Tatizo kubwa la vijana wa CCM ,wazee wa CCM na viongozi wa serikali ni elimu na sio siasa!

mr mkiki

JF-Expert Member
Sep 22, 2016
5,583
11,659
“Naambiwa hukai jimboni, unazunguka majimbo mengine. Nataka ushinde tuendeleze kazi ya PAC”. Nikacheka, kisha nikajibu “Wewe PAC ya nini wakati utakuwa Waziri?”, … ” Unajua sitaki uwaziri. Nataka kusimamia Serikali.”

Hayo ndio yalikuwa mazungumzo yetu ya mwisho na Deo Haule Filikunjombe. Alinipigia simu hiyo saa mbili usiku siku sita kabla ya ajali iliyochukua maisha yake.

Siku ya Jumatano Oktoba 14, 2015 saa Sita na robo mchana nikiwa Old Moshi kwenye mazishi ya Mzee Estomih Malla (aliyekuwa mgombea wa Ubunge ACT Wazalendo Jimbo la Arusha Mjini ), simu yangu inaita.

Sikupokea. Nikaandika ujumbe mfupi wa simu kuwa nipo msibani. Deo akaniomba namba ya simu ya rafiki yetu mmoja anaitwa Gharib kwani yeye kapoteza simu yake.

Nikamwandikia kumpa namba hiyo. Sikuwasiliana tena na rafiki yangu.

Saa kumi na moja jioni nikiwa natoka kijiji kimoja kwenda kingine katika Jimbo la Chilonwa tunaepuka ajali baada ya gari yetu kuyumba zaidi ya 3 kabla ya kutulia barabarani.

Sote ndani ya gari tukiwa tumesha mshukuru Mungu kwamba ‘it’s over’ tunamshukuru tena Mungu kwa kutuepusha na ajali. Dereva wetu, baada ya kimya kirefu, akasema “lazima kuna kitu kitatokea. Hili sio jambo la kawaida”.

Tulipanga kulala Kahama baada ya kumaliza mikutano ya Chilonwa. Baadaye nikaamua tulale Dodoma kisha tuondoke alfajiri. Saa Tatu usiku, nikiwa na chakula mezani napigiwa simu na Said Yakubu, Afisa mwandamizi wa Bunge kuulizwa alipo rafiki yangu.

Baada ya hapo sikutia chochote tumboni mpaka Ijumaa usiku baada ya kuthibitisha kuwa rafiki yangu amepoteza maisha na kuupokea Mwili wake na kuuhifadhi katika hospitali ya Lugalo.

Ulikuwa usiku mgumu sana. Hapakuwa na yeyote mwenye taarifa za alipo rafiki yangu. Licha ya kumtuma Dereva wa rafiki yangu kwenda eneo la Msolwa na baadaye Dereva wangu Patrick Muhidini bado habari zilikuwa hazifiki. Tulipata uhakika wa kwamba Deo ametutoka baada ya kumwomba rafiki yetu Axel wa kampuni ya Shell atusaidie kupata Helkopta ya utafutaji. Hiyo ndio ilitupa taarifa ya uhakika.

Wakati huo ndugu jamaa na marafiki wakifanya kazi ya ziada kumfariji mke wa marehemu Habiba-Sarah Filikunjombe na watoto.

Naamini sitasahau siku naupokea na kuuona mwili wa rafiki yangu Deo. Siku ya pili baada ya ajali mbaya sana ya Helkopta kuchukua maisha yake katika umri mdogo na katika maisha yenye matumaini makubwa. Licha ya Siasa, Deo alikuwa mfanyabiashara aliyejijenga mwenyewe na kukuza biashara yake kwa haraka sana.

Siku chache kabla ya kifo chake alikuwa ameingia kwenye biashara ya ndege. Kifo chake, kwa namna ya pekee, kimemkuta kwenye aina ya biashara aliyokuwa ameingia. Picha za mwili wake katika hali ya ajali zinaniijia tangu nimemwona akiwa katika hali ya mauti.

Kumwona rafiki yako katika hali ya kifo ni wakati mgumu sana.Kutokana na urafiki wangu mkubwa na Deo, watu wengi hufikiri tulijuana kabla. Nimekutana na Deo mwezi Novemba Mwaka 2010 mara baada ya uchaguzi.

Nilipigiwa simu na mtu nisiyemjua akiomba tuonane na kwamba yeye ni Mbunge wa Jimbo la Ludewa. Tukakutana Ubungo Plaza. Kijana mtanashati, amenyoa panki na mwenye ucheshi sana. Akaniambia kaka Mimi nataka kuwa kama wewe pia nikusaidie kazi.

Nikamwuliza kivipi? Akasema naomba niwe na wewe kwenye Kamati ya Bunge. Nataka niwe Makamu Mwenyekiti wako.

Nikamwambia mbona Kamati hazijaundwa? Akasema Tayari ameongea na Spika na Spika kamwambia kuwa kama anataka afanye kazi na mimi basi amwingize Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) kwani tayari ameniweka Mimi huko.

Nikamwuliza kwanini anataka POAC, akasema ndipo anapoona panafaa kuisimamia Serikali na alinifuatilia Bunge la Tisa akaona namna nilivyofanya kazi. Tukazungumza mengine kisha nikamuaga. Katika orodha ya wajumbe wa Kamati alikuwamo dada Esther Bulaya.

Nikamwuliza kama anamjua Deo maana naona anakuja kwa kasi sana. Esther akaniambia kuwa ‘ Jamaa ni mzuri sana’ hivyo tufanye naye kazi. Kesho yake tukakutana tukapitia orodha upya, nikamwomba Deo aende kwa Spika kumshauri majina ya kutoa na majina ya kuongeza ili kamati iwe madhubuti. Tukaenda Dodoma.

Dodoma kukawa na zengwe kubwa kutoka baadhi ya wabunge kwamba nisiwe mwenyekiti. Waziri mmoja mwandamizi akamtaka Spika aniondoe kwenye Kamati hiyo na amweke Hamad Rashid, Mbunge wa Wawi.

Kwa kuwa Deo alishamaliza kazi ya Spika, juhudi hizo hazikufanikiwa. Lakini pia mimi nilikuwa nina mahusiano ya karibu sana na Hamad Rashid, naye alikataa katakata kuhamishiwa POAC.

Hata hivyo juhudi hizo ziliendelea na ikabidi Deo aandae ‘rebellion’ ya wabunge 8 kupinga maelekezo ya chama chao. Usiku wa kuamkia uchaguzi nikapata fursa ya kuzungumza na Rais Kikwete kuhusu hatari ya chama chake kupanga wenyeviti wa kamati za kuisimamia Serikali.

Ilipofika asubuhi mambo yalibadilika. Kikosi alichopanga Deo kilionyesha ‘rebellion’ ya wazi kabisa na hivyo tukaingia kwenye uchaguzi na kushinda Kwa kura 13 kati ya 15 zilizopigwa.

Deo alionyesha uwezo mkubwa wa kufanya Siasa za Bunge kabla hata ya kuanza kazi hiyo ya Ubunge. Tangu hapo, tukiungana na Kangi Lugola wa Mwibara, ikawa ni ‘ Utatu wa Kijasiri’ Kwa maneno ya Marehemu rafiki yangu, kaka yangu na ndugu yangu Deo Haule Filikunjombe.

Tulianza kushika ajenda moja baada ya moja. Ajenda ya kwanza iliyoonyesha uwezo mkubwa wa Deo ilikuwa ni kashfa ya upimaji magari kutoka nje ambao Shirika la TBS liliweka mawakala wa upimaji ambao hawana uwezo na kwa misingi ya rushwa.

Niliamua kuunda kamati ndogo kuchunguza suala hilo na nikamweka Deo na Kangi kama wajumbe wa kamati hiyo. Pia nikawaweka Christowaja Mtinda na Felister Bura, wajumbe mahiri wa Kamati ili kukamilisha kikosi cha kazi. Kwa kutumia mbinu za kipolisi ( Deo na Kangi waliwahi kuwa maafisa wa polisi ) waliifanya kazi ile kwa namna ya kipekee na kugundua ufisadi mkubwa sana.

Matokeo ya kazi yao ndio yalipelekea aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBS kufungwa jela na kuubadili kabisa mfumo wa ukaguzi wa bidhaa kabla ya kuingizwa nchini. Ujasiri wake ulijidhihirisha kuanzia hapa na ulikomaa zaidi katika sakata la Tegeta Escrow ambapo alisimama kidete kuhakikisha Kamati ya PAC inakamilisha kazi yake kwa uadilifu mkubwa.

Yeye ndiye aliyesoma sehemu ya Taarifa Maalumu ya Kamati iliyohusu kuwawajibisha Mawaziri. 
Deo hakujali misimamo ya chama chake anaposimamia ukweli. Alikuwa Mbunge wa kwanza kutoka chama kinachounda Serikali kuweka sahihi kwenye karatasi ya sahihi za kumwondoa Waziri Mkuu.

Kumwondoa Waziri Mkuu ni kuiangusha Serikali na Deo hakujali ilimradi alikuwa anaweka misingi madhubuti ya uwajibikaji. Uzalendo wa Deo haukuwa na mashaka hata kidogo. Kwake yeye Tanzania ilikuwa mbele ya jambo lolote lile.

Urafiki wa Deo ulikuwa wa kitiifu. Kuna wakati mmoja wa marafiki zangu ambaye mimi ndiye niliyemtambulisha kwa Deo alijaribu kutaka kutufarakanisha. Alichokifanya Deo ni kumwambia uso kwa uso kuwa mimi nimekujua wewe kwa sababu ya Zitto na kanuni za urafiki zinataka kwa sasa marafiki wa Zitto wote tuwe na Zitto.

Ilikuwa ni kipindi cha mpito kutoka chama nilichokuwamo kwenda kwenye chama kipya ambacho sasa naweza kusema Deo alishiriki kikamilifu katika uanzishaji wake na uendeshaji wake mpaka mauti yanamkuta.

Ni nadra sana katika maisha ya sasa kuwa na rafiki wa namna hii, ambaye anavuka mipaka ya vyama kwa sababu ya kumsaidia rafiki yake.Ingawa ulikuwa ni urafiki wa miaka 5 tu, lakini ulikuwa ni urafiki wenye mizizi.

Nilimwona Deo kama kaka yangu naye aliniona hivyo. Familia zetu zilianza kuwa na ukaribu na hata wazazi wetu, ambao wote walifariki kwa kufuatana mwezi Kwa mwezi, sote tulishiriki kuwahudumia kwa pamoja.

Kifo cha Deo kinabakia kama ndoto kwangu. Hata hivyo dini zinataka kushumkuru Mungu kwa yote.

Njia sahihi ya kumuenzi Deo ni kukumbuka namna alivyoishi na sio namna alivyopoteza maisha. Tanzania imepoteza mzalendo mtiifu kwa nchi.

Tanzania imepoteza kijana mwenye ujasiri wa ajabu na ambaye alikuwa hazina muhimu kwa nchi yetu.

Deo Filikunjombe alikuwa mtiifu, mzalendo na mjasiri.

mr mkiki.
 
Back
Top Bottom