SoC02 Tatizo la kiwewe (trauma) katika jamii, sababu, madhara na jinsi ya kuepuka

Stories of Change - 2022 Competition

Bernardo45

New Member
Jul 21, 2022
2
1
UTANGULIZI
Kiwewe (trauma) Ni moja ya matatizo ambayo kwa sasa yanaiathiri kwa kiasi kikubwa jamii yetu ilhali wanajamii wengi hawatambui au hawana ufahamu mkubwa juu ya tatizo hili. Hivyo kupitia andiko hili kwa ufupi jamii ielezee maana ya Kiwewe, Sababu zinazopelekea Kiwewe ,madhara yake na JINSI gani jamii au wanajamii wanaweza kuepuka au kuondokana na tatizo la Kiwewe.

MAANA YA KIWEWE

Kiwewe ni hali inayompata mtu na kuathiri uwezo wake wa kimwili, kiakili, kihisia( Emotional) na kisaikolojia. Mtu mwenye tatizo la Kiwewe hupelekea hisia zake kuathirika, akili na saikolojia yake kutokuwa sawa, yaani kutumia muda mwingi kuwaza mambo mabaya kama vile kutaka kuwadhuru wengine, kuwaza kuua au kuniua, kukata tamaa juu ya mambo fulani n.k.
Hivyo katika jamii zetu watu wenye matatizo ya Kiwewe wapo na tunaishi nao ingawa hawajapata msaada wa kujua Nini wafanye ili kuondokana na tatizo hilo na jamii pia Haina Elimu ya kutosha kuwasaidia watu hawa, ndio maana matukio yasiyo ya kawaida katika jamii yamezidi mfano, kuuana kwa kuchomana visu, moto, kupigana risasi, ubakaji, ushoga, ulawiti kwa watoto wadogo na mengine mengi.

SABABU ZINAZOPELEKEA MTU KUPATA KIWEWE
Zipo sababu nyingi ambazo huweza kusababisha mtu kupata tatizo la kiwewe, kwa upande wangu natoa baadhi ya sababu hizo nazo ni 5 kama ifuatavyo:

1. Msongo wa mawazo.
Kitaalam inajulikana kama (stress).

Moja kati ya sababu zinazopelekea saikolojia ya mtu kutokuwa sawa ni pamoja na mtu huyo kuwa na msongo wa mawazo. Msongo wa mawazo humpelekea mtu kupata tatizo la Kiwewe na hivyo kutokuwa na mtazamo Chanya wa mambo mbalimbali katika jamii.

Katika jamii zetu watu wengi wanapata tatizo la Kiwewe kutokana na kuwa na msongo wa mawazo na hawajui namna ya kuondokana na msongo wa mawazo huku wengi wakiamini tiba pekee ya msongo wa mawazo ni pombe.

Hivyo, hushindwa kuondokana na tatizo hilo na hivyo kuambulia tatizo la Kiwewe.

2. Ushuhudiaji wa matukio ya kutisha.

Moja ya sababu kubwa ya mtu kupata hali ya Kiwewe ni pamoja na mtu huyo kushuhudia matukio ya kutisha kama vile mauaji ya kutisha, sinema za kutisha na matukio yenye vitisho ya kichawi au kishirikina nyakati za usiku wa giza, n.k.

Mtu anaposhuhudia moja ya matukio haya huweza kupata tatizo la Kiwewe na tatizo hilo hudumu kwa mtu huyo hasa kila anapokumbuka tukio aliloshuhudia.

Matukio ya namna hii yapo katika jamii na yanazidi kuathiri watu na kuongeza tatizo la Kiwewe.

3. Udhalilishwaji katika mitandao ya kijamii yaani ( Social Network Bullying).

Mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Instagram, Whatsapp, Telegram n.k ni miongoni mwa vyombo vya upashanaji habari vyenye nguvu zaidi kwa sasa.

Matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii hupelekea udhalilishwaji wa wengine. Mfano, usambazaji wa picha na video za utupu za wengine katika mitandao hiyo.

Tabia hii katika jamii imezidi kukithiri kupitia makundi ya WhatsApp na Telegram na kurasa nyingine za Udaku kama vile Mange Kimambi App.

Mbali na picha na video hizo,pia baadhi ya maneno, sauti na video hutunika kuwadhalilisha watu katika mitandao hiyo.

Hivyo, muathirika wa udhalilishwaji huu huweza kupata tatizo la Kiwewe na hivyo kutokuwa na mtazamo Chanya wa mambo mbalimbali ikiwemo maisha yake mwenyewe. Hivyo hii pia ni sababu mojawapo ya tatizo la Kiwewe.

4. Usaliti wa kimapenzi.
Hii pia ni moja ya sababu zinazopelekea wanajamii wengi kupata tatizo la Kiwewe; Hasa pale mtu aliyempenda kweli na kwa dhati mpenzi wake anapogundua kuwa mpenzi wake huyo humsaliti.

Hupata matatizo ya kisaikolojia na Kiwewe kisha huanza kufikiria mambo mabaya. Ndio maana kutokana na usaliti wa kimapenzi jamii imeshuhudia mauaji ya kuchomana moto, kuchomana visu na kupigana risasi yakitokea kwa kasi.

Hii yote ni kutokana na Kiwewe kilichosababishwa na usaliti wa kimapenzi.

5. Ugumu wa maisha.
Ugumu wa maisha hupelekea mtu kuwa na msongo wa mawazo, na msongo huo wa mawazo huiathiri saikolojia yake na mwisho kumfanyanya apate Kiwewe.

Mtu mwenye Kiwewe juu ya ugumu wa maisha huwaza mambo mbalimbali ambayo ni hasi kwa jamii kama vile kujiua kutokana na kuikosa thamani ya kuishi. Pia kutokana na Kiwewe Cha ugumu wa maisha Ndio maana jamii inashuhudia mambo yasiyofaa kama vile mauaji, ujambazi, wizi, ushoga, uporaji na uvamizi yote haya hufanywa na watu walioathirika na tatizo la Kiwewe ili waweze kujipatia kipato.

Hivyo, kutokana na sababu hizo na nyingine nyingi zinazopelekea tatizo la Kiwewe, basi jamii Bado Ina kazi kubwa ya kufanya kukabiliana na tatizo hilo.

MADHARA YATOKANAYO NA KIWEWE.
kutokana na uwepo wa tatizo la Kiwewe, basi tatizo hili Lina madhara kadha wa kadha kwa jamii na madhara hayo tunayashuhudia kwa kiasi fulani katika jamii zetu.

Kwa ufupi yafuatayo ni baadhi tu ya madhara yatokanayo na tatizo la Kiwewe ingawa yapo madhara mengi zaidi.

1. Matatizo ya Akili (Mental Problems).

Mtu mwenye tatizo la Kiwewe kama ilivyoelezwa mwanzo huathirika kisaikolojia na kiakili pia. Hivyo, kama mtu huyu hatopata msaada wa kitaalam haraka kuondokana na matatizo hayo basi hupata matatizo ya Akili ya kudumu.

Jamii zetu zimezungukwa na watu wengi wenye matatizo ya Akili ambao huitwa machizi au vichaa na kwa sababu jamii zetu zinaamini Sana katika Imani za kishirikina basi watu Hawa huaminiwa kuwa wamerogwa.

Ingawa wengi wao ukifuatilia historia zao zinasemekana kuwa wamepatwa na matatizo ambayo ni miongoni mwa sababu zinazopelekea Kiwewe. Hivyo, matatizo ya akili ni miongoni mwa madhara yatokanayo na tatizo la Kiwewe.

2. Mauaji ( Murderous)
Tatizo la Kiwewe hupelekea saikolojia ya mtu kutokuwa sawa na hivyo kutokuwa na mtazamo Chanya katika jamii vilevile kupitia tatizo hilo watu wengi hushindwa kuzihimili hasira zao na hivyo kijikuta wanafanya vitendo vinavyopelekea mauaji. Mfano, mtu anayepata tatizo la Kiwewe kutokana na usaliti wa mapenzi hupelekea kuamua kumuua mpenzi wake au mfumanizi wake kutokana na hasira inayoibuka kutokana na Kiwewe. Jamii imeshuhudia matukio mengi ya mauaji kutokana na Kiwewe mengine yakiripotiwa na vyombo vya habari huku mengine yakiwa hayaripotiwi.

Hivyo, Tatizo la Kiwewe ni changamoto yenye madhara makubwa katika jamii na taifa kwa ujumla kwani kupitia mauaji haya taifa hupoteza nguvu kazi lakini pia watu muhimu katika maisha ya wategemezi wao huondoka na kuwaacha wategemezi katika hali mbaya na hivyo kupelekea ongezeko la watoto yatima na watu wanaoishi katika mazingira magumu.

3. Matukio ya kujiua. (Suicides)
Kama nilivyoeleza mwanzo katika sababu zinazopelekea tatizo la Kiwewe na kugusia kwamba mtu aliyeathirika na tatizo la Kiwewe huweza kufikiria kujiua na kukatisha maisha yake kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kusalitiwa, ugumu wa maisha au msongo wa mawazo.
Mtu mwenye tatizo la Kiwewe anaweza kutoishia kufikiria kujiua tuu Bali anaweza kujiua kabisa na hivyo madhara yake kwa taifa na kwa jamii pia hayana tofauti kubwa Sana na madhara yatokanayo na mauaji.

4. Ushoga (Homosexuality)
Moja ya sababu zinazopelekea tatizo la Kiwewe ni ugumu wa maisha. Mtu mwenye tatizo la ugumu wa maisha hufikiria mambo mengi hasa pale anapohitaji kupata kitu fulani lakini kutokana na kutokuwa sawa kiuchumi hushindwa kupata kitu hicho.

Basi huwaza kutumia njia zisizofaa kujipatia kipato. Miongoni mwa njia hizo ni kishiriki mapenzi ya jinsia moja ili kupata kile anachohitaji. Jamii inashuhudia vijana wengi wenye tatizo la Kiwewe wakijihusisha na mapenzi ya jinsia moja yaani ushoga ili wapate mahitaji Yao.

Vilevile, watu walioathirika na Kiwewe kutokana na usaliti wa kimapenzi huamua kujihusisha na ushoga ili kuondoa mawazo Yao. Hivyo, jamii Bado inazidi kuathirika kutokana na Kiwewe.

5. Ukatili wa kijinsia.
Pia jamii pia inaathirika na tatizo la Kiwewe kupitia ukatili wa kijinsia unaofanywa na baadhi ya wahanga wa tatizo la Kiwewe. Kwani katika jamii matukio ya ubakaji na ulawiti kwa wanawake na watoto yamekuwa yakiripotiwa ya kupindukia siku Hadi siku.

Hii yote ni kutokana na jamii kutokuwa na Elimu ya kutosha juu ya tatizo la trauma (Kiwewe). Vilevile kutokana na jamii kutojua namna ya kuwasaidia watu hawa, baadhi ya wanajamii wamekuwa ndio chanzo Cha kuzidisha tatizo hilo kwani wapo ambao huwatenga watu hao na wengine huwateta na kuwanyanyapaa jambo ambalo sio sawa.

Wahanga wa usaliti wa kimapenzi huweza kujikuta wakibaka ama kulawiti watu wazima au watoto wadogo kwa sababu kwao suala la mapenzi na ndoa huwa lishapoteza thamani kabisa.

Hivyo jamii na serikali kwa ujumla ina kazi kubwa kuhakikisha inasaidia watu wenye matatizo ya akili na Kiwewe ili kupunguza madhara yake.

JINSI YA KUEPUKA AU KUONDOKANA NA KIWEWE.
Kwa utafiti wangu mdogo niliojaribu kuufanya nimegundua kuwa katika nchi zilizoendelea suala lolote linalohusiana na Saikolojia limepewa kipaumbele Sana na hivyo serikali za nchi hizo huajiri watu wenye utaalam wa kutosha ( professionalists) kwa ajili ya kuwasaidia watu wanapata trauma (Kiwewe) kabla madhara yake hayajawa makubwa vilevile kuwasaidia watu wengine kuepuka kupata tatizo la Kiwewe.

Katika nchi zetu zinazoendelea Bado kuna changamoto ya uelewa juu ya tatizo la Kiwewe (trauma) lakini pia wataalam wa kutosha kuisaidia jamii katika suala hilo Bado hawatoshi.
Hata hivyo, zifuatazo ni baadhi tu ya njia ambazo zinaweza kitumiwa kuondokana au kuepukanana na tatizo la Kiwewe.

1. Utoaji wa Elimu ya masuala ya saikolojia mara kwa mara.
Serikali inapaswa kuandaa mpango wa utoaji wa Elimu ya saikolojia mara kwa mara katika jamii ili kuwapa msaada wahanga wa tatizo la Kiwewe vilevile kuwasaidia watu wasio na tatizo la Kiwewe kuweza kuliepuka tatizo hilo.

Kwa kufanya hivyo, kutapunguza idadi ya matukio mbalimbali ambayo yanaripotiwa katika jamii kutokana na tatizo la Kiwewe ingawa hayatajwi moja kwa moja kuwa yamesababishwa na wahanga wa Kiwewe.

2. Utafiti wa kitaalam juu ya matatizo hayo na ripoti kwa jamii.
Katika vyuo mbalimbali nchini kina kozi zinazhusiana na mambo ya saikolojia kwa maana hiyo basi jamii Ina wataalam wa kutosha wenye uelewa wa Mambo ya kisaikolojia na Kiwewe.

Wataalam Hawa wanapaswa wawezeshwe na serikali au mashirika binafsi katika kufanya tafiti za kitaalam kwa kina na kutoa ripoti za tafiti hizo ili kuisaidia jamii.

Vilevile wataalam Hawa wanaweza kujitolea tu kutoa msaada kwa jamii juu ya tatizo hilo na hivyo kuepusha madhara kwa jamii na taifa kwa ujumla.

3. Kutibu msongo wa mawazo kitaalam.

Watu wengi katika jamii wenye tatizo la msongo wa mawazo hawana uelewa wa namna gani ya kutibu na kuondokana na tatizo hilo. Wengi huamini kwamba wanaweza kuondokana na msongo wa mawazo kwa kukesha baa wakinywa pombe Kali na kulewa jambo ambalo sio sahihi na huathiri afya zao. Hivyo, jamii itambue umuhimu wa kuwashirikisha wataalam wa afya na Saikolojia ili waweze kuwapa msaada wa kitaalam kuondokana na tatizo la msongo wa mawazo kwani tatizo hilo likizidi hupelekea Kiwewe na hivyo madhara yake ni makubwa katika jamii.

4. Matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii wanapaswa kuitumia vyema na kwa usahihi ili kuepuka kufanya udhalilishaji kwa watu wengine ambapo kitendo Cha udhalilishaji hupelekea wahanga wa udhalilishwaji huo kipata tatizo la Kiwewe na madhara yake ni makubwa kwa jamii

5. Elimu ya kutosha juu ya mapenzi, uchumba na ndoa. Watu wengi katika jamii hujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi Bila kuwa na Elimu ya kutosha na hivyo wanaposalitiwa hujikuta katika matatizo ya trauma ( Kiwewe).

Hivyo, ili kuepukanana na hilo basi wataalam wa mambo hayo wanapaswa kutoa Elimu ya kutosha kwa wanajamii juu ya kipi kifanyike kabla kuingia kwenye mahusiano na kipi kifanyike baada ya kusalitiwa. Hii itadaidia kupunguza tatizo la Kiwewe kwa kiasi kikubwa.

Njia nyinginezo ni pamoja na kuwa na mtazamo Chanya katika mambo mbalimbali na magumu tunayokumbana nayo katika jamii, pia ushirikishanaji miongoni mwa wanajamii katika matatizo mbalimbali ambayo huweza kupelekea msongo wa mawazo. Vilevile serikali na jamii kipambana na changamoto ya ugumu wa maisha.

MWISHO
Msisitizo mkubwa uwekwe kwa jamii juu ya tatizo la Kiwewe kupitia majukwaa mbalimbali na machapisho mbalimbali ili kupunguza ukithiri wa matukio ya kutisha katika jamii.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom