TANZIA: Aliyewahi kuwa Meya wa Dar, Dr. Didas Massaburi afariki, Rais atuma Salamu za rambirambi

Informer

JF-Expert Member
Jul 29, 2006
1,582
6,627
Aliyewahi kuwa Meya wa Dar na Mbunge wa Afrika Mashariki, ndg Didas Masaburi amefariki dunia usiku huu hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa.

Mazishi ya aliyekuwa Meya wa jiji hili Didas Masaburi yanatarajiwa kufanyika jumatatu Chanika ndani ya eneo la chuo alichokuwa akikimiliki.

Masaburi alifariki usiku wa kuamkia leo akiwa na umri wa miaka 56. Ameacha wake watatu na watoto 17.

Kwa mujibu wa mtoto wake wa kwanza Steven Masaburi amesema baba yake alifariki jana saa mbili usiku lakini wakati wa uhai wake alikuwa akisema mara kadhaa kwamba siku akifariki azikwe katika eneo hilo
"Mzee alikuwa ni mtu wa matani sana lakini siku zote alikuwa akisema akifariki azikwe katika eneo hili ambalo alikuwa akitumia muda mwingi kujitaftia riziki"

Aliwahi kuwa Meya wa Dar es Salaam mwaka 2010- 2015 na mgombea ubunge wa CCM mwaka 2015 katika jimbo la Ubungo.
image.jpeg


Taarifa za kuugua kwake ziliwekwa hapa JF > Meya mstaafu wa Dar, Dkt Didas Masaburi alazwa Muhimbili.


========

UPDATE:

Rais Magufuli atuma Salamu za Rambirambi familia ya Meya Mstaafu wa Jiji la Dar es Salaam Marehemu Didas Masaburi.
14725547_1008276552616652_4879696274680473689_n.png

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameitumia salamu za rambirambi familia ya Meya Mstaafu wa Jiji la Dar es Salaam Dkt. Didas Masaburi aliyefariki dunia jana tarehe 12 Oktoba, 2016 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.

Katika salamu hizo Rais Magufuli amesema amepokea taarifa ya kifo cha Dkt. Didas Masaburi kwa mshituko na masikitiko makubwa na kwamba anaungana na familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki katika kipindi hiki kigumu cha huzuni ya kuondokewa na mpendwa wao.

"Poleni sana familia ya Dkt. Didas Masaburi, najua huu ni wakati mgumu sana kwenu, lakini niwahakikishie kuwa sote tumeguswa sana na msiba huu kwa kuwa tumempoteza mtu muhimu, msomi mzuri, kiongozi aliyelitumikia Taifa kwa moyo wake wote na aliyesimamia kile alichokiamini" amesema Rais Magufuli katika salamu hizo.

Aidha, Dkt. Magufuli amewapa pole wanachama na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wamempoteza Mwana CCM mwenzao pamoja na Viongozi na watumishi wa Jiji la Dar es Salaam ambao walifanya nae kazi alipokuwa Meya wa Jiji.

Amemuombea kwa Mwenyezi Mungu ampumzishe mahali pema peponi.

"Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Amina" amemalizia Rais Magufuli.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam
 
R.I.P tumuombee alazwe mahala pema ppeponi maana ni safari yetu wote haipaswi kuhukumu! Amina
 
Back
Top Bottom