Tasnifu za njano5: Kwa maslahi ya chama, mh. Mbowe kiri makosa au kanusha tuhuma

Dotto C. Rangimoto

Verified Member
Nov 22, 2012
1,993
2,000
CHUGUU LA ZAMANI:
Leo naomba kujadili umuhimu na ulazima wa uongozi wa CHADEMA chini ya Mbowe kujibu hadharani hoja zao hao wanaoitwa wasaliti wa chama. Midhali umma umezisikia hizo hoja hadharani basi kuna umuhimu na ulazima wa uongozi kuzijibu kwa mifano na vielelezo hai ili kulinda na kutunza heshima ya chama, lakini kubwa kwa uongozi huo kujisafisha kwa wanaCHAMA.


MAYAI:
Kama kweli kuna wahafidhina na wabadhilifu ndani ya chama chetu, basi kidogo kidogo hawa wafuasi wa wahafidhina na wabadhilifu wataelewa somo na ipo siku watasema "tungejua.." lakini watakuwa wamechelewa kwani nyota ya shamsi itakuwa inachomozea magharibi na kuzamia kaskazini, naam, kitakuwa ni kipindi cha nakama na kila mtu akipambana kunusuru nafsi yake bila kuzingatia maslahi mapana ya chama na taifa kwa ujumla wake na ikifikia hapo CCM watatuimbia mapambio ya maombolezo tayari kwa kuzikwa rasmi. Tandika majani blangeti udongo, mtenda mema kaenda.


Kama kweli kuna hao wahafidhina na wabadhilifu, niko na imani nia na juhudi za Chacha Wangwe zingali zinaishi ndani yetu sisi vijana wachache na ipo siku ndoto ya Chacha Wangwe itatimia kwa kuwa na CHADEMA kama taasisi badala ya CHADEMA ya watu wachache wenye hulka za Panya na Nyani. Panya tabia yake ni kung'ata huku anapuliza wakati Nyani hukiuka sharia na kanuni za uendeshaji wa mahakama pindi akiletewa kesi ya ngedere aliyeiba mahindi.


Watu wanahoji kamati kuu iliona makosa ya watu wa upande wa Zitto tu na kuyajadili huko, lakini wale wote waliokuwa wanatumia mitandao kumchafua Zitto na chama hawajaonwa na CC pamoja na kwamba watu hao wanajulikana? Huu ni unyani, upanya nitaufafanua mbele.


Hatuwezi kushinda uchaguzi ujao wa 2015 kama uongozi wa sasa hauaminiki pamoja na ushupavu wake. Ili tushinde uchaguzi ujao tunatakiwa kuwa na uongozi shupavu, imara na wenye kuaminika. Uongozi wa sasa inabidi uwe hivyo na uongozi ujao ni lazima uwe hivyo.


Lakini pia tunahitaji wanaCHAMA wasio ona soni kuukemea uongozi kama ukipotoka, wanao amini juu ya misingi ya chama badala ya mtu na wanao jitoa kwaajili taifa kwanza kabla ya chama; kwa kufanya hivi chama kitaonekana kina wanaCHAMA wafia nchi na hivyo kuongeza mvuto kwa chama.


WanaCHAMA wasasa, hususani hawa wanao shinda humu kwenye mitandao wanakubali kuimba wimbo wa usaliti bila kuutaka uongozi ujibu hoja za hao wasaliti, yaani, wanajadili mtoa hoja badala ya kujadili hoja.


Mfano mwanaCHAMA anaweza kuhoji, hivi ni kweli chadema ina kamati ya tenda? wajumbe wa hiyo kamati ni wakina nani? na kiongozi wa hiyo kamati ni nani? ni kweli mwenyekiti wetu mbowe anaingilia kazi za kamati hii kwaajili ya maslahi yake ya kibiashara? Hivi ni kweli hadi sasa mbowe alichukua milioni 80 kwaajili ya kununua vifaa vya chama? Je kamati ya tenda(kama ipo) inafanya kazi gani ikiwa Mbowe ndiye anayefanya kazi za hiyo kamati? Hivi ni kweli hivyo vifaa hadi sasa havijafika? Kwanini huku tukiendelea kuimba wimbo uliochuja wa usaliti tusimtake Mbowe ajibu hoja hizi?


Pia hivi ni kweli kuwa hoja ya fedha kwenye kamati kuu ilikuwa haijadiliwi hadi mwisho? Hivi pia ni kweli Mbowe huwa anakikopesha chama bila maandishi na huja kujilipa kwa kiasi kikubwa kuliko hata kile alichokikopesha chama? Nimesoma waraka wa Chacha Wangwe, hivi ni kwanini Chacha aliitwa msaliti ikiwa hoja zake zilikuwa na mashiko na zenye kuhitaji majibu? Kwanini kila anayemkosoa mbowe na kuhoji matumizi ya chama huitwa msaliti? Hivi ni kweli mbowe hutumia mbinu ya kikoloni na ya kiccm katika kupambana na wapinzani wake ndani ya chama? Kama sivyo huu wimbo wa usaliti unalengo gani ikiwa wahusika wana hoja zenye lengo la kujenga chama katika misingi ya kidemokrasia na uwazi?


Kitendo cha mtu kujifanya anakisaidia chama kifedha kwa kukikopesha kisha anakuja kujilipa fedha nyingi kuliko hata deni lenyewe ni sawa na kitendo cha kung'ata na kupuliza, huu ndio upanya wenyewe.


Uongozi wa sasa hauaminiki, pamoja na kwamba wakosoaji wake wamekiuka katiba wakati wakifanya hivyo lakini bado kwa sisi ambao tuko nje ya vikao vya maamuzi na ambao hizi tuhuma dhidi ya uongozi tumezisikia na umma ambao hizi tuhuma umezisikia pia, ni vema uongozi ukazijibu hadharani kwa mifano hai ili uongozi na chama kwa ujumla wake kipate kuaminika kwa wanachama na umma ambao tunajua unahitaji chama makini na chenye uwezo wa kujiongoza na kujisimamia kabla ya kupewa majukumu ya kudhamini serikali.


MCHWA:
UONGOZI usipozijibu hizi tuhuma hadharani basi CHADEMA kitakuwa chama hodari cha kulipua mabomu ya ufisadi na kwa vyovyote vile itaaminika kuwa hayo mabomu ndio yaliyoipaisha CHADEMA na kuwa chama kikuu cha upinzani na si uongozi imara, mzuri, na uwazi kama inavyoamika; Hapa namaanisha(kama tuhuma zikithibiti) tumekuwa chama kikuu cha upinzani si kwasababu uongozi wa Mbowe mzuri bali tumekuwa chama kikuu cha upinzani kwasababu ya wabunge wetu tangu enzi ya Dr.Slaa wamekuwa wakifichua MACHAFU na MADUDU ya serikali bila woga.


Uongozi mzuri na imara husimamia demokrasia ya ushindani, huwa na uwazi katika matumizi yake ya fedha, mwenyekiti kama kiongozi mkuu haingilii kazi za idara, mabaraza, kurugenzi na kamati za chama ambazo zimeundwa kwa mujibu wa katiba.


KUMBIKUMBI:
Chini ya uongozi wa Mbowe demokrasia ilikanyagwa pale Zitto alipoambiwa asigombee uenyekiti mwaka 2009, chini ya uongozi wa Mbowe, Chacha Wangwe ameitwa msaliti kisa tu amehoji matumizi ya chama na kitendo cha Mwenyekiti kukikopesha chama bila maandishi na kisha kujilipa fedha nyingi, chini ya uongozi wa Mbowe, mwenyekiti wa chama taifa anaingilia kazi za kamati ya tenda kwa kuchukua milioni 80 za kununua vifaa vya chama na pia kujiingiza katika ununuzi wa magari na pikipiki za chama ili hali ipo kamati yenye jukumu hilo.


Chini ya uongozi wa Mbowe tuna wanaCHAMA mashabiki wa watu na wengi wao wamelipa ada ya uanachama kwa mwaka ule tu waliojiunga. Ziara za kichama za viongozi wakuu na zile kazi za M4C zimezalisha mashabiki wengi kuliko wanachama. Mfano Dr.Slaa alikuja huku Mikoa ya Kusini na kufungua matawi na kusimamia uchaguzi wa matawi hayo.


Lakini alipoondoka yale matawi hayafanyi kazi na unaweza kusema kama yamekufa na wale wanachama wameishia kuwa mashabiki wa Dr.Slaa. Sababu Dr.Slaa alipoondoka huku nyuma hajaacha mtu wa kuwafundisha wale wanaTAWI falsafa na itikadi ya chadema, wenye jukumu la kufundisha na kutoa semina kwa wanaCHAMA wapya ni makatibu wa majimbo, wilaya na kata. Makatibu hawa wanatumia muda mwingi kuganga njaa za kaya zao, hivyo hawana muda wa kutosha wa kufanya kazi za chama. Hapa ndipo unapokuja umuhimu wa makatibu wetu kulipwa mishahara au kupewa posho za kujikimu.


Tutaendelea kuimba wimbo wa kuacha ushabiki kwa watu lakini watu wataendeleza ushabiki kama watu hao hawatufundishwa itikadi na falsafa za chama chetu, mwanaCHAEMA mwenye kuijua itikadi na falsafa ya chadema basi ataipenda chadema kwa kuzingatia itikadi na falsafa yake, mtu huyo hatosubiria kugombea uongozi ndio alipe ada ya uanachama na hato teteleka hata kama kiongozi mwandamizi na mwenye mvuto wa chama akifukuzwa chamani.


Chini ya uongozi wa Mbowe vikao na maamuzi ya kamati kuu hayaheshimiwi; kwa mfano iliamuliwa na kamati kuu hadi mwezi huu uchaguzi wa ndani uwe umekwisha kamilika lakini ndio kwanza ratiba na tarehe ya uchaguzi imetangazwa sasa tena mara baada ya yule ambaye aliye semekana kuwa angegombea uenyekiti kupata majeraha ya kisiasa kutokana na maamuzi ya kamati kuu, pia kuna fedha inasemeka kamati kuu iliazimia zisiguswe lakini hizo fedha usalama wake uko shakani na kuna uwezekano mkubwa chama kumpigia goti Mbowe kwaajili ya fedha za kugharamia uchaguzi mkuu ujao.


Chini ya uongozi wa Mbowe kikao cha kamati kinatumika kama njia au kikao cha kutekeleza mikakati ya Mbowe ya kuwadhibiti wapinzani wake wa kisiasa ndani ya chama: rejea kutangazwa kwa tarehe na ratiba ya uchaguz mara baada ya Zitto kuvuliwa nyadhifa zake na kuna kila dalili ya mwanasiasa huyo kijana kufukuzwa kisa uenyekiti au kutamani vilaji vya wakubwa. Chini ya uongozi wa Mbowe kila wanao hoji matumizi na kukosoa uongozi huishia kuitwa wasaliti, wanatumiwa na CCM na TISS.


MALIKIA NA MUMEWE.
Kama kweli chini ya uongozi wa Mbowe hali ndani ya chama ndivyo ilivyo, basi si kweli hata kidogo kuwa tumekuwa chama kikuu cha upinzani kwasababu Mbowe ni kiongozi mzuri, bali tutakuwa tumekuwa chama kikuu cha upinzani kwasababu wabunge wetu kazi zao kibunge ni nzuri na zenye kumfikiria mlala hoi; hapa rejea kazi za kibunge za Dr.Slaa, Zitto, Mnyika, Halima Mdee, Mch Msigwa. Hapa nimezingatia kazi zao kama mawaziri vivuli na zile hoja binafsi walizoziwasilisha. Dr.Slaa EPA na Zitto sakata la BUZWAGI zilipandisha chati ya CHADEMA.


Lakini pia tumekuwa chama kikuu cha upinzani kwasababu watanzania wameshachoka siasa za Lipumba na Seif kujifanya wao ndio wenye uwezo wa kuongoza kuliko mwanachama wowote wa CUF na pia watanzania wameshaichoka CCM na MADUDU YAKE. Hivyo walipoona wabunge wetu wamefanya kazi nzuri katika bunge la tisa kama wapinzani, wakaona CHADEMA ni chama cha kuweza kuaminiwa uchaguzi unaofuata ambao ulikuwa ni wa 2010; imani yao ikapelekea CHADEMA kuwa chama kikuu cha upinzani.


CHURA NA NYOKA.
Nimesema uongozi wa Mbowe ni imara lakini sasa hauaminiki, sababu ya kutoaminika ni kutokana na tuhuma walizo ziibua wakosoaji wake wa ndani ya chama. Kitendo cha uongozi wa chama kinachotaka kudhamini serikali kushindwa kuaminika ni sawa na kumbikumbi waliojivunja mbawa ili wajenge chuguu lao kuwa kivuno kwa chura kabla ya kukamilisha azima yao, hii ni hatari kwa mustakabali wa kuzaliana na kuongezeka kwa mchwa.


CHUGUU JIPYA:
Yalopita si ndwele tugange yajayo, lakini pia hayo yaliyopita huwa ni "ndwele" kama wahusika hawatakiri maovu waliyoyafanya aidha kwa bahati mbaya au kwa kukusudia na kama hawata azimia kuyaacha sanjari na kujuta. Au yaliyopita huwa "ndwele" endapo wahusika hawata yakanusha maovu wanayo tuhumiwa kwa ushahidi uso kuwa na shaka yoyote.


Hivyo uongozi wa Mbowe unatakiwa kukiri makosa na kisha tusonge mbele kiroho safi, au ukanushe tuhuma kwa ushahidi usio kuwa na shaka yoyote. Ushahidi usiokuwa na shaka yoyote si lazima uthibitike mahakamani au kwenye baraza la kusikiliza shauri, bali kwa watu waliokaa kwa nia njema ya kujenga bila kigegezi huweza kuona ushahidi huo kwenye kikao chao na kisha kuutangaza ili umma waujue.


Kwa kukiri makosa au kukanusha tuhuma kutarudisha imani ambayo sasa imeshaanza kupotea, hivyo basi tutanza upya huku tukiendelea pale tulipoishia kama chuguu jipya na imara lililojengwa mara baada ya kumbikumbi wawili kuruka vihunzi vya nyoka, chura, binadamu, kuku na kila aina ya hatari ambayo aghalabu huwakabili malikia na mfalme wa kumbikumbi na mara baada ya kuvunja mbawa zao na kuanza kutembea ili kupata eneo zuri tayari kwa kujenga chuguu.


Katika kulijenga chuguu letu liwe imara na kupunguza wanaCHAMA mashabiki kwa watu, naamini program ya CHADEMA MSINGI itaondoa uanachama wa ushabiki, lakini napendekeza makatibu wetu wa CHAMA, BAVICHA, BAWACHA, na WAZEE ngazi ya kata ndio waaminiwe kwa program ya CHADEMA NI MSINGI, hao ndio wapewe MAFUNZO na kisha kwa kushirikiana viongozi wa matawi yaliyopo kwenye kata zao wataweza kutuletea MATOKEO MAZURI katika program hii.


Pia matawi yetu ambayo yamepatiwa mafunzo ya CHADEMA MSINGI yafanye kazi kama serikali kivuli kwenye mtaa wao kama mtaa wao unaongozwa na mwenyekiti aliyetokana na CCM au wa chama kingine tafauti na CHADEMA, kwani nina amini mafunzo hayo pia yatahusu umuhimu na ulazima wa mwanaCHADEMA kushiriki katika kujiletea maendeleo katika mtaa anaoishi na kusimamia rasilimali za mtaa zilizopo kwenye mtaa husika.


TANBIHI:
Lengo la makala hii ni kutaka uongozi wetu chini ya Mbowe kukiri makosa au kukanusha tuhuma na si lengo la makala hii kutuhumu na haipo hapa kutuhumu, kwani naamini makosa kwa vingozi au/na tuhuma kwa viongozi hupunguza na huchafua haiba njema ya chama kwa umma. Kukiri makosa au kukanusha tuhuma hung'arisha haiba ya chama kwa umma.


Naomba niwaambie wanaCCM wanao chochea kuni kwa haya yanayo tokea sasa ndani ya chama chetu, kwamba ninyi wanaCCM ni kama wale walio lukumila uji wa mgonjwa asubuhi kwa kudhani mgonjwa atakufa hatimaye kabla hata ya adhuhuri wakafa wenyewe. Nani asiyejua kuwa kiza kikizidi ndio usiku wayoyoma? Nani asiyejua kuwa "kesho" haijandikwa bali hutengenezwa na mja mwenyewe?

MUNGU IBARIKI CHADEMA NA VIONGOZI WAKE.

Njano5.
0784845394.
 

capito

JF-Expert Member
Nov 16, 2011
418
250
Jiandae kwa matusi na kuitwa msaliti maana umegusa pabaya, kuna watu wanaamini kuwa Mbowe na Dr. Slaa ni malaika. Hayo yote ambayo yamekuwa yakisemwa kuanzia kwa marehemu Chacha Wangwe ambae pia tuliabiwa ni msaliti mpaka yanayosemwa leo wenzetu hawayasikii au wameamua kutoyasikia na kuyaona ingawa yanaandikwa kila siku. Wa mwenye dhambi Zitto
 

Mjomba Mkude

JF-Expert Member
Nov 21, 2013
287
195
Naskia majina ya walioficha mabilioni uswizi yametoka leo.? Alafu yule jamaa Ludo alijipenyeza tena kwenye Kongamano la Vijana Chadema hivi ni kweli..?
 

Lunyungu

JF-Expert Member
Aug 7, 2006
8,863
1,250
Njano 5 unaweza kuanza kufanya kazi zingine za kukupatia kipato badala ya huu ujinga wako wa kila siku .Iacheni Chadema ifanye siasa .Kama hutaki acha na ondoka .
 

Dotto C. Rangimoto

Verified Member
Nov 22, 2012
1,993
2,000
Njano 5 unaweza kuanza kufanya kazi zingine za kukupatia kipato badala ya huu ujinga wako wa kila siku .Iacheni Chadema ifanye siasa .Kama hutaki acha na ondoka .

lengo la siasa za chama ni kuchukua dola,,,sasa chama kitafanya siasa hizo bila uongozi kukanusha tuhuma au kukiri na kupisha uongozi mwingine usiokuwa na makosa???? au kaka hujaielewa hoja ya makala hii???? au ulitaka niimbe usaliti tu ndio unielewe?
 

nrashu

Senior Member
Oct 4, 2010
144
170
Uongozi wa chadema hauminiki??? kweli? kama hauminiki mbona unazidi kuwa strong day after day? achana na propaganda njoo huku site useme hayo maneno yako. uone maendeleo ya chadema ni msingi. Vijana wamepita nyumbani kwangu wana tafuta kuandikisha wanachama. kumbuka kila jambo lazima liwe na chanzo.
Ushauri wangu kwako ni kama una tuhuma ambazo unaweza kuzidhibitisha fuata taratibu/katiba kuziwasilisha. Hao wote unaowazungumzia ni wanasiasa. Unawataja wabunge mahiri kwa kuibua hoja halafu wawe kwenye uongozi dhaifu!! Haileti mantiki ndugu njano5.
Kama Mwenyekiti anawapiga vita wapinzani wake na wapinzani wake ndicho mnachofanya. Wewe ni mwanachama wa kawaida, tena hai unahaki zako za kikatiba zitumie! acha kuendelea kutumia media ambayo haifanyi maamuzi.
 

gastone

JF-Expert Member
Apr 3, 2012
329
0
Njano 5 unaweza kuanza kufanya kazi zingine za kukupatia kipato badala ya huu ujinga wako wa kila siku .Iacheni Chadema ifanye siasa .Kama hutaki acha na ondoka .

wanachadema wa aina yako hawana tofauti na wafuasi wa kibwetere.....kwako mbowe na slaa ni malaika hivyo kamwe hawawezi kufanya makosa!! nakusihi uwe unafanya tafakuri japo kidogo tu ktk kujiridhisha kwa baadhi yamambo kuliko hivi sasa unavyofanya, kwa kifupi hukisadii chama kwa mawazo yako!!! tafakari......
 

Naytsory

JF-Expert Member
Nov 3, 2011
2,176
2,000
Kundi la wanaoitwa wasaliti hawakutoa hizo tuhuma kwa umma wala jukwaani ila zilinaswa kwa bahati mbaya / nzuri, sasa sielewi kusudi la njano kama ni jema au la! Lakini niaminivyo ikiwa tuhuma hizo wahusika hawakuthubutu kupanda nayo jukwaani wala kusemea kwenye vikao halali vya ndani na hakuna hata aliyethubutu kuwaita waandishi wa habari kuelezea hizo tuhuma, sasa mnataka Chadema wakanushe maneno ya mtaani? Nani yuko nyuma ya tuhuma hizo, nani kaibua na yuko tayari kuzitetea? Mtoa mada amesema sababu ya zzk kuvuliwa vyeo ni uenyekiti, usipotoshe Watanzania ukweli unafahamika, hao wengine nao walitaka uenyekiti? Panda na hizo tuhuma jukwaani au ita waandishi wa habari kawaeleze kama una uhakika nazo, uone kama hazitakanushwa.
 

gastone

JF-Expert Member
Apr 3, 2012
329
0
Hata wenyewe wameogopa kuhutubia hilo jukwaani na hata kwa waandishi wa habari, sasa nani akanushiwe?

kamanda, dr kitila ambaye alikuwa mjumbe kamati kuu amekiri kuuandaa na hata kuuhariri - aache kupotezea mbowe ajibu tuhuma na sio kulebo washindani wake kwa jina la usaliti/uhaini!
 

Dotto C. Rangimoto

Verified Member
Nov 22, 2012
1,993
2,000
Uongozi wa chadema hauminiki??? kweli? kama hauminiki mbona unazidi kuwa strong day after day? achana na propaganda njoo huku site useme hayo maneno yako. uone maendeleo ya chadema ni msingi. Vijana wamepita nyumbani kwangu wana tafuta kuandikisha wanachama. kumbuka kila jambo lazima liwe na chanzo.
Ushauri wangu kwako ni kama una tuhuma ambazo unaweza kuzidhibitisha fuata taratibu/katiba kuziwasilisha. Hao wote unaowazungumzia ni wanasiasa. Unawataja wabunge mahiri kwa kuibua hoja halafu wawe kwenye uongozi dhaifu!! Haileti mantiki ndugu njano5.
Kama Mwenyekiti anawapiga vita wapinzani wake na wapinzani wake ndicho mnachofanya. Wewe ni mwanachama wa kawaida, tena hai unahaki zako za kikatiba zitumie! acha kuendelea kutumia media ambayo haifanyi maamuzi.

Ungekuwa unawashauri hivi wanaomchafua au kumkosoa Zitto ingekuwa vizuri sana. Pamoja na hayo makala yangu haikosoi uongozi na wala haituhumu uongozi, bali makala yangu imenukuu tuhuma inazituhumiwa uongozi kutoka kwa wakosoaji wake, lengo la kuzinukuu hapa ni kutaka uongozi uzikanushe au ukiri makosa kwa lengo la kukisafisha chama.

Pia elewa tuhuma hiz ziko hadharani na watu wote wamezisoma kupitia waraka wa kitila na ule waraka wa chacha wangwe, sasa itakuwa haileti mantiki endapo mbowe akizikanusha ndani ya chama au ndani ya vikao vya chama ikiwa wapiga kura na wanachama wengine wasiongia kwenye vikao watakuwa hawajui kama zilikanushwa au wahusika walikiri makosa. nafikiri umenielewa.
 

Dotto C. Rangimoto

Verified Member
Nov 22, 2012
1,993
2,000
Kundi la wanaoitwa wasaliti hawakutoa hizo tuhuma kwa umma wala jukwaani ila zilinaswa kwa bahati mbaya / nzuri, sasa sielewi kusudi la njano kama ni jema au la! Lakini niaminivyo ikiwa tuhuma hizo wahusika hawakuthubutu kupanda nayo jukwaani wala kusemea kwenye vikao halali vya ndani na hakuna hata aliyethubutu kuwaita waandishi wa habari kuelezea hizo tuhuma, sasa mnataka Chadema wakanushe maneno ya mtaani? Nani yuko nyuma ya tuhuma hizo, nani kaibua na yuko tayari kuzitetea? Mtoa mada amesema sababu ya zzk kuvuliwa vyeo ni uenyekiti, usipotoshe Watanzania ukweli unafahamika, hao wengine nao walitaka uenyekiti? Panda na hizo tuhuma jukwaani au ita waandishi wa habari kawaeleze kama una uhakika nazo, uone kama hazitakanushwa.


kwenye press yao serina Kitila amekiri kundaa na kuhariri waraka ulijaa tuhuma chungu mno kwa uongozi wa mbowe, na mbaya zaidi kitila na mwenzie mwigamba hawajuti hata sasa kuandaa ule waraka, hii ina maanisha wana uhakika wa kile walichokituhumu, kwa muktadha huo ndio maana tunaomba mbowe akanushe au akikiri makosa.
 

Fede Masolwa

Verified Member
Oct 26, 2013
528
195
mpaka leo sielewangi kabisa makala zako wee kijana, ila unakuwa mlengo moja sana kuliko kubalnce mambo, samahn lakin...
 

chayowa1981

JF-Expert Member
Feb 3, 2012
219
225
Haaa! Hii thread, pamoja na uzuri wake watu wameamua kususia! Ama kweli ukilipenda boga basi na ua lake.....
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom