona kiongozi kuwa fisadi, au mwenye tuhuma za rushwa, au mzembe tu katika uongozi - sio tatizo hata kidogo, ni ujanja unaokubalika! Tunapotaka kuchagua viongozi wetu suala la historia yao ya utendaji, kashfa zao, tuhuma zao, wala hilo haliingii kichwani hata siku moja!

Sasa tatizo kubwa ni kwamba katika vipengele vinne vya maendeleo, hiki cha watu ndicho cha msingi sana, kwa sababu hiki ndicho kitafanya kuwa na siasa safi, kuwe na uongozi bora na ardhi (resources) itumike kwa mnaufaa ya kuendeleza nchi. Kipengele cha watu ndio hasa chimbuko la mabadiliko katika nchi yeyote ile, na hapa ndipo tatizo letu kubwa kabisa lipo katika Tanzania. Sisi ni watu wa ajabu kabisa tusiotaka maendeleo ya nchi yetu wenyewe.

Tunalalamika umasikini bila kujua kwamba uwezo wa kubadilisha nchi yetu upo ndani yetu wenyewe. Hatuna uzalendo, tunafanya kazi kigoigoi, mara nyingi tukitaka tusimamiwe na wanyapara ndie tuweze kufanya kazi. Na utaona hili katika tofauti ya sekta ya umma na sekta binafsi hapa Tanzania. Watazania tunataka tusimamiwe ili tufanye kazi, kwa namna ya punda na fimbo. Sekta binafsi Tanzania zinastawi si tu kwa kuwa wana mishahara bora zaidi ya sekta ya umma, bali pia kwa kuwa wanasimamia kwa ukaribu zaidi. Sisi Watanzania lazima tusimamiwe kama punda ndio tunafanya kazi! Inadhalilisha lakini ndio ukweli.

Haisaidii chochote kuwa na ardhi yenye madini nk, kama msingi wa maendeleo wa "watu" katika nchi ni mbovu, na ukweli ni kwamba msingi huo Tanzania ni mbovu; viongozi bora hatuna, na watu wenyewe si wazalendo!

Sasa kikubwa ni kubadilisha tabaka la watu, na kutoka lisilo "la kizalendo" na nchi yao na kuwa lenye uzalendo mkubwa. Sasa hili ni gumu sana. Na huenda hata linahitaji tukio kubwa kutupata ili tubadilike, ili tuwe na uchungu na nchi yetu. Labda tutasema vita vya kagera ilipasa kutubadilisha, lakini haikuwa ndefu ya kutosha. Najua maneno mazito haya, lakini huenda ukweli ni kwamba amani yetu ya muda mrefu ndio imekuwa tatizo letu - "laana ya amani". Angalia nchi zenye uzalendo wa hali ya juu, zote zina historia ya majanga makubwa ya namna moja au nyingine - Germany, Israel, Japan, Marekani, nk. Jirani zetu hapa Rwanda genocide iliwashtua sana, na huenda imekuwa kichocheo kikubwa cha uzalendo kwa nchi yao kwa sasa.

Lakini je, kweli tunahitaji janga la kitaifa ili tuwe na uzalendo na nchi yetu?

Watanzania tunahitaji sana kubadilika katika kufikiri kwetu!
 
Back
Top Bottom