Tathmini ya Utawala wa Ali Hassan Mwinyi (1985-1995) kama Rais wa Tanzania

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
AA182AC4-C7B6-42F7-8AFB-80A492089970.jpeg


Kwa sababu ya miaka 23 mfululizo ya kutawaliwa na Kiongozi mmoja, baadhi ya Watanzania waliathirika kisaikolojia kiasi kwamba waliamini hakuna kama Nyerere, na wengine wakahofu kuwa bila Nyerere, Tanzania haingekwenda, na labda amani ingetoweka!

Yalikuwa ni maluweluwe ya kisaikolojia! Mwaka 1984, Mwalimu Nyerere alitangaza azma ya kustaafu au kung’atuka kwa msamiati wake mwenyewe. Maswali yakawa mengi. Nani atakuwa Rais baada ya Nyerere? Nani ataweza kuvaa viatu vya Nyerere?

Watu wakaanza kuwafikiria watu wa kuweza kumrithi Nyerere na kuliweka sawa Taifa kiuchumi. Sio siri, mitaani, watu walikuwa wakimtaja Salim Ahmed Salim. Kutajwa kwa Salim kulitokana na ukweli kuwa kulikuwa na jambo alilofanya wakati alipokuwa Waziri wa Ulinzi.

Kulikuwa na magari fulani ambayo yaliingia Tanzania na kupewa Jeshi la wananchi Tanzania. Watu waliamini kuwa Salim alikuwa na ushawishi mkubwa wa Kimataifa ambao ungeiwezesha nchi kujenga ushirikiano wa Kimataifa na kupata nafuu ya kiuchumi.

Binafsi sikusikia jina jingine la mrithi wa Nyerere zaidi ya Salim. Tangu hapo, sikumjua kabisa Ali Hassan Mwinyi licha ya kwamba alikuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ukiacha fununu za mitaani, ndani ya Chama cha Mapinduzi, kitendawili kikawa kigumu kana kwamba kila mwana CCM aliogopa kuvaa viatu vya Mwalimu!

Kwa saikolojia ya wakati ule, ni kweli kila mmoja alikuwa na haki ya kujiogopa hivyo kwani Taifa liliaminishwa kuwa Tanzania ni Nyerere, na Nyerere ni Tanzania. Viwili hivyo visingeliweza kuachana kirahisi.

Mzigo wa nchi ulishamuelemea Mwalimu hasa liuchumi, na kwa kweli, alikuwa hana namna isipokuwa kujiuzulu. Kila mmoja akawa anachelea mzigo ule mzito angeubebaje?

Bila kutarajia, Makamu wa Rais Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, akatwishwa mzigo huo mzito. Siisahau kauli yake alipokuwa akifanya mikutano ya hadhara kabla na baada ya Urais.

“Nchi kubwa ya Tanzania inahitaji mabavu kama ya Mwalimu.” Hii ilikuwa ni kauli ya kuomba ushirikiano wa wananchi. Akatoa mfano wa mtu ambaye wenziwe wamemsadia kupanda juu ya mti na kisha kumtelekeza ilihali chini kuna machupa!” Hii ilikuwa ni kauli ya kuomba Watanzania wenziwe wasimwache peke yake baada ya kumchagua kuwa Rais.

Hebu sasa tumtazame Rais Mwinyi katika maeneo mannne,; Jamii, Siasa, Uchumi na Elimu.

Jamii katika Serikali ya Awamu ya Pili

Moja ya changamoto alizokuwa nazo Rais mpya wa Awamu ya pili ilikuwa ni kuhakikisha kuwa utangamano na Umoja wa Watanzania unadumu licha ya mabadiliko ya uongozi wa nchi.

Mwinyi alichunga maadili yaleyale ya mtangulizi wake katika kudumisha mambo hayo. Licha ya Uzanzibari wake lakini haikuwa zamu ya Wazanzibari kuukweza uzanzibari wao.

Watanzania wote walibaki kama walivyokuwa wakati wa Nyerere. Licha ya Uislamu wake, haukuwa wakati wa Waislamu kujikweza bali kila dini ilipata nafasi iliyokuwa nayo hapo kabla.

Sanasana Maaskofu walionekana kuwa na sauti zaidi kila lilipokuja suala la siasa na dini. Katika miaka mitano ya mwanzo, Mwinyi aliweza kuibadili saikolojia ya Watanzania kwamba kumbe Watanzania wengine wanaweza kuongoza nchi kinyume na mazoea yaliyojengeka kuwa bila Nyerere mambo yangeharibika!

Baada ya kumuamini Mwinyi, baadhi ya wanaCCM walianza kupiga debe kuwa Mwalimu amwachie Mwinyi hata Uenyekiti wa Chama. Hata baadhi ya watu mitaani, baada ya kuondokewa na bumbuazi la muda mrefu la kisiasa, waliona Nyerere basi yatosha! Amwachie Mwinyi kofia zote mbili.

Awamu ya Kwanza ya Rais Ali Hassan Mwinyi ilipita salama ukiacha mapambano ya askari polisi na wakata Miwa, Kilombero Morogoro. Kwa kiasi kikubwa uhusiano wa Serikali na wanajamii ulikuwa chanya.

Msukosuko mkubwa kwa Mwinyi na serikali yake ulianza katika awamu yake ya pili ambapo jamii ya Waislamu iliona kama vile inanyanyasika kijamii kwa sababu baadhi ya wananchi wenzao waliamua kuuza nyama ya nguruwe katika maeneo yenye Waislamu wengi jambo ambalo halikuwepo katika kipindi chote cha Rais Nyerere.

Vyombo vya Usalama vya Mwinyi vilionekana kushindwa kuimudu kadhia hiyo, na matokeo yake ugomvi mkubwa ukarindima baina ya Waislamu na Vyombo vya dola na sheria.

Kukamatwa kwa Masheikh, akiwemo Sheikh Kassim Bin Juma, kwa operesheni kamakamata ya Waziri wa Mambo ya Ndani, na baadae “Naibu Waziri Mkuu”, cheo ambacho hakikuwepo kabla yake na kikafutika baada yake, wengine wakidhani kilikuwa ni ‘kilemba cha ukoka”, kuliichafua kabisa haiba ya Mwinyi machoni mwa Waislamu!

Matusi na kashfa za Mrema kwamba Waislamu ni ‘wavuta bangi’, na kwamba ni ‘watumiaji wa dawa za kulevya’, au “mateja” kwa lugha ya sasa, yalizidi kumjengea chuki Mwinyi nyoyoni mwa makundi ya Waislamu.

Ulikuwa ni msukosuko mkubwa uliovuruga kabisa uhusiano wa Serikali ya Alhaji Mwinyi na Waislamu jambo ambalo lilimkondesha mheshimiwa Rais. Jamii ya Waislamu ilimtazama Mwinyi kama mtu aliyekuwa akiuelemea upande wa Waislamu kila ulipotokea mgongano wa kiimani baina ya dini kuu mbili nchini.

Jambo la pili lililozidi kuvuruga uhusiano wa Waislamu na Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Rais Mwinyi ni kifo cha kutatanisha cha Prof. Kighoma Ali Malima, Mungu amrehemu.

Hii ilikuwa ni jirani na Uchaguzi Mkuu wa Rais wa 1995 ambapo Prof. Malima alipanga kugombea Urais kwa tiketi ya chama kimojawapo cha upinzani. Hasira za Waislamu zikamfanya Mwinyi amalize kipindi chake katika mazingira magumu sana.

Mwenyewe, mara kwa mara, aliomba Waislamu wamvumilie, wasiwape la kusema watu wasiowatakia kheri! Kipindi cha mwisho cha Mwinyi kilikuwa kigumu kijamii, na kama ni hamu ya Urais basi ilimwisha hapo. Kwani barua za kichungaji nazo zilimnyima raha.

Kwa upande mwingine Wakristo nao walimshutumu Mwinyi kwa barua za kichungaji. Mchungaji Christopher Mtikila alipata kutoa andiko la kumuelezea Mwinyi kama mtu aliyefika njia panda.

Mtikila alimshutumu Mwinyi kwa udini katika siasa za utawala. Barua ya Mtikila ilikuwa ni moja tu ya barua za kichungaji zilizoandikwa kushutumu serikali ya Mwinyi. Baadhi zilishinikiza hasahasa kupigwa marufuku kwa mihadhara ya mlingano wa dini ya Waislamu. Hata hivyo, ukweli unabaki kuwa Mwinyi alijitahidi sana kuepuka mikwaruzano na Maaskofu, Wachungaji na walei.

Siasa katika Awamu ya Pili

Kisiasa, Uongozi wa Mwinyi ulifanikiwa katika mambo makuu mawili; kufunguliwa kwa milango ya demokrasia na Uhuru wa Vyombo vya Habari. Dhana ya demokrasia, japo haikutumika katika chaguzi za kipindi chake, lakini angalau miaka miwili kabla ya kuondoka madarakani nchi ilifungua mlango wa demokrasia ambapo siasa za vyama vingi zilianza wakati yeye akiwa madarakani.

Kwa pamoja na Uhuru wa Vyombo vya habari, nchi ikajenga mazingira mapya kutoka yale ya utawala usiokosolewa kuja utawala uliokosolewa hadharani. Kwa mara ya kwanza ikashuhudiwa demokrasia ya Rais kuchorwa na kusemwa vibaya.

Vijana wa Chuo Kukuu cha Dar es Salaam wao walifikia hatua mbaya zaidi pale walipoifuja demokrasia hiyo kwa kuchora picha za matusi dhidi ya Rais Ali Hassan. Kama tutakavyoona katika kipengele cha elimu, Mwinyi alileta nafuu kubwa ya maisha ya Wanataaluma Chuoni hapo.

Japo waliomtusi walikuwa na madai yao halali, lakini ukweli kuwa hali ya Chuo Kikuu hicho kihuduma ilibadilika kulinganisha na enzi za Nyerere ulitosha kabisa kuwasuta wasomi hao.

Japo wanataaluma walianza kuonesha mfano mbaya wa matumizi ya uhuru wa kujieleza ambao haukuwepo enzi za Nyerere lakini bado Mwinyi hakufunga mlango wa demokrasia.

Kwa mara ya kwanza tangu miaka ya 1960, Watanzania wakaanza kushuhudia majukwaa ya upinzani dhidi ya Chama tawala na serikali. Ukizungumzia mwanzo wa mageuzi ya kisiasa basi lazima utayakuta ndani ya kipindi cha Mwinyi.

Japo Nyerere alijitokeza kuelezea muundo wa vyama vya siasa katika kuunda mfumo wa vyama vingi lakini hayo aliyasemea katika kipindi cha Mwenzie. Katika kipindi chake, Nyerere alipiga marufuku mfumo uliokuwepo wa vyama vingi vya siasa.

Inaposemwa mfumo wa vyama vingi ulirudi tena mwaka 1992, huenda vijana wadogo wanashindwa kuelewa. Ni kwamba Vyama vingi vilikuwepo hadi mwanzoni mwa miaka ya uhuru lakini Serikali ya Nyerere ikavifutilia mbali.

Serikali ya Mwinyi ndiyo iliyorudisha tena mfumo huo hata kama ni kwa shinikizo la Mataifa ya Magharibi. Karibu vyama vyote vikubwa vya Siasa vya Upinzani vilianza shughuli zao katika kipindi cha Mwinyi.

Mwinyi aliondoka madarakani mwaka 1995, miaka mitatu baada ya Mfumo wa Vyama vingi kuanza. Alikuwa ni baba wa mageuzi ya kisiasa, na baba wa Uhuru wa Vyombo vya habari. Ni Kwa nukta hii, Mwinyi anapata alama nyingi za mafanikio ya kisiasa. Tunampa alama 60.

Msukosuko wa kwanza wa kisiasa alioupata Rais Mwinyi ulikuwa ni ule wa kundi la G55 lililoanzisha vuguvugu la serikali ya Tanganyika likitaka muundo wa serikali tatu. Mwalimu Nyerere alimsaidia Mwinyi kuzima moto huo wa Utanganyika.

Msukosuko wa pili alioupata Mwinyi kisiasa ulikuwa ni ule wa kutukaniwa mkewe. Mwalimu Nyerere aliikebehi serikali ya Mwinyi kuwa ilikuwa inashauriwa na mama Sitti! Kumbe basi wanawake hawana sababu ya kumuenzi Mwalimu Nyerere.

Uchumi katika Awamu ya Pili

Kama kuna eneo lililoung’arisha mapema utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi basi lilikuwa ni lile la Uchumi. Mwinyi aliaswa na wataalamu wa uchumi kuwa aachane kabisa na fikra zilizoshindwa na Mwalimu Nyerere kama alitaka kufanikiwa katika eneo hili.

Alipokea kijiti cha uongozi wakati nchi ikiwa katika hali ngumu mno kiuchumi. Wengi mwanzoni hawakumpa wastani mkubwa wa mafanikio kwa kuamini kuwa kama alishindwa Nyerere, Mwinyi angeweza wapi!

Mwinyi alikuta foleni za unga wa njano na magendo ya bidhaa. Hata ‘sigara kali’ achilia mbali ‘sports’ na SM, ziliuzwa kwa bei ya kuruka! Foleni zilikuwa ndefu, na za kuchosha ambazo wakati mwingine zilikuwa za kusubiria bidhaa ambazo hata dukani hazijafikishwa kutoka RTC/Ugawaji.

Kabla ya mikokoteni kufikisha magunia mawili-matatu ya unga wa njano, au mchele mdundiko, au kitumbo uliotoka Japan, watu kwanza walipanga mawe au makorokoro yoyote yale kwa sababu ya jua kali la saa nane mchana.

Wakati mwingine, sio tu kupumzika kivulini, bali mawe yaliwakilisha watu kwenye foleni kwa sababu wenyewe kwanza walikwenda kufanya shughuli nyingine baada ya kuambiwa kuwa mkokoteni ungefika saa kumi na moja jioni, na si saa saba mchana kama ilivyoelezwa mwanzo.

Foleni zilikuwa za kusukumana kwani watu walikuwa wengi kuliko bidhaa. Ndiyo kusema, wengine walirudi nyumbani mikono mitupu baada ya jitihada za kusukumana ili kulifikia dirisha la duka kushindikana. Wengine walizirai kwenye foleni! Ugumu hasa ulikuwa katika kupata sukari au mchele uliokuja kwa nadra.

Mara nyingi, mchele na sukari vilipatikana kwa magendo majumbani mwa watu. Walanguzi walikuwa wakitazama au kuangalia huku na kule kabla ya kukupimia kibaba cha sukari, na wakati mwingine vibaba vyenyewe vilikuwa “mkude”.

“Vibaba-mkude” ni vibaba vya kupunjia. Kwanza unalanguliwa lakini pili unapunjwa. Ilikuwa ukienda sokoni unatazamwa usoni. Kisha unaulizwa unataka nini. Kama ulitaka mchele, basi mtu alibonyea bonye uvunguni mwa kikazi chake cha biashara na kubenjua gunia lililofichwa vizuri.

Unapimiwa kibaba mkude bila wewe mwenyewe kuona. Kwa kuwa ulihitaji mchele, na umeupata baada ya kuhangaika sana, basi huulizi tena. Tangu hapo, unatakiwa uondoke haraka sana baada ya kupimiwa, usiweke kiwingu cha kuleta “manjagu” bure.

Mteja alitakiwa awe ‘shapu’, hakuna kuzubaa-zubaa! Na mtu alipokwenda kwenye nyumba yenye mchele au sukari ya magendo, hakutakiwa kupitia mlango wa mbele, bali azunguuke uchochoroni na kupitia mlango wa nyuma. Ukitoa sauti kali kuuliza sukari au mchele, hupati! Hawakuuzii ng’o, unaambiwa hakuna!

Hali ilikuwa mbaya mpaka watu wakatumia njia zisizofaa kusafirisha bidhaa kutoka eneo moja kwenda jingine. Mageti ya kuzuia magendo yaliwekwa njiani. Nakumbuka tukio moja ambapo walanguzi, katika kufanya ujanja wa kupitisha magunia ya sukari, walitumia Sanduku kama jeneza.

Wakalifunika shuka za kuzikia, na walipofika jirani na geti wakapaza sauti za nyiradi wanazosoma Waislamu wanapokwenda kuzika. Askari walipoona hivyo, wakapunga mkono kuruhusu msafara wa “mazikoni” upite. Kumbe haukuwa mwili wa mtu au ‘maiti’ bali yalikuwa ni magunia ya sukari.

Mameneja wa RTC ndio walioshamirisha magendo kwani walikuwa wakiwatumia “watoto wa mjini” kutoa bidhaa kwa mlango wa nyuma kutoka kwenye magodaoni ya Shirika la Ugawaji.

Nyerere aliamini kuwa, kwa kutumia sekta ya Umma kuhodhi bidhaa labda alikuwa anashinda vita dhidi ya ubepari kumbe alijenga mazingira ya kuwatesa wananchi wake na kuwanufaisha Maafisa wabadhirifu.

Kiwango cha ubadhirifu wa mali ya Umma kilikuwa ni kikubwa kinyume na madai ya baadhi ya watu kuwa wakati wa Nyerere hakukuwa na ufisadi na ubadhirifu!

Fagio la Chuma aliloanza nalo Mwinyi lilitokana na ukweli huo kuwa alikuta ubadhirifu umeshamiri wakati Nyerere akipiga siasa na kusifiwa kinafiki!

RTC halikuwa tena shirika la kusaidia wananchi bali lilikuwa ni shirika la kuwatesa wananchi kwani bidhaa zilifichwa kwa makusudi na zikatolewa kwa mlango wa nyuma kwenda mikononi mwa walanguzi.

Matokeo yake, sukari, mchele, sabuni za kufulia na kuogea, sigara, dawa za mswaki vyote vikapatikana kwa mwendo wa kuruka. Si hivyo tu, bali ilifika mahala hata magodaoni ya Shirika la Ugawaji yakaishiwa kabisa, na kubaki na maharage yasiyowiva hata ukitia maji mara kumi na mbili!

Karibu bidhaa zote za viwanda ziliadimika kwa sababu hatukuwa na uzalishaji wa kutosha wa ndani, na mipaka ilifungwa kisiasa na kuzuia bidhaa za nje. Sekta ya Umma aliyotumia Nyerere kuzalisha bidhaa ilifeli vibaya.

Viwanda vyote havikudumu kwa sababu ya kukosa tija. Wananchi walivaa nguo mbovu, na za viraka au kama zilivyoitwa wakati ule ‘midabwada’. Walivaa makatambuga kama yale ya wamasai kwa sababu ya kukosekana kwa viatu.

Kwa kifupi, hiyo ndiyo hali aliyoikuta Ali Hassan Mwinyi. Ilikuwa ni nchi ngumu mno ambayo, alimanusura, ingesababisha serikali ya Mwalimu Nyerere ipinduliwe lakini jaribio la Maafisa wa Jeshi lilizimwa.

Majalada ya kesi ya uhaini ya Mwaka 1984 yanabaki kama kumbukumbu ya jaribio la mapinduzi walilotaka kulifanya wanajeshi baada ya kuona Nyerere hakushaurika wala hakuwa na namna ya kukosolewa!

Mbali ya hatari ya kupinduliwa, Nyerere aliondoka madarakani ili kuepuka kusalimu amri kwa mabepari. Yeye, kama mpinzani wa Mataifa yaliyoitwa ya Kibepari, hakutaka kusalimu amri kwa niaba ya Taifa lake lililokwama kiuchumi.

Alichelea kula matapishi yake! Lakini hali mbaya ya uchumi wa nchi yake ilihitaji hatua hiyo ya kusalimu amri kwa mabepari. Akaona bora ampishe mwingine ili asalimu amri kulinusuru Taifa kiuchumi huku yeye akiendelea na mapambano yake ya kinadharia zaidi dhidi ya mfumo wa kibepari kupitia Tume yake ya Kusini.

Aliporudi kutoka kwenye mizunguuko yake, chama chake kikampa nafasi ya kupiga domo la kuvunja mbavu! Akawa kama babu mpiga hadithi za kuvutia usingizi! Zilikuwa ni hekaya za Mwalimu Nyerere. Kwa hakika, Taifa lilihitaji mtu mwingine wa kuliokoa kiuchumi.

Kwa hiyo, Ali Hassan Mwinyi alikuwa na kibarua kigumu cha kufufua uchumi uliokufa kabisa. Jambo la msingi lilikuwa ni kubadili fikra kutoka zile za Mwalimu zilizoididimiza nchi kiuchumi kuja zile za kufunguka kiuchumi.

Lakini Mwinyi hakukosa upinzani katika kubadili fikra za Nyerere. Nyerere alitaka kuingilia kazi za Ikulu. Zilipatikana tetesi kuwa Rais huyu alikaribia kuachia madaraka kwa sababu ya bughudha ya Nyerere!

Akina Kolimba na Malecela walifanya chini juu kuhakikisha kuwa Mwinyi anatekeleza fikra mpya, na kuachana na zile zilizoshindwa za Nyerere. Madai ya Mwalimu kwamba wanasiasa hao walikuwa wakimshauri vibaya Rais Mwinyi yalitokana na upinzani wao dhidi ya fikra zake.

Kwa kweli zama za Ujamaa zilikwisha, zama za kutembelewa na wageni wa kisiasa wa kikomunisti, ‘choka mbaya’, “njaa kali,” kutoka Vyama vya Kisoshalisti vya Soviet Union, Albania, Bulgaria n.k. zilikuwa zimepita.

Sasa ulikuwa ni wakati wa kufungua milango kukaribisha wawekezaji wa kiuchumi kutoka pande zote za dunia ukiwemo ulimwengu wa Magharibi.

Wanasiasa, viongozi na wataalamu waliomzunguuka Rais Mwinyi walimsaidia kushikilia msimamo wa kuweka kando fikra za Nyerere.

Waliona kuwa wakati Mwalimu alikuwa akipiga siasa, wananchi walikuwa wanateseka! Hasira za Mwalimu Nyerere dhidi ya wanasiasa hao zikawa ni kumtungia kitabu Malecela na kumsusa kisiasa.

Kolimba naye akaja kufa katika mazingira ya kutatanisha! Hata hivyo, Mwinyi, kwa kiasi kikubwa, aliweza kuachana na fikra butu za Mwalimu. Eti leo hii, kuna watu wanaosema kuwa Tanzania haitapata tena Nyerere mwingine!

Kizazi kipya kinajibu, ‘afadhali tena afadhali. Tanzania haihitaji tena mtawala wa aina ya Nyerere! Tusiite mizimu wala tusitukuze wafu kwa sisa za kutengeneza, bali tuwapime waliohai na kuwasifu kwa yale waliyoyafanya. Kina Mwinyi, kina Mkapa, Kina Kikwete wamefanya ya kusaidia wananchi, tusiwafunike kwa vivuli vya mizimu!

Tangu hapo, laiti demokrasia ingelikuwepo, yangehitajika mabadiliko ya haraka sana kumpunguzia muda wa kutawala Nyerere ili kulinusuru Taifa kiuchumi.

Taifa lilihitaji mtu wa aina ya Mwinyi mapema. Laiti Mwinyi ndio angeanza mwaka 1961, Tanzania ingekuwa mbali sana kimaendeleo, na ingezitimulia vumbi nchi jirani ikiwemo Kenya inayoonekana kutushinda kwa kila kitu isipokuwa siasa za majukwaani.

Muda mfupi tu baada ya Mwinyi kuingia madarakani na kubadili mtazamo wetu wa kiuchumi, mambo yakaanza kubadilika kiasi cha kuwashangaza watu. Magenge ya ulanguzi yakatoweka baada ya bidhaa kupatikana kwa wingi.

Watanzania wakaanza kufanya biashara na nchi nyingine, waliokwenda Kenya kupeleka machungwa, na wao kurudi na sabani za kufulia na kuogea, waliokwenda Uganda, waliokwenda Uarabuni, alimuradi kila mmoja alikwenda alikotaka.

Soko la bidhaa mbalimbali likashamiri. Badala ya watu kutafuta bidhaa, bidhaa zikatafuta watu. Nguo mpya za dukani bwerere, mitumba bwerere, sabuni kibao, fegi (japo hazifai kiafya) teletele, magari makubwa na madogo kibao, Televisheni kibao, Radio kibao.

Rukhsa ya Rais Mwinyi ikawa na manufaa makubwa kuliko shari ya kufunga mipaka aliyokuwa nayo mtangulizi wake. Ndipo Watanzania walipoanza kujutia miaka mingi ya utawala wa Nyerere!

Bora Nyerere angechukua miaka 10. Miaka 10 ya Mwinyi ilikuwa na faida kubwa kwa Watanzania kuliko miaka 23 ya Mwalimu Nyerere. Hata alipoanza fujo za kutukana utawala wa mwenziwe kuwa ulishauriwa na “Mwanamke”, watu walimzomea na kumkumbusha enzi zake za foleni za bidhaa! Katika eneo la Uchumi, Mwinyi tunampa alama 70.

Elimu katika Awamu ya Pili

Mkuu wa shule moja, Bw. Mohammed Ismail Patel (Mhe. Januari Makamba au John Nchimbi wanamjua kwa sababu walisoma katika shule yake), aliwahi kudhalilishwa enzi za kamatakamata ya Wahujumu Uchumi.

Mkuu huyo alikamatwa na kupakiwa nyuma ya Landrover ya Polisi kwa tuhuma za kuhujumu uchumi! Sababu ni kwamba sekta binafsi hata kama ilikuwa ya elimu bado ilitazamwa kama chanzo cha ubepari uliomkera Mwalimu Nyerere!

Mtu ambaye anawapatia wananchi wako elimu unamdhalilisha! Kwa kweli Mwalimu hakulitakia mema Taifa kielimu. Kuibana sekta binafsi ya elimu na kushindwa kuipanua sekta ya umma ya elimu kuliwakosesha vijana wengi elimu ya sekondari na ya juu.

Vijana ambao walikuwa na vipaji mbalimbali vya kulisaidia Taifa lao, na kujiendeshea maisha yanayoeleweka, wakaangukia kwenye magenge ya wahuni na wavuta bangi baada ya kuishia darasa la saba.

Wengine wakaishia kuwa wabeba mizigo na wasukuma mikokoteni. Angalau katika kipindi cha Mwinyi, sekta binafsi ya elimu ilianza kupumua. Zaidi ya hivyo, serikali ya Mwinyi iliwajengea watu wengi uwezo wa kiuchumi kwa njia za biashara, na hivyo kujiongezea kipato cha kuweza kusomesha watoto wao katika shule binafsi.

Idadi ya wazazi walioweza kusomesha watoto katika sekta binafsi ikaongezeka. Fursa za Elimu zikaanza kufunguka kwa wingi. Twaweza kusema Mwinyi alipanua wigo wa sekta ya elimu na waliofuata kama tutakavyoona katika makala zao, wakapanua zaidi. Katika eneo hili, Mwinyi tunampa alama 40.

Hisani: Tathmini ya Utawala wa Ali Hassan Mwinyi 1985-1995

Soma pia > Rais wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi afikisha miaka 95. Heri ya kuzaliwa Mzee Ruksa!
 
Alifungua milango Na madilisha watu wakaenda Pakistan kuleta heroin. Mafisadi na mabeberu kunyakua migodi yetu
 
Kunawatu mna muda wa kuchezea, hii siyo thesis bali hisia za Mwandishi...., eti Mwl. Nywerere alikasirika akamtungia Malechera kitabu, what a gimmick!
 
Public opinion is very fickle. Waliomuona JK dhaifu na hovyo juzi leo wanamuona shujaa
 
kweli kabisa opinion will remain opinion, tukitaka kupata usahihi wa hukumu ya kihistoria tuwe na vigezo vya kisayansi visivyoweza kupingwa na mtu yeyote wala kumpendelea mtu yeyote.
japo muwasilishaji amefanya vizuri katika kuchambua hoja zake.
 
Kama kuna Rais kuwahi kutokea hapa Tanzania na kuwa mpole na mwenye utu basi ni rais Ally Hassan Mwinyi. Yeye alikuwa akikosolewa sawa,usimpomkosoa sawa.

Katika utawala wake aliwahi kukebehiwa kuwa mke wake ndie anayeongoza nchi, mke wake alikamatwa na dhahabu uwanja wa ndege. Alikuwa anatukanwa hadharani kuwa ameuza nchi kwa magabachori na waarabu .

Pamoja na kukosolewa kwa kushindwa kupambana na rushwa , upendeleo wa kidini kwa waislamu na kumpa nguvu ya kutoa maamuzi mke wake. Hatukusikia watu wamepigwa risasi na wanaojiita wasiojulikana, hatukisikia waandishi wa habari wanapotea.

Kwa hiyo kila utawala una namna ya kutawala.
 
Kama kuna rais kuwahi kutokea hapa Tanzania na kuwa mpole na mwenye utu basi ni rais Ally Hassan Mwinyi. Yeye alikuwa akikosolewa sawa,usimpomkosoa sawa.

Katika utawala wake aliwahi kukebehiwa kuwa mke wake ndie anayeongoza nchi, mke wake alikamatwa na dhahabu uwanja wa ndege. Alikuwa anatukanwa hadharani kuwa ameuza nchi kwa magabachori na waarabu .

Pamoja na kukosolewa kwa kushindwa kupambana na rushwa , upendeleo wa kidini kwa waislamu na kumpa nguvu ya kutoa maamuzi mke wake. Hatukusikia watu wamepigwa risasi na wanaojiita wasiojulikana, hatukisikia waandishi wa habari wanapotea.

Kwa hiyo kila utawala una namna ya kutawala.
Ukiulizwa hao "WATU" waliopigwa risasi na utawala kwa kukosoa. Tutaambiwa Tundu Lissu😂😂
 
Uongozi wa waislam kwa kiasi kikubwa huwa wanamtanguliza Mungu sio kama hawa wakatoliki wenye mijiroho ya chuma
 

Similar Discussions

5 Reactions
Reply
Back
Top Bottom