Taratibu za Utekelezaji wa Hukumu (Procedures on Execution of Decrees)

Apr 26, 2022
64
98
JINSI YA KUKAZIA HUKUMU:

Unaposhinda kesi ya madai, hautakiwi kuishia hapo tu na kutunza hukumu yako ndani. Kama unataka kufaidika na matunda ya hiyo hukumu inabidi uanze mchakato mwingine unaitwa utekelezaji wa hukumu, wengine wanaita KUKAZIA HUKUMU (kwa kiingereza au kisheria ni Execution).

Mfano umemshtaki mtu kwenye kesi ya madai na hukumu imetoka umeshinda kesi, labda Mahakama imekupa tuzo imeamuru ulipwe, je utafanyaje ili uweze kulipwa? Inabidi ufungue kesi ndogo ya pili uombe utekelezaji wa hiyo hukumu au tuzo. Sasa execution (kukazia hukumu) ni nini na unaombaje kukazia hukumu, hiyo ndio mada yetu leo.

Makala hii imeandaliwa na kuletwa kwako nami Zakaria Maseke - Advocate / Wakili
zakariamaseke@gmail.com
(0754575246)
(0746575259 - WhatsApp).

Lengo ni kutoa elimu ya sheria kwa jamii. Kwa kusoma makala hii utajifunza mambo yafuatayo:

1: Maana ya kukazia hukumu (utekelezaji wa hukumu/tuzo).
2: Tofauti kati ya hukumu (judgement) na tuzo (decree).
3: Sifa za Decree (tuzo) halali.
4: Jinsi ya kurekebisha tuzo (decree) iliyokosewa.
5: Wanaohusika kwenye kutekeleza hukumu/tuzo (parties).
6: Utafanyaje mdaiwa (judgement debtor) akifa kabla hujakazia hukumu?
7: Jinsi ya kukazia hukumu/tuzo (procedure)
8: Ukomo wa muda wa kukazia hukumu (time limit for execution).
9: Njia za kukazia hukumu (ways).
10: Jinsi ya kukazia hukumu dhidi ya serikali.
11: Jinsi ya kukazia hukumu kutoka nje ya nchi / execution of foreign judgements (utaratibu, nyaraka, masharti na vigezo).
12: Jinsi ya kupinga zoezi la kukazia hukumu au nafuu zilizopo kama hujaridhika na mchakato wa kukazia hukumu. N.k.

1: MAANA YA KUKAZIA HUKUMU:

Sheria ya Mwenendo wa kesi za Madai (ambayo wanasheria tunaiita kwa kifupi “CPC”, haitoi maana ya kukazia hukumu. Lakini kuna kesi mbalimbali ambapo Mahakama imefafanua maana ya kukazia hukumu.

Mfano, kwa mujibu wa kesi ya Re overseas Aviation Engineering (GB) ltd (1962), ni kesi ya Uingereza lakini imenukuliwa na kuungwa mkono (kuthibitishwa) na Mahakama ya Rufani ya Tanzania.

Kwenye hiyo kesi, Mahakama ilifafanua maana ya kukazia hukumu (execution), kwamba “ni mchakato wa kutekeleza hukumu (amri) ya Mahakama, na mchakato huu hukamilika pale tu anayedai akilipwa au akipata chochote alichotunukiwa kwenye hukumu (tuzo/decree).”

Kwa kiingereza nanukuu, execution “is the process for enforcing or giving effect to the judgement of the court; and it is completed when the judgement creditor gets the money or other things awarded to him by the judgement.”

Kwa hiyo kukazia hukumu (execution) ni mchakato wa kutekeleza uamuzi wa Mahakama kwa ajili ya manufaa ya aliyeshinda kesi. Bila kukazia hukumu uamuzi uliotolewa na Mahakama hautakuwa na maana yoyote.

ZINGATIA: Kukazia hukumu sio suala la kutekeleza hukumu kama hukumu yenyewe. Hatukazii hukumu (judgement) bali TUZO (DECREE) au AMRI ya Mahakama iliyotokana na hiyo hukumu yenyewe.

2: TOFAUTI KATI YA HUKUMU (JUDGEMENT) NA TUZO (DECREE):

Kuna tofauti kati ya hukumu (judgement) na DECREE (TUZO). Hizi ni nyaraka (documents) mbili tofauti kabisa, usije ukadhani ni kitu kimoja. La hasha! Ingawa unaweza kupatiwa vyote vikiwa vimebanwa au vimeambatanishwa pamoja lakini hiyo haina maana kuwa ni kitu kimoja.

Hukumu huwa ni ndefu sana, inasimulia kila kitu, kuanzia stori ya kilichotokea (mgogoro ulikuwa ni nini), submission (hoja) za pande zote mbili, jinsi Mawakili au Wadaawa (parties) walivyokuwa wanabishana, ushahidi uliotolewa, uchambuzi na uamuzi wa Mahakama.

Lakini DECREE (TUZO) ni dondoo (summary) tu ya vile ulivyoomba Mahakamani na kile ulichopewa. Decree ni kile ambacho Mahakama sasa imeridhia au imeamuru ulipwe baada ya kushinda kesi. Ni kurasa (page) moja tu au mbili sio kama hukumu. Na lazima baada ya hukumu kutolewa na decree (tuzo) itolewe. Kwa sababu bila decree (tuzo) hakuna namna utatekeleza hiyo hukumu.

Unachotakiwa kufanya baada ya kushinda kesi ni kuandika barua kuomba nakala ya hukumu na tuzo.

3: SIFA ZA DECREE (TUZO)

Ili tuzo itekelezeke kuna sifa au vigezo:

{i} Lazima iendane na hukumu husika. Iendane na hukumu kwa maana ya tarehe ya tuzo inatakiwa kufanana na tarehe ya kwenye hukumu, pia Hakimu au Jaji aliyesikiliza na kusaini hukumu, huyo huyo ndiye anatakiwa asaini na tuzo, na wahusika kwenye tuzo wawe ni wale wale walioko kwenye hukumu. Rejea Order XX(6) ya Sheria ya Mwenendo wa kesi za Madai (ambayo tunaiita kwa kifupi “CPC”.

Decree ikikosa hizo sifa itakuwa na dosari (defective decree). Na kama ina dosari (defective) basi haiwezi kutekelezwa.

4: JINSI YA KUREKEBISHA DECREE (TUZO) ILIYOKOSEWA:

Sio kila wakati decree inayotolewa iko sawa. Mfano kwenye hukumu Mahakama iliamua ulipwe million 100 ila kwenye decree wameandika million 10. Kama wewe ni Wakili na mteja wako amepewa decree (tuzo) ambayo imekosewa utafanyaje? Kama decree imekosewa usihofu. Solution ipo section 96 ya CPC. Ukisoma section 96 inatoa fursa ya kurekebisha decree yenye makosa.

Na mchakato wa kurekebisha decree iliyokosewa ni rahisi sana, unaandika tu barua unaambatanisha (una attach) na hiyo decree iliyokosewa, unampelekea Mheshimiwa Hakimu ili atumie mamlaka aliyo nayo chini ya kifungu cha 96 cha CPC kurekebisha hiyo decree.

5: PARTIES INVOLVED IN EXECUTION PROCEEDINGS (WAHUSIKA KWENYE KUTEKELEZA HUKUMU / PARTIES):

Kuna wahusika (parties) wakuu wawili kwenye kukazia hukumu:-

(i) Decree holder au judgement creditor (ndiye yule aliyeshinda kesi) yaani mdai na
(ii) Judgement debtor (mdaiwa).
Maana zake zipo section 3 ya CPC.

6: UTAFANYAJE MDAIWA (JUDGEMENT DEBTOR) AKIFA KABLA HAJAKULIPA?

Kama baada tu ya kusomewa hukumu na kupewa decree, mdaiwa atafariki, Je! mdai (decree holder) anaweza kuendelea kutekeleza hukumu wakati mdaiwa hayupo?

Ndiyo, decree holder (mdai) anaweza kuendelea kukazia hukumu dhidi ya msimamizi wa mirathi (legal representative) wa huyo mdaiwa aliyefariki. Kwa hiyo msimamizi wa mirathi anawajibika kukusanya na kulipa madeni ya marehemu. Urithi ni pamoja na madeni. Soma section 41(1) ya CPC.

Na itakuwaje kama hakuna msimamizi wa mirathi, mfano mtu amefariki bila kuacha wosia na familia haitaki kukaa kikao cha familia ipendekeze msimamizi wa mirathi? Je! ni lazima decree holder usubiri mpaka msimamizi wa mirathi ateuliwe??? (Ukikutana na changamoto kama hiyo ndio muda wa kutafuta Wakili).

Je, kama mali za marehemu hazitoshi kulipa madeni, mfano mali alizoacha marehemu ni million tano wakati deni ni million kumi (10), je unaweza kumdai msimamizi wa mirathi akulipe kutoka kwenye mali zake binafsi? Hapana! Kama mali za marehemu hazitoshi huwezi kudai kulipwa hadi kwenye mali binafsi za msimamizi wa mirathi. Sheria inasema uishie kumdai kwenye mali zilizoachwa na marehemu tu. Section 41(2).

NI MAHAKAMA IPI HUTEKELEZA HUKUMU (DECREE)?

Decree (tuzo) hutekelezwa na Mahakama iliyoitoa au wakati mwingine inaweza kuhamishwa kwenda kutekelezwa kwenye Mahakama nyingine. Section 33 ya CPC.

SABABU ZA KUHAMISHA DECREE
(TRANSFER OF DECREE):

Decree (hukumu) inaweza kuhamishwa kwenda kutekelezwa kwenye Mahakama nyingine kufuatia maombi ya decree holder au mahakama yenyewe kwa sababu zifuatazo (Section 34 CPC):

(i) Kama mhusika anayetakiwa akulipe anaishi au anafanyia biashara au kazi eneo lingine tofauti na ilipo Mahakama iliyotoa hukumu/tuzo. Section 34(1)(a).

(ii) Kama mali husika unayotaka kulipwa iko kwenye mipaka ya Mahakama nyingine tofauti na Mahakama iliyotoa hukumu. Mfano kesi imefunguliwa Mahakama ya Wilaya Musoma, lakini mali inayotakiwa kufanyiwa execution iko Kisutu, Mahakama ya Musoma inaweza kuhamisha hiyo decree kwenda Kisutu. Soma section 34(b) & (c) ya CPC.

(iii) Na sababu zingine ambazo Mahakama itaona zinafaa.

NB: Decree (tuzo) ikihamishwa sharti iende kwenye Mahakama yenye mamlaka. Kwa sababu kisheria, sio kila Mahakama inaweza kutekeleza hukumu. Mfano Tume ya Usuluhishi na uamuzi ya migogoro ya wafanyakazi (CMA), haina uwezo wa kutekeleza tuzo (award) zake yenyewe.

7: JINSI YA KUKAZIA HUKUMU (EXECUTION PROCEDURES):

Kwanza lazima yule aliyeshinda kesi (decree holder) afanye application (apeleke maombi) Mahakamani. Kwa lugha nyingine ufungue kesi nyingine ya pili. Maombi yanaweza kufanyika kwa njia ya mdomo au kwa njia ya maandishi (written form).

Utaomba kwa mdomo ikiwa tu madai yako yanahusu pesa (monetary decree) na huyo unayemdai hizo hela mpo naye Mahakamani wakati amri ya Mahakama ya kumtaka alipe inatolewa. Soma Order XXI rule 10(1), (1A) ya CPC. Hii ni kama njia mbadala (exception) tu.

Ila kwa ujumla (the general rule), maombi ya kukazia hukumu yanatakiwa kuwa kwenye maandishi. Kwenye maombi yako unatakiwa kutaja unaomba kukazia hukumu kupitia mtindo (njia) gani? Mfano kwa kushika na kuuza mali za mdaiwa, kukamata na kuzuia account za bank za mdaiwa, kumkamata na kumfunga mdaiwa jela n.k. Soma Order XXI rule 10(2) ya CPC.

Maombi ya maandishi yanafanyika kwa kujaza fomu maalum, FOMU NAMBA TANO (5) ambayo format au muundo wake unapatikana kwenye sheria inaitwa, Civil Procedure (Approved Forms) Notice, GN. No. 388 of 2017.

Zingatia: Kama sheria imetoa fomu maalum, huwezi kuja na muundo mwingine au fomu yako yoyote unayotaka, lazima utumie iliyowekwa na sheria.

Pamoja na hiyo fomu unatakiwa kuambatanisha na nakala ya TUZO ya Mahakama (DECREE) iliyothibitishwa (certified copy of the decree). Soma Order XXI rule 10(3). Ukipeleka maombi bila kuambatanisha tuzo ina maana unaiomba Mahakama kutekeleza hewa, maana hakuna decree. HAKIKISHA UNAAMBATANISHA TUZO, na sio tu tuzo (decree), ila CERTIFIED DECREE (iliyothibitishwa) na iendane na hukumu, na iwe imesainiwa na Hakimu. (Kama hukupata decree baada ya kesi andika barua kuomba nakala yake).

Document (nyaraka) zingine ni kama unaomba kutekeleza hukumu inayohusu mali za ardhi (landed property) au mali yoyote ambayo umiliki wake unaweza kuthibitishwa kupitia ushahidi wa nyaraka, nakala ya hiyo nyaraka lazima pia iambatanishwe.

Mfano kama ni ardhi ambayo iko surveyed (imepimwa) na imesajiliwa utaambatanisha nakala ya hati ya umiliki iliyothibitishwa (certified copy of certificate of title). Kama ni ardhi ambayo haijawa surveyed (haijapimwa) utaambatanisha sale agreement (hati ya mauziano). Au kama haukuinunua labda ulipewa utaambatanisha deed of gift.

Kama vyote hivyo havipo, tafuta mtathimini (qualified valuer) afanye tathmini, kisha uipeleke ile valuation report ipite kwa chief government valuer (mtathmini mkuu wa Serikali) aipitie na kuithibitisha alafu ambatanisha. (Inategemeana na property (mali husika) unaweza ukaweka hata kiapo/affidavit unaenda kwa kamishina wa viapo (Wakili) anakuandalia.

Baada ya hapo peleka maombi yako Mahakamani kama bado uko ndani ya muda na umpe nakala (copy) ya maombi upande wa pili. Mahakama itayapitia kuona kama umefata sheria. Kama kila kitu kiko sawa, Mahakama itatoa notice (taarifa) kwa upande wa pili, na baadae utapangiwa tarehe ya kusikiliza hayo maombi yako.

Kitu kingine, ili uweze kuomba kukazia hukumu inabidi muda wa kukata rufaa dhidi ya ile hukumu uwe umepita na hakuna rufaa yoyote iliyoletwa Mahakamani, LAKINI SIO LAZIMA. Maana HATA KAMA KUNA RUFAA, kwamba yule wa upande wa pili akiwa hajaridhika amekata rufaa, bado sheria inasema RUFAA HAIZUII KUENDELEA KUKAZIA HUKUMU, labda awe ameomba stay of execution (kusimamisha utekelezaji wa hukumu hadi rufaa yake iishe).

Ila kama mdaiwa hajaomba ukaziaji wa hukumu usimame wewe unaweza kuendelea kukazia hukumu yeye akiwa anaendelea kukata rufaa. Soma Order XXXIX Rule 5 ya CPC. Sasa angalizo: Akishinda rufaa yake, akarudi akakuta wewe huku umeshabomoa nyumba yake au umeshika mali zake umeuza n.k., ina maana tunasema decree imekuwa reversed (tuzo imepinduliwa), mdaiwa atarudi Mahakamani kuomba umrudishe alipokuwa mwanzo, ama umlipe fidia au urudishe mali zake. Hapo wewe ndo utageuka tena kuwa mdaiwa. (Sio busara kukimbilia kukazia hukumu mapema).

NANI ANAWEZA KUOMBA KUTEKELEZA HUKUMU (WHO MAY APPLY)?

Anayeruhusiwa kuomba kutekeleza hukumu ni yule aliyeshinda kesi (decree holder) au legal representative (muwakilishi wake kisheria kama msimamizi wa mirathi n.k.).

8: UKOMO WA MUDA WA KUKAZIA HUKUMU ( TIME LIMIT FOR EXECUTION):

Muda ni miaka kumi na miwili (12) tangu ile siku decree (tuzo) ilipotolewa. Soma section 39(1) ya CPC. Miaka 12 ikiisha utakua umechelewa, ila unaweza kuomba kuongezewa muda kwa kutoa sababu za msingi kuonesha ulikuwa wapi au kwa nini hukuomba kukazia hukumu ndani ya muda.

9: NJIA ZA KUKAZIA HUKUMU (MODES OF EXECUTION):

Kuna njia nyingi za kukazia hukumu;-

1: KUKAMATA NA KUKABIDHI (SEIZURE AND DELIVERY).

Inatumika zaidi kama unataka kukazia hukumu inayohusu vitu au mali (property, hasa mali inayohamishika (movable property). Utafanya application (maombi) kuiomba Mahakama itoe amri ya kukamata kitu au vitu vya mdaiwa na kukabidhi hicho kitu kwenye Mahakama iliyotoa amri ya kukamata au kumkabidhi aliyeshinda hiyo kesi. Kazi ya kukamata mali inafanywa na madalali wa Mahakama. (Kikubwa hakikisha hicho kitu au mali ni ya mdaiwa kweli). Soma section 42(a) ya CPC.

2: KUMKAMATA NA KUMFUNGA MDAIWA (ARREST AND DETENTION AS A CIVIL PRISONER):

Njia hii inatumika pale ambapo mdaiwa ana uwezo wa kulipa deni ila hataki kulipa makusudi. Utaratibu ni ule ule, unapeleka maombi (application) Mahakamani kuomba kukazia hukumu kwa kumkamata na kumuweka jela mdaiwa kama mfungwa wa madai. Soma section 44, 42(c) na Order XXI rule 35(2) ya CPC.

Watu wengi wanasema deni halimfungi mtu, lakini sio kweli. Kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa kesi za Madai (CPC) kuna mazingira ambapo kutolipa deni la mtu kunaweza kufanya ukafungwa. Na mara nyingi inatumika mwishoni kabisa njia zingine zote zikishindikana.

VIGEZO NA MASHARTI KABLA YA KUMFUNGA MTU JELA KWA KOSA LA MADAI YA HELA:

(i) Kabla ya kumkamata na kumfunga mdaiwa, sheria inasema inatakiwa Mahakama itoe notice (taarifa) kwa mdaiwa kumuita aje aieleze Mahakama anafikri kwa nini asikamatwe na kufungwa jela? Kama akishindwa kuja utaomba Mahakama itoe hati ya kumkamata (arrest warrant) na sheria imetaja muda gani anatakiwa kukamatwa. Hatakiwi kukamatwa usiku (kabla hakujakucha au baada ya jua kuzama) na hutakiwi kuvunja mlango labda kama mdaiwa yumo ndani na hataki kufungua kwa makusudi. Soma section 44(1)(a) & (b) ya CPC.

Kama mdaiwa baada ya kupewa notice (taarifa) atakuja lakini akashindwa kutoa sababu za msingi kuiridhisha Mahakama, basi Mahakama itaamuru aende jela.

(ii) Pili, huyo mtu unayemdai lazima awe na uwezo wa kulipa lakini hataki kukulipa kwa makusudi. Huu utaratibu mara nyingi unatumika dhidi ya watu ambao wako vizuri, wana hela ila wana viburi (ni watata), wana uwezo wa kukulipa ila hawataki kutii sheria mpaka walazimishwe. Ila ukiwa maskini, hauna kitu, sheria inasema utaachiwa huru. Hivyo umaskini ni defense nzuri kwa mtu anayedaiwa. Soma.Order XXI rule 39(1) ya CPC.

Kama mtu unayemdai hana cha kukulipa hiyo inakuwa “tuzo hewa (empty decree)”, kumaanisha kwamba una decree (tuzo) ambayo huwezi kuitekeleza. Mahakama imesema ulipwe million lakini huyo mtu hana hiyo million.

NB: Kuwa na madeni mengi ya kulipa sio defense, usije ukatumia defense ya umaskini kwa kisingizio kwamba una madeni mengine unayotakiwa kulipa, sasa unaogopa ukilipa yote utaishiwa.

(iii) Sharti lingine, ni lazima wewe mdai uwe na uwezo wa kulipa subsistence allowance (posho) ambayo itatumika kumlisha huyo mtu wakati anatumikia kifungo gerezani. Na hiyo hela unailipa mapema kabla ya tarehe moja ya kila mwezi, ikifika hatua ukashindwa kulipa anaachiwa huru. Soma section 46(1)(iv) na Order XXI rule 38 ya CPC.

Pia, hiyo hela unayolipa kumlisha akiwa gerezani, itajumlishwa kwenye gharama za kesi na litakuwa deni, lakini haitahesabika wakati wa kukazia hukumu, isije mwisho akashindwa tena kulipa ukampeleka jela tena. Hiyo itabaki deni tu ambalo atakuja kukulipa kama gharama ya kesi (costs) lakini hairuhusiwi kumkamata tena kwa madai ya hela uliyotumia kumlisha. Order XXI rule 38(5).

Kabla ya kumfunga mdaiwa, taarifa itapelekwa jela ili wajue status (hadhi) ya huyo mtu ili wakwambie vitu gani muhimu kuwa navyo. Kwa sababu mfungwa wa madai hatakiwa kula chakula kama cha wafungwa wengine waliofungwa kwa makosa ya jinai kama vile wizi, ubakaji n.k., wewe uliyeomba mtu afungwe kama mfungwa wa madai unawajibika kumlisha vizuri kama ambavyo huwa anakula akiwa nyumbani kwake. Order XXI rule 38(2) ya CPC.

Akikwambia nyumbani kwake huwa anasoma gazeti kila siku itabidi umnunulie. Kama hali maharage anakula samaki tu, itabidi umnunulie. Hiyo ndio sababu jela wanataka wajue hadhi ya maisha ya huyo mtu ili wakwambie mnyumbuliko / breakdown ya hizo gharama ulipe.

Kwa sababu lengo la aina hii ya utekelezaji wa hukumu (kwa kumfunga mdaiwa jela) sio adhabu, isipokuwa ni kumlazimisha mdaiwa alipe. Kwa hiyo huwezi kumpeleka jela akaishi maishi ya mateso.

Muda wa kufungwa itategemeana, ila mdaiwa anaweza kufungwa hadi miezi sita. Pia mdai unaweza kuomba mdaiwa aachiwe huru ila kuachiwa huru haimaanishi deni limekufa, na kuna uwezekano wa kukamatwa tena. Soma section 46(1), (2) & (3) ya CPC.

Kama kesi ni madai ya hela, mdaiwa akilipa kiasi anachodaiwa na gharama za aliyeenda kumkamata (arresting officer), ataachiwa huru muda huo huo hata kama amekaa siku moja tu gerezani. Section 46(1)(b)(i) ya CPC.

Kwa uelewa zaidi kuhusu mfungwa wa madai, pitia sections 44 - 47 za CPC na Order XXI rule 35 - 39.

3: KUKAMATA NA KUUZA MALI YA MDAIWA (ATTACHMENT AND SALE):

Njia hii nayo inatumika pia kukazia hukumu zinazohusu madai ya hela (monetary decrees) pale ambapo mdaiwa hana hela ya kulipa ila ana mali ambayo ina thamani sawa na deni analodaiwa. Section 42(b), Order XXI rule 40 hadi 100.

Utaratibu ni ule ule, unapeleka maombi (application) Mahakamani kuomba kukazia hukumu kwa kukamata na kuuza mali ya mdaiwa (attachment and sale) ili mali zake ziuzwe kinachopatikana kitumike kulipa deni.

Kama mali (property) iliyokamatwa na kuuzwa haitoshi kumaliza deni, mdai anaweza tena kurudi Mahakamani kuomba kukamata na kuuza mali nyingine ya mdaiwa, mpaka pale deni litakapolipwa lote. Kwa hiyo ni wajibu wako, wewe mdai kufanya uchunguzi ujue mdaiwa anamiliki mali gani. Na ili usisumbuke ni vizuri ukamate mali ambayo ikiuzwa mara moja inamaliza deni lote.

Na sheria inatoa utaratibu wa kuuza, hauuzi tu unavyotaka na unatumia madalali wa Mahakama (court brokers) sio wewe mwenyewe na taarifa lazima irudishwe Mahakamani ambako amri ya kukamata ilitoka. Na kama baada ya kuuza na kulipa deni kuna kiasi kimebaki, inatakiwa mdai apewe. Hutakiwi kunufainika kwa kuchukua zaidi ya kiasi unachodai.

Na mali ya mdaiwa inatakiwa kuuzwa kwenye mnada wa hadhara (public auction). Hela inayopatikana itaingizwa kwenye akaunti ya Mahakama ili baadae wamlipe mdai au inaweza kuingizwa moja kwa moja kwenye akaunti ya mdai kutegemeana na amri ya Mahakama.

ZINGATIA: Sio kila mali inaweza kukamatwa na kuuzwa, kuna baadhi ya mali sheria imekataza kuzikamata. Ukitaka kujua ni zipi, rejea section 48 ya CPC. Mfano mali ya ndoa n.k.

4: KUTOLEWA NDANI NA KUBOMOA (EVICTION AND DEMOLITION):

Hii inahusu mali zisizohamishika kama vile ardhi (nyumba). Mfano umemshtaki mu kwa kuvamia eneo lako na umeshinda kesi, sasa unataka aondoke akuachie eneo lako (vacant possession) lakini yeye hataki kutoka, USITUMIE NGUVU KUMUONDOA, utaratibu ni ule ule, utapeleka maombi (application) Mahakamani kuomba huyo mtu afukuzwe aondoke kwenye eneo lako ili wewe uingie pale kama mmiliki halali.

ZINGATIA: Hairuhusiwi kubomoa au kumuondoa mtu ndani USIKU au weekend (siku ambayo sio ya kazi).

5: KUOMBA MKATABA UTEKELEZWE KAMA MLIVYOKUBALIANA (SPECIFIC PERFORMANCE):

Hii pia ni njia nyingine ya kutekeleza au kukazia hukumu kwenye kesi zinazohusu mikataba. Kama wewe hutaki kulipwa fidia ila unataka mkataba utekelezwe kama mlivyokubaliana awali, utaomba specific performance.

Mfano, umemshtaki mtu kwa kuvunja mkataba umeshinda kesi, lakini bado anasita sita kutekeleza wajibu wake kwenye mkataba, unaweza kutekeleza hiyo hukumu kwa kuomba alazimishwe kutekeleza wajibu wake kama mlivyokubaliana.

6: GARNISHEE ORDER (GARNISHMENT):

Hapa, una attach (kukamata) deni au fedha za mdaiwa huko huko ziliko, kama unajua mdaiwa ana hela sehemu fulani (iwe ni bank au kwa mtu fulani), basi utapeleka maombi (application) Mahakamani kuomba Mahakama imwamuru huyo mwenye hizo hela azishikilie na baadae azilete Mahakamani ili ulipwe wewe. Kwenye maombi (application) yako unatakiwa utaje account number ya mdaiwa na majina ya mmiliki wa akaunti.

Aina hii ya utekelezaji wa hukumu haipo kwenye sheria za Tanzania ila imetokana na maamuzi ya Mahakama za Uingereza (common law), na sheria za Tanzania zinaruhusu matumizi ya common law kutokana na historia ya nchi yetu. (Soma sheria inaitwa the Judicature and Application of Laws Act [CAP. 358] kwa kifupi tunaiita “JALA” kifungu cha 2(3)).

Njia hii inatumika hasa kukazia hukumu zinazohusu pesa (monetary decrees), haitumiki kukazia hukumu zinazohusu mali (property) zingine ambazo sio fedha.

Hapa kunakuwa na watu watatu (three parties):

(i) Decree holder (anayedai hela baada ya kushinda kesi).
(ii) Garnishee (mtu wa katikati (third party) ambaye anashikilia hela za mdaiwa, na
(iii) Mdaiwa mwenyewe (anayetakiwa kulipa).

Sasa kuna hatua mbili:

1: Hatua ya kwanza inaitwa GARNISHEE ORDER NISI. Kwenye hii hatua, baada ya mdai kupeleka maombi (application) Mahakamani, Mahakama itaamuru yule garnishee - mtu wa tatu (third party) ambaye anashikilia hela za mdaiwa, amzuie mdaiwa asitoe hizo hela kwenye account au asimlipe mdaiwa hizo hela, ili kumlinda huyu mtu anayemdai.

ZINGATIA: Hiyo amri haitolewi moja kwa moja kwa mdaiwa ila inatolewa kwa third party (garnishee), yule mwenye hela za mdaiwa, mfano meneja wa benki au creditor (mkopeshaji). Na, zuio sio la kutoweka hela bali kutokutoa au kutopewa hela. Kwa sababu huyu mdaiwa anajua ana deni na anajua kuna siku hizo hela zinaweza zikatolewa akalipwa mdai, kama ni Bank anaweza kwenda akazitoa zote.

Lengo ni kumzuia mdaiwa asichukue kiasi fulani cha hela ambacho kitamuathiri mdai. Mfano kama ni Bank, utakuwa unaruhusiwa tu kwenda kuweka hela ila huruhusiwi kutoa, na kama ukitaka kutoa utawekewa kikomo (kiwango) cha kiasi unachoweza kutoa ili usiathiri kiwango unachotakiwa kulipa kwenye hukumu.

Kumbuka kwenye hatua ya kwanza wanazuia zile hela tu, lakini bado kunakuwa hakuna amri ya Mahakama inayomtaka third party (anayeshikilia hizo hela) kuzitoa kwenye akaunti ya mdaiwa na kulipa deni. Bali, amri iliyotolewa hapo inahusu tu kumzuia mdaiwa asichukue hela. (Usipofanya hivyo anaweza kuzitoa zote, mwisho hata ile amri ya pili inayofata ya kulipa itakuwa haina maana).

Baada ya hapo Mahakama itatoa notice (taarifa) kwa yule mwenye hizo hela (garnishee), aje aieleze Mahakama kwa nini hukumu isitekelezwe kwa yeye kutoa kiasi fulani cha hela za mdaiwa alizo nazo na kumlipa mdai? Na mdaiwa (judgement debtor) atapewa notice pia.

Hapo sasa huyo creditor au bank inaweza kujitetea labda wakasema wao hawana au hawadaiwi hela na judgement debtor. Ndio maana ukiamua kutumia hii njia, hakikisha umefanya utafiti, ujue mdaiwa ana akaunti yenye hela kwenye taasisi fulani ya fedha au ana deni mahali fulani, na kwamba hiyo hela au hilo deni linatosha kukulipa?

Garnishee akisema hana hela za mdaiwa, basi inakuwa ni swali au issue ambayo Mahakama itakaa kuijadili na kuja na uamuzi.

2: Hatua ya pili, kama yule anayedaiwa akija akishindwa kutoa sababu za msingi kuishawishi Mahakama kwa nini ile decree isitekelezwe kama ambavyo decree holder (mdai) ameomba, basi hatua ya pili ni amri nyingine kamilifu inayoitwa “GARNISHEE ORDER ABSOLUTE” itatolewa na Mahakama kumuamuru third party (yule mwenye hizo hela za mdaiwa mfano bank) kutoa kiasi fulani cha hela na kuzilipa ama kwenye akaunti ya Mahakama (ili baadae mdai alipwe) au kuzilipa moja kwa moja kwenye account ya mdai (decree holder).

Zingatia: Wakati unaomba kukazia hukumu unatakiwa kusema unataka kukazia hukumu kupitia njia gani? Na ukitumia njia moja kati ya hizo isipofanikiwa kumaliza deni lako, unaruhusiwa tena kuomba kutumia njia nyingine itakayokusaidia kumaliza deni, mpaka utekelezaji wa hukumu ukamilike.

UTEKELEZAJI WA HUKUMU DHIDI YA SERIKALI (EXECUTION AGAINST THE GOVERNMENT)

Ukishinda kesi ya madai dhidi ya Serikali , je unaweza kuitekeleza hiyo hukumu? Naam, unaweza. Kuhusu utaratibu wa kukazia hukumu dhidi ya serikali soma Order XXI rule 2A ambayo inatuelekeza kwenye kifungu cha 15 cha sheria ya mashauri dhidi ya serikali (the Government Proceedings Act).

Ukisoma hicho kifungu cha 15 cha hiyo sheria, utagundua utekelezaji wa hukumu dhidi ya Serikali ni rahisi sana ukilinganisha na decree zingine. Kwa sababu hapa hakuna fomu maalum.

Unaandika barua tu kwenda Mahakamani unaambatanisha na tuzo (certified decree) alafu Mahakama itatoa hati ya malipo (certificate of payment). Alafu hiyo certificate of payment na decree itaenda kwa Katibu Mkuu wa Hazina (the Permanent Secretary of the treasury).

Zingatia sheria inayotumika kwenye utekelezaji wa hukumu dhidi ya Serikali sio CPC bali ni sheria ya mashauri dhidi ya serikali (the Government Proceedings Act). CPC inakupa mwongozo tu wa sheria gani urejee ili kujua procedures (utaratibu).
(Sasa swali ni je Serikali ikikataa kukulipa utafanyaje?) Jibu ni mtafute Wakili akushauri.

UTEKELEZAJI WA HUKUMU KUTOKA NJE YA NCHI (EXECUTION OF FOREIGN JUDGEMENTS OR RECOGNITION AND ENFORCEMENT OF FOREIGN JUDGEMENTS IN TANZANIA):

How to enforce foreign judgements in Tanzania (jinsi ya kutekeleza hukumu ya nje ya nchi hapa Tanzania). Je inawezekana kutekeleza hukumu ya kigeni nchini Tanzania? Ndio inawezekana.

Kama decree imetolewa na Mahakama ya nje ya nchi mfano Kenya na unataka kuitekeleza (execute) nchini Tanzania, labda Mdaiwa yuko Tanzania na mali zake ziko Tanzania, utaratibu upo kwenye Sheria inaitwa Reciprocal Enforcement of Foreign Judgements Act, CAP 8.

MAANA YA HUKUMU YA KIGENI (MEANING OF A FOREIGN JUDGEMENT):

Hukumu ya kigeni (foreign judgement) kwa kifupi ni hukumu ambayo umeshinda kwenye Mahakama ya nje ya nchi sasa unataka kuitekeleza hiyo hukumu kwenye nchi nyingine. Mfano kesi ilifanyika Kenya, ila mali za mdaiwa zipo nchi nyingine au mdaiwa anaishi na kufanya biashara nchi nyingine n.k. sasa unataka uende hiyo nchi nyingine kukazia (kutekeleza) hukumu.

Kila nchi ina utaratibu wake. Kwa Tanzania, kama kesi yenu ilisikilizwa nje ya nchi na uamuzi ukatoka umeshinda kesi, mfano unatakiwa ulipwe, ukitaka kuitekeleza hiyo hukumu hapa Tanzania lazima ufuate masharti ya kwenye sheria husika inaitwa the ‘Reciprocal Enforcement of Foreign Judgements Act,’ [CAP. 8 R.E. 2019] na Rules zake.

VIGEZO NA MASHARTI ILI HUKUMU ILIYOTOLEWA NA MAHAKAMA YA NJE YA NCHI IWEZE KUTEKELEZWA HAPA TANZANIA (CONDITIONS TO ENFORCE FOREIGN JUDGEMENT IN TANZANIA).

(i) Kwanza, lazima kuwepo na Reciprocal arrangements kati ya hiyo nchi na Tanzania. (Makubaliano ya nchi zote kutambua na kutekeleza hukumu iliyotolewa na Mahakama ya nchi nyingine).

Reciprocal arrangements ni makubaliano kati ya hiyo nchi na Tanzania ya kutambua na kutekeleza hukumu ya mwenzio. Utajuaje nchi ambazo ziko kwenye hayo makubaliano na Tanzania? Zamami zilikuwa kwenye jedwali la hiyo sheria (Reciprocal Enforcement of Foreign Judgements Act, CAP 8).

(ii) Pili, Hukumu yenyewe iwe ilitolewa na Mahakama yenye mamlaka kisheria. (the original court must have had jurisdiction). Ili hiyo hukumu iweze kutekelezwa Tanzania, ni lazima iwe imetolewa na Mahakama yenye mamlaka kisheria huko ilikotoka. Soma section 6(1)(a)(ii) of the Enforcement of Foreign Judgements Act,’ [CAP. 8 R.E. 2019]

(ii) Pili, uamuzi uwe umefika tamati (the decision must be final and conclusive). Uamuzi uwe umetolewa na kesi imefika mwisho (to its finality), kwa maana kwamba hakuna jambo linalosubiria tena kusikilizwa (au liko pending) Mahakamani. Soma Section 3(2) ya sheria hiyo hiyo.

(iii) Tatu, hiyo hukumu isiwe kinyume na mila, desturi, maadili na sheria za Tanzania (should not be contrary to public policy, laws and morality of Tanzania). Section 6(1)(a)(i) and (v).

(iv) Usiwe umeshinda kesi kwa ulaghai (should not have been obtained by fraud). Section 6(1)(a)(iv). Hiyo decree (hukumu) isiwe imepatikana kwa udanganyifu.

(v) Isiwe Res Judicata (kesi ambayo ni marudio ilishawahi kusikilizwa na hukumu ikatoka). Section 6(1)(b).

(vi) Kusiwepo na viashiria kwamba mdaiwa hakupata haki ya kusikilizwa (judgement debtor should have been accorded right to be heard in the original country). Section 6(1)(a)(iii).

(vii) Iwe haihusiani na madai ya tozo kama kodi au faini, penalty n.k. Section 3(2)(b).

(viii) Usiwe umeshalipwa kila kitu huko nje (it has not been wholly satisfied). Section 4(1)(a).

(ix) Ina uwezekano wa kutekelezwa kwenye nchi ilipotoka (it could be enforced by execution in the country of original court). Section 4(1)(b).

(x) Hukumu ya kigeni inatakiwa kusajiliwa Mahakama Kuu (foreign judgement must be registered in the High Court of Tanzania).

UTARATIBU (PROCEDURES) NA DOCUMENTS.

Utaratibu (procedure) ni kwamba, utaomba Mahakama itambue hiyo hukumu (recognition), baada ya hapo unaendelea na kuitekeleza hiyo hukumu kama hukumu nyingine yoyote. Judgement creditor (yule aliyeshinda kesi huko nje ya nchi) anatakiwa kufungua Mahakama Kuu Maombi ya kusajili ile hukumu iliyotolewa nje ya Nchi. Maombi yafanyike ndani ya miaka sita (6) tangu siku ya hukumu. Soma section 4(1) ya the Reciprocal Enforcement of Foreign Judgements Act, [CAP. 8 R.E. 2019].

Kwenye maombi yako, unatakiwa pia kuambatanisha nakala ya hukumu husika. Kama hiyo hukumu haiko kwa lugha ya kiingereza au iko katika lugha nyingine tofauti na Kiingereza, basi kuwepo na tafsri yake kwa kiingereza. Pia hukumu hiyo iwe imethibitishwa (certified) huko ulikotoka.

EFFECTS OF REGISTRATION:

Hukumu ya kigeni ikishakuwa registered (ikisajiliwa) inakuwa na nguvu kisheria kama hukumu zingine za hapa Tanzania na unaweza kwenda Mahakamani kukazia hukumu (kudai ulipwe) kwa kutumia utaratibu wa kawaida kisheria. Section 4(2)(a).

REMEDIES (NAFUU) ZILIZOPO WAKATI WA KUKAZIA HUKUMU:

Kama hujaridhika na maamuzi yaliyotoka yakielekeza utekelezaji wa hukumu kufanyika kwa namna fulani, labda accounts zako za bank zimezuiwa, au wanataka kuuza mali yako wakati wewe hauhusiki na kesi au wameuza mali yako kimakosa au bila kufuata taratibu za minada n.k. kuna njia nyingi za kupinga (ku- challenge) mchakato wa kukazia hukumu.

(i): OBJECTION PROCEEDINGS:

Ni nafuu aliyo nayo mtu ambae hakuwa sehemu ya kesi (third party), lakini mali yake imekamatwa inataka kuuzwa ili kukazia hukumu.

Kama unaona una maslahi kwenye mali inayotaka kubebwa na aliyeshindwa kesi na unaona kitendo hicho kitakuathiri, basi unaweza kufungua kesi (objection proceedings) kupinga mali hiyo isikamatwe au kuuzwa. Hakikisha unafungua kesi ya kupinga mali kukamatwa kabla mchakato wa kukazia hukumu haujaisha. Ukiweka pingamizi, Mahakama itaahirisha hiyo mali isiuzwe kwanza hadi pingamizi lako liishe kusikilizwa.

Nyaraka (documents) zinazotumika kufungua hiyo kesi au hayo maombi (objection proceedings) ni Chamber summons na affidavit. Kifungu ni Order XXI rule 57 ya Sheria ya Mwenendo wa kesi za Madai (ambayo wanasheria tunaiita kwa kifupi “CPC.”

Kwenye hiyo kesi au maombi yako ya kupinga (objection proceedings), wewe ambae hukuwa sehemu ya kesi utakuwa muombaji (applicant), ukiwashtaki huyo ambaye ameshinda kesi (decree holder) anayetaka kukamata mali yako na huyo mdaiwa wake (judgement debtor) aliyeshindwa kesi, ndo watakuwa wajibu maombi (respondents).

NB: Zingatia mambo yafuatayo:

(i) Uwe una haki au maslahi (CLAIM OF RIGHT) kwenye hiyo mali inayotaka kuuzwa. Kama utafungua tu kesi kwenye mali ambayo huathiriki chochote hata ikiuzwa, ili kutaka tu kuchelewesha mchakato wa kukazia hukumu, Mahakama haitahangaika na wewe. Kama huna haki au maslahi kwenye hiyo mali, wewe utakuwa mere busy body (mtu anayezurura zurura tu Mahakamani). Maombi yako yatatupiliwa mbali (pengine utalipa na gharama juu). Soma Order XXI rule 57 ya CPC.

(ii) Maombi yafanyike kabla mchakato wa utekelezaji hukumu haujaisha. Sio wameshauza ndo wewe unaenda kupinga. Utakuwa unapinga kitu ambacho hakipo.

Kama usipofanikiwa, ikiwa maombi yako yatakataliwa na Mahakama, nafuu iliyopo tena ni kurudi kufungua kesi mpya. Washtakiwa (defendants) watakua ni wale wale decree holder (aliyeshinda kesi) na yule aliyeshindwa (mdaiwa).

(2): STAY OF EXECUTION:

Hii ni nafuu kwa mtu aliyeshindwa kesi mfano umeambiwa ulipe, lakini hujaridhika, unataka kukata rufaa (appeal) au kuomba revision kwenye Mahakama ya juu.

Kwa sababu ukishindwa kesi, ukaambiwa ulipe, hayo maamuzi yanayosema ulipe unaweza kuyakatia rufaa au kuomba revision n.k. (thus, the decision which is subject of execution is subject to appeal, revision or even review).

Utaratibu ni kwamba, unapeleka maombi Mahakamani kuomba mchakato wa kukazia hukumu usimamishwe kwanza mpaka rufaa yako iishe kusikilizwa. Nyaraka (documents) ni chamber summons na affidavit. Kifungu mojawapo ni Order XXI rule 24 ya CPC.

Usipofanya hivyo (usipoomba stay of execution), utakata rufaa lakini huku aliyeshinda kesi naye ataendelea kukazia hukumu kama kawaida. Lakini kama utashinda rufaa sio kuwa haitakuwa na maana yoyote, ingawa mali utakuta pengine imeshauzwa au nyumba imevunjwa, lakini una haki ya kuomba akurudishe ulipokua mwanzo, na hapo ndipo tuzo inapinduliwa (decree is reversed) mdai anageuka mdaiwa. Ndo maana mwanzo nilisema usikimbilie kuuza au kubomoa nyumba ya mtu haraka, kibao kinaweza kukugeukia.

Lakini kiumjula mdaiwa ili uwe salama, hata kama umetoa taarifa (notice) kuwa unataka kukata rufaa, omba pia kusimamisha mchakato wa kukazia hukumu (stay of execution), kwa sababu rufaa huwa haisimamishi automatic mchakato wa kukazia hukumu kama wewe haujaomba. (Appeal is not an automatic bar to execution). Soma Order XXXIX rule 5. Ukikata rufaa peke yake utakuja kumaliza unakuta nyumba imeuzwa au imebomolewa, kuja kurudishwa ulipokuwa inaweza isiwe rahisi.

Zingatia:

(i) Maombi yatumwe kwa wakati, muda wowote kabla mchakato wa kukazia hukumu haujaisha. Sio hukumu imeshatekelezwa, mali imeuzwa, wewe ndo unaenda kuomba kusimamisha kukazia hukumu (stay of execution).

(ii) Pia, huwezi kuomba hukumu isimame kutekelezwa kama hujaanza kuchukua hatua yoyote kukata rufaa au kuomba revision. Mfano onesha hata notice of appeal n.k.

(iii) Ili mchakato wa kukazia hukumu usimamishwe lazima uombe. Usipoomba hata kama umekata rufaa wataendelea tu kuuza. Siku unashinda rufaa unakuta execution imeshafanyika. Na hiyo execution itakua sahihi kabisa kwa sababu wewe haukuomba mchakato usimamishwe.

Kuna wengine wanaitumia kama gia au mchezo wa kuchelewesha kulipa madeni. Sio kwamba mtu hataki kulipa, ila ameona hali yake ya kifedha sio nzuri, anahitaji muda zaidi, anaamua kufungua tu rufaa isiyo na mashiko ili kupoteza muda aendelee kujiimarisha kiuchumi. Wakati uamuzi unakaribia kutoka anaiondoa anasema niko tayari kulipa. Sikufundishi kufanya hivyo, ila haya mambo yanafanyika. Sasa na Mahakama haikubali kirahisi rahisi kusimamisha zoezi la kukazia hukumu - kuna masharti. (Ukitaka kuyajua tafuta Wakili).

3: KUFUNGUA KESI:

Hii ni njia nyingine ikiwa hujaridhika na uamuzi kuhusu utekelezaji wa hukumu. Na hii inatumika baada ya kuwa mchakato wa kukazia hukumu umekamilika. Kama execution imeisha alafu wewe umeathirika kwa namna moja ama nyingine, fungua kesi ya madai. Anayefungua kesi ni yule mwenye haki au maslahi.

4: RUFAA (APPEAL):
Rufaa ni nafuu nyingine ukishindwa kesi na kuambiwa ulipe. Mfano execution imefanyika Mahakama Kuu, unaweza kwenda Mahakama ya Rufaa kwa ruhusa ya Mahakama. (Section 5(2)(c)).

5: KUTENGUA UUZAJI (SET ASIDE SALE):

Kama amri ya Mahakama ilikuwa inahusu kuuza mali lakini ilitolewa isivyo sahihi (improperly issued), unaweza kuomba kuitengua. Zingatia: Unaomba kutengua kama kulikuwa na order (amri) ya kuuza wakati wa execution, vinginevyo huwezi kuomba ku set aside. Pili, kama unaamini kwamba amri hiyo haikutolewa sawasawa na sheria.

-----MWISHO—-

Makala hii imeandikwa na ZAKARIA MASEKE (Wakili / Advocate)

Angalizo: Natoa angalizo, wale wazee wa kukopi machapisho ya watu na kuweka majina yenu. Ni kosa kisheria. Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayejimilikisha andiko hili. Unaruhusiwa tu kusambaza lakini usibadili yaliyomo. Ni heri uanze kuandika ya kwako mpya.

Disclaimer: Lengo la hii makala ni kutoa elimu kwa jamii. Huu sio ushauri wa kisheria kwa mtu yeyote. Kama unahitaji ushauri wa kisheria wasiliana na Mawakili.

(Nakaribisha maoni na nyongeza, ikiwa kuna sehemu hujaelewa omba ufafanuzi au uliza swali, kuuliza ni bure kabisa).

Imeandaliwa na kuletwa kwako nami Zakaria Maseke,
Advocate / Wakili
(0754575246)
(0746575259 - WhatsApp).
zakariamaseke@gmail.com.
 
Back
Top Bottom