Tanzania yaunga mkono rasilimali asilia kuingizwa Pato la Taifa

BabuK

JF-Expert Member
Jul 30, 2008
1,845
329
TANZANIA inaunga mkono kuanzishwa kwa mfumo wa kujumuisha thamani ya rasilimali asilia katika tathmini ya Pato la Taifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal, jana wakati akihutubia mkutano wa Maendeleo Endelevu wa Bara la Afrika, unaozungumzia kuhusu mchango wa maliasili katika kutathimini Pato la Taifa sambamba na kutathimini juu ya athari za mazingira katika nadharia ya kukua kwa maendeleo ya nchi, mkutano unaofanyika katika Jiji la Gaborone nchini Botswana.

“Ni imani ya Serikali ya Tanzania kuwa mpango huu utasaidia kutoa nafasi ya nchi kujikagua hasa kwa kuzingatia rasilimali zinazotumika na faida inayopatikana. Tena mpango huu utatoa nafasi kwa nchi kujiuliza kama matumizi ya rasilimali zake yanalenga kutambua faida ya sasa na siku zijazo ili kuhakikisha kuwa mazingira yanabakia kuwa salama kwa ajili ya vizazi vijavyo,” alisema Makamu wa Rais.

Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, dhana ya kutathimini mazingira na kujumisha rasilimali asilia kwenye hesabu za Pato la Taifa, kunaweza kusaidia nchi kufikia maamuzi ambayo yataliwezesha taifa kupata maendeleo endelevu hali ambayo itachangia jitihada za kupunguza umasikini na kukuza uchumi.

Katika mkutano huo ambao Dk Bilal anamwakilisha Rais Jakaya Kikwete, pia kulijadiliwa umuhimu wa Serikali za Afrika kutazama upya sera na mikakati ya nchi hizo na kuweka mikakati inayolenga katika kutunza mazingira itakayowezesha kupata maamuzi ya busara yatakayohakikisha upatikanaji wa maendeleo endelevu.

Bilal alisema, Tanzania iliona umuhimu wa rasilimali asilia tangu nchi ilipopata Uhuru mwaka 1961 ambapo iliweza kutenga asilimia 30 ya eneo la nchi kwa ajili ya wanyama na viumbe hai. Tena ziliwekwa sera nzuri zilizolinda uvunaji wa rasilimali hizo kwa manufaa ya taifa.

Akifungua mkutano huo, Rais Seretse Khama Ian Khama wa Botswana alisema nchi yake imeandaa mkutano huo kwa lengo la kutaka kuzungumzia masuala ya Afrika kwa pamoja juu ya maendeleo endelevu na kuangalia namna nchi hizo zinavyoweza kutumia utajiri wa raslimali za asili katika kukuza maendeleo ya nchi zao.

Katika mkutano huo, Botswana na Tanzania zimepongezwa kwa uhifadhi wa maliasili na mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadaye.
 
Back
Top Bottom