TANZIA: Mhariri wa Magazeti ya Raia Mwema na Jamhuri, Godfrey Dilunga afariki Dunia

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,490
54,884
Godfrey Dilunga, Mhariri wa gazeti la Jamhuri na kwa muda mrefu sana Mhariri Mkuu wa gazeti la Raia Mwema ametangulia mbele ya haki.

Dilunga alikuwa mhariri wa gazeti la Raia Mwema kwa muda mrefu na alianza kuwa mhariri wa Gazeti la Jamhuri kuanzia Februari 2019.

Marehemu alianza kuugua mwezi Julai na baadae kulazwa Hospitali ya Mwananyamala kabla hajahamishiwa Hospitali ya Taifa, Muhimbili.

Msiba upo Kimara jijini Dar na mipango kusafirisha mwili kwenda Morogoro kwa mazishi inafanywa.

Bwana alitoa na Bwana amejitwalia kilicho chake,sifa na utukufu vimrudie yeye aliye tupatia Dilunga kama zawadi. Pole kwa mke na watoto wake ni ngumu lakini yuko Mungu ayafanyaye Magumu kuwa mepesi.

IMG_20190917_115356.jpg


==========

Kutoka Jamhuri:

Tunatangaza Kifo cha Godfrey Dilunga

Kampuni ya Jamhuri Media Limited inasikitika kutangaza kifo cha mfanyakazi wake, Godfrey Dilunga aliyefariki dunia leo alfajiri Septemba 17, 2019 kwa maradhi ya tumbo.

Dilunga alilazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Septemba 9, mwaka huu akitokea Hospitali ya Mwananyamala kwa rufaa kutokana na tatizo la maumivu ya tumbo.

Madaktari na wauguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wamejitahidi kwa kila hali, ila Mungu amempenda zaidi.

Kampuni ya Jamhuri Media Limited kwa kushirikiana na familia ya Dilunga tunaandaa taratibu za kuaga mwili hapa jijini Dar es Salaam na maziko yanatarajiwa kufanyika Morogoro alikozaliwa katika siku itakayotangazwa na familia.

Mwili utasafirishwa kwenda Morogoro kesho Septemba 18, 2019. Msiba uko Kimara Stopover kwa dada.

Dilunga ameajiriwa JML tangu Februari 1, 2019 kama Mhariri wa Gazeti la JAMHURI, ambako amefanya kazi hadi mauti yalipomfika.

Kabla ya kujiunga JAMHURI, Dilunga amepata kufanya kazi na Gazeti la Raia Mwema na Mtanzania miaka ya nyuma.

Kwa muda mfupi aliofanya kazi Gazeti la JAMHURI, Dilunga amekuwa mtu wa msaada na ametoa mchango mkubwa katika kuboresha maudhui ya gazeti hili la Uchunguzi. Hakika pengo lake ni vigumu kuzibika. Tunasikitika sana.

Tunawashukuru madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Mwananyamala na Muhimbili, wahariri, waandishi wa habari, maafisa uhusiano, wanasiasa na watu mbalimbali ambao wamefika Muhimbili kumjulia hali wakati wa ugonjwa wake na tunaomba tuuendeleze mshikamano tuliouonyesha katika kipindi hiki, sasa na baadaye.

Dilunga alizaliwa Oktoba 28, 1976. Ameacha mjane na watoto watatu. Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe.

Deodatus Balile


Mkurugenzi Mtendaji


Jamhuri Media Limited
 
ooooh...Imetokea nini kwa huyu kijana?Mara ya mwisho nimekutana naye kwenye "Kavazi la Mwalimu Nyerere" pale COSTECH,akiwa miongoni mwa watu wanaojadili Mchango wa Kingunge Ngombale Mwilu katika siasa za Tanzania.

Bahati mbaya sitaweza kukuzika sababu ya umbali...

Kapumzike kijana mpole na mwelevu.

Mungu akupe pumziko la Milele.
 
Mwenyezi Mungu awe pamoja na familia yake, ndugu na marafiki na aiweke roho yake mahali pema peponi.
 
Back
Top Bottom