Tarime, Mara: Mmiliki wa mabasi ya Zacharia awapiga risasi maafisa wa Usalama wa Taifa, ashikiliwa na Polisi

Mmiliki wa Mabasi ya Zacharia, Peter Zacharia anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuwapiga risasi maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa wakiwa katika kutimiza majukumu yao.

Habari zaidi nitaweka hapa.

----

Tarime/Musoma. Taarifa za kutoweka kwa Mfanyabiashara maarufu na kada wa CCM, wilayani Tarime, Peter Zakaria zimezua taharuki kwa wakazi wa mji huo.

Zakaria, ni mmiliki wa mabasi ya Zakaria yanayofanya safari za Musoma, Tarime kwenda maeneo mbalimbali nchini.

Awali, leo Juni 30 zilizagaa taarifa kuwa mfanyabiashara huyo ametekwa na akapatikana kisha akapelekwa hospitali ya Wilaya ya Tarime kwa matibabu.

Baada ya taarifa hizo, wakazi wa mji huo walimiminika hospitalini hapo kwa nia ya kutaka kuthibitisha kama yupo au la lakini jeshi la polisi lilifyatua mabomu ya machozi kuwatawanya.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorius Luoga amesema hawezi kuzungumzia tukio hilo hadi Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya atakapotoa taarifa rasmi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi Tarime/Rorya, Heny Mwaibambe amesema mfanyabiashara huyo hakutekwa bali anashikiliwa kwa mahojiano lakini hakutaka kuzungumzia kwa undani suala hilo.

Kabla ya matukio haya, jana Juni 29 ilisikika milio ya risasi katika kituo cha mafuta cha mfanyabiashara huyo kilichopo Tarime mjini.

Tutaendelea kuwapa taarifa zaidi za tukio hili.

UPDATE;

Unaweza kusema taarifa za kutoweka kwa mfanyabiashara maarufu na kada wa CCM wilayani Tarime, Peter Zakaria zimetolewa ufafanuzi.

Leo Jumamosi Juni 30, 2018 Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima ametoa ufafanuzi kuhusu tajiri huyo ambaye ni mmiliki wa kampuni ya mabasi ya Zakaria kuwa hajatwekwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Malima amesema mfanyabiashara huyo amekamatwa na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa na kufikishwa kituo cha polisi mjini Tarime kwa ajili ya kuhojiwa, akituhumiwa kuwajeruhi kwa risasi maofisa wawili wa idara hiyo.

Amesema kabla ya tukio hilo, maofisa watano wa Usalama wa Taifa walifika katika kituo cha mafuta kinachomilikiwa na Zakaria kwa nia kujaza mafuta kwenye gari lao, “ wenzao wawili walishuka kwenye gari ghafla wakashambuliwa kwa risasi na Zakaria aliyekuwepo eneo hilo.”

"Baada ya wenzao kujeruhiwa kwa risasi, maofisa wengine walifanikiwa kumdhibiti Zakaria na kumtia mbaroni na kumkabidhi kwa polisi wanaoendelea kumhoji.”

Malima hakutaka kulizungumzia kwa undani tukio hilo lililotokea jana Juni 29, 2019 saa 2:30 usiku na kubainisha kuwa waliojeruhiwa wamelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Tarime huku mmoja akidaiwa kuwa katika hali mbaya.

Tangu jana usiku, mji wa Tarime umekumbwa na taharuki baada ya taarifa za mfanyabiashara huyo kudaiwa kutekwa kuzagaa mitaani.

UPDATES: II

Musoma/Tarime. Mmiliki wa kampuni ya mabasi ya Zakaria, Peter Zakaria anashikiliwa na polisi kwa mahojiano kwa tuhuma za kuwajeruhi kwa risasi watu wawili wanaodaiwa kuwa ni maofisa usalama wa Taifa.

Ingawa mazingira ya tukio hilo na nini maofisa hao walifuata kwenye kituo cha mafuta kinachomilikiwa na mfanyabiashara huyo hayajajulikana, mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alisema jana mjini Musoma kuwa, tukio hilo lilitokea saa mbili usiku wa Juni 29.

Malima alisema baada ya kuwajeruhi kwa risasi maofisa hao, Zakaria alidhibitiwa na maofisa wengine ambao walimfikisha Kituo cha Polisi mjini Tarime.

Akifafanua, mkuu huyo wa mkoa alisema kabla ya tukio hilo, maofisa usalama watano walifika katika kituo hicho cha mafuta kwa nia kujaza mafuta gari lao, ndipo wenzao wawili walishuka na ghafla kushambuliwa kwa risasi.

“Baada ya wenzao kujeruhiwa kwa risasi, maofisa wengine walifanikiwa kumdhibiti Zakaria na kumtia mbaroni na kumkabidhi kwa polisi wanaoendelea kumhoji,” alisema.

Kwa mujibu wa Malima, maofisa waliojeruhiwa wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime kwa matibabu huku mmoja akidaiwa kuwa katika hali mbaya.

Kuhusu tukio la polisi kutumia mabomu ya machozi kuutawaanya umati wa wananchi waliokusanyika eneo la hospitali hiyo, kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe alisema lililenga kurejesha utulivu baada ya wananchi kuhamaki wakitaka kuingia kumuona Zakaria kutokana na kuzagaa taarifa kuwa amejeruhiwa na kulazwa.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, mmoja wa wafanyakazi wa kituo cha mafuta, alidai Zakaria alifyatua risasi ili kujihami baada ya kuhisi kuwa watu walioshuka kwenye gari wakielekea ofisini kwake walikuwa majambazi.

“Kwa kawaida muda ule bosi huwa anapokea fedha za mauzo kutoka sehemu mbalimbali za biashara zake ikiwamo mabasi na vituo vya mafuta. Kitendo cha watu watano kufika na wawili kushuka kuelekea ofisini kwake kiliibua hofu ya usalama kutokana na matukio ya ujambazi, ndipo akaamua kujihami,” alisema mfanyakazi huyo.

Alisema baada ya wenzao kujeruhiwa, watu watatu waliobaki kwenye gari waliteremka na kumkamata Zakaria huku wakijitambulisha kuwa maofisa usalama, hali iliyozua mvutano walipotaka kuondoka naye kwa sababu wafanyakazi hawakuwa na uhakika iwapo walikuwa wema au wahalifu.

Mvutano huo ulisababisha milio ya risasi na watu hao kuondoka na Zakaria kwa nguvu huku wakisababisha hofu kuwa huenda mfanyabiashara huyo ametekwa, jambo lililoibua taharuki mjini Tarime.

UPDATE III

Tarime. Tukio la kukamatwa kwa mfanyabiashara wa Kanda ya Ziwa, Peter Zakaria limechukua sura mpya baada ya familia na walioshuhudia tukio hilo kutoa maelezo yanayokinzana na Mkuu wa Mkoa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mjini Tarime jana, baadhi ya walioshuhudia tukio hilo, akiwemo msemaji wa familia, Samuel Chamete na meneja wa kituo cha mafuta ambako tukio hilo lilitokea, Samuel Athumani walisema taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima inakinzana na ukweli.

“Nilikuwepo na nilishuhudia tukio kuanzia mwanzo hadi mwisho. Wale watu hawakuja kujaza mafuta kwa sababu kituo kilishafungwa tangu saa 12:00 jioni,” alisema Athumani.

Alisema, “Baada ya kuona gari lao limesimama muda mrefu bila wahusika kushuka, nilimtuma mfanyakazi kuwauliza iwapo wana shida tuwasaidie na wakajibu hawana shida.”

Meneja huyo alisema baada ya kumaliza kuangalia taarifa ya habari ya saa mbili usiku, bosi wake (Zakaria) aliaga ndipo ghafla watu wawili walitoka ndani ya gari na kumkamata ili kumuingiza kwa nguvu ndani ya gari lao.

Alisema Zakaria alipiga kelele akimwita kwa jina lake ili akamsaidie.

“Nilikimbilia eneo la tukio nikasikia sauti ya mpige risasi huyo. Hapo ndipo nikasikia milio ya risasi na ghafla nikawa nimeshakamatwa na kulazwa chini na watu hao,” alisema Athumani.

Alisema kuwasili kwa basi la kampuni ya Zakaria kutoka Mwanza kuliwaokoa kwa kuwa abiria, wafanyakazi na wananchi wengine wakiwamo waendesha pikipiki walikwenda kutoa msaada.

Samuel Chomete (65), msemaji wa familia alisema tukio hilo limeibua hofu kuhusu usalama na uhai wa Zakaria kutokana na jinsi lilivyotokea na taarifa zilizotolewa na viongozi na mamlaka za Serikali.

“Hatujui lengo la waliojaribu kumteka mdogo wangu Zakaria, lakini tunaamini hawakuwa na nia njema ndiyo maana walifika usiku bila taarifa kama wanaokwenda kukamata jambazi,” alisema Chomete.

Alisema licha ya kuwa mfanyabiashara maarufu na kada wa CCM, Zakaria pia ni mfadhili wa masuala mbalimbali ya chama na kijamii ambaye angeweza kuitwa na kwenda mwenyewe Polisi iwapo alihitajika kwa jambo lolote.

“Tunamshukuru Mungu aliweza kupambana na watu kujitokeza kumsaidia. Pengine naye angepotea kama wengine wanaoripotiwa kupotea katika siku za hivi karibuni,” alisema.

Alisema, “Tumeiachia Serikali usalama na maisha ya Zakaria, akidhurika hata kidole familia tutaelekeza lawama zote dhidi ya Serikali kwa sababu imethibitika wahusika ni watumishi wa Serikali.”

Akizungumza na Mwananchi jana, mkuu wa mkoa wa Mara, Malima alisisitiza usahihi wa taarifa yake kwa vyombo vya habari juzi akisema iwapo walioshuhudia wana kauli na maelezo kinzani, ukweli utajulikana suala hilo likifikishwa mahakamani.

“Nisikilize kwa makini, mimi ndiye mkuu wa mkoa, nimetoa taarifa juzi kwa waandishi wa habari na mwakilishi wa Mwananchi alikuwapo. Kama familia na mashuhuda wanasema tofauti mimi siwezi kusema lolote. Tusubiri suala hilo lifike mahakamani na yote yatajulikana huko,” alisema.

Malima alisema, “Siwezi kusema hivi jana halafu kesho niseme vingine na keshokutwa niseme tofauti. Mwananchi ni chombo makini mtaamua namna ya kushughulika na kauli kinzani mnayopata kutoka kwa mashuhuda na familia.”

Juzi akizungumzia tukio hilo mjini Musoma, Malima alikanusha taarifa zilizodai Zakaria alikuwa ametekwa akisema alikamatwa na maofisa usalama waliomdhibiti baada ya yeye kuwajeruhi kwa risasi wenzao wawili walioshuka kwenye gari walipofika kujaza mafuta kwenye kituo chake mjini Tarime.

Fedha zatoweka

Chomete aliyesema alionana na Zakaria muda mfupi kabla ya kuzungumza na Mwananchi, alisema familia haijui ziliko Sh16.3 milioni alizokuwa nazo Zakaria kwenye mkoba muda mfupi kabla ya kukamatwa.

Mwenyekiti wa mtaa wa Starehe mjini Tarime kilipo kituo cha mafuta tukio lilikotokea, Bashiri Selemani alisema,

“Kwa siku tatu mfululizo nililishuhudia gari lililohusika katika tukio likiwa limeegeshwa nyuma ya kituo cha mafuta cha Zakaria wakijifanya kulifanyia matengenezo, hii inaonyesha walikuwa kwenye mtego kufuatilia nyendo za Zakaria.”

Selemani pia ni diwani wa Nyamisangura na makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Tarime

Chanzo: Mwananchi

Habari zaidi, soma=>Mwenyekiti wa UVCCM aliyesema Peter Zacharia katekwa na watu wasiojulikana, apandishwa kizimbani
Hivi kesi hii imeishia wapi?
Watu wa Tarime tunaomba mtupe mrejesho juu ya suala hili ili tujue.
 
Back
Top Bottom