Tarangire yakabiliwa na Simba wajane, yatima

asha ngedere

Member
Nov 6, 2009
92
11
Tarangire yakabiliwa na Simba wajane, yatima

Na Daniel Mbega, Iringa

HAWAFI kwa Ukimwi wala malaria, lakini Simba madume wametoweka katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire. Matokeo yake wameacha wajane na yatima.
Hifadhi nzima kwa sasa ina Simba dume mmoja tu, wawili wengine walikimbia baada ya ‘kuzidiwa’ na utoaji wa huduma kwa Simba majike kwenye hifadhi hiyo.
Naam. Hayo ndiyo matokeo ya ujangili, janga la kitaifa ambalo kwa hakika linatishia uwepo wa rasilimali za asili kwa faida ya wachache wanaotaka kuchuma mahali wasipopanda.
Akiwasilisha mada katika warsha ya wahariri wa habari iliyoandaliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Meneja wa Program ya Ujirani Mwema katika shirika hilo, Ahmed Mbugi, katika kipindi cha miaka mitatu tu (2008 hadi 2010), jumla ya Simba waliouawa kijangili kwenye Hifadhi ya Tarangire ni 62, huku madume wakiwa ndio wengi.
“Mwaka 2008 waliuawa Simba 15, mwaka 2009 Simba waliouawa walikuwa 30 na mwaka 2010 jumla ya Simba 17 waliuawa kwenye hifadhi hiyo. Majangili wanawinda zaidi madume, matokeo yake hifadhi nzima ikabaki na Simba madume watatu tu, lakini kwa sasa wawili wamekimbia hifadhini kwa sababu ya kuzidiwa na utoaji wa huduma kwa majike, amebaki dume mmoja,” anasema Mbugi.
Hali hiyo, anasema, “…Imesababisha kuwepo kwa wajane na yatima wengi kwa wanyama hao, hali inayotishia ongezeko lao kwa miaka ijayo kwani dume mmoja naye anaweza kuchoka na hata kufa. Pengine hata wadogo waliopo sasa, watakapokua hawataweza kuzaliana kwa vile wanyama hao hawawezi kujamiiana kutoka familia moja.”
Lakini mauaji hayo hayakuwapata Simba tu, kwani katika kipindi hicho pia watu 58 waliuawa na wanyama hao wakali, “…wengi wakiwa katika harakati ya kuwawinda Simba kwenye makazi yao,” anaongeza Mbugi.
Hali inaonekana kuwa mbaya zaidi katika Hifadhi ya Manyara kuhusu uwepo wa Tembo ambapo katika kipindi cha mwaka 2007 hadi 2009, jumla Tembo 104 waliuawa kijangili.
“Binadamu waliojeruhiwa na Tembo katika kipindi hicho walikuwa 63,” anasema na kuongeza kwamba wengi kati ya watu hao ni wale wanaofanya shughuli zao katika ushoroba wa Tembo.
Mbugi anasema hali hiyo imeifanya TANAPA kuongeza juhudi katika mpango wa ujirani mwema kwa kuwashirikisha wanajamii wanaoishi pembezoni mwa hifadhi zote huku shirika likisaidia miradi mbalimbali ya kijamii.
“Miradi hii wanaibua wananchi wenyewe, hatuwezi kwenda kuwajengea vyoo wakati mahitaji yao ni zahanati. Kwa kufanya hivi tunataka kujenga ushirikiano wa karibu na kuwaelimisha wanajamii kwamba maliasili hizi ni za Watanzania wote,” anasema.
TANAPA, kupitia program hiyo, inachangia asilimia 70 kwenye miradi yote ya kijamii, wakati asilimia 30 ni nguvukazi za wananchi husika na Mbugi anasema, “…Katika kipindi cha miaka 10, yaani kuanzia 2003/2004 – 2012/2013, shirika hilo limetoa jumla ya Shs. 13,848,784,463.19 kusaidia miradi 1,003 ya jamii.
Katika mwaka wa fedha 2003/2004, TANAPA ilifadhili miradi 94 iliyogharimu Shs. 805,821,034.24; mwaka 2004/2005 jumla ya Shs. 618,502,682.95 zilitumika katika miradi 60; mwaka 2005/06 jumla ya Shs. 865,860,778 zilitumika katika miradi 65; mwaka 2006/07 jumla ya Shs. 1,212,619,300 zilitumika katika miradi 90; mwaka 2007/08 walitumia Shs. 3,447,154,353 katika miradi 141; na mwaka 2008/09 walitumia Shs. 1,736,751,235 katika miradi 87.
Aidha, kwa mwaka wa fedha 2009/10 walifadhili miradi 98 iliyogharimu Shs. 2,320,893,785; mwaka 2010/11 walitumia Shs. 536,136,868 kugharamia miradi 33; mwaka 2011/12 walitumia Shs. 744,244,212 kugharamia miradi 26 na mwaka 2012/13 wametumia Shs. 1,560,800,212 katika miradi 36 ya jamii.
Fedha hizo, anasema, zinatokana na asiliamia ya mapato yatokanayo na hifadhi hizo, “…hasa baada ya kutoa gharama za bajeti ya idara husika.”
Ufadhili huo wa TANAPA, anasema Mbugi, umesaidia kupunguza migogoro baina ya hifadhi na wananchi na pia umepromoti uhifadhi wa mazingira huku mpango ukisaidia kuibua ajira kwa kusaidia makundi mbalimbali ya jamii.
Mpango wa Ujirani Mwema, awali ukijulikana zaidi kama Huduma za Uhifadhi kwa Jamii (CCS) ulianzishwa mwaka 1985 kufuatia mkutano uliofanyika Seronera ambao ulikuwa na madhumuni ya kujadili masuala ya Mpango wa Ikolojia katika Hifadhi ya Serengeti.
Katika mkutano huo ilielezwa kwamba, wanyama wengi walikuwa wanatoweka kwa sababu ya uwindaji haramu ambapo ilibainishwa kwamba Nyati walikuwa wamepungua kutoka 70,000 hadi 40,000 katika hifadhi hiyo.
“Tembo walikuwa wamepungua kutoka 2,500 hadi 500 wakati Faru walipungua kutoka 1,000 hadi 20 tu,” anasema na kuongeza kwamba hali hiyo ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na ujangili uliofanywa na wananchi wa maeneo yanayozunguka hifadhi kwa matumizi ya nyumbani na biashara.
Anaongeza kwamba, malengo ya program hiyo ni kuongeza uhusiano mwema kati ya hifadhi na jamii na kuhakikisha maslahi ya TANAPA yanahubiriwa katika ngazi zote kwa kutoa taarifa katika vijiji husika.
Mpaka sasa TANAPA inasimamia hifadhi 15 ambazo ni Arusha, Gombe, Katavi, Kilimanjaro, Kitulo, Mahale, Lake Manyara, Mikumi, Mkomazi, Ruaha, Rubondo, Saadani, Serengeti, Tarangire, na Udzungwa.
Hifadhi zote hizo zinazungukwa na jumla ya mikoa 28, wilaya 52 na vijiji 536 huku hifadhi za Kilimanjaro na Serengeti zikizungukwa na vijiji 88 kila moja.
Daniel Mbega ni Naibu Mhariri Mtendaji wa gazeti la DARAJA LETU, ambalo ni la Nyanda za Juu Kusini ambako kumekuwa nyuma zaidi katika maendeleo ya utalii nchini.
 
Hiyo ni habari njema kwa nyumbu na pundamilia. Wasiongezeke hao.
 
Haitoshi tu kulalamika, wanafanya nini kuwalinda hao wanyama wasiuawe?

Sent from my BlackBerry 9300 using JamiiForums
 
...hii habari haijakaa kisayansi. Hawa simba sio miti kwamba unakwenda na kuwahesabu mmoja mmoja. Angeeleza utafiti umefanyika lini, wa aina gani na formula ipi maana hata tafiti zina margin of errors n.k. Wangesema tawiri sawa lkn hizi ni km blah blah !!
Hao madume waliokimbia walitoa taarifa wapi, na wamekimbilia kenya ? :)
 
...hii habari haijakaa kisayansi. Hawa simba sio miti kwamba unakwenda na kuwahesabu mmoja mmoja. Angeeleza utafiti umefanyika lini, wa aina gani na formula ipi maana hata tafiti zina margin of errors n.k. Wangesema tawiri sawa lkn hizi ni km blah blah !!
Hao madume waliokimbia walitoa taarifa wapi, na wamekimbilia kenya ? :)

Huwa wanatumia helicopter mkuu ni rahisi mno kuwahesabu hata wewe unaweza wakikuchukua kwenye helicopter yao, wala haihitaji utafiti wa kisayansi sana.
 
Back
Top Bottom