TASAF III yaboresha mafanikio afya, elimu

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
MPANGO wa Uhawilishaji wa fedha za ruzuku kwa kaya masikini, unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika awamu yake ya tatu umeonesha mafanikio kwa kuongeza uzito kwa watoto wachanga na mahudhurio shule za msingi wilayani hapa.

Mafanikio hayo yameonekana tangu mfuko huo ulipoanza kutoa ruzuku kwa kaya masikini Agosti, mwaka jana ambapo baadhi walengwa wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kupata huduma za afya hasa wajawazito na watoto wanaohudhuria kliniki kuonekana kuhamasika na afya zao kuboreka.

Muuguzi wa zahanati ya Gera iliyoko kata Gera, wilayani hapa, Yunis Kalimbo, alisema tangu Tasaf ianze kutekeleza mradi wa kutoa ruzuku kwa kaya masikini, kumekuwapo mabadiliko katika jamii.

Alisema miongoni mwa mabadiliko hayo ni kuongeza idadi ya wajawazito na watoto wanaohudhuria kliniki, jambo ambalo halikuwa kawaida hapo awali.

“Hali ya uzito kwa watoto imeongezeka, na mafanikio yanaonekana hata kwenye kadi zao za kliniki wengine wametoka rangi ya kijivu na kufika rangi ya kijani, hivyo hivyo na waliokuwa na rangi ya kijani nao wamesonga mbele....,”alisema Kalimbo.

Aidha, muuguzi huyo ametoa rai kwa walengwa wa mradi huo kutambua umuhimu wa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), ili kuweza kuchangia na kujipatia huduma ya afya kwa uhakika, na kuwezesha vituo na zahanati zilizoko maeneo ya vijijini kuwa na dawa muhimu zikazowasaidia kimatibabu.

Kuhusu mahudhurio kwa wanafunzi, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kashaka, Wilbert Justine alithibitisha kuwepo mahudhurio mazuri darasani tangu baadhi ya kaya masikini zilipoanza kupokea fedha za ruzuku kutoka Tasaf.
 
Back
Top Bottom