TANZIA Kuga Peter Mziray afariki dunia Hospitali ya Rabininsia. Alikuwa mgombea urais 2010

kirerenya

JF-Expert Member
Aug 27, 2013
1,696
2,252
Kuga Peter Mziray aliyekuwa mgombea urais mwaka 2010 kupitia tiketi ya APPT-maendeleo amefikwa na mauti alasiri leo katika hospitali ya Rabininsia Tegeta na sasa mwili wake umehifadhiwa Muhimbili.

Bwana ametoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Amina

Kuga.jpeg

Kuhusu michango,maoni na ushauri wa Kuga P. Mziray soma...
- Ni aibu kwa Wagombea Urais [NCCR,CUF,TLP] kushindwa na Peter Kuga Mziray
- Kuga Mziray (mjumbe bunge la katiba) afunguka kuhusu Muundo wa Serikali
- Peter Kuga Mziray: Wapinzani mna jukumu la kulinda amani uchaguzi mkuu 2015
- Kuga Peter Mziray: Naunganisha nguvu ya vyama tukamuone Rais

-----
Wasifu(CV) ya Kuga Peter Mziray kwa hisani ya Julius Mtatiro

HISTORIA YAKE

Peter Kuga Mziray alikuwa ni Rais Mtendaji wa chama cha APPT Maendeleo, alishawahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya siasa na kitaaluma ni Mtaalamu wa Mifugo na Uchumi wa Kilimo.

Mziray alizaliwa tarehe 10 Oktoba 1959 katika kijiji cha Kankokoro, kata ya Kihurio, wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro.

Alianza elimu ya msingi wilayani Same katika Shule ya Msingi Jitengeni kati ya mwaka 1966 – 1972 kisha akaendelea na Sekondari Mkoani Dar Es Salaam katika Shule ya Sekondari Pugu kwa kidato cha I hadi IV kati ya mwaka 1973 – 1976. Masomo ya juu ya sekondari (Kidato cha V na VI) aliyapata katika Shule ya Selondari Mkwawa mkoani Iringa kati ya mwaka 1977 – 1978.

Baada ya kumaliza kidato cha sita, Mziray alihudhuria mafunzo ya lazima ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwenye kambi za Bulombora, Kigoma na Buhemba mkoani Mara kati ya mwaka 1979 – 1980.

Mziray alijiunga na Benki ya NBC tawi la barabara ya Boma mjini Moshi na kufanya kazi kama karani kati ya mwaka 1981 – 1983 na halafu Mwaka 1981 – 1983 aliajiriwa kama Msimamizi wa Uzalishaji katika kiwanda cha kusindika ngozi ya ng’ombe, mbuzi na kondoo kilichokuwa jijini Mwanza.

Mwaka 1983, Mziray alikwenda nchini Urusi kuanza masomo ya kitaalam katika Chuo Kikuu cha Lumumba kilichoko Moscow. Alisomea Shahada ya Ufugaji wa Wanyama (Animal Husbandry) na kuihitimu, baadaye akaendelea tena na shahada ya uzamili katika fani hiyohiyo na kuhitimu mwaka 1989 akiwa mtaalamu wa mifugo aliyebobea.

Alipokuwa nchini Urusi alifanikiwa kuongoza Chama Cha Wanafunzi Watanzania walioko Urusi kama Katibu Mkuu (kilikuwa na wanachama zaidi ya 600), alifanya kazi kubwa ya kutatua matatizi ya wanafunzi huko ughaibuni, akishirikiana kwa karibu na Ubalozi wa Moscow (USSR).

Mziray alirejea nchini Tanzania na kuajiriwa na wizara ya Kilimo na Mifugo mwaka huohuo 1989. Mwaka 1991 alikwenda nchini Uingereza kwa masomo ya muda mfupi katika Chuo Kikuu cha Bradford ambako alitunukiwa Cheti cha Mipango ya Miradi ya Kilimo. Wakati huohuo alianza kusomea masuala ya Uchumi wa Kilimo kwa ngazi ya Stashahada katika Chuo Kikuu cha Reading kuanzia mwaka 1992 hadi alipohitimu mwaka 1993 na kuunganisha tena shahada ya uzamili ya Uchumi wa Kilimo/Mifugo ambayo aliikamilisha mwaka 1994.

Wakati Mziray anajiendeleza kimasomo nchini Uingereza alikuwa mwajiriwa serikalini na hata alipohitimu masomo yake mwaka 1994 alikuwa mwajiriwa wa wizara hiyohiyo ya Kilimo.

Aliporejea nchini kutoka nje, aliendelea kutoa mchango wake kwa nchi yetu akishiriki kubuni na kuanzisha miradi mbalimbali ya kilimo na ufugaji ambayo ilipitishwa na wizara, kuwatembelea wakulima na wafugaji ili kutoa ushauri na kufanya machapisho mbalimbali juu ya kilimo na mifugo hadi alipoamua kustaafu rasmi mwaka 2000.

Mziray amebobea vizuri katika lugha tatu za kimataifa: Kiswahili, Kiingereza na Kirusi na amemuoa Harumi na wana watoto na familia yenye furaha.

MBIO ZA UBUNGE

Mziray alianza mbio za ubunge mwaka 1995, alifanya hivyo kupitia NCCR – Mageuzi na akashindwa kupenya kura za maoni za ndani ya chama hicho katika jimbo la Same Mashariki. Alirejea kazini na kuendelea na utumishi kwa sababu sheria ilikuwa inaruhusu hali hiyo.

NCCR ilipovurugika na baadhi ya wanachama wake na viongozi kujiondoa na kwenda TLP, Mziray naye alikuwa mmoja wao na mwaka 2000 akapata nafasi ya kuwania ubunge wa Jimbo la Same Mashariki kupitia TLP, aliamua kuacha kazi wizarani na kwenda jimboni ambako alipambana na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Daniel Yona. Mziray hakufanikiwa kushinda ubunge mwaka huo.

Baadaye mwaka 2001 aliomba ridhaa ya TLP ili apitishwe na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki. Alikuwa miongoni mwa watanzania waliojieleza bungeni kuomba nafasi hiyo lakini hakufanikiwa kuchaguliwa kwa sababu chama chake kilikuwa na wabunge wachache na moja moja kikakosa uungwaji mkono kwa sababu nafasi za ubunge ule huchukuliwa kwa kiasi kikubwa na wabunge kutoka vyama vyenye wabunge wengi.

Baada ya kuona mambo hayaendi ndani ya TLP, Mziray alishirikiana na wenzake kadhaa kuasisi chama kipya, kikiitwa PPT – Maendeleo (Sasa kinaitwa APPT Maendeleo) na mwaka 2005 akagombea ubunge wa Same Mashariki kwa tiketi ya PPT.

Mziray alifanikiwa kumtikisa Bi. Kilango Malecela wa CCM kiasi ambacho wengi walidhani Mziray angeshinda. Matokeo yalipotangazwa, Mziray alipata kura 11,665 (34.7%) akiachwa kwa kadri na Bi Kilango ambaye alipata takribani mara mbili ya ushindi wa Mziray “Bi Kilango alipata kura 20,333 (60.4%)”.

MBIO ZA URAIS

Peter Mziray alianza mbio za urais mwaka 2010 baada ya kupitishwa na chama chake APPT Maendeleo kwa ajili ya jukumu hilo. Wakati anagombea Urais watu wengi hawakuwa wanamfahamu vizuri na ilidhaniwa kuwa anapoteza muda lakini matokeo yalipotangazwa, aliibuka kwenye nafasi ya nne akipata asilimia 1.15 (kura 96,933).

Mwaka huo pia chama chake kilipata madiwani watatu na mmoja wa viti maalum kutoka mikoa ya Mara na Kilimanjaro na kikaingia kwenye orodha ya vyama vya siasa vichanga vinavyopata ruzuku.
 
Fanga mpango wa picha wengine tumemsahau
Nabulete habari kamili vipi alikuwa anaumwa?
 
Dah! Aisee.

Kuga Mziray alikua mshikaji wangu sana. Nimekua nae sana maeneo ya Kinondoni. Kuga alikua akifika DDz ananipigia sim tukajumuike, au kwa John Feza ananipigia kama niko maeneo ya jirani tukapige stori na kubadilishana mawazo

Ni mkubwa sana kwangu, sawa na mzee ila tulikua tunaelewana sana, tulitokea tu kufahamiana maeneo ya starehe. Alikua na vyombo vyake vya muziki nadhani vilikua hapo hunters kama sijakosea, akawa akaniomba nimtaftie mnunuzi.

Nimesikitika sana. Duniani kweli tunapita.

Poleni sana ndugu wafiwa.
 
Mungu aiweke roho ya Marehemu mahali inapostahili kutokana na matendo yake hapa duniani , hasa ya kisiasa na kijamii .
 
R.IP. Brother Kuga Mziray!
You've run a tough race in life...You've Completed your Part in this World.
Most importantly You placed yourself to fight and realize the wellbeing of our Society...
Those who heard your voices and struggles will cherish your Humanity!
May The Lord Rest Your Soul in Eternal Peace ...Amen!
 
Back
Top Bottom